Watu wa Malawi wakati wanasubiri Bus nchini Afrika Kusini ili kurudishwa nchini Mwao Watu wa Malawi wakati wanasubiri Bus nchini Afrika Kusini ili kurudishwa nchini Mwao  (AFP or licensors)

Wito wa Baraza la Makanisa Afrika Kusini:utu,haki na mshikamano wa kibinadamu

Rais wa Baraza la Makanisa la Afrika Kusini(SACC),Askofu Mkuu Sithembele Sipuka,alitoa wito wa kuchukuliwa hatua za haraka kushughulikia vurugu dhidi ya raia wa kigeni wa Afrika huku akiwahimiza raia wa Afrika Kusini kukataa chuki na kukumbatia maadili ya utu na mshikamano wa kibinadamu.

Sr. Christine Masivo, CPS – Vatican.

Katika mkutano wa Baraza la Makanisa la Afrika Kusini (SACC) na Rais Cyril Ramaphosa katika Jengo la Umoja,na  uliofanyika mnamo tarehe 17 Juni 2026 Askofu Mkuu Sithembele Sipuka alisema, ushiriki huo ulifuatia barua ya kichungaji iliyotolewa hivi karibuni na Baraza la Makanisa (SACC) kwa wanachama wake na watu wote wenye mapenzi mwema kuhusu vurugu zinazoelekezwa juu ya raia wa kigeni katika sehemu mbalimbali za nchi. Askofu Mkuu alitoa shukrani kwa Rais kwa kuhudhuria mkutano huo na kusikiliza wasiwasi uliotolewa na viongozi wa Kanisa.

Sote tumeumbwa kwa sura ya Mungu

Tuko pamoja kuonesha wasiwasi wetu mkubwa kuhusu mateso ya wanadamu wenzetu, wengi wao Waafrika wenzetu ambao wamenyanyaswa, wamehamishwa makazi, wametishiwa, na kunyimwa haki zao," Askofu Mkuu Sipuka alisema. "Kanisa haliwezi kukaa kimya wakati utu wa binadamu unakiukwa." SACC ilisisitiza kwamba watu wote wana utu wa kibinadamu uliotolewa na Mungu, na hivyo vurugu, vitisho, na kulengwa kwa jumuiya zilizo katika mazingira magumu haviwezi kamwe kuhalalishwa. Ni kinyume na roho ya Ubuntu na haiendani sambamba na uelewa wa Kikristo wa mwanadamu. Viongozi wa Kanisa wakati wa mkutano waliitaka serikali kuchukua hatua madhubuti dhidi ya vitendo haramu vya vikundi na harakati ambazo zimechukua sheria mikononi mwao, huku wakishughulikia wasiwasi kuhusu uhamiaji na usimamizi wa mipaka.  Askofu Mkuu alisisitiza kwamba jukumu la kutekeleza sheria liko kwa serikali na taasisi zake, sio kwa watu binafsi au vikundi vinavyofanya kazi nje ya sheria.

Sababu halisi ya uchungu wa jamii

Baraza la Makanisa Afrika Kusuni (SACC) lilibainisha kwamba kuchanganyikiwa miongoni mwa Waafrika Kusini kunatokana na ukosefu wa ajira unaoendelea, umaskini, utoaji duni wa huduma, ufisadi, na kupungua kwa imani ya umma kwa taasisi. "Tulizungumza kwa uaminifu kuhusu hali ambazo zimechangia hasira tunayoiona katika jamii nyingi, watu wanapambana, wanahisi wamepuuzwa na hawajasikilizwa," Askofu Mkuu Sipuka alielezea. Ukweli huu hauhalalishi vitendo vya vurugu na lazima utambuliwe, na chanzo kikuu cha machafuko ya kijamii kutafutwa.

Hata kama kila raia wa kigeni angeondoka Afrika Kusini, nchi bado ingekabiliwa na ukosefu wa ajira, utoaji duni wa huduma, ufisadi, uhalifu, na ukosefu wa usawa wa kiuchumi. Askofu Mkuu Sipuka alisema kwamba raia wa kigeni mara nyingi wamekuwa kizingizio cha changamoto ambazo ni za ndani na ngumu zaidi, na kwamba matatizo ya kiuchumi ya nchi hayawezi kutatuliwa kwa kuwalenga wahamiaji na wakimbizi.

Wajibu wa serikali

Kuhusu maandamano ambayo yamepangwa kufanyika tarehe 30 Juni 2026, Baraza la Makanisa Afrika Kusini (SACC) ilihimiza serikali kuhakikisha hatua za kutosha za usalama ili kuzuia mashambulizi zaidi na kulinda jamii zilizo katika mazingira magumu. Askofu Mkuu Sipuka alisema, Baraza lilipokea uhakikisho kutoka kwa Rais kwamba vyombo vya kutekeleza sheria vitawekwa na kwamba hatua zitachukuliwa ili kudumisha utulivu wa umma. Kanisa lilikaribisha nguzo tano zilizoainishwa na rais katika hotuba yake kama mfumo muhimu wa kukabiliana na mgogoro huo. Viongozi wa Kanisa walisisitiza kwamba ahadi ya sera lazima sasa iwekwe katika vitendo vinavyoonekana na vinavyopimika, kwani kujitolea kwenye karatasi haitoshi. "Jamii zinahitaji kuona utekelezaji mzuri, utawala unaowajibika na hatua za vitendo zinazoshughulikia hitaji la kibinadamu la haraka na sababu za msingi za kutokuwa na utulivu."

Kukataa unyonyaji

Baraza la Makanisa Afrika Kusini liliendelea kuwataka watu wote kukataa chuki dhidi ya wageni, taarifa potofu, na vurugu, na kuhakikisha kwamba masuala yote yanayohusiana na uhamiaji yanapaswa kushughulikiwa kupitia michakato halali na ya kikatiba badala ya kupitia vitisho na tahadhari. Askofu Mkuu alitoa wito zaidi kwa makanisa na mashirika ya kijamii kuwasaidia wale walioathiriwa na vurugu za hivi karibuni kupitia usaidizi wa kibinadamu kwa chakula, malazi, huduma za matibabu na usaidizi wa kiuchumi. "Familia nyingi ziko katika mazingira magumu na zinahitaji huruma, mshikamano na utunzaji unaowakumbusha kwamba hawako peke yao," alisema.

Kujenga na kusimama kwa ajili ya ubuntu

Askofu Mkuu Sipuka alikumbusha taifa historia yao. Wakati wa mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi, wengi wao walikimbilia na kukaribishwa huku wakipata msaada na mshikamano katika nchi nyingine katika bara la Afrika. Aliwasihi raia wasisahau historia hiyo na kupinga juhudi za kuwagawanya Waafrika dhidi ya kila mmoja. "Mgeni si adui yetu," alisema. "Kama watu wa imani, tumeitwa kutambua ubinadamu wa kila mtu na kujenga jamii iliyojengwa juu ya haki, utu, amani, na uwajibikaji wa pande zote. Ni kupitia kujitolea kama huko pekee ndipo Afrika Kusini inaweza kupata upatanisho na mshikamano wa kijamii.

Baraza la makanisa Afrika Kusini

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku. Just click here

18 Juni 2026, 13:31