Liturujia ya Neno la Mungu Dominika 17 ya Mwaka A wa Kanisa: Ujumbe mkuu ni huu; Ufalme wa Mungu hauwezi kuthaminishwa na kitu chochote. Ili kuupata ni lazima kujiweka chini ya ulinzi na maongozi ya Mungu, Liturujia ya Neno la Mungu Dominika 17 ya Mwaka A wa Kanisa: Ujumbe mkuu ni huu; Ufalme wa Mungu hauwezi kuthaminishwa na kitu chochote. Ili kuupata ni lazima kujiweka chini ya ulinzi na maongozi ya Mungu,   (@Vatican Media)

Tafakari Dominika 17 ya Mwaka A wa Kanisa: Ufalme wa Mbinguni

Yesu kwa kuyatimiza mapenzi ya Baba ameanzisha ufalme wa Mungu ambao ujio wa utawala wake unatekelezwa kwa fumbo la Pasaka; mateso, kifo na ufufuko wake. Naye anasema “Nami nikiinuliwa juu ya nchi nitawavuta wote kwangu” (Yoh. 12:32). Watu wote wanaitwa kuingia katika ufalme huu, ndio maisha ya muungano na Mungu, maisha ya uwepo wa Mungu na maisha ya uendelezaji wa tunu za kimungu katika maisha ya kila siku ya mwanadamu.

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, dominika ya 17 ya mwaka A wa kiliturujia katika Kanisa, kipindi cha kawaida. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Leo XIV kwa Maadhimisho ya Siku ya Sita ya Babu, Bibi na Wazee duniani tarehe 26 Julai 2026 unanogeshwa na kaulimbiu: "Sitakusahau kamwe." Rej. Isa 49:15. Hii ni siku maalum ya kuwakumbuka, kuwashukuru na kuwapongeza wazee kwa hekima na upendo wao, mwaliko kwa jamii kushikamana kwa dhati na wazee. Mwenyezi Mungu anaahidi kwamba, kamwe hatamsahau mja wake kwani amechora sura yake kwenye kiganja cha mikono yake na kwamba, upendo wake ni mkuu kuliko upendo kwa mama kwa mtoto wake. Mwenyezi Mungu anazungumza na waja wake kama rafiki, na kila mtu binafsi na kwa watu wote katika ujumla wao na hata leo hii maneno yake yanawahusu hata watu katika ulimwengu mamboleo: "Sitakusahau kamwe" yakisemwa moja kwa moja kwa kila mtu. Haya ni maneno yanayowajaza watu faraja na matumaini. Ni jibu kwa hisia chungu inayousumbua moyo: "Bwana ameniacha; Bwana wangu amenisahau" (Isa 49:14.) Ujumbe mkuu ni huu; Ufalme wa Mungu hauwezi kuthaminishwa na kitu chochote. Ili kuupata ni lazima kujiweka chini ya ulinzi na maongozi ya Mungu, kuzishika na kuziishi amri na maagizo yake, na sio kuvitegemea vitu au watu.

Kwa Fumbo la Msalaba Kristo ameanzisha Ufalme wa Mbinguni
Kwa Fumbo la Msalaba Kristo ameanzisha Ufalme wa Mbinguni   (Vatican Media)

Kristo Yesu kwa kuyatimiza mapenzi ya Baba ameanzisha ufalme wa Mungu. Ufalme ambao ujio wa utawala wake unatekelezwa kwa fumbo la Pasaka; mateso, kifo chake Msalabani na ufufuko wake. Naye anasema “Nami nikiinuliwa juu ya nchi nitawavuta wote kwangu” (Yoh. 12:32). Watu wote wanaitwa kuingia katika ufalme huu, ndio maisha ya muungano na Mungu, maisha ya uwepo wa Mungu na maisha ya uendelezaji wa tunu za kimungu katika maisha ya kila siku ya mwanadamu. Ni katika tumaini hili Zaburi ya wimbo wa mwanzo inasema hivi; “Mungu yu katika kao lake takatifu. Mungu huwakalisha wapweke nyumbani. Yeye huwapa watu wake nguvu na uwezo” (Zab. 68:5-6). Na Mama Kanisa sala ya mwanzo anasali hivi; “Ee Mungu, wewe ndiwe mlinzi wa wenye kukutumaini; pasipo wewe hakuna lililo thabiti, hakuna lililo takatifu. Utuzidishie huruma yako; utusimamie na utuongoze, ili tutumie vema mambo ya dunia, hali tumeambata na ya milele.”

