Wito wa kumtumikia Mungu kwa wengine kwa upendo na ukarimu
Na Sr. Ernestina Patrick Lasway SAC.
Shirika la Masista wa Upendo wa Mtakatifu Karoli Borromeo (Trier) ilianzishwa tarehe 18 Juni 1652 huko Nancy, Ufaransa na Emmanuel Chauvenel, nao wanaendelea kuishi utume wa mwanzilishi wao kwa upendo na huduma Ulimwenguni kote. Sasa, Shirika hili linahudumu kikamilifu kichungaji na kijamii nchini Tanzania, wakitoa utume wao wa kiroho na wa kibinadamu kwa watu. Watawa hawa wanaishi karama yao ya "Umoja na Mungu katika Upendo unaodumu," ikiwaita watawa kulea ustawi wa kiroho na kimwili wa watu wote.
Safari ya kwenda Tanzania
Shirika la Masista wa Upendo la Mtakatifu Karoli Borromeo, walifika Tanzania mwaka 1985, wakitokea Uholanzi. Walianzisha Jumuiya yao ya kwanza huko Mtinko, katika Jimbo la Singida. Kwa miaka mingi, Masista wamehudumu kwa uaminifu katika utume mbalimbali, ikiwa ni pamoja na elimu, katekesi, na huduma ya kichungaji. Kadri utume wao ulivyopanuka, Masista walitambua hitaji linaloongezeka miongoni mwa watawa wa kike na wakiume, mapadre, na waamini walei kwa ajili ya mahali pa ukimya, kupumzika, na upyaishaji kiroho. Utambuzi huu ulisababisha kuanzishwa kwa Nyumba ya Mafungo, Kituo cha Semina, na Ukumbi wa Matukio mbalimbali katika Jimbo Kuu ya Arusha. Hili ni jibu kwa mwaliko wa Yesu Kristo katika Injili ya Mtakatifu Marko isemayo: “Njoni twende sehemu ya upweke mpate kupumzika kidogo.”(Mk 6:31). Kituo cha Mafungo cha Mtakatifu Karoli kilitazamwa kama mahali patakatifu ambapo watu wangeweza kukutana na Mungu katika maombi na tafakari, mbali na ratiba zenye shughuli nyingi.
Kituo cha Makazi cha Mtakatifu Karoli, Tengeru
Kituo cha Makazi cha Mtakatifu Karoli huko Tengeru, Arusha, kilifunguliwa rasmi tarehe 14 Oktoba 2017. Sr. Agatha alisema kwamba, “kituo hiki kilianzishwa kwa kujibu mahitaji ya wakati wetu na kushiriki karama ya shirika, kwa kutoa huduma ya kiroho na kimwili, yaani, nafasi za maombi kwa watu binafsi, vikundi kwenye mafungo, na wale wanaohitaji kupumzika tu." Kituo hiki kiko karibu na mji wa Arusha unaojulikana kama kitovu cha utalii na shughuli za kimataifa nchini Tanzania, kituo hicho kinawakaribisha wageni kutoka kote ulimwenguni.
Ukarimu kama huduma
Ukarimu ndicho kitu kinachozingatiwa katika utume wa shirika hili. Sr. Juliana na Sr. Michaella, wanaohudumu katika kituo hicho, walieleza kwamba, kuwakaribisha wageni ni njia ya kumtumikia Mungu. "Ni furaha kubwa kuwakaribisha na kuwahudumia wageni mahalia na nje ya Tanzania, masista hao walielezea, “mgeni anapofika na baadaye kuondoka kwa furaha na amani, inatupa faraja kubwa kwani kupitia huduma hii, tunajifunza kutoka kwa wageni wetu, nao pia wanajifunza kutoka kwetu. Sisi ni watumishi tu, tunahakikisha kwamba kila mtu anayekuja hapa anakutana na Mungu," Mbali na huduma za malazi na mapumziko, kituo hicho kina ukumbi mkubwa wa matumizi mbalimbali unaotumika kwa semina, kongamano, mikutano, na sherehe, ikiwa ni pamoja na kipaimara, harusi, na upadrisho. Kupitia huduma hii, Masista wanashuhudia karama yao ya upendo, ukarimu, na ubora katika huduma.
Utunzaji,uendelevu na kujitegemea
Kuwahudumia wageni pia ni kuhakikisha kuna chakula bora na malazi salama. Ili kusaidia hili, Masista hutunza bustani za mboga na bustani za matunda, wakitoa mazao mapya kwa matumizi ya kila siku. "Kwa kulima chakula chetu wenyewe, tuna uhakika kwamba tunachowalisha wageni ni salama, kwani hatutumii kemikali," anabainisha Sr. Agatha. Masista pia wana miradi midogo ya mifugo, ikiwa ni pamoja na kuku, ng'ombe, nguruwe, na sungura. Mipango hii husaidia kupunguza gharama huku ikihakikisha wageni wanapata chakula kilicho bora, ikiashiria kujitolea kwa masista katika usimamizi nauendelevu unaowajibika.
Utume na jamii mahalia
Masista wakifuata maonoya mwanzilishi wao, wao hufuata utume wao kwa kushirikiana na amii mahalia. Wanatoa mafundisho ya katekesi katika shule na parokia, pamoja na elimu xza ujuzi wa maisha na kuwawezesha watu kujitegemea zaidi. Kupitia misheni hii ya pamoja, jamii hupata uwepo na upendo wa Kristo unaoonyeshwa kupitia huduma ya kila siku ya masista.
Matunda na changamoto za utume
Tangu kuanzishwa kwa Kituo cha mapumziko cha Tengeru kimewakaribisha wageni kutoka sehemu nyingi za dunia kwa mafungo, semina, na mikutano. Katika kituo hiki kuna wageni wengi na hii ni ishara ya shukrani na uaminifu. "Tunawathamini na kuwashukuru wageni mahalia na wakitaifa. Maoni na mapendekezo yao hutusaidia kuboresha huduma zetu," alisema Sr. Agatha. Maoni haya yanatusaidia kukidhi mahitaji ya wageni kwa wakati unaofaa. Kama huduma yoyote ya ukarimu, changamoto zipo. Miongoni mwao, idadi inayobadilika ya wageni na wasiwasi wa kiafya wa mara kwa mara unahitaji kubadilika na umakini. Kwa bahati nzuri, vituo vya matibabu vilivyo karibu huhakikisha kwamba wageni wanapata huduma inayofaa inapohitajika.
Nyumbani mbali na nyumbani
Kituo hiki cha watawa cha Mtakatifu Karoli Karoli na Makazi ya mapumziko na sala kinawakilisha kauli mbiu yake kama nyumbani mbali na nyumbani. Kwa Masista wenye ujuzi wa ukarimu, upishi, na lugha, wageni wanaozungumza Kiswahili, Kiingereza, Kijerumani, na Kifaransa wanahisi kukaribishwa na kueleweka. Wote wanaotafuta mahali pa kupumzika na upyaishaji wa kiroho wanaalikwa katika mazingira haya ya amani nje kidogo ya jiji la Arusha, ambapo Shirika la Masista wa Upendo la Mtakatifu Karoli Borromeo wanaendelea kumtumikia Mungu kupitia upendo, sala na ukarimu.
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here.