2026.05.30 Mkutano wa SECAM. na CCEE huko  Lussemburgo. 2026.05.30 Mkutano wa SECAM. na CCEE huko Lussemburgo. 

Luxembourg:Maaskofu wa Ulaya na Afrika kuhusu uinjilishaji na Sinodi

Mkutano wa 10 ulihitimishwa hivi karibuni huko Luxembourg ulionza Mei 25 hadi 28,ulioandaliwa na Maaskofu wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Ulaya(CCEE)na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu wa Afrika na Madagascar(SECAM) huko Luxembourg kwa mada:"Uinjilishaji na Sinodi:Njia za Bara,”ambapo inaonesha hamu ya pamoja ya kutembea pamoja,kusikilizana na kupambanua pamoja changamoto za kichungaji na fursa za kimisionari zinazokabili mabara hayo mawili.

Na Christine Masivo CPS – Vatican.

Shirikisho la mabaraza ya Maaskofu barani  Ulaya (CCEE) na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu wa Afrika na Madagascar (SECAM) walikusanyika huko Luxembourg kwenye Mkutano  wa 10 kunzia tarehe 25 hadi 28 Mei 2026 kwa kuongozwa na mada: "Uinjilishaji na Sinodi: Njia za Bara Mara ya mwisho walifanya mkutano wao kuanzia tarehe 24 hadi  26 Januari 2024 huko  Nairobi, Kenya. Mkutano huo  ulioandaliwa na Jimbo Kuu la Luxembourg na Kardinali Jean-Claude Hollerich, Askofu Mkuu wa Luxembourg na Makamu Rais wa CCEE, uliendeleza ushirikiano wa kidugu wa muda mrefu kati ya Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu wa Ulaya na Shirikisho Mabaraza ya Maaskofu wa Afrika na Madagascar, kama ishara halisi ya ushirika unaounganisha makanisa barani Afrika na Ulaya ndani ya Kanisa moja la Ulimwengu.

“Sisi ni Kanisa la kimisionari”

Kardinali Fridolin Ambongo, Askofu Mkuu wa Kinshasa na rais wa SECAM alisema kwamba mkutano huo “ulikuwa wa wakati muafaka na wa mapendo kwani Kanisa lote limealikwa kuongeza uelewa wake wa Kisinodi kama kipimo muhimu cha maisha ya kikanisa na utume. Kwa upande wa  Sinodi, uinjilishaji wa Kanisa na Sinodi hauwezi kutenganishwa, kwani sisi ni Kanisa la kimisionari, Kanisa linalosikiliza, kupambanua, kutembea pamoja, na kumtangaza Kristo kwa imani na matumaini mapya.” Alisisitiza juu kurejea umisionari unaounganisha mabara hayo mawili, zawadi ya kihistoria ya kimisionari kwa Afrika na mchango unaokua wa Afrika,  kwa Kanisa la ulimwengu ikiwa ni pamoja na Ulaya.

Katika hotuba yake ya uzinduzi, Askofu Mkuu Gintaras Grusas wa Vilnius na Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Ulaya(CCEE), alisisitiza kwamba Uinjilishaji na Sinodi haviwezi kutenganishwa: “Uinjilishaji unaelezea sababu ya utume wa Kanisa, huku Sinodi ikielezea jinsi ya Kanisa linalosikiliza, kupambanua na kutembea pamoja.” Kwa njia hiyo aliwaalika washiriki “kuishi Semina hiyo kama kubadilishana zawadi kati ya Ulaya na Afrika na kama mchango katika utekelezaji wa Sinodi.” Licha ya Afrika na Ulaya kuishi hali tofauti za kichungaji, kuna wasiwasi wa pamoja kuhusu uinjilishaji, miito, malezi ya kipadre, huduma ya vijana, uhamiaji, mazungumzo ya kidini, na utafutaji wa ushuhuda halisi wa Kikristo katika jamii ya kisasa. Semina hiyo ilitoa fursa ya kipekee si tu kwa ajili ya tafakari ya kitaalimungu na ubadilishanaji wa kichungaji, bali pia kwa ajili ya utambuzi wa kiroho wa pamoja.

Roho ya Sinodi

Kwa Askofu Mkuu huyo alisisitiza kuwa “Kama maaskofu kutoka mabara mawili, tumeitwa kusikiliza kwa makini kile ambacho Roho Mtakatifu anakisema kwa Kanisa leo  hii kupitia uzoefu, matumaini, mapambano, na karama za Makanisa yetu  mahalia. Safari ya kisinodi inatukumbusha kwamba kusikilizana kwa pamoja ni kitendo cha ushirika na uinjilishaji. Safari ya hivi karibuni ya kichungaji ya Papa Leo XIV barani Afrika iliangazia jukumu muhimu ambalo Afrika inachukua katika maisha na utume wa Kanisa la ulimwenguni kote, na Papa alihimiza Kanisa barani Afrika kuendelea kuwa ishara ya matumaini, upatanisho, imani hai na nguvu ya kimisionari kwa ulimwengu mzima huku likiimarisha ushirika miongoni mwa Makanisa  mahalia na kuimarisha ushirikiano ndani ya Kanisa la ulimwengu wote unaohusiana na ujumbe wa Mkutano huo.”

Matumaini ya wote

Askofu Mkuu José Manuel Imbamba  wa Jimbo Kuu la  Saurimo na Makamu Rais wa SECAM, aliwasilisha muktadha wa “uinjilishaji wa Kiafrika kama uwanja wa matumaini na ukuaji wa kimisionari, na kwamba Afrika inahama kutoka ‘eneo la utume’ hadi kuwa wamisionari, akitaja changamoto kubwa ya umaskini, vurugu, uhamiaji, udhaifu wa vijana, ukosefu wa usawa na udhaifu wa familia.”

“Njia ya Kisinodi inawaalika mabara yetu kusonga mbele zaidi ya mbinu za kichungaji zilizotengwa na kugundua upya uzuri wa kutembea pamoja kama Watu wa Mungu mmoja, na uhusiano kati ya Afrika na Ulaya si tu katika suala la kihistoria au kitaasisi, bali kama ushirikiano wa kweli wa kikanisa katika huduma ya Uinjilishaji.” Aliendelea “Ulaya ilituma wamisionari kwa ukarimu barani Afrika, ikipanda mbegu za Injili ambazo leo hii zinaendelea kuzaa matunda mengi  barani kote na Kanisa barani Afrika linashukuru sana kwa urithi huu wa kimisionari. Afrika inatambua jukumu lake la kimisionari kwa Kanisa la Ulimwengu wote kupitia mchango unaoongezeka wa mapadre wa Kiafrika, watawa, wamisionari, na waamini walei ambao sasa wanahudumu katika majimbo mengi na jumuiya za kikanisa kwa  Ulaya yote,  si kama jibu la vitendo kwa mahitaji ya kichungaji au uhaba wa miito, bali kama mfano unaoonekana wa ushirika wa kikanisa na utajiri wa pande zote mbili.”

Mifumo ya kichungaji

“Afrika inatoa Kanisa la ulimwengu wote nguvu ya imani, nguvu ya ujana, hisia kubwa ya jumuiya, maisha ya kiliturujia yenye nguvu, na shauku ya kimisionari.” Na Ulaya, kwa upande wake, “inaendelea kutoa urithi tajiri wa kitaalimungu, kiroho, kiakili, na kikanisa ambao unabaki kuwa muhimu kwa maisha ya Kanisa. Kuna haja inayoongezeka ya kutafakari kwa undani zaidi jinsi ya kuimarisha na kupanga vyema ushirikiano wa kimisionari kati ya mabara yetu kutafuta mifumo mipya ya kichungaji, muundo wa ushirikiano na aina za malezi ambazo zitaruhusu Makanisa yetu kusaidiana kwa ufanisi zaidi katika uaminifu kwa injili na kukabiliana na changamoto za kisasa. Kwa upande wa Askofu Alexandre JOLY, Askofu wa Troyes, alielezea “jinsi uinjilishaji barani Ulaya kama ukweli unaokisiwa na vivuli na mwanga, unyenyekevu, udhaifu na kupoteza kumbukumbu, lakini pia wakatekumeni wapya, wamisionari vijana, uinjilishaji wa kidijitali, njia ya uzuri, na wito mpya wa kushuhudia.”

CCEE NA SECAM

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here.

02 Juni 2026, 10:54