Yesu, akiwa anakaribia kuondoka kati ya wanafunzi wake na kuingia katika Fumbo Takatifu la Pasaka, anawaambia wanafunzi wake na anatuambia sisi sote kuwa, “Sitawaacha Ninyi Yatima.” Yesu, akiwa anakaribia kuondoka kati ya wanafunzi wake na kuingia katika Fumbo Takatifu la Pasaka, anawaambia wanafunzi wake na anatuambia sisi sote kuwa, “Sitawaacha Ninyi Yatima.”   (@Vatican Media)

Tafakari Dominika ya Sita Pasaka Mwaka A: Sitawaacha Yatima!

Huu ni ujumbe wa matumaini na faraja. Yesu, akiwa anakaribia kuondoka kati ya wanafunzi wake na kuingia katika Fumbo Takatifu la Pasaka, anawaambia wanafunzi wake kuwa, “Sitawaacha Ninyi Yatima.” Anatuahidi Roho Mtakatifu, Msaidizi, Roho wa Kweli, atakayetufariji, kutufundisha na kutukumbusha yale yote aliyotufundisha Kristo. Kristo anatualika kuishi katika upendo na muunganiko wa kudumu pamoja naye, upendo ambao hauthibitishwi tu kwa maneno!

Na Padre Bonaventura Maro, C.PP.S., -Kolleg St. Josef, Salzburg, Austria.

Utangulizi: Wapendwa Familia ya Mungu, ni Dominika ya 6 ya Pasaka mwaka A wa Kanisa. Tunakaribia mwishoni mwa kipindi cha Pasaka, na Mama Kanisa anatuandaa kwa ajili ya Adhimisho la Sherehe ya Kupaa kwa Bwana na ile ya Pentekoste. Ujumbe wa leo ni ujumbe wa matumaini na faraja. Yesu, akiwa anakaribia kuondoka kati ya wanafunzi wake na kuingia katika Fumbo Takatifu la Pasaka, anawaambia wanafunzi wake na anatuambia sisi sote kuwa, “Sitawaacha Ninyi Yatima.” Anatuahidi Roho Mtakatifu, Msaidizi, Roho wa Kweli, atakayetufariji, kutufundisha na kutukumbusha yale yote aliyotufundisha Kristo. Kristo anatualika kuishi katika upendo na muunganiko wa kudumu pamoja naye, upendo ambao hauthibitishwi tu kwa maneno, au kwa kufuata juu juu amri zake, bali upendo uliojikita katika utii wa hiari wa Amri zake. Katika Dominika hii, tunaalikwa kufungua mioyo yetu ili Roho Mtakatifu apate makao ndani mwetu, na atupe nguvu ya mashuhuda Hodari wa Injili, kama anavyotuambia mtume Petro, kuwa tayari kumjibu kila mtu aulizaye Habari za tumaini lililo ndani yetu, kwa upole na kwa hofu. Somo la Injili: Ni kutoka katika Injili ya Yohane 14:15-21. Somo la Injili Takatifu ni sehemu ya hotuba ndefu ya Kristo katika karamu ya mwisho kabla ya kuingia katika mateso, na kifo chake inayoanzia sura ile ya 13 ya Injili hii ya Yohane. Kristo anaongea kwa mara ya mwisho na Mitume wake waliokuwa na hofu, upweke na huzuni kwa kuwa Kristo alikwishawaambia juu ya mambo ambayo yangempata. Kwamba atasalitiwa na Yuda, Petro pia atamkana, na kwamba mwisho ataondoka, na huko atakakokwenda wao wasingeweza kufika kwa wakati ule. Katika mazingira haya ya taharuki, Yesu alianza sura hii ya 14 kama tulivyosikia katika Dominika iliyopita ya 5 ya Pasaka kwa neno la faraja, “Msifadhaike mioyoni mwenu”. Aliwaahidi kwamba anakwenda kuwaandalia makao, na kwamba atarudi tena. Katika Dominika hii ya sita ya Kipindi cha Pasaka Mwaka A wa Kanisa, Kristo Yesu anaendelea tena kuwapa moyo Mitume wake kwa kuwaambia, “Sitawaacha ninyi yatima, akirudia kuwaambia tena, naja kwenu.” Ahadi hii ilitimia siku ya Pentekoste, Roho Mtakatifu alipowashukia Mitume, nao wakaanza mara moja kuwa mashuhuda Hodari wa Ufufuko wake, katika Yudea, Samaria hadi miisho yote ya dunia. Hebu tutazame mgawanyiko wa Injili hii ambao utatusaidia kuelewa kwa kina ujumbe mkuu unaotuongoza katika Liturujia nzima ya Neno la Mungu katika Dominika hii, kwa namna ya pekee tupokaribia kuadhimisha Sherehe ya kupaa Bwana mbinguni na Sherehe ya Pentekoste. Sehemu ya kwanza ni ile aya ya 15, na 21, sehemu ya pili ni aya 16-17 na sehemu ya tatu ni aya 18-20.

