2026.07.18 Askofu Mkuu wa Leopoli ya Kilatini, Mokrzycki 2026.07.18 Askofu Mkuu wa Leopoli ya Kilatini, Mokrzycki 

Askofu Mkuu wa Lviv,Ukraine:Watu wamechoka,tumaini letu liko kwa Mungu

Askofu Mkuu Mieczysław Mokrzycki aliandamana na Katibu wa Vatican wa Mahusiano na Mataifa na Mashirika ya Kimataifa, Askofu Mkuu Paul Richard Gallagher, wakati wa misheni yake katika nchi ya Ulaya Mashariki.“Kwa bahati mbaya, vita vinaendelea na kwa sasa hatuoni hata matumaini yoyote ya mwisho wake.Ni Mungu pekee anayeweza kuvikomesha.”

Na Roberto Paglialonga huko Lviv-Ukraine.

"Watu wote wa Ukraine wamechoka sana. Na kwa bahati mbaya, kwa sasa, hatuoni matumaini yoyote ya mwisho wa vita." Maneno ya Askofu Mkuu Mieczysław Mokrzycki, Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki wa Lviv, katika mahojiano na Vatican News. Kwa sasa yuko Ukraine akisindikizana na ziara ya Askofu Mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu wa Vatican wa Mahusiano na Mataifa na Mashirika ya Kimataifa, ambaye alitembelea nchi hiyo kama mjumbe maalum wa Papa kwa ajili ya sherehe zinazoadhimisha miaka 35 ya kurejeshwa kwa miundo ya Kanisa Katoliki la Kilatini. Kituo cha kwanza cha ziara hiyo ilikuwa ni Lviv, jiji lililo karibu na mpaka wa Poland.

Askofu Mkuu, karibu miaka minne na nusu imepita tangu kuanza kwa mgogoro huo. Hali ya watu wa Ukraine ikoje leo?

Kwa bahati mbaya, vita vinaendelea, na kwa sasa hatuoni matumaini yoyote ya kuisha. Watu wote wa watu wa Ukraine wamechoka kwa sababu kila mtu ameathiriwa na vita hivyo. Wanafamilia wanapigana, au majirani na wafanyakazi wenzake wanapigana. Pia kumekuwa na vifo vingi. Tunapokea habari za kusikitisha kila mara kutoka upande wa mbele. Watu hapa pia wanapoteza matumaini kwa sababu si kila mtu anayeweza kupata kazi, na wengi wanahama, wakiacha nyumba zao kuungana tena na waume au wake zao walioondoka kwenda Ulaya miaka minne au mitano iliyopita. Hata hapa Lviv, ingawa hakuna mapigano kila siku, mara nyingi tunasikia ving'ora vya mashambulizi ya anga. Watu wanakimbia kujificha, kazi inakatizwa, na masomo ya shule pia yamekatizwa. Lakini watu wanaendelea kwenda kanisani, wanaomba, na wanaweka tumaini lao kwa Mungu pekee. Ni Yeye pekee anayeweza kukomesha vita hivi vikali.

Lviv imepigwa mara kadhaa wakati wa mgogoro huo. Watu wanawezaje kupona na kurudi kwenye maisha ya kawaida baada ya bomu?

Si rahisi, kwa sababu karibu kila shambulio huwaacha watu wakiwa wamejeruhiwa au wamekufa, na nyumba na mali huharibiwa. Hata hivyo, mwaka huu, tulisherehekea kumbukumbu ya miaka 25 ya ziara ya Mtakatifu Yohane Paulo II, ambapo alituambia: "Msiogope. Hata katika nyakati hizi mtakutana na magumu, lakini pamoja na Kristo mtayashinda." Ndiyo maana tumaini letu pekee ni maombi. Watu huja kanisani, huomba. Kila siku baada ya Misa tunasali na kufanya mikusanyiko ya maombi ili kuomba rehema ya Mungu na amani katika nchi yetu.

Siku ya Dominika, Askofu Mkuu Gallagher alisafiri kwenda Berdychiv. Kuna umuhimu gani katika ya kusherehekea katika madhabahu ya Mama Yetu wa Mlima Karmeli, na  ni thamani gani ya mkutano huu wa kijamii unaweza kuleta?

Berdychiv ni madhabahu yetu ya kitaifa. Watu huenda huko kutoka  Ukraine yote kumwomba Bikira Maria atuombee. Zaidi ya yote, tunahitaji umoja huu, nguvu hii inayotokana na sala, mshikamano, na maneno ya matumaini. Ninaamini kwamba Askofu Mkuu Gallagher, ambaye anatutembelea kwa mara ya pili (alitembelea Ukraine kwa mara ya kwanza mnamo Mei 2022, wiki chache tu baada ya kuzuka kwa vita), atajaza mioyo yetu amani, furaha, na matumaini, kwa sababu anamwakilisha Papa Leo XIV, ambaye anabaki karibu na nchi yetu kupitia maombi yake ya amani. Wakati wa sala ya Malaika wa Bwana, Baba Mtakatifu mara nyingi hutukumbuka na kutupatia baraka zake. Tunatumaini kwamba ziara hii, ambayo pia inajumuisha mikutano rasmi na serikali ya Ukraine, itazaa matunda ya amani katika nchi yetu.

Akofu Mkuu, watu wengi Magharibi wanaonekana wamezoea vita. Ni kama vile imekuwa kawaida mpya. Kanisa nchini Ukraine linaweza kufanya nini ili kuamsha dhamiri kwa sababu ya amani?

Mikutano ya Maaskofu, pamoja na mapadre na maaskofu wetu, inaendelea kutoa wito wa amani. Mara kwa mara tunasafiri nje ya nchi kuwatembelea maaskofu ndugu zetu, mapadri wenzetu, na marafiki. Wanatukaribisha kila wakati na kutupa fursa ya kuzungumza na jamii zao za parokia. Ninaamini hatupaswi kamwe kuwa wasiojali mateso ya nchi zingine, ikiwa ni pamoja na Nchi Takatifu. Zaidi ya yote, ni lazima tuonyeshe umoja wetu kama ndugu wakristo na tukumbuke kila mmoja wetu. Tunawaomba watu watuunge mkono kupitia maombi na kupitia misaada ya kibinadamu, ambayo bado inahitajika haraka hapa Ukraine.

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here.

20 Julai 2026, 12:59