Tafakari Dominika 14 ya Mwaka A wa Kanisa: Mungu Ni Faraja na Kitulizo cha Kweli
Na Padre Bonaventura Maro, C.PP.S., -Kolleg St. Josef, Salzburg, Austria.
Utangulizi: Wapendwa wanafamilia ya Mungu, ni Dominika ya 14 ya Mwaka A wa Kanisa. Hija ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Leo XIV Kisiwani Lampedusa inalenga kuikumbusha Jumuiya ya Kimataifa kwamba, changamoto ya wakimbizi na wahamiaji duniani inapaswa kushughulikiwa katika msingi wa upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu; kwa kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za wakimbizi na wahamiaji. Kisiwa cha Lampedusa ni mahali pa huzuni na masikitiko makubwa, lakini pia ni mahali bandari ya matumaini kwa watu waliopondeka na kuvunjika moyo. Baba Mtakatifu Leo XIV amefanya hija hii ya kichungaji akifuata nyayo za Mtangulizi wake Papa Francisko ambaye alitembelea Kisiwani hapa tarehe 8 Julai 2013 mara tu baada ya kuchaguliwa kwake kuliongoza Kanisa Katoliki. Injili ya Msamaria Mwema inaonesha kwamba, mshikamano, upendo na udugu wa kibinadamu ni njia ya uzima wa milele na inayowaokoa wale ambao wameangukia kati ya wanyang’anyi. Huu ni mwaliko kwa watu wa Mungu kujenga kwanza ujirani mwema, kwa kuwaonea huruma wale wanaoteseka pamoja na kujitahidi kuwahudumia kwa hali na mali. Katika maisha yetu ya kila siku tunakutana na mitihani, changamoto, Misalaba na mizigo mizito inayotuelemea. Yaweza kuwa magonjwa ya muda mrefu, hali ngumu za kiuchumi, msongo wa mawazo, matatizo ya kifamilia, misiba, kushindwa na mengine mengi. Katika hayo yote, tunatamani pumziko. Dominika ya leo inatupa nafasi ya kutafakari, Je, kimbilio letu ni wapi? Kimbilio langu ni wapi? Ni wapi tunapata faraja na kitulizo cha kweli? Ni wapi tunapata pumziko la kweli? Ni kwa Mungu peke yake. Kristo Masiha, Mungu pamoja nasi, yupo katikati yetu, anatualika, “Twende kwake, tupate pumziko la kweli.” Katika Dominika hii tumshukuru Mungu ambaye kwa njia ya Mwanaye Mpenzi Yesu Kristo, ametupatia na anatuahidi sisi sote pumziko la kweli. Tuombe neema ya kuwa wanyenyekevu na wapole ili tumtambue Kristo Yesu mkombozi aliye katikati yetu.
Somo la 1: Ni kitabu cha Nabii Zekaria 9:9-10. Somo la kwanza ni kutoka katika Kitabu cha Nabii Zekaria, 9:9-10. Nabii Zekaria katika somo la kwanza anatoa unabii wa kimasiya. Nabii Zekaria alitokea kipindi ambacho taifa la Yuda lilikwishatoka utumwani Babeli na kurudi katika nchi yao na kuanza kujijenga tena upya kama taifa, walilijenga upya hekalu la Yerusalemu na wakayajenga tena upya matumaini yao kwa Mungu. Ni kipindi ambacho pia taifa la Yuda halikuwa na mfalme, na hivyo, nguvu yao, matumaini yao na kitovu cha umoja na ustawi kilikua ni hekalu na katika matumaini kwamba siku zinakuja ambapo Mwenyezi Mungu atamwinua Masiya atakayewaongoza na kuwaunganisha tena kama taifa. Unabii wa Nabii Zekaria katika somo hili la kwanza ni kuwa Masiha huyo atakayekuja atakuwa ni mfalme mwenye haki, mnyenyekevu na atawapatia wokovu. Kama alama ya unyenyekevu mkubwa wa Masiha, tofauti na wafalme wengine, atapanda punda badala ya farasi ikiwa ni ishara ya amani, ishara ya unyenyekevu. Uamuzi wake wa kupanda punda unaashiria pia kuwa masiya hatakuwa mfalme mwenye kuongoza kwa nguvu za kivita bali atakua ni mwenye kuongoza kwa upole, amani na kwa unyenyekevu mkubwa. Somo hili linatukumbusha jinsi matumaini ya masiya yalivyosaidia kuhifadhi imani ya taifa la Israeli hata walipokuwa katika nyakati ngumu za maisha yao. Nabii anatoa picha ya Mungu anayekuja na kukaa kati ya watu wake, Si Mfalme anayetisha, si Mfalme wa vita bali mfalme atakayeingia katika hali za kawaida kabisa za maisha ya watu, katika upole, katika upendo, amani na unyenyekevu mkubwa. Mfalme huyu ndiye Kristo na utabiri huu unatimia pale masiya anapoingia Yerusalemu siku ya Dominika ya Matawi.