Ufalme wa Mungu unasimikwa katika haki, amani, upendo na utakatifu
Ufalme wa Mungu unasimikwa katika haki, amani, upendo na utakatifu   (@Vatican Media)

Somo la kwanza ni la kitabu cha kwanza cha Wafalme (1Fal. 3:5, 7-12). Ni simulizi la Mungu kumtokea Sulemani katika ndoto akiwa Gibeoni, lilikokuwa sanduka la agano, alipoenda kumtolea sadaka na kuomba msaada katika utawala wake. Mungu alimwambia; “Omba upendacho nami nitakupa”. Sulemani aliomba moyo wa hekima ajue kutofautisha jema na baya, ili aweze kuwaongoza vyema watu wake. Ombi hili lilionekana jema mbele za Mungu, kwa kuwa hakujitakia maisha ya siku nyingi, wala utajiri kwa nafsi yake, wala roho za adui zako. Hivyo akampa moyo wa hekima na akili, ambayo hajawahi kuwa nao mtu yeyote kabla yake, na hajawahi kutokea mtu mwingine kama yeye. Huku kutaka kuwaongoza watu kadiri ya sheria ya Mungu, kulimpa Sulemani kibali cha kupewa zaidi ya alichoomba. Ndiyo maana Yesu anasema hivi; “Tafuteni kwanza ufalme wa Mungu, mengine yote mtapewa kwa ziada.” Ni katika muktadha huu zaburi ya wimbo wa katikati inasema hivi; “Sheria yako Bwana naipenda mno ajabu. Bwana ndiye aliye fungu langu, nimesema kwamba nitayatii maneno yako. Sheria ya kinywa chako ni njema kwangu, kuliko maelfu ya dhahabu na fedha. Nakuomba fadhili zako ziwe faraja kwangu, sawa sawa na ahadi yako kwa mtumishi wako. Rehema zako zinijie nipate kuishi, maana sheria yako ni furaha yangu. Ndiyo maana nimeyapenda maagizo yako, kuliko dhahabu, naam, dhahabu iliyo safi. Maana nayaona mausia yako yote kuwa ya adili, kila njia ya uongo naichukia. Shuhuda zako ni za ajabu, ndiyo maana roho yangu imezishika. Kufafanusha maneno yako kwatia nuru, na kumfahamisha mjinga hekima yako” (Zab. 118: 97, 57, 72, 76-77, 127-130).

Ufalme wa mungu umetundikwa juu ya Msalaba
Ufalme wa mungu umetundikwa juu ya Msalaba   (@Vatican Media)

Somo la Pili ni kutoka katika Waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi (Rum. 8:28-30). Ujumbe wake mkuu ni huu; Mungu ametuchagua kuwa katika ufalme wake tangu zamani, kuanzia mwanzo wakati wa uumbaji. Ndiyo kusema, alituchagua tangu milele kwa kuwa maisha yetu yamo katika umilele wake. Dhambi ilipotutenga naye, wakati ulipowadia, ametushirikisha tena uzima huu kwa njia ya Yesu Kristo Mwanae wa Pekee, kwa kuwa kwa upendo wake alikusudia kutushirikisha furaha ya milele katika utukufu wake. Tunasoma hivi; “Twajua ya kuwa katika mambo yote, Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake. Maana wale aliowajua tangu asili, aliwachagua tangu asili wafananishwe na mfano wa Mwana wake, ili Yeye awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi. Na wale aliowachagua tangu asili, hao akawaita; na wale aliowaita, hao akawahesabia haki; na wale aliowahesabia haki, hao akawatukuza.”

Ufalme wa Mbinguni umefanana na hazina iliyofichika
Ufalme wa Mbinguni umefanana na hazina iliyofichika   (@Vatican Media)

