Ask.Mkuu Fortunatus Nwachukwu,Katibu Mkuu wa Baraza la Kipapa la Uinjilishai wakati wa Congamano la Dunia SIGNIS 2026 Ask.Mkuu Fortunatus Nwachukwu,Katibu Mkuu wa Baraza la Kipapa la Uinjilishai wakati wa Congamano la Dunia SIGNIS 2026  

Ask.Mkuu Nwachukwu:Mawasiliano katika huduma ya Injili!

Katika mahojiano na Vatican News wakati wa Kongamano la Dunia la SIGNIS 2026,Askofu Mkuu Nwachukwu,Katibu Mkuu wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji,alisema kwamba wawasilianaji Wakristo wanaitwa kuwa wanafunzi kabla ya kuwa wahusika wakuu,huku wakijenga utambulisho unaotokana na malezi ya kibinadamu na kiroho kabla ya kuunda jukwaa la kidijitali katika huduma ya Injili.

Na Rocío García – Kigali, Rwanda.

Askofu Mkuu Fortunatus Nwachukwu alishiriki katika kikao cha kwanza cha jumla cha Kongamano la SIGNIS 2026, likiongozwa na kauli mbiu ya "Mawasiliano ya Kidijitali kwa Maelewano ya Utamaduni na Ustawi wa Mazingira." Wakati wa hotuba yake, alisema kwamba ubinadamu unakabiliwa na chaguo: kubaki katika ulimwengu uliojaa mkanganyiko, kujitosheleza na kelele, au kujenga upya pamoja kuta za jiji ambapo Mungu na ubinadamu wanaweza kukaa katika ushirika.

Wakati muhimu sana wa sala katika eneo la Kumbu Kumbu ya mauaji ya kimbari,Kigali Rwanda
Wakati muhimu sana wa sala katika eneo la Kumbu Kumbu ya mauaji ya kimbari,Kigali Rwanda

Kama jibu la changamoto hii, alirudia mwaliko wa Papa Leo XIV wa kujenga ustaarabu wa upendo, kazi ambayo, alisema, inaweza kukamilika kama "matofali kwa matofali" na wanafunzi wanaobeba kamera, maikrofoni na kompyuta za mkononi: wanaume na wanawake, wanaamini kwamba ufuasi wa utume lazima utangulie kabla ya ushawishi. Akijenga juu ya tafakari hiyo kuhusu utambulisho na dhamira ya mzungumzaji Mkristo, Askofu Mkuu alizungumza na Vatican News, akitoa ufahamu zaidi kuhusu wito na jukumu la wale wanaohusika katika mawasiliano.

Wawasilianaji: Mitume Katika Nafasi Mpya za Uinjilishaji

Alipoulizwa kuhusu sifa zinazopaswa kuwatambulisha wawasilianaji wanaotumikia utume wa uinjilishaji, Askofu Mkuu Nwachukwu alisisitiza kwamba wameitwa kufanya aina ya mawasiliano ambayo inakuwa njia ya wokovu, inayoweza kuwasilisha upendo wa Mungu na kutangaza uwepo wa Yesu Kristo. Akikumbuka amri ya Yesu ya "kuwafanya mataifa yote kuwa wanafunzi," alieleza kwamba, wakati huo, mataifa yalieleweka hasa kama maeneo ya kimwili.

Hata hivyo, leo hii, nafasi mpya zimeibuka ambapo watu hukutana, huingiliana na kujenga jumuiya, ikiwa ni pamoja na Instagram, TikTok, YouTube na majukwaa mengine ya kidijitali. Kwa sababu hiyo, alisema, Habari Njema ya Bwana haijaitwa kubaki katika nafasi za kimwili tu, bali lazima pia ifikie ulimwengu wa kidijitali.

Washiriki wa Kongamano la Dunia na Mkutano wa Wajumbe wa SIGNIS wa mwaka 2026, wakiwemo mapadri, watawa wanawake, waamini walei, waandishi wa habari na wataalamu wa mawasiliano kutoka nchi mbalimbali.
Washiriki wa Kongamano la Dunia na Mkutano wa Wajumbe wa SIGNIS wa mwaka 2026, wakiwemo mapadri, watawa wanawake, waamini walei, waandishi wa habari na wataalamu wa mawasiliano kutoka nchi mbalimbali.

Katibu Mkuu wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji pia alisisitiza umuhimu wa kukumbatia wito huu kwa ufahamu kamili, ili kila kipande cha maudhui kinachochapishwa, kama vile makala, picha au utayarishaji wa sauti na taswira visiwe vyombo vya taarifa tu. Badala yake, vinapaswa kukuza ushirika na matumaini, kujenga madaraja, kuhimiza kukutana na kufungua njia mpya ambazo ujumbe wa Injili unaweza kufikia mioyo ya watu.

Utambulisho Mzito Kabla ya Kuwasiliana

Alipoulizwa ni ujumbe gani angetoa kwa wawasilianaji wa siku zijazo, Askofu Mkuu Nwachukwu alirudi kwenye baadhi ya tafakari alizoshirikisha  wakati wa jopo la SIGNIS 2026. Wito wake wa kwanza, hasa kwa wawasilianaji vijana, ilikuwa rahisi lakini ya msingi: "Jenga akili yako kabla ya kujenga jukwaa lako." Alielezea kwamba maandalizi ya ndani, malezi ya mwanadamu na ukomavu wa kiroho lazima viwe kabla ya kutafuta ushawishi katika nyanja ya kidijitali.

Watawa washiriki katika Kongamano la SIGNIS 2026,Kigali Rwanda
Watawa washiriki katika Kongamano la SIGNIS 2026,Kigali Rwanda

Pia aliwahimiza wawasilianaji kuhakikisha kwamba kila safari ya kidijitali inakuwa njia ya kukutana badala ya ile ya ukabila, utengano au mgawanyiko. Katika muktadha huo, alisisitiza umuhimu wa kuunganisha utunzaji wa nyumba yetu ya pamoja katika masimulizi yao, akikumbusha kwamba "utunzaji wa kazi ya uumbaji ni sehemu muhimu ya historia  wanazosimulia." Kwa kuhimitimishwa, Askofu Mkuu Nwachukwu aliwakumbusha wawasilianaji kwamba dhamira yao imejikita katika utambulisho mkubwa: kuwa wanafunzi mbele ya wahusika wakuu, wajenzi wa madaraja badala ya mawakala wa mgawanyiko, na mashuhuda wa tumaini la Injili katika ulimwengu ambao pia unahitaji kukutana na Mungu katika nafasi mpya za kidijitali za leo hii.

Washiriki wa Kongamano la SIGNI2026 wakitembelea makanisa mahalia nchini Rwanda
Washiriki wa Kongamano la SIGNI2026 wakitembelea makanisa mahalia nchini Rwanda

Imesasishwa  tarehe 8 Agosti 2026, saa 5:23 asubuhi, na Angella Rwezaula.

ASK.MKUU FORTUNATUS,KATIBU MKUU WA BARAZA LA KIPAPA LA UINJILISHAJI

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata taarifa mpya kwa kujisajili kwenye jarida letu la kila siku. Just click here.

08 Agosti 2026, 11:23