Somo la Injili: Ni Injili ya Mathayo 11:25-30: Tukisoma sehemu iliyotangulia Injili ya leo yaani sura ya 11:20-24, Yesu anailaani miji ya Korazini, Bethsaida na Capernaumu kwa kuwa alihubiri huko, alifanya huko mujiza mingi lakini wengi watu wengi wa miji hii hawakumkiri kama Mwana wa Mungu, na wala hawakuguswa na miujiza ile. Walishindwa kumtambua Mwenyezi Mungu aliyekuwa akitenda kazi katika nafsi ya Kristo. Walikosa unyenyekevu. Kristo anaanza katika aya ya 25 kwa kumshukuru na kumtukuza Mungu, anamtambua na kumkiri Mungu kama Muumba wa Mbingu na nchi ambaye amewaficha siri za Ufalme wa Mbinguni wenye hekima na akili na akawafunulia watoto wachanga. Wenye hekima na akili ni akina nani? Hawa walikua ni Mafarisayo na Waandishi ambao hawakua tayari kumpokea wala kujifunza kutoka kwa Kristo. Walifikiri walimjua vyema Mungu kwa sababu walikua walimu wa sheria na wataalamu wa maandiko, na wakasahau namna ambavyo Masiya Mwana wa Mungu angetokea kati ya watu wake. Na Watoto wachanga ni akina nani? Katika utamaduni wa kufundisha wa Wayahudi, wale waliokua wanafundisha waliitwa “Baba”, Rabi au Waalimu. Na yeyote aliyekua mwanafunzi alikua ni mtoto kwa Baba/Rabi/Mwalimu. Hivyo ilimpasa mtoto kwa maana ya mwanafunzi kuwa mnyenyekevu na mtii, kukaa miguuni kwa Baba au Rabi au Mwalimu kwa muda wa kutosha ili aweze kumwelewa na kuelewa yote aliyofundishwa. Kristo anavyowasifu watoto wachanga, anawasifu wale wote ambao kwa unyenyekevu, wapo tayari kumpokea, kumsikiliza yeye na kuweza kuelewa siri za Ufalme wa Mbinguni, tofauti na mafarisayo na waandishi ambao walikataa kumsikiliza Yesu. Kristo Yesu anaendelea kusema, “Njooni kwangu msumbukao na wenye kuelemewa na mizigo nami nitawapumzisha”: Kristo anawaalika wote ambao wanasumbuka na kuelemewa na mizigo.