Sitawaacha Yatima; Naja Kwenu
Sitawaacha Yatima; Naja Kwenu

Fundisho la kwanza: Kumpenda Kristo ni kumwamini, kuzishika na kuziishi amri zake, ili kudumu katika Pendo lake. Sehemu ya kwanza ya Injili hii ya leo ni aya ya 15 na ile ya 21. Ukiitazama mistari hii miwili, utagundua inasema kitu kilekile kwa maneno tofauti kidogo, ikitengeneza kama mabano yanayofungia mafundisho ya Roho Mtakatifu katikati. Katika aya ya 15 Kristo anawaambia Mitume wake, “Mkinipenda mtazishika amri zangu” na kwenye aya ya 21 anawaambia tena, “Yeye aliye na amri zangu na kuzishika, yeye ndiye anipendaye…” Tunaweza kujiuliza hapa swali moja la msingi sana. Ni upendo na Amri gani anavyovizungumzia Kristo katika aya hizi mbili? Ni vile vile alivyozungumzia alivyoweka ile amri kuu ya mapendo katika sura ya 13:34 alipoweka amri kuu ya mapendo? Katika sehemu zote mbili (Yohane 14:15, 21 na Yohane 13:34, amri mpya), neno lililotumika ni Agapē. Huu sio upendo tu, ni maamuzi thabiti. Sio upendo wa hisia (Eros) au wa kirafiki na kindugu tu (Philia), bali ni upendo unaotafuta, kuyatii na kutimiza daima mapenzi kwa hiari. Ndio upendo huu walipaswa kuwa nao Mitume kwa Kristo, kumwamini Kristo kwamba alitumwa na Baba, na kumfuata kwa Utayari na utii. Ingawa walishindwa kwa wakati ule walipokuwa na Yesu, lakini baadaye waliimarishwa na Roho Mtakatifu na wakatoka wakiwa wapya kabisa. Ndugu mpendwa, hakuna namna yoyote tunaweza kusema tunampenda Kristo kama hatuzishiki na kuzifuata amri zake. Kumpenda Kristo kwanza kabisa ni kumwamini kwamba alitoka kwa Baba. Na kumwamini huku ni kujitoa katika Utayari wa kweli wa moyo, roho, nguvu na akili katika kuzishika amri zake. Amri aliyotupa ni amri kuu ya mapendo, kumpenda Mungu na kupendana sisi kwa sisi kama Kristo mwenyewe alivyotupenda sisi, akajitoa uhai wake kwa ajili yetu sisi kondoo wake. Katika Dominika ya leo ni wakati kila mmoja anapata nafasi ya kutafakari, Je, Upendo wangu kwa Mungu na kwa wengine upoje, nina upendo wa namna gani?  Huenda ninampenda Mungu kwa kuwa amenibariki, lakini yajapo majaribu na magumu, ninamsahau kabisa Mungu wangu. Huenda ninampenda Mungu kwa kuwa mambo yangu yapo shwari, ila ijapo misukosuko, hofu, mitihani namwona Mungu kama ni mdogo kuliko changamoto na mitihani yangu. Ninatamani kupendwa na Mungu, lakini wakati huo huo mimi sina upendo kwa dhat kwa wengine. Huenda ninasema kwa mdomo tu kwamba ninampenda Mungu, au ninawapenda wengine lakini katika uhalisia wa maisha yangu halionekani lolote. Mara nyingi pia tunatii amri za Mungu pale tunapoona zina maslahi kwetu. Kristo Yesu anatukumbusha kuwa kumpenda yeye ni kutii hata pale amri zake zinapokwenda kinyume na matakwa, tabia na mitazamo yetu, kupenda bila kikomo hata maadui zetu, kusaheme bila mipaka hata waliotuumiza, kusema ukweli hata kama itakugharimu, kutetea haki hata kama itahatarisha maslahi yangu, kusimamia imani yangu hata kama itanidai sadaka kubwa. Peke yetu hatuwezi, ndio sababu tunamhitaji Roho Mtakatifu.

