Mababa wa Kanisa wanasema kwamba, fadhila ni tabia ya kawaida na imara ya kutenda mema. Mababa wa Kanisa wanasema kwamba, fadhila ni tabia ya kawaida na imara ya kutenda mema.   (Vatican Media)

Tafakari Dominika 13 Mwaka A wa Kanisa: Fadhila na Maisha ya Kikristo!

Fadhila ni tabia ya kawaida na imara ya kutenda mema. Yamruhusu mtu si kutenda mema tu bali kutoa kilicho chema cha nafsi yake. Mtu wa fadhila huelekea mema kwa hisi pamoja na nguvu za kiroho. Hutafuta mema na kuyachagua kwa matendo halisi. Kuna fadhila za kibinadamu ambayo ni hali thabiti, maelekeo imara, ukamilifu wa kawaida wa akili na utashi zinazotawala matendo ya binadamu, zinazoratibu harara na kuongoza mwenendo kufuata akili na imani.

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, dominika ya 13 ya mwaka A wa kiliturujia katika Kanisa, kipindi cha kawaida. Kiini cha ujumbe umejikita katika uhusiano uliopo kati ya fadhila za kibinadamu na za kimungu. Mababa wa Kanisa wanasema kwamba, fadhila ni tabia ya kawaida na imara ya kutenda mema. Yamruhusu mtu si kutenda mema tu bali kutoa kilicho chema kabisa cha nafsi yake. Mtu wa fadhila huelekea mema kwa hisi zake zote pamoja na nguvu za kiroho. Hutafuta mema na kuyachagua kwa matendo halisi. Kuna fadhila za kibinadamu ambayo ni hali thabiti, maelekeo imara, ukamilifu wa kawaida wa akili na utashi zinazotawala matendo ya binadamu, zinazoratibu harara na kuongoza mwenendo kufuata akili na imani. Zinawezesha raha, kujitawala na furaha katika kuishi maisha mema kimaadili. Fadhila adili hupatikana kwa juhudi za kibinadamu kuungana na upendo wa Mungu. Shabaha ya mtu mwenye fadhila ni kuwa kama Mungu. Kuna fadhila kuu ambazo hutenda kazi kama bawaba nazo ni: Busara, haki, nguvu, na kiasi. Rej. KKK 1803-1803. Kuna fadhila tatu za Kimungu: imani, matumaini na mapendo.

Kuna fadhila tatu za Kimungu: Imani, matumaini na mapendo
Kuna fadhila tatu za Kimungu: Imani, matumaini na mapendo   (@Vatican Media)

“Fadhila za kibinadamu zinapatikana kwa njia ya malezi, matendo ya makusudi, udumifu kwa njia za juhudi zinazorudiwa-rudiwa. Nazo zahuishwa, zatakaswa na kuinuliwa na neema ya Mungu, kuunda tabia na kurahisisha kutenda mema” (KKK 1810). Hivyo, “Fadhila za kimungu zinaweka msingi, zinahuisha, na kuainisha utendaji adili wa Mkristo. Zinapasha habari na kuzihuisha fadhila zote za maadili. Zinamiminwa na Mungu katika roho za waamini kuwawezesha kutenda kama watoto wake, na kustahili uzima wa milele. Nazo ni amana ya uwepo na tendo la Roho Mtakatifu katika nguvu za binadamu” (KKK 1813). Hivyo, “fadhila za kibinadamu zinajipandikiza katika fadhila za kimungu ambazo zinarekebisha nguvu za mwanadamu apate kushiriki hali ya kimungu” (KKK 1810). Na ni katika kutenda mema tunashiriki hali ya kimungu, tunakuwa na muunganiko na Mungu aliye mtakatifu na hivyo tunaweza kuishi maisha ya kitakatifu hapa duniani na baadae kuushiriki utakatifu wake mbinguni na kumsifu milele yote. Ni katika muktadha huu wimbo wa mwanzo unaotoka Zaburi 47:2, unasema hivi; “Enyi watu wote, pigeni makofi, mpigieni Mungu kelele kwa sauti ya shangwe.” Na mama Kanisa katika sala ya mwanzo anasali hivi; “Ee Mungu, umependa kutufanya sisi tuwe wana wa nuru kwa neema uliyotufadhili. Tunakuomba utujalie tusifunikwe na giza la udanganyifu, bali tukae daima peupe katika nuru ya ukweli wako.”