Mizigo anayoiongelea Kristo ni sheria nyingi walizoziweka Mafarisayo na waalimu wa sheria, sheria takribani 613 ambazo kila Myahudi alipaswa kuzifuata. Kristo anafundisha amri moja kuu, Amri ya Mapendo, ambayo inazibeba amri hizi nyingine zote. Ni amri ya upendo inayoongozwa na upole na unyenyekevu, yeye mwenyewe akiwa ndiye kielelezo kama tulivyosikia katika utabiri wa Nabii Zekaria. Hivyo, Kristo anaahidi kutoa pumziko kwa wote ambao wapo tayari kuongozwa naye, walio tayari kujivika nira yake na kujifunza kutoka kwake. Ni kukubali daima kutembea pamoja naye, huku tukiongozwa na Amri yake, amri nyepesi ya Upendo. Kama vile nira inavyowafunga wanyama wawili, nasi tunafungwa pamoja na Kristo, tukimruhusu sasa achukue mizigo yetu, na aende pamoja nasi, nguvu zake zikifidia udhaifu wetu wa kibinadamu. Yeye anachukua sehemu kubwa ya uzito wa mizigo yetu. Nabii Isaya anasema, "Hakika ameyachukua masikitiko yetu magonjwa yetu na udhaifu wetu, amejitwika huzuni zetu...” Isa 54:3. Ili tufaidi pumziko hili la kweli kutoka kwa Kristo hatuna budi kuwa wanyenyekevu kama Kristo mwenyewe, aliye mpole na mnyenyekevu wa moyo. Kwa maneno hayo, Yesu anakamilisha utabiri wa nabii Zekaria na ni kama anawatangazia watu kwamba yule masiya mliyekuwa mnamngoja sasa amefika na yupo kati yenu. Kristo ni mpole na mnyenyekevu wa Moyo naye anatuongoza kwa upole katika safari yetu kwenda kwa baba yetu wa Mbinguni.
Somo la Pili: Ni kutoka katika Waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi 8:9, 11-12. Somo la pili ni kutoka katika Waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi 8:9, 11-12. Katika somo hili, Mtume Paulo anazungumzia nafasi ya Roho Mtakatifu kwa wale waliompokea Kristo yaani kwa waliobatizwa. Wale ambao wamekwishampokea Kristo; Hawapo tena chini ya utawala wa mwili kwa sababu roho wa Mungu anakaa ndani yao. Matendo haya ya mwili ni vilema mbalimbali vinavyotupelekea kuanguka katika dhambi, na kutufanya kushindwa kumtambua Kristo aishiye ndani mwetu, kama vile majivuno, ubahili, uchavu, wivu, ulafi n.k. Licha ya hayo, bado lipo tumaini daima ndani mwetu. Roho huyu aishiye ndani mwetu ana nguvu ya kuleta mabadiliko ya ndani, ana uwezo wa kuibadili miili yetu ambayo ipo katika hali ya kufa kwa sababu ya dhambi na kuihuisha tena, kwa sababu ni roho huyu huyu aliyemfufua Kristo kutoka wafu. Mtume Paulo anaelewa fika udhaifu ubinadamu na maelekeo ya mwili. Anachowaandikia warumi katika somo hili ni kuwatia moyo wasiuangalie tu udhaifu wa mwili wala maelekeo yake bali wamkazie macho Roho wa Mungu aliye ndani yao ili wasiendelee kutawaliwa na matendo ya mwili bali yale ya Roho.
Ndugu wapendwa, kutokana na masomo yetu yote ya leo tunapata mafundisho yafuatayo. Jambo la kwanza: Mwenyezi Mungu anatukumbuka katika shida, katika huzuni na mahangaiko yetu. Nabii Zekaria anaitwa na Mungu kutabiri juu ya ujio wa Masiha ambaye atawaletea ukombozi taifa la Israeli lilokuwa limetawanyika. Zacharia maana yake “Mwenyezi Mungu anatukumbuka” mwenyezi Mungu aliwakumbuka watu wake waliokuwa utumwani kwa muda mrefu, waliokuwa wamebea mizigo mizito ya maumivu ya utumwa, walipoteza ardhi yao, wakapoteza hekalu lao, wakatawanyika makabila yote. Mungu anawaahidia tena Masiha, mfalme ambaye anawakusanya tena na kuwaleta kuwa taifa moja kama mwanzo. Mara kadhaa tunaweza kupita katika mitihani mingi hata tukafikiri Mwenyezi Mungu ametuacha. Mwenyezi Mungu katika nyakati zote hizi hatuachi, anakwenda nasi. Anatukumbuka na daima anabaki mwaminifu kwa ahadi zake hata kama zinachelewa. Ahadi hii ya Masiya inatimia miaka 600 baadaye ndipo anazaliwa Yesu Masiya. Twapaswa kusubiria utimilifu wa Ahadi za Mungu kwa unyenyekevu, upole na ustahimilivu. Mwenyezi Mugu anakumbuka ndoto zetu ambazo zinaonekana wakati fulani kufifia, anakumbuka mipango yetu ambayo nyakati fulani inaonekana isiyo na matumaini tena, anakumbuka hali zetu mbalimbali, pengine ni magonjwa ya muda mrefu, changamoto za familia za muda mrefu, migogoro katika ndoa, Mungu, anakukumbuka.