Injili ni kama ilivyoandikwa na Mathayo (Mt. 13:44-52). Ni mafundisho ya Yesu kuhusu thamani ya ufalme wa Mungu na namna ya kuupata. Katika mafundisho yake, Yesu anatumia mifano mitatu, ambapo mifano miwili yaani; mfano wa lulu yenye thamani na hazina iliyofichika, ujumbe wake ni huu; ufalme wa Mungu hauwezi kuthamanishwa ni kitu chochote kile. Na kwa mfano wa Juya, ujumbe wake ni kuwa sio wote waliobatizwa wakawa wakristo, wana wa Kanisa, katika hukumu ya mwisho wataingia moja kwa moja katika ufalme wa mbinguni, bali ni wale watakaoziishi vyema ahadi za ubatizo, wakaiishi vizuri imani yao kwa kuzishika amri na maagizo ya Mungu, kwa kuwahudumia wengine kwa moyo wa upendo, ndio watakaoingia katika ufalme wa Mungu mbinguni. Lakini ufalme wa Mungu ni nini? Ni hali ya uwepo wake unaoleta furaha ndani ya wale waliompokea ndani yao na kuishi kadiri ya amri na maagizo yake. Hivyo ufalme huu unaanza kujengwa na kudhihirika hapa hapa duniani, na ukamilifu wake ni Mbinguni. Ndiyo maana katika sala ya Baba yetu tunasali hivi; “Ufalme wako ufike, utakalo lifanyike duniani kama mbinguni.” Duniani tunakuwa katika ufalme wa Mungu tunapoishi katika uwepo wa Mungu na kutimiza mapenzi yake, tukiwa ndani na pamoja na Kanisa, fumbo la mwili wa Kristo. Lakini kuwepo ndani ya Kanisa na kuwa tu na ushirika nalo, haitoshi kuingia katika ufalme wa mbinguni, bali ni mwaliko wa awali wa kuingia katika huo ufalme. Ni katika kudumu katika kutenda mema mpaka siku ya kufa, ndiko kutatustahilisha kuingia katika uzima wa milele, utimilifu wa furaha ambayo mwanadamu daima anaitafuta.

Mfalme Sulemani aliomba heskima
Mfalme Sulemani aliomba heskima   (@Vatican Media)

Na kwa kuwa furaha ni hali ya kuridhika inayoletwa na tendo jema. Hivyo kutenda matendo mema ni kutimiza mapenzi ya Mungu, na ndiko kunakotupatia furaha, na hivyo kuanza kuwa katika ufalme wa mbinguni kwa kuanza kuionja furaha tukiwa bado tuko hapa duniani, na ukamilifu wa furaha hii ni kuuona uso wa Mungu milele yote mbinguni, kama mzaburi anavyosema; “Ilikuwa hamu ya Moyo wangu kuuna uso wa Ee Bwana” (Zab. 27:8). Hii ndiyo sababu ya Mtume Paulo kusema kuwa; “Kama lengo la maisha yetu lipo katika vitu vya ulimwengu huu, basi sisi ni watu wakusikitikiwa sana” (1Kor 15:19.) Hivyo ufalme wa Mungu ni lulu yenye thamani kuliko vitu yote, na ili tuweze kuutambua tunahitaji Hekima ya Mungu ili kuyajua mapenzi yake na kutambua kuwa ni katika kuyatimiza mapenzi yake kunatuletea furaha ya kweli hapa duniani, ukamilifu wake ukiwa mbinguni. Lakini kutimiza mapenzi ya Mungu si kazi rahisi kama anavyosema Mtume Paulo; “Maana Ufalme wa Mungu si shauri la kula na kunywa tu, bali unahusika na kuwa na uadilifu, amani na furaha iletwayo na Roho Mtakatifu. Anayemtumikia Kristo namna hiyo, humpendeza Mungu na kukubaliwa na watu” (Rum 14:17). Naye Kristo mwenyewe anasema; “Anayetaka kuwa mfuasi wangu, lazima ajikane mwenyewe abebe msalaba wake na anifuate” (Mt 16:24).

Mfalme Sulemani aliomba hekima ili kuwaongoza watu wake
Mfalme Sulemani aliomba hekima ili kuwaongoza watu wake   (@Vatican Media)

Basi tumwombe Mungu atujalie roho ya hekima, ili tuzitambue siri za ufalme wake, tuziishi vyema ili tuweze kustahilihswa kuufikia uzima wa milele kama anavyosali mama Kanisa katika sala ya kuombea dhambihu akisema hivi; “Ee Bwana, tunakuomba upokee vitu hivi ulivyotukirimia ambavyo tunakutolea. Nayo mafumbo haya matakatifu yatutakase hapa duniani kwa nguvu ya neema yako, na kutufikisha kwenye furaha za milele”. Na katika sala baada ya Komunio anasali: “Ee Bwana, tumepokea sakramenti takatifu iliyo ukumbusho wa siku zote wa mateso ya Mwanao. Tunakuomba sakramenti hii aliyotujalia Mwanao kwa mapendo makuu ituletee wokovu”. Na hili ndilo tumaini letu. Tumsifu Yesu Kristo!

Tafakari D 17 Mwaka A
23 Julai 2026, 16:11