Liturujia ya Neno la Mungu katika Dominika ya 17 ya Mwaka A wa Kanisa inatutafakarisha juu ya, “Gharama na Thamani ya Ufalme wa Mbinguni.” Liturujia ya Neno la Mungu katika Dominika ya 17 ya Mwaka A wa Kanisa inatutafakarisha juu ya, “Gharama na Thamani ya Ufalme wa Mbinguni.”   (©somkak - stock.adobe.com)

Tafakari Dominika 17 Mwaka A wa Kanisa: Gharama na Thamani ya Ufalme wa Mbinguni

Liturujia ya Neno la Mungu Dominika hii inatutafakarisha juu ya, “Gharama na Thamani ya Ufalme wa Mbinguni.” Katika maisha yetu tunajishughulisha kutafuta mambo mengi, ambayo ni ya muda ya kupita tu. Katika hayo yote tunapaswa kwanza kumtafuta Mungu na Ufalme wake. Liturjia ya Neno la Mungu inatualika hivyo kufanya chaguo la makusudi, sahihi na la busara, la kuweka kwanza vipaumbele vya kiroho mbele ya matamanio ya muda mfupi ya ulimwengu huu.

Na Padre Bonaventura Maro, C.PP.S., -Kolleg St. Josef, Salzburg, Austria.

Utangulizi: Wapendwa wanafamilia ya Mungu, ni Dominika ya 17 mwaka A wa Kanisa. Liturujia ya Neno la Mungu katika Dominika hii inatutafakarisha juu ya, “Gharama na Thamani ya Ufalme wa Mbinguni.” Katika maisha yetu ya kila siku, tunajishughulisha kutafuta mambo mengi, ambayo ni ya muda ya kupita tu. Katika hayo yote tunapaswa kwanza kumtafuta Mungu na Ufalme wake usiopita kamwe. Liturjia ya Neno la Mungu inatualika hivyo kufanya chaguo la makusudi, sahihi na la busara, la kuweka kwanza vipaumbele vya kiroho mbele ya matamanio ya muda mfupi ya ulimwengu huu. Tuombe neema na nguvu ya kuutafuta kwanza Ufalme wa Mbinguni, hazina iliyositirika katikati yetu. Somo la 1: Ni kitabu cha kwanza cha 1 Fal 3:5, 7-12. Somo la kwanza kutoka kitabu hiki cha Kwanza cha Wafalme, linatupa habari ya Mfalme Sulemani ambaye kabla ya kuanza kutawala alikwenda kutolea sadaka kwa Mwenyezi Mungu katika madhabahu huko Gibeoni. Katika kutolea sadaka, Mwenyezi Mungu anamtokea na anamwambia “Omba utakalo nikupe”. Sulemani tofauti na matazamio ya wengi, hakujitakia maisha ya siku nyingi; wala hakutaka utajiri kwa nafsi yake; wala hakutaka roho za adui zake. Anasema, “Kwa hiyo nipe mimi mtumishi wako moyo wa kusikia ili niwahukumu watu wako, na kupambanua mema na mabaya.” Sulemani alitambua jambo lenye thamani zaidi ya yote. Anaomba Hekima ya Mungu. Mwenyezi Mungu anakubali ombi lake na akamwongezea fahari, mali na maisha marefu. Anampatia hata na yale ambayo hakuyaomba. Dominika tarehe 26 Julai 2026 Mama Kanisa anaadhimisha Siku ya Sita ya Babu, Bibi na Wazee kwa kunogeshwa na kauli mbiu: "Sitakusahau kamwe." Rej. Isa 49:15. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, hii ni Siku maalum ya kuwakumbuka, kuwashukuru, kuwapongeza na kuwaenzi wazee kwa hekima na upendo wao, mwaliko kwa Kanisa na jamii katika ujumla wake kushikamana kwa dhati na wazee. Mwenyezi mungu anaahidi kwamba, kamwe hamsahau mja wake kwani amechora sura yake kwenye kiganja cha mkono wake.