Kristo yuko kati ya waja wake kwa njia ya Roho wake Mtakatifu
Kristo yuko kati ya waja wake kwa njia ya Roho wake Mtakatifu   (@Vatican Media)

Fundisho la Pili: Kristo anatuahidi zawadi ya Roho Mtakatifu, Msaidizi, ndiye Roho wa Ukweli, amefunua kwetu Fumbo la Utatu Mtakatifu. Sehemu ya pili ya Injili hii (Yohane 14:16-17) inahusu Ahadi ya Roho Mtakatifu kama Msaidizi wa Kudumu. Hapa ndipo Yesu anapofunua kwetu jinsi gani waamini watakavyoweza kuishi yale maisha ya utii na upendo aliyoyataja katika aya ya 15 na aya ya 21. Katika lugha ya Kigiriki, lugha asili ya Agano jipya, Neno hili Msaidizi, twaweza kulielewa kwa maana pana zaidi. Yesu anasema atatupa msaidizi mwingine, kwa kigiriki, Allos Parakletos. Neno “Allos” linamaanisha msaidizi wa aina ile ile kama yeye. Roho Mtakatifu ataendeleza kazi ilele aliyoianzisha Kristo hapa duniani kwa namna mpya, sasa ikiendelezwa na mitume ambao ndio Kanisa la mwanzo. Na hapa tunaona kwa namna fulani Fumbo la Utatu Mtakatifu likifunuliwa kwetu na Kristo. Neno hili Paraclete lina maana ya Msaidizi, Mtetezi (kama alivyo wakili mahakamani), Mfariji, au Mshauri anayesimama daima upande wetu. Tofauti na uwepo wa Yesu wa kimwili ambao ulikuwa na ukomo wa muda na mahali, Roho Mtakatifu anaahidiwa kukaa na kanisa na sisi waamini milele. Hakuna wakati ambapo mwamini atatengwa na uwepo huu wa Roho Mtakatifu. Anaitwa “Roho wa Kweli” kwa sababu anafunua ukweli wa Mungu na kumuongoza mwamini kuona mambo jinsi yalivyo kwa jicho la Kimungu. Ulimwengu (mfumo wa maisha uliotengwa na Mungu) hauwezi kumpokea kwa sababu ulimwengu unategemea macho ya nyama (kuona), wakati Roho anatambuliwa kwa macho ya imani (kujua). Ni baada ya Pentekoste Kristo anatimiza Ahadi hii, hakuwaacha yatima, aliwaletea Msaidizi. Ndugu mpendwa, ni dhahiri kwamba hatuwezi kuzishika amri za Yesu (Aya ya 15) kwa akili na nguvu zetu tu sisi wenyewe. Roho Mtakatifu ndiye anayetupa hamu na uwezo wa kutenda kadiri ya amri za Mungu. Yeye tunaweza kusema ndiye ndiye injini ya maisha yetu ya kiroho. Kumbe katika Dominika hii tunajifunza kuwa ili kumsikia na kumtambua Roho Mtakatifu, ni lazima kwanza tujitofautishe na ulimwengu. Ulimwengu una kelele nyingi; tunajifunza kutafuta utulivu wa ndani ili kumtambua huyu mgeni wa ajabu anayekaa ndani yetu, Roho wa ukweli, Roho Mfariji. Katika ulimwengu huu uliotawaliwa na mafundisho mengi ya uwongo, walimu wengi wa kupotosha ukweli wa Injili, tunahitaji sana nguvu ya Roho Mtakatifu. Ulimwengu ambapo shetani anafanya kazi katika kivuli cha elimu, Injili ya mafanikio, utajiri, maarifa, maendeleo, Hekima ya kidunia, sayansi na technolojia, tunahitaji Roho Mtakatifu atusaidie katika kung’amua yale yaliyo ya Kimungu katikati ya msongamano wa mambo mengi ya ulimwengu huu, kuyashika, kuyaamini, kuyaishi, kuyashuhudia na kuyafundisha yale ya Kimungu bila woga.

Mwaliko kwa waamini kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu
Mwaliko kwa waamini kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu   (@Vatican Media)

