Ujumbe mkuu umejikita katika ukuu wa huruma ya Mungu na uvumilivu wake kwetu sisi wanae. Kwamba Mungu Baba yetu anatupenda sana. Ujumbe mkuu umejikita katika ukuu wa huruma ya Mungu na uvumilivu wake kwetu sisi wanae. Kwamba Mungu Baba yetu anatupenda sana.  

Tafakari Dominika 16 ya Mwaka A wa Kanisa: Ukuu Na Uvumilivu wa Huruma ya Mungu

Ujumbe mkuu umejikita katika ukuu wa huruma ya Mungu na uvumilivu wake kwetu sisi wanae. Kwamba Mungu Baba yetu anatupenda sana. Hivyo kwa udhaifu wetu tunapotenda dhambi hatuhukumu na kutuadhibu mara moja kwa haraka, bali anatuongoza kwa upendo katika kweli, akitupata nafasi ya kuongoka na kufanya toba, ili tuishi maisha mema na maadilifu. Huu ni mwaliko kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanatumia ukuu na uvumilivu wa Mungu kutubu!

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, Dominika ya 16 ya Mwaka A wa kiliturujia katika Kanisa, kipindi cha kawaida. Ujumbe mkuu umejikita katika ukuu wa huruma ya Mungu na uvumilivu wake kwetu sisi wanae. Kwamba Mungu Baba yetu anatupenda sana. Hivyo kwa udhaifu wetu tunapotenda dhambi hatuhukumu na kutuadhibu mara moja kwa haraka, bali anatuongoza kwa upendo katika kweli, akitupata nafasi ya kuongoka na kufanya toba, ili tuishi maisha mema na maadilifu. Ni katika muktadha huu Zaburi ya wimbo wa mwanzo inasema hivi; “Tazama, Mungu ndiye anayenisaidia; Bwana ndiye anayenitegemeza nafsi yangu. Kwa ukunjufu wa moyo nitakutolea dhabihu; ee Bwana, nitalishukuru jina lako, maana ni jema” (Zab. 54:4, 6). Na mama Kanisa katika sala ya mwanzo anasali hivi; “Ee Bwana, uwarehemu watumishi wako, uwazidishie kwa wema baraka za neema yako. Hivyo waendelee kuzishika daima amri zako kwa moyo wa matumaini, imani na mapendo.”

Waamini Jengeni Utamaduni wa kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani
Waamini Jengeni Utamaduni wa kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Somo la Kwanza ni Kitabu cha Hekima ya Sulemani (Hek 12:13, 16-19). Ujumbe wake mkuu umejikita katika huruma na uvumilivu wa Mungu kwa wenye dhambi na wakosefu. Licha ya kuwa anauwezo wa kutuadhibu wakati na mda wowote tunapotenda dhambi na kukengeuka, lakini kwa hekima na huruma yake, anatuacha tuendelee kuishi, akitupatia nafasi ya kubadilika, kutubu, kumrudia Yeye na kuomba msamaha. Maneno ya Sulemani tunayasoma hivi; “Walakini, desturi yako unauzuia, hata uwezo wako, na kuhukumu kwa upole, na kututawala kwa uvumilivu mwingi…uwezo unao, na wakati wote utakapo unaweza kuutumia…Lakini endapo watu wametenda dhambi unawajalia toba.” Hivyo neno la mwisho la Mungu kwetu sisi wanawe ni hili: Nimekusamehe mwanangu, nenda na amani, usitende dhambi tena. Hulka hii ya Mungu ilimfanya mzaburi atafakari na kuandika maneno haya ya wimbo wa katikati akisema; “Kwa maana Wewe, Bwana, u mwema, umekuwa tayari kusamehe, na mwingi wa fadhili, kwa watu wote wakuitao. Ee Bwana, uyasikie maombi yangu, uisikilize sauti ya dua zangu. Mataifa yote uliowafanya watakuja; watakusujudia Wewe, Bwana, watalitukuza jina lako; kwa kuwa ndiwe uliye mkuu. Wewe ndiwe mfanya miujiza, ndiwe Mungu peke yako. Lakini Wewe, Bwana, U Mungu wa rehema na neema, mvumilivu, mwingi wa fadhili na kweli. Unielekee na kunifadhili mimi mkosefu” (Zab. 86: 5-6, 9-10, 15-16). Lakini licha ya kuwa huruma ya Mungu ni ya milele, haina mipaka, na Mungu ni mvumilivu kiasi hicho. Lakini huruma hii ni kwa wale wanaotubu makosa yao na kuziacha njia zao mbaya. Kwa wanaokaza shingo zao na kubaki katika maovu yao, uvumilivu wa Mungu unafikia kikomo chake kwa kifo chao, na mwisho wao ni kuangamia katika moto wa milele.

Jitahidini kuijongea Mahakama ya Huruma ya Mungu
Jitahidini kuijongea Mahakama ya Huruma ya Mungu   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Somo la Pili ni la Waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi (Rum. 8:26-27). Ujumbe wake ni kuwa hali yetu binadamu ni dhaifu, hali kadhalika na sala zetu. Lakini Roho wa Mungu aliye ndani yetu, anazifanya sala zetu zipate mastahili na kusikilizwa na Mungu. Hapa msisitizo ni kuwa Mungu kwa upendo wake ametujalia Roho wake awe msaada kwetu. Tunasoma hivi: “Roho hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo; lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa. Na Yeye aichunguzaye mioyo, aijua nia ya Roho ilivyo, kwa kuwa huwaombea watakatifu kama apendavyo Mungu”. Hii ndio sababu ya Mungu kutuvumilia tukitenda dhambi, akisubiri neema na baraka za Roho Mtakatifu zifanye kazi ndani mwetu, ili tuweze kuongoka na kumrudia Yeye na kuishi kitakatifu. Injili ni ilivyoandikwa na Mathayo (Mt. 13:24-43). Ujumbe wake umejikita katika kukua na kuenea kwa ufalme wa Mungu, na uvumilivu na huruma ya Mungu kwa wakosefu. Ujumbe huu unaelezwa kwa mifano mitatu: mfano wa punje ya haradali, mfano wa chachu na mfano wa ngano na magugu kuachwa ili vikue pamoja mpaka mda wa mavuno. Huruma hii ya Mungu inafumbatwa katika uvumilivu wake na imani kuwa mwanadamu mdhambi anaweza kubadilika na kumrudia Yeye. Kumbe mwovu kunawiri si kwa sababu Mungu haoni uovu wake, bali ni huruma na uvumilivu wake Mungu ndivyo vinayompa mdhambi nafasi ya kutubu na kubadilika. Ni vyema kutumia vizuri muda tunaopewa na Mungu, tujipatanishe naye mapema, tusingoje hata siku ya mwisho, siku ya hukumu. Kila mara tuikimbilie Sakramenti ya Kitubio ambayo kwayo Mungu anapitishia huruma yake kwetu sisi wadhambi. Mfano wa magugu umebeba mafundisho mengi. Kwanza kabisa unatufundisha kuwa kwa njia ya uumbaji Mungu amepanda ndani ya kila nafsi ya mtu kila lililojema kwa maisha yake. Adui Shetani ndiye anayefanya kazi ya kupanda magugu ndani ya nafsi zetu. Hivyo kila mmoja ana wajibu wa kujilinda na yule mwovu asije kupanda ndani mwake uovu wake. Wazazi wana wajibu wa kuwalinda na kuwaelekeza vyema watoto wao ili asiwepo yeyote wa kupanda magugu ndani ya nafsi zao. Tukumbuke kuwa mtoto asipokuwa na msingi nzuri wa maadili toka nyumbani, ni rahisi kwa yule mwovu kupanda yaliyo mabaya ndani mwake.

Mwenyezi Mungu anatoa muda wa toba na wongofu wa ndani
Mwenyezi Mungu anatoa muda wa toba na wongofu wa ndani   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Pili, unatuasa kuacha tabia ya kuwahukumu wengine, na kuwawekea alama ya huyu mwema na huyu ni mbaya. Hukumu ni ya Mungu peke yake anayejua siri ya mioyo ya watu kama anavyosema Mtume Paulo : “Basi msihukumu…acheni mpaka Bwana atakapokuja. Yeye atayafichua mambo ya giza yalofichika, na kuonesha wazi nia za mioyo ya watu” (1Kor. 4:5). Tatu, unatuasa pia tusiwe wabaguzi kwa watu wasio na uwezo. Watumishi walitaka kung’oa magugu ili ngano ikue vizuri. Utamaduni wa kifo umeanza kwa dhambi ya ubaguzi kwa kuwanyanyasa, kuwatenga na pengine kuwatokomeza kabisa kwa kukatisha maisha ya wasiojiweza na wanyonge kama walemavu, vikongwe, wagonjwa mahututi au hata ambao bado hawajauona mwanga wa jua, wasio na hatia wala uwezo wa kujitetea, ili mradi tu walio wazima waishi vizuri. Viacheni vyote vikuwe hata wakati wa mavuno. “Hapo ndipo mtakapotambua tena tofauti iliyopo kati ya waadilifu na waovu : naam, kati ya mtu anayemtumikia Mungu na asiyemtumikia” (Mal 3:18). Basi tumwombe Mungu Roho Mtakatifu atujalie neema na baraka zake tuweze kutumia vyema uvumilivu wa Mungu kutuacha tuendelee kuishi akitupata muda wa kutubu, atujalie moyo wa toba na kubadilika ili hukumu ya mwisho itukute tukiwa ngano bora na hivyo, tukusanywe katika ufalme wa mbinguni. Kwa nguvu zetu wenyewe hatuwezi chochote. Daima tuwe watu wa sala tukiomba msaada wa Mungu Baba yetu hasa kwa Sadaka ya Misa Takatifu kama anavyosali Mama Kanisa katika sala ya kuombea dhabihu akisema hivi : “Ee Mungu, ulihalalisha kafara mbalimbali za zamani katika Sadaka hii moja iliyo kamili. Uipokee Sadaka hii tunayokutolea sisi watumishi wako amini. Uibariki kama ulivyoibariki ile sadaka ya Abel, ili kitu alichokutolea kila mmoja wetu kwa kuuheshimu utukufu wako, kitufae sote kwa wokovu. Na katika sala baada ya komunyo anahitimisha akisali hivi : “Ee Bwana, tunakuomba uwe na sisi taifa lako. Na kama ulivyotujalia mafumbo haya ya mbinguni, utuondoe katika maisha ya zamani na kutuweka katika maisha mapya.” Na hili ndilo tumaini letu, Tumsifu Yesu Kristo!

Tafakari D16 Mwaka A
17 Julai 2026, 17:31