Jambo la pili: Tuyavue na kuyakatilia mbali mambo yote yanayotuzuia kumtambua Kristo, Mungu aliye katikati yetu. Mafarisayo na Waandishi walishindwa kumtambua Kristo kama Masiya, walishindwa kutambua nguvu ya Mungu inayotenda kazi ndani ya Kristo na hivi wakashindwa kumtambua kama Masiya aliyetabiriwa na manabii. Kumbe ili kumtambua Kristo Masiha, Mungu aliye katikati yetu, Mungu anayetukumbuka na kutuonea huruma, twapaswa kuandaa mazingira ya kumtambua katikati yetu. Sisi tunaweza kufungwa na mambo mengi yakatuzuia kumtambua Kristo anaposema nasi. Kiburi cha uhai, akili, mali, vyeo, umaarufu, elimu, madaraka heshima juu ya mambo ya kidunia nk. Kristo anakuja kwangu, anakuja kwako kwa namna ya kawaida kabisa, anajifunua kwetu kupitia watu wa kawaida kabisa ambao pengine hatuwezi hata kufikiria. Tunahitaji fadhila ya upole na unyenyekevu wa moyo ili kumtambua Kristo. Tunaalikwa pia kuyapokea kwa unyenyekevu mafundisho ya Kanisa kama mamlaka fundishi aliyoiacha Kristo Mwenyewe na hivi tutaweza kumtambua Kristo kwa njia ya Neno lake na mafundisho yake matakatifu. Tumpokee kwa upole na unyenyekevu katika Ekaristi Takatifu, ili akae daima ndani ya mioyo yetu. Tumwendee katika sala na Tafakari binafsi tukimpelekea mizigo yetu, yeye aliye makimbilio na nguvu yetu. Tutambue na kukiri udogo na udhaifu wetu mbele za Mungu na kwamba bila yeye sisi hatuwezi jambo lolote.
Jambo la Tatu: Sifa za Masiya zinatufundisha namna njema ya kuongoza taifa la Mungu kwa wale wote wenye mamlaka na utawala. Nasi sote tusiwe chanzo au sababu ya mizigo mizigo kwetu wenyewe na kwa wengine. Nabii Zekaria anatoa sifa za Masiya tofauti na wafalme na watawala wengine wote wa kidunia. Masiya atatawala kwa upole, hekima na unyenyekevu kinyume na watawala na wafalme wa kidunia walioongoza kwa mabavu na kwa vita. Dominika hii ni mwaliko kwa viongozi wote, wa kanisa na serikali kuongoza taifa la Mungu kwa upole na unyenyekevu kwa mfano wa kristo mwenyewe Mchungaji wetu Mwema. Kristo anatabiriwa kuwa atawaongoza watu kwa amani, atakuwa sio mfalme wala masiya atakayetumia nguvu za kivita, dhuluma na mabavu bali hekima ya Mungu itakua juu yake. Tuwaombee viongozi wetu ili waweze daima kuongozwa na Roho Mtakatifu na Hekima ya Kimungu katika yote wanayotenda au wanayopaswa kuamua kwa niaba ya taifa lote la Mungu. Mara kadhaa badala ya kuwasadia watu kupunguza uzito wa mizigo yao, twaweza kwa maneno, mawazo, matendo na kutokutimiza wajibu kuwa chanzo cha mizigo mizito kwa wengine kuanzia ngazi ya familia, jumuiya zetu, kanisa na taifa. Tuombe neema ya kuwa msaada kwa wengine katika mitihani mbalimbali wanayopitia, na kuwa sehemu ya suluhisho la changamoto zao. Nasi pia twapaswa kutojibebesha mizio isiyo ya lazima rohoni mwetu. Mara kadhaa tumekuwa wagumu kusamehe, tunabeba vinyongo rohoni, majivuno, wivu, chuki, visasi, maumivu na historia zetu za kale. Hivi vyote vinatuelemea rohoni. Tuombe neema ya kuachilia.