Fundisho la Tatu: Roho Mtakatifu anatuondolea hofu, huzuni na upweke. Yesu hakutuacha Yatima bali anaendelea bado kuwa kati yetu. Sehemu ya tatu (Yohane 14:18-20) inahusu Uwepo wa daima wa Kristo aliyefufuka kupitia Roho Mtakatifu aliyewashuka Mitume siku ya Pentekoste. Hapa Yesu anafafanua kuwa kuondoka kwake kimwili si mwisho wa uhusiano wao, bali ni mwanzo wa aina mpya na ya ndani zaidi ya uwepo wake. Anawaambia maneno haya ya faraja, “Sitawaacha ninyi Yatima, naja kwenu” Katika utamaduni wa wakati huo, yatima hakuwa tu mtoto aliyefiwa na wazazi, bali pia mwanafunzi aliyempoteza mwalimu wake (Rabi), akibaki bila ulinzi, mafundisho, wala utambulisho. Yesu anatumia neno hili kuondoa hofu ya wanafunzi ya kubaki pweke atakapoondoka kwao. Anaposema “naja kwenu,” hamaanishi tu kurudi kwake mwisho wa dunia, bali anamaanisha kuja kwake baada ya ufufuko, na kuja kwake kupitia Roho Mtakatifu siku ya Pentekoste. Yesu anautofautisha ulimwengu (ambao utamwona kama mfu aliyeshindwa baada ya mateso na kifo chake) na waamini (watakaomwona kama mshindi aliyefufuka). Kristo anaendela kuwaambia, katika aya ya 19, “Na kwa sababu mimi ni hai, ninyi nanyi mtakuwa hai” kumbe, Uzima wetu wa kiroho unategemea uzima wake; tukiungana naye, tunashiriki uzima usio na mwisho ambao hata mauti haiwezi kuugusa. Haya yote ni matokeo ya uwepo wa Roho Mtakatifu ambaye Mitume walimpokea siku ile, yaani siku ya pentekoste nasi sote tukishirikishwa katika ubatizo wetu.  Ni kwa njia ya ubatizo nasi tumepokea Ahadi hii ya Kristo ya kuishi milele. Kifo na mauti havina nguvu tena. Ndugu mpendwa, katika safari yetu ya maisha, katika mapambano yetu ya kila siku kuna nyakati nasi tunahisi upweke kwa sababu mbalimbali. Katika hali hiyo, Kristo anatupa moyo kwamba, haupo peke yako. Tunajifunza kuwa hatupo peke yetu katika mapambano ya maisha. Unapojisikia kutelekezwa na marafiki, ndugu, jamaa hasa nyakati za shida, misiba, magonjwa, Ahadi hii ya Yesu inatupa matumaini mapya kabisa ya ndani. Kil ambatizwa anao wajibu wa kuwa Nabii, kuhani na Mfalme katika ulimwengu huu unaoonekana kuwa yatima katika Nyanja mbalimbali. Kuwa Nabii ni kufundisha Neno la Mungu, kuonya, kukemea. Katika ulimwengu ambapo kumekua na mmomonyoko mkubwa wa maadili, tunaalkwa kuwa walimu thabiti wa Imani. Tunaitwa kuwa makuhani, kujitoa sadaka kwa wengine, kumdhihirisha Kristo kwa nafsi zinazoteseka, waliojikatia tamaa na kuona hawana thamani tena. Kwa njia ya Roho Mtakatifu tunakuwa wafalme, kuongoza wengine kumjua Kristo na kuujua ukweli wa Injili. Kristo anatutumia mimi na wewe, kudhihirisha uwepo wake wa kudumu katika ulimwengu huu.

Roho Mtakatifu ni Mfariji wa kweli
Roho Mtakatifu ni Mfariji wa kweli   (@Vatican Media)

Somo la 1: Ni kitabu cha Matendo ya Mitume 8:5-8, 14-17. Fundisho la Nne: Mateso na magumu yasiturudishe nyuma katika kutenda mema, katika kuishuhudia imani yetu. Somo la kwanza kutoka katika kitabu hiki cha Matendo ya Mitume 8:5-8, 14-17 ni matokeo ya utimilifu wa Ahadi ile ya Kristo aliyowaahidi mitume wake, Ahadi ya Roho Mtakatifu. Baada ya Pentekoste, mitume walianza kuhubiri Injili kwanza kule Yerusalemu. Baada ya kuteswa na kuuwawa kwa Stephano, mambo yalianza kubadilika. Waumini wa Kanisa la Mwanzo walianza kupitia mateso mengi na madhulumu kwa sababu ya imani yao. Lakini badala ya mateso haya kudhoofisha na kuua kanisa, yalisababisha waamini kutawanyika, na hivyo kupeleka Injili mbali zaidi. Mateso hayakuwa ishara ya kushindwa bali neema ya kuitangaza zaidi Injili ya Kristo hata katika maneo yaliyokuwa hayana thamani kama samaria. Ndugu mpendwa, sisi pia tumepokea zawadi ya Roho Mtakatifu kwanza kabisa katika ubatizo wetu, na kisha tukaimarishwa katika utimilifu wa mapaji hayo katika sakramenti ya Kipaimara. Tunaendelea kuimarishwa kila siku kwa neno la Kristo na kwa sakramenti ili tuendelee kuwa thabiti na wenye nguvu na ari ya kuitangaza Injili. Nguvu hii ya Kristo iliyo ndani mwetu ndio inayotufanya kuendelea kuamini na kutumaini licha ya magumu, maumivu, machozi, hatupaswi kurudi nyuma. Tunapoingia kwenye matatizo au kupitia changamoto fulani, hata ziwe kubwa namna gani, mfano kufukuzwa kazini, kudhulumiwa mali, kupoteza wapenddwa wetu, kuