Kanisa Kuu la Loikaw nchini Myanmar Kanisa Kuu la Loikaw nchini Myanmar  (@Daniele Bellocchio)

Myanmar:Kurudishwa kwa Kanisa Kuu la Loikaw kwa Jumuiya Katoliki

Kurudishwa kwa Kanisa Kuu la Kristo Mfalme huko Loikaw kunaashiria ishara muhimu ya matumaini kwa Jumuiya ya Wakatoliki wa Myanmar baada ya miezi mingi ya uvamizi wa kijeshi.Licha ya maendeleo haya,Askofu Celso Ba Shwe wa Jimbo la Loikaw alisema “dhamira ya Kanisa inabaki kuzingatia kusindikiza mamia ya maelfu ya watu waliokimbia makazi yao ndani,waliotawanyika katika kambi na maeneo ya mbali.

Na Sr. Christine Masivo, CPS - Vatican.

Jimbo la Loikaw huko Kayah nchini Myanmar limepokea ishara ya matumaini ya kurudishwa kwa Kanisa Kuu la Kristo Mfalme na kituo chake cha kichungaji, ambacho kilikuwa kimekaliwa na jeshi tangu Novemba 2023. Eneo hilo lilitumika kama kituo cha kijeshi wakati wa mzozo uliozuka kufuatia mapinduzi ya kijeshi ya Myanmar mnamo Februari 2021. Kwa hiyo, "hii inakuwa ishara ya matumaini.” Katikati ya migogoro, kutokuwa na uhakika, na ugumu, imani inaendelea kudumisha jumuiya zinazotamani amani, upatanisho, na kurudi kwenye maisha ya kawaida.

Matumaini katika jumuiya mahalia

Askofu Celso Ba Shwe alitoa shukrani na furaha kwa kurejea kwa Kanisa kuu, akielezea kama wakati wa matumaini kwa Jumuiya ya Wakatoliki wa eneo hilo, akibainisha kuwa “majengo hayo yanaendelea kuhitaji matengenezo makubwa kabla ya kuanza tena jukumu lao kama vituo vya ibada na huduma ya kichungaji.” Ukarabati wa sehemu kadhaa umefanywa lakini kituo cha kichungaji bado hakina umeme na maji. Waamini wanarudi polepole na kuleta matumaini kwenye Jimbo ya kupanga upya shughuli zake za kichungaji. Hata hivyo Askofu mwenyewe hajarudi kuishi huko. Utume wake alisema unabaki pale ambapo watu wake wako miongoni mwa waliohamishwa.

Miongoni mwa waliokimbia makazi yao

Kulingana na Shirika la Kipapa la  Habari za Kimisionari, Fides, mgogoro huo ulisababisha moja ya migogoro mikubwa zaidi ya kibinadamu nchini, na kulazimisha mamia ya maelfu kukimbia makazi yao. Askofu Ba Shwe, alibainisha kuwa zaidi ya watu 300,000 waliokimbia makazi yao wametawanyika katika mamia ya kambi kote katika Jimbo.

Kwa sasa Askofu anaishi katika Kanisa la Mama wa Mungu Sbansu na aliendelea kusafiri mara kwa mara hadi kwenye kambi za wakimbizi na jamii zilizotawanyika. Parokia nyingi zinabaki tupu na zimefungwa huku familia zikitafuta usalama katika misitu, vijiji vya mbali na makazi ya muda. Askofu alisema, "uwepo wa Makanisa katika kambi ni aina mpya ya huduma ya kimisionari." Mapadre na wafanyakazi wa kichungaji wanaishi miongoni mwa waliokimbia makazi yao, wakishiriki mapambano yao ya kila siku na kutoa msaada wa kiroho. "Hii ni njia tofauti ya kuwa padre," alielezea. "Huduma ya kichungaji haizuiliwi tena katika majengo ya kanisa bali inafanywa popote pale watu walipo." Wanatarajia kusherehekea sakramenti pia.

Kutafuta upatanisho

"Kuna umoja na mshikamano miongoni mwa jamii inayowaunga mkono kwa kusaidiana huku ikisaidia wafadhili kuwawezesha wengi kuishi," Askofu alisema. Kujitolea kwa pamoja kunaonesha uwepo wa Mungu miongoni mwa watu wake kwani imani inabaki kuwa chanzo cha nguvu huku jamii zikisubiri siku ambayo zinaweza kurudi nyumbani. Watoto na vijana hawapati elimu na hivyo basi wasiwasi unaongezeka kwa kizazi kipya cha Myanmar. Kwa kukabiliana na hali hiyo, watawa na wafanyakazi wa Kanisa hupanga shule zisizo rasmi na shughuli za kielimu kwa kutumia rasilimali chache zinazopatikana.

Licha ya hitaji la kibinadamu, Askofu alitoa wito wa upatanisho miongoni mwao, akiamini kwamba amani ya kudumu inaweza kupatikana tu kupitia mazungumzo na umoja miongoni mwa viongozi wa kisiasa, vikundi vyenye silaha na mamlaka. "Tunataka amani na upatanisho," alisema. "Bila upatanisho, hakuna amani." Uwepo wa Makanisa unabaki kuwa muhimu pamoja na mapungufu yake. Kupitia maombi, kutia moyo na ukaribu na mateso, Kanisa linaendelea kushuhudia, kutumaini, na kuamini kwamba Mungu hawaachi kamwe watu wake.

KANISA LA MYANMAR

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku. Just click here

16 Juni 2026, 13:16