Fadhila za Kimungu ni msingi wa maisha adili na matakatifu
Fadhila za Kimungu ni msingi wa maisha adili na matakatifu   (@Vatican Media)

Somo la Kwanza ni la Kitabu cha Pili cha Wafalme (2Waf 4:8-11, 14-16). Ni simulizi la mwanamke mshunemu na Nabii Elisha. Mwanamke huyu ni tajiri, mwema, na mkarimu, lakini hakujaliwa mtoto na mme wake alikuwa mzee. Katika wema wake, alimkaribisha na kukarimu Elisha kwa chakula, na alipotambua kuwa ni mtu wa Mungu, alimuandalia chumba cha kupumzika na kulala, ikiwa alichelewa kurudi katika kazi zake. Kwa wema na ukarimu wake, Elisha alimuomba Mungu kwa imani akamjalie mtoto, hamu ya moyo wao ikatimia. Hii inatufundisha kuwa matendo mema, yanayoongozwa na fadhila ya upendo na imani, yanatuletea baraka na neema kutoka kwa Mungu aliye asili ya wema wote. Na “mwenye haki ataishi kwa imani, na imani hai hutenda kazi kwa upendo” (KKK 1814). Hivyo “imani bila matendo imekufa; imani ikinyimwa matumaini na mapendo haiwezi kumwunganisha mwamini kikamilifu na Kristo, na hawezi kuwa kiungo cha mwili wake” (KKK 1815.) Ni katika muktadha huu zaburi ya wimbo wa katikati inauimba wema na utukufu wa Mungu ikisema hivi; “Fadhili za Bwana nitaziimba milele; kwa kinywa changu nitavijulisha vizazi vyote uaminifu wako. Maana nimesema, fadhili zitajengwa milele; katika mbingu utauthibitisha uaminifu wako. Heri watu wale waijuayo sauti ya shangwe, Ee Bwana, huenenda katika nuru ya uso wako. Kwa jina lako hufurahi mchana kutwa, na kwa haki yako hutukuzwa. Maana fahari ya nguvu zao ni Wewe. Na kwa radhi yako pembe yetu itatukuka. Maana ngao yetu i-na Bwana, na mfalme wetu ni wake Mtakatifu wa Israeli” (Zab. 88: 1-2, 15-18.)

Ukarimu ni ndoana ya baraka na neema kutoka kwa Mungu
Ukarimu ni ndoana ya baraka na neema kutoka kwa Mungu   (@VATICAN MEDIA)

Somo la Pili ni kutoka katika Waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi (Rm 6:3-4, 8-11). Fundisho kuu ni Sakramenti ya ubatizo na matunda yake. Ubatizo ni ishara au alama inayoashiria kufa kwetu kuhusu dhambi na kufufuka kwetu pamoja na Kristo. Huku ndiko kuingia katika ushirika na Kristo, ushirika wa uhakika na mkamilifu wa kufa na kufufuka naye. Ushirika huu tunaouingia kwa njia ya ubatizo kwa jina la Yesu Kristo unatuwezesha kupata maondoleo ya dhambi na kumtapokea Roho Mtakatifu. Sisi tulipoingia ushirika na Yesu tulifutiwa deni la dhambi kwa thamani ya damu yake. Mtume Petro kuhusu fundisho hili anaeleza kuwa fidia iliyolipwa kutuweka huru, siyo fedha wala dhahabu, bali ni damu azizi ya Mwanakondoo asiye na doa, ndiye Kristo Yesu Bwana wetu (rej. 1Pet 1:18). Injili ni kama ilivyoandikwa na Mathayo (Mt 10:37-42). Ni miongozo, maagizo na masharti ya kumfuata Kristo. Kwanza kabisa ni sharti la kumpa Yeye, Mungu nafsi ya ya kwanza kwa kila kitu, kwa kuwa hakuna kitu chochote kinachopaswa kuchukua nafasi yake. Hii ni kwa sababu Yeye ni asili na chanzo, kielelezo na chemchemi ya kila kitu na uzuri wote. Yeye ni upendo wenyewe. Tukimuweka pembeni na nafasi yake kuchukuliwa na mengine, mengine yote yanakosa maana, yanakosa thamani na mwelekeo. Lakini Yeye akiwa wa kwanza, mengine yote yanapata maana na mwelekeo mwema na mzuri. Hivyo kumpenda Mungu kuliko vitu vyote kwa ajili yake mwenyewe, kunatuwezesha kujipenda wenyewe na kuwapenda wengine kama sisi wenyewe (KKK 1822).