Maadhimisho ya Siku ya Babu, Bibi na Wazee Duniani kwa mwaka 2026
Maadhimisho ya Siku ya Babu, Bibi na Wazee Duniani kwa mwaka 2026   (ANSA)

Katika somo hili ningependa tutafakari mambo yafuatayo ili yatusaidie kuelewa ujumbe ambao Mama Kanisa anapenda kututafakarisha katika Dominika hii ya 17 A. Fundisho la kwanza: Mwenyezi Mungu anatualika kuchagua daima lile lililo bora zaidi kwa ajli ya Ufalme wa Mbinguni. Tuweke vipaumbele kwa mambo ya Mbinguni. Katika somo hili la kwanza, Mfalme Sulemani alipata nafasi ya kuongea na Mungu alipokwenda kusali huko Gibeoni, na Mungu akampa nafasi ya kumwomba lolote apendalo. Yeye alitambua ni jambo lipi kati ya mengi ambayo angeweza kuomba ambalo alipaswa kuomba kwa wakati ule. Hakujipendelea, hakuomba mali, hakuomba utajiri, hakuomba maisha marefu wala hakuomba maanguko kwa maadui zake. Aliomba Hekima ya Mungu, alitambua bila kuwa na sheria ya Mungu ndani mwake asingeweza kuliongoza vyema taifa hili kubwa la Mungu. Mfalme Sulemani alitambua kuwa hazina ya kweli sio utajiri, vyeo, wala maisha marefu, bali ni moyo wa utii wenye hekima ya kiungu ya kupambanua mema na mabaya.Ndugu mpenda, sisi nasi kila mmoja wetu, kwa nyakati mbalimbali tunapata nafasi ya kusali na kuongea na Mungu. Mwenyezi Mungu anakuja kwetu kwa namna mbalimbali na kwa nyakati mbalimbali hali kadhalika. Katika Dominika hii tujiulize kila mmoja wetu. Tunapopata nafasi ya kusali, kuzungumza na Mungu, tunaomba nini hasa? Nini vipaumbele vyetu vya kwanza? Je, tunaomba atupatie utajiri, vyeo na mali za dunia hii? Tunaomba atupatie ushindi dhidi ya maadui zetu? Huenda nyakati mbalimbali tunaomba hata maanguko kwa wengine. Tunaomba nguvu na uwezo ili wengine watutambue, ili kuwakomoa wengine hasa wale waliotudharau, waliotuumiza, waliotufelisha wakati fulani. Nini kinaanza kwenye sala yangu? Nini vipaumbele vyangu katika sala yangu? Sala yangu imejaa mimi zaidi kuliko wengine? Ndugu mpendwa, pengine hatupati yale tunayoomba kwa Mungu kwa sababu tunashindwa kuomba jambo sahihi kwa Mungu. Sulemani aliomba jambo sahihi na Mungu akampa yote hata na yale ambayo hakumwomba. Tuombe nasi neema ya kutambua yale yaliyo ya muhimu, yatufaayo si tu katika maisha haya bali pia kuupata uzima wa milele, na tusali na kuomba hayo.

Jengeni moyo na utamaduni wa kusikiliza kwa makini
Jengeni moyo na utamaduni wa kusikiliza kwa makini   (@Vatican Media)