Jambo la nne: Mtume Paulo anatukumbusha kuwa tunapobatizwa twapaswa kuachana na matendo yote ya mwili na kumruhusu Roho Mtakatifu afanye kazi ndani yetu. Tunapobatizwa tunaanza maisha mapya, maisha ya Roho ndani ya Kristo. Hivyo hatupaswi kukumbatia tena maisha ya zamani kwa sababu kwa ubatizo tunakufa na kufufuliwa pamoja na Kristo. Tunapaswa kukumbatia maisha mapya, maisha ya neema ndani ya Kristo aliye kielelezo na mfano wa maisha ya kimungu. Anatualika kukumbatia sheria mpya, sheria ya upendo ili tuweze kuona mambo yote katika jicho na mtazamo wa Kimungu. Anatualika kutokubeba tena mzigo wa dhambi na udhaifu wetu wa kale. Historia zetu mbaya zisituhukumu na kutufanya kushindwa kwenda mbele kwa matumaini mapya. Kristo alishinda kwa ajili yetu ili sisi tusiishi tena katika hofu, tusiishi maumivu ya mizigo mizito moyoni, bali katika misalaba yetu tuone tumaini katika msalaba wa Kristo aliyeshinda kwa ajili yetu. Tuwe na ujasiri wa kusema daima, “Kristo alishinda kwa ajili yangu, nami nitashinda nikiwa naye.” Jambo la Tano: Tukiyazingatia hayo yote, Mwenyezi Mungu atatupa Pumziko la kweli. Mwenyezi Mungu anaahidi Pumziko kwa wale wote wanaomtii, walio tayari kujivika nira yake iliyo laini, walio tayari kujifunza kutoka kwake. Pumziko hili ndilo uzima wa milele ambao wamewekewa tayari wale watakaoshika maagizo ya Kristo.
Taalimungu ya Mapumziko inaturudisha katika Kitabu cha Yoshua ambapo Mwenyezi Mungu aliwaahidi taifa la Israeli kwamba, kama watashika na kuyatii maagizo ya Mungu, atawapa pumziko katika nchi ya ahadi, nchi ya maziwa na asali. Nchi yetu ya Ahadi ni mbinguni ambapo tutapata pumziko la kweli pamoja na Kristo, na malaika na watakatifu wote. Ulimwenguni humu tutapata masumbuko, lakini Kristo Yesu anatuambia daima jipeni moyo, mimi nimeushinda ulimwengu. Kila mara tunapokutana na Kristo, tumwombe daima aende nasi. Hatuwezi kamwe kupata pumziko la kweli katika mambo ya kidunia. Twaweza kuhangaika peke yetu kutafuta pumziko na tukamsahau Krito, kisha tukakosa vyote. Tujinyenyekeshe mbele zake, tufungue kabisa mioyo yetu kwake, tuweke matumaini yetu yote kwake. Tuseme naye, yeye aliyeshiriki maumivu na msalaba mzito ili atupatie sisi pumziko, anataka kweli sisi sote tupate hilo pumziko la kweli kwake. Yesu Msalaba wangu ni mzito, mtihani yangu ni migumu, majaribu ninayokutana nayo ni makubwa, lakini bado natambua nguvu ya Neno lako. Nifunge daima pamoja na pendo lako ambalo kwalo ulinifia msalabani, ili unipatie uhuru wa kweli. Nina imani na tumaini imara katika pendo lako. Hitimisho: Katika dominika hii tumshukuru Mungu ambaye kwa njia ya Mwanaye Mpenzi Yesu Kristo, ametupatia sisi sote pumziko la kweli. Tuombe neema ya kuwa wanyenyekevu na wapole ili tumtambue Kristo aliye katikati yetu, hata katika nyakati za giza za maisha yetu.