Fadhila za kibinadamu zinapatikana kwa njia ya malezi
Fadhila za kibinadamu zinapatikana kwa njia ya malezi   (@Vatican Media)

Jambo la pili limebebwa na agizo hili; “Mwenye kuiona nafsi yake ataipoteza; naye mwenye kuipoteza nafsi yake kwa ajili yangu ataiona.” Hapa Yesu anamaanishi kuwa kule kumpenda Yeye na kuwa tayari kujitoa bila kujibakiza ndiko kunakotupa uhuru kamili katika kujipenda wenyewe na kuwapenda wengine. Ni katika muktahda huu, sala ya Ekaristi ya nne ikimuelekea Mungu Baba inasema hivi; Kristo Yesu Mwanao, “alijitoa mwenyewe afe ili apate kutimiza mapenzi yako, naye alipofufuka katika wafu akaangamiza mauti na kutuletea uzima mpya. Kisha alimtuma Roho wako wewe Baba awe malimbuko ya waamini. Naye Roho Mtakatifu akaitimiza kazi ya mwanao hapa duniani na kukamilisha utakatifu, ili tusiishi kwa ajii yetu sisi wenyewe, bali kwa ajili yake Yeye aliyekufa na kufufuka kwa ajili yetu sisi.”Na jambo la tatu linahusu matunda ya kuwapokea na kuwahudumia wengine. Yesu anasema hivi; “Awapokeaye ninyi, anipokea Mimi; naye anipokeaye Mimi, ampokea Yeye aliyenituma. Ampokeaye nabii kwa kuwa ni nabii, atapata thawabu ya nabii; naye ampokeaye mwenye haki kwa kuwa ni mwenye haki, atapata thawabu ya mwenye haki. Na mtu awaye yote atakayemnywesha mmojawapo wa wadogo hawa kikombe cha maji ya baridi, kwa kuwa ni mwanafunzi wangu, amin, nawaambia, haitampotea kamwe thawabu yake.”

Bebeni Misalaba Yenu Kila Siku!
Bebeni Misalaba Yenu Kila Siku!   (@Vatican Media)

Kwa maelezo haya, Yesu anaweka huduma tunazopaswa kuwatendea wengine katika makundi makuu matatu. Kwanza, ni kuwapokea na kuwahudumia watumishi wake ili kupata thawabu ya watumishi. Pili, ni kuwapokea na kuwahudumia walio wadogo na wahitaji katika maisha ya kila siku. Na tatu ni kuwa watu wa haki na kutetea haki za wanyonge. Katika huduma zote hizi hakuna iliyo ndogo ambayo ikitendwa kwa moyo wa upendo isiweze kutustahilisha kuingia katika ufalme wa mbinguni, maadam imetendwa kwa upendo. Hivyo, “Mfuasi wa Kristo hatakiwi kushika imani tu na kuiishi, bali anapaswa aiungame, aishuhudie kwa uhakika, na aieneze…kuwa tayari kumkiri Kristo mbele za watu na kumfuata katika njia ya Msalaba... Huduma na ushuhuda wa imani ni vya lazima kwa wokovu” (KKK 1816.) Mwisho ni fadhila ya matumaini, ndiyo inayotuwezesha kutamani heri ya Ufalme wa mbinguni na uzima wa milele, kwa kutumainia ahadi za Kristo, sio kwa kutegemea nguvu zetu, bali kwa msaada wa neema ya Roho Mtakatifu ambaye kwaye tunahesabiwa haki kwa neema yake na kufanywa warithi wa uzima wa milele (rej. KKK 1817). Ni katika tumaini hili mama Kanisa katika sala ya kuombea dhabihu anasali hivi; “Ee Mungu umependa kutuletea baraka za mafumbo yako. Tunakuomba utujalie ibada zetu ziafikiane na hii sadaka takatifu tunayokutolea.” Na katika sala baada ya Komunyo anasali hivi; “Ee Bwana, tunakuomba kafara hii takatifu tuliyokutolea na kuila itutie uzima wako. Hivyo tuwe tumeungana nawe siku zote kwa mapendo, tupate kuzaa matunda yenye kudumu daima”. Na hili ndilo tumaini letu. Tumsifu Yesu Kristo!

Tafakari D 13 Mwaka A
26 Juni 2026, 09:26