Fundisho la pili: Tukikubali kuongozwa na Mungu, tutakua daima na Moyo msikivu, tukiongozwa daima kwa Sheria yake. Je sisi tunapata maongozi na ushauri wetu wapi kwanza?  Mfalme Sulemani alichaguliwa katika kipindi kigumu. Tukumbuke kuwa Baba yake, Mfalme Daudi alikua ni Mfalme mkubwa, aliyeongoza vyema taifa la Mungu. Sulemani anavyojipima anaona kabisa hakuenea katika viatu vya Daudi Baba yake. Alikua ni kijana mdogo bado tena asiye na uzoefu katika nafasi ile kubwa aliyokabidhiwa na Mungu. Anasema, “Na sasa, Ee BWANA, Mungu wangu, umemtawaza mtumishi wako kuwa mfalme badala ya Daudi baba yangu; nami ni mtoto mdogo tu; sijui jinsi ya kutoka wala kuingia”. Hivyo anatambua kwamba watu wake wangeweza kumpotosha na kushindwa kufanya yale yampendezayo Mungu. Anatambua kuwa hisia na matamanio yake vingeweza kumpotosha akashindwa kuwaongoza vyema watu wa Mungu. Akifahamu kuwa mtawala hupotoshwa katika ushauri wa jinsi ya kutenda, alimweka Mungu mbele kama mshauri wake mkuu katika utawala huo. Alikwenda kusali na kuomba na kusikiliza kwanza maongozi ya Mungu. Na tutaona pia wakati alipomwacha Mungu na kushauriwa na watu wa mataifa, ndipo ulikua mwanzo wa anguko lake. Ndugu mpendwa, sisi nasi kila mmoja wetu kimsingi kwa ubatizo ni kiongozi. Katika Ubatizo tunapokea majukumu ya kifalme, kikuhani na kinabii. Lakini wajibu wetu ni kukubali daima na siku zote kuongozwa na Kristo ili tutende yale yampendezayo Mungu na kufanya maamuzi sahihi kadiri ya amri na mapenzi ya Mungu. Katika safari yetu hiyo, mambo hayawi wakati wote rahisi. Zipo changamoto mbalimbali tunazokutana nazo kila mmoja wetu katika safari yake ya maisha kaditi ya wito wake. Kuna nyakati za hofu, tunapotazama uzito wa majukumu yaliyo mbele yetu, familia, watoto, utume wetu, tunaona kabisa viatu hivi ni vikubwa sana kuliko sisi, tunaweza kukata tamaa. Lakini pale tunapoendelea kubaki katika maongozi ya Mungu, tukakubali kuongozwa na sheria yake, basi hapo tunapata nguvu na mwanga wa kuendelea mbele. Ni wazi kwamba nyakati fulani pia wanadamu waweza kutupoteza, wapo watu waweza kutushauri vibaya. Kama kiongozi ni rahisi kupotezwa na hisia na matamanio binafsi, ni rahisi hata kupotezwa na watu wanaotoa ushauri mbaya kwa manufaa yao. Lakini pia, tunapokosa utulivu wa ndani wa kuisikiliza kwanza sauti ya Mungu, sauti nyingi zinazotuita hasa pale tunapokuwa katikati ya kilindi cha matatizo, matatizo na sintofahamu, zaweza mara nyingi kutupotezea lengo. Ni rahisi sana kusikia sauti nyingi, hasa pale tunapotafuta kuelewa mapenzi ya Mungu katika maisha yetu. Katika magonjwa, katika misiba, katika maumivu, katika misukosuko, huja sauti nyingi sana. Tunahitaji utulivu wa ndani kama Mfalme Sulemani ili tusije kupoteza Lulu ya Imani ndani mwetu. Twapaswa daima kusikia Mungu anasema nini nasi kwa namna nyingi na kwa nyakati mbalimbali, katika sala na tafakari, na kwake lipo daima jibu la maswali yetu.

Tujenga na kudumisha moyo wa sala na shukrani
Tujenga na kudumisha moyo wa sala na shukrani   (@Vatican Media)

Fundisho la tatu: Moyo wa sala na shukrani unatufanya tutambue wema na ukuu wa Mungu ndani mwetu. Tunaposali tuwaombee pia na wengine. Mfalme Sulemani mara tu baada ya kuchaguliwa kuwa Mfalme, alikwenda Hekaluni huko Gibeoni kusali na kumtolea Mwenyezi Mungu sadaka ya shukrani. Na huko Mwenyezi Mungu alijifunua kwake. Mfalme Sulemani alitambua kuwa alihitaji sana Hekima ya Mungu kuliko chochote, alihitaji neema na Baraka za Mungu ili vimwongoze katika kuamua kwa haki na hekima. Alitambua kuwa ni Mungu aliyemjalia yale yote, aliyemketisha katika kiti cha ufalme na kwamba ataendela kumwongoza kwa wema na ukarimu wake mkuu. Ndugu mpendwa, Moyo wa sala na shukrani unatufanya tutambue daima hazina ya Mungu anayeishi ndani mwetu. Moyo wa shukrani ndio ufunguo mkuu unaofungua macho yetu ya ndani ili kuiona hiyo hazina iliyositirika. Pasipo shukrani, mwanadamu anakuwa na upofu wa kiroho unaomfanya aukanyage utajiri wa neema ya Mungu uliopo ndani ya maisha yake bila kuutambua. Mwanadamu asiye na shukrani anaishi katika hali ya kulalamika na kutoridhika. Macho yake daima yanatazama yale ambayo hana, mali zaidi, vyeo vikubwa zaidi, au mafanikio ya wengine. Anapohangaika hivi, anashindwa kuona hazina kubwa alizonazo tayari. Shukrani inamfanya mtu atulie na kusema, “Asante Mungu kwa hivi nilivyo, kwa uhai, imani, na familia uliyonipa.” Hapo ndipo anapoanza kugundua kuwa neema ya kuwa mtoto wa Mungu na amani ya moyo ni lulu ya thamani kubwa kuliko vitu vyote anavyohangaikia kuvitafuta. Sulemani hakujiangalia yeye, hakujiombea yeye, alitanguliza wengine kwanza, alifikiria wengine kwanza na Mungu akampatia hata na yale aliyopaswa kuomba kwa ajili yake. Tunapoomba baraka za Mungu kwa ajili yetu, tusisahau kuwaombea wengine. Mara kwa mara sala zetu zaweza kuwa za kibinafsi na kichoyo, tukijiombea sisi wenyewe na kusahau kuwa wapo wengine wengi wanaohitaji msaada wa sala zetu.

Sala ni mawasiliano kati ya mwamini na Muumba wake
Sala ni mawasiliano kati ya mwamini na Muumba wake   (@Vatican Media)

Somo la Injili: Ni Injili kama ilivyoandikwa na Mathayo 13:44-52. Katika Dominika hii ya 17A, tunatafakari sehemu ya mwisho kabisa ya sura hii ya kumi na tatu ya Injili ya Mathayo, ambapo Bwana wetu Yesu Kristo anahitimisha hotuba yake kwa wanafunzi wake juu ya Ufalme wa Mbinguni kwa mifano. Katika dominika hii tunasikia mifano mitatu ya mwisho; Mfano wa Hazina iliyositirika katika shamba, Mfano wa Lulu yenye thamani na Mfano wa Juya (wavu). Mifano hii miwili ya kwanza (hazina na lulu) inasisitiza jinsi ya kuupata na kuuishi Ufalme wa Mungu kwa gharama yoyote, wakati mfano wa tatu (wavu) unasisitiza uwajibikaji na mwisho wetu hapa duniani. Katika dominika hii ningependa tutafakari mafundisho yafuatayo ili yatusaidie kuelewa ujumbe ambao Mama Kanisa amependa kututafakarisha. Fundisho la kwanza: Ufalme wa Mungu ndiyo hazina na yenye thamani kubwa iliyositirika katikati yetu. Ni kwa neema ya Mungu tunaweza kugundua hazina hii. Katika Mfano wa Kwanza, Bwana wetu Yesu Kristo anaufananisha Ufalme wa Mbinguni na hazina iliyositirika katika shamba, ambayo mtu alipoiona, aliificha; na kwa furaha yake akaenda akauza alivyo navyo vyote, akalinunua lile shamba. Wakati wa Yesu, hakukuwa na benki kama ilivyo wakati wa sasa. Nchi ya Israeli ilikuwa ikivamiwa mara kwa mara na majeshi ya kigeni kama Waroma na Waashuru. Hivyo watu wengi walikuwa wakifukia dhahabu, fedha, au vitu vya thamani chini ya ardhi ili visiporwe. Ikitokea mmiliki akafa vitani au uhamishoni, hazina hiyo ilibaki imefichwa hadi mtu mwingine atakapogundua kwa bahati mbaya wakati wa kulima.  Ndugu mpendwa, katika mfano huu wa kwanza, tunaona kwamba yule mkulima hakuwa anatafuta hazina; alikuwa akifanya kazi zake za kawaida za kulima shambani lakini akaikuta ghafula hazina ile ambayo ilisitirika shambani mwake. Hii inamaanisha kuwa neema ya Mungu na wito wake mara nyingi vinatukuta katikati ya maisha yetu ya kawaida kabisa ya kila siku, hata wakati hatujajiandaa. Mtu yule alipotambua thamani ya hazina ile, aliona kila kitu alichokuwa nacho kabla hakina thamani tena kulinganisha na hazina hiyo. Kumbe, mtu anapomjua Yesu kwa dhati, mambo ya kidunia, utajiri, vyeo, na anasa, hayawezi kuchukua nafasi ya kwanza. Ndicho alichofanya Mfalme Sulemani, alitafuta kwanza sheria ya Mungu na kutimiza mapenzi yake, mambo mengine yote akayapata kwa ziada.

Kutafuta na kutimiza mapenzi ya Mungu katika maisha
Kutafuta na kutimiza mapenzi ya Mungu katika maisha   (TANZANIA EPISCOPAL CONFERENCE)

Fundisho la pili: Kila anayegundua Lulu na Hazina ndani mwake hapaswi kusita katika kufanya maamuzi: Utafutaji wa makusudi wa Ufalme wa Mungu. Katika mfano wa pili, Bwana wetu Yesu Kristo anaufananisha Ufalme wa Mbinguni na Lulu yenye thamani. Katika ulimwengu wa kale wa Kiroma, lulu zilikuwa na thamani kubwa kuliko hata dhahabu. Zilikuwa ishara ya utajiri wa hali ya juu na heshima. Wafanyabiashara walisafiri umbali mrefu (hadi Bahari ya Shamu au Bahari ya Hindi) kutafuta lulu safi. Na walipoipata walikwenda na kuuza vyote ili kuinunua lulu hiyo. Tofauti na mfano wa hazina, ambayo mtu anaikuta kwa bahati mbaya, lulu inawakilisha kile ambacho mwanadamu amekuwa akikitafuta kwa makusudi maisha yake yote, ndiyo uzima wa milele. Ndugu mpendwa, Tofauti na yule mkulima aliyepata hazina kwa bahati mbaya, mfanyabiashara wa lulu alikuwa akitafuta kwa makusudi kabisa. Hii inawakilisha watu wanaohangaika kila siku kutafuta ukweli, amani ya moyo, na maana ya kweli ya maisha haya, kupitia sala na tafakari, hadi wanapomgundua Yesu Kristo kuwa ndiye jibu lao la mwisho. Mfanyabiashara alipata lulu moja ya thamani kubwa sana. Hii inamaanisha kuwa Yesu Kristo na injili yake ndio ukweli mkuu wa kipekee unaotosheleza kiu yote ya mwanadamu. Ukishampata yeye, unatambua kuwa hakuna falsafa, utajiri, wala cheo chochote cha ulimwengu huu kinachoweza kulinganishwa naye. Ukweli huu ndio alioutafuta Mtakatifu Agustino kwa muda mrefu, na alipompata Kristo, Roho yake ikapata pumziko la kweli. Nini kinanichelewesha kumtafuta Kristo na Ufalme wake? 

Hakuna chochote kile kinachoweza kulinganishwa na Ufalme wa Mbinguni
Hakuna chochote kile kinachoweza kulinganishwa na Ufalme wa Mbinguni

Fundisho la Tatu: Ufuasi wetu kwa Kristo unatudai kulipa gharama, kuwa tayari kuacha yote na kuitafuta hazina ya kweli. Katika mifano yote miwili, mfano wa hazina na lulu inayojulikana kama mifano pacha, yule mkulima na yule mfanyabiashara walilazimika kuuza vyote walivyokuwa navyo ili wapate hazina ya kweli. Mkulima na mfanyabiashara waliondoa kila kitu walichomiliki ili wapate nafasi ya kumiliki hazina mpya. Ndugu mpendwa, Kristo anatualika kuachilia yale mambo yote ya ndani ya nafsi zetu yanayomzuia Kristo kutawala. Anatualika kuacha Ubinafsi na Kiburi, kutanguliza Mapenzi ya Mungu na mahitaji ya wengine kabla ya matamanio yetu binafsi. Anatualika Kuachilia vinyongo na kutosamehe. Moyo uliojaa kinyongo hauna nafasi ya kuhifadhi hazina ya neema ya Mungu. Kusamehe ni kuuza haki yako ya kulipa kisasi ili upate amani ya Kristo. Wakati mwingine, kushikilia lulu ya imani kutakugharimu uhusiano wako na ulimwengu. Ili kuilinda hazina hii, unapaswa kuwa tayari kuacha mambo yanayotupa faida ya nje. Katika kazi au biashara zako, unaweza kukutana na fursa za kupata pesa nyingi kwa njia zisizo halali au za dhuluma. Kuuza vyote hapa ni kukataa fedha hizo chafu ili ubaki na lulu ya unyoofu na dhamiri safi mbele ya Mungu. Ni kuwa tayari kuacha makundi au marafiki wanaokuvuta kwenye ulevi, uasherati, au maisha ya anasa yanayokutenganisha na Kanisa na yanayokuzuia kupiga hatua za kimaendeleo. Kununua shamba au lulu kulihitaji hatua za haraka na nguvu. Huwezi kuipata hazina iliyositirika ukiwa mkristo “goigoi,” anayeahirisha mambo kwa kuwa kesho ipo, kwa kuwa nina afya njema sasa, kwa kuwa nina mali, kwa kuwa nina vyeo. Ni kukubali kujinyima, na kufanya kila mara jitihada za haraka kwa ajili ya kumtafuta Mungu, kwa kuwa muda ni mfupi sana. Nafasi ni sasa, muda wa wokovu ni leo.

Kuna Gharama na Thamani katika Ufalme wa Mbinguni
Kuna Gharama na Thamani katika Ufalme wa Mbinguni   (AMECEA)

Fundisho la nne: Ufalme wa Mungu unawakaribisha watu wote bila ubaguzi, lakini uamuzi wa kuingia na kuishi ndani yake bado ni uchaguzi binafsi. Katika mfano wa mwisho, Bwana wetu Yesu Kristo anaufananisha Ufalme wa Mbinguni na Juya au wavu uliotupwa baharini, nao ukakusanya samaki wa kila namna. Hata lilipojaa, walilivuta pwani; wakaketi, wakakusanya walio wema vyomboni, bali walio wabaya waliwatupa. Ndugu mpendwa, Mfano huu unaeleza uhalisia wa Ufalme wa Mungu. Wavu uliotupwa baharini ndiyo ujumbe wa Injili, uliohubiriwa na Kristo na wanafunzi wake na hata sasa unahubiriwa na Kanisa kwa ulimwengu wote, bila ubaguzi, kwa watu wa kila kabila, lugha, jamaa na taifa, kwa wema na waovu hali kadhalika. Wavu ukiwa ndani ya maji unakusanya samaki wazuri na wabaya kwa pamoja, na wote wanabaki humo ndani hadi wavu utakapovutwa pwani, ambapo wavuvi waliketi na kutenga samaki wema na kuwatupa wale wabaya. Kumbe, katika jamii na Kanisa, kama ilivyokuwa kwa mfano wa magugu na ngano, wapo watu wema na watu wabaya na wote wanaishi na kuchanganyika pamoja hadi mwisho wa nyakati. Ni wazi kwamba ipo hukumu mwisho wa maisha yetu ya hapa duniani nayo itaamua hatima ya maisha yetu yajayo. Lakini bado nafasi tunayo kila mmoja kujitafakari wakati bado tunaishi. Je mimi ni samaki wa namna gani ndani ya wavu? Haitoshi tu kuwa ndani ya Kanisa, haitoshi tu kuitwa Mkristo, bali nina wajibu wa kuwa samaki bora, ili nistahilishwe kuingia mbinguni. Muda bado tunao wa kubadilika, na Mungu hatuhukumu mara moja, hatutupi mara kwenye tanuru ya moto. Anatupa neema yake ili tutambue wajibu, gharama na thamani ya kuutafuta uziama wa milele.

Wakristo wanahimizwa kumfungulia Mungu hazina ya moyo wao
Wakristo wanahimizwa kumfungulia Mungu hazina ya moyo wao

Fundisho la tano: Wajibu wetu sisi wafuasi wa Kristo ni kutoa nasi katika hazina ya mioyo yetu, Mafundisho ya Kristo na Ufalme wake, yeye ambaye kwake upo utimilifu wa yale ya Kale. Kristo anahitimisha sehemu hii ya hotuba yake kwa kuuliza swali, “Mmefahamu yote hayo?” Wakamwambia, Naam. Akawaambia, “Kwa sababu hiyo kila mwandishi mwenye elimu ya Ufalme wa Mbinguni amefanana na mtu mwenye nyumba, atoaye katika hazina yake vitu vipya na vya kale”. Kristo anamfananisha Mwandishi mweye elimu ya Ufalme wa Mbinguni na mtu atoaye katika hazina yake vitu vipya na vya kale. Vitu vya kale vilimaanisha mafundisho ya Agano la Kale na vitu vipya vilimaanisha utimilifu wa mafundisho na Ahadi za Agano la Kale katika Agano jipya, kwa njia ya maisha na utume Bwana wetu Yesu Kristo. Kumbe mfuasi mwaminifu wa Kristo, hakupaswa kuyadharau mafundisho ya Agano la Kale kwa kuyashika yale ya Kristo, wala kuyakataa ya Kristo na kuyashika yale ya Torati na Manabii. Bali mtumishi mwaminifu, anayashika yale ya Kristo, akiona utimilifu wa Torati na Ahadi za Agano la kale ndani yake. Ndugu mpendwa mfano huu wa Kristo unahitimisha hotuba yake juu ya Ufalme wa Mbinguni akitukumbusha nasi sote kama wanafunzi wake wajibu wetu wa kuwa na mzani sahihi katika maisha, si tu ya kiroho bali hata maisha yetu ya kawaida ya kila siku. Kristo anatualika kuwa daima tayari kujifunza kila siku ili kuijaza ghala yetu kwa hazina mpya, yaani mioyo yetu, kwa Neno lake, kwa fadhila za Kimungu, kwa mafundisho ya Kanisa, ili nasi kutoka katika hazina hiyo tuweze kuwasaidia na wengine. Hatuwezi kutoa katika hazina yetu kila ambacho sisi wenyewe hatuna. Hatuwezi kuwasaidia wengine wakainuka kiimani kama sisi tumelala na kurudi nyuma. Hatuwezi kuwasaidia wengine kutambua na kuutafuta uzima wa milele kama sisi hatuna mwamko huo. Hali kadhalika, tunaishi katika ulimwengu uliosheheni mambo mengi mapya na ya kisasa, ambayo yaweza kupingana moja kwa moja na Ujumbe wa Injili ya Kristo. Ipo hatari kubwa ya kumezwa na mafundisho mengi ya kisasa, na kusahau ilipo hazina yetu ya kweli, yaani katika Injili ya Kristo. Lakini pia yapo mambo mengi, mbinu mpya za kisasa zinazoweza kusaidia Kristo akajulikana na kupendwa, Injili ikaenea kwa kasi na watu wengi wakamjua Mungu. Kumbe Kristo anatualika tuwe na mzani sahihi katika maisha, ili sote tuweze kufahamu na kuitafuta hazina iliyo ya thamani zaidi katika maisha yetu yaani uzima wa milele.

Waamini wanahimizwa kutafuta hazina ya Ufalme wa Mbinguni
Waamini wanahimizwa kutafuta hazina ya Ufalme wa Mbinguni   (TANZANIA EPISCOPAL CONFERENCE)

Somo la Pili: Ni waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi 8:28-30. Katika somo la Pili, mtume Paulo anatukumbusha kuwa kila mmoja wetu ameumbwa kwa mpango. Yawezekana mtu akakataa mpango wa Mwenyezi Mungu lakini mpango huo ni wa milele, upo katika umilele wa Mungu. Mpango huo wa Mungu ndiyo wokovu wetu ambao tumeupata kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo. Kumbe kila mmoja wetu anaitwa na kwa neema ya Mungu anashirikishwa mpango huu wa Mungu wa ukombozi. Wanaoitwa na Mungu wanapaswa kuiishi Injili ya Kristo ambayo daima inafanya mabadiliko ndani yao, wamepokea ubatizo na sakramenti nyingine ili ziwape nguvu na uhai kiroho. Kwa hivyo Mungu hawezi kutukomboa pasipo sisi kushiriki. Alituumba pasipo sisi lakini hatatukomboa pasipo kila mmoja kufanya uchaguzi na kuona thamani ya ukombozi huu iliyo ndani ya Kristo Yesu, na kuitafuta kwa moyo wote. Hitimisho: Tuombe neema na nguvu ya kumtafuta Mungu, kuishi na Mungu na kufa tukiwa tumeungana na Mungu, yeye aliye hazina ya kweli iliyositirika katikati yetu, ili tuupate uzima wa milele.

Tafakari D 17 Mwaka A
24 Julai 2026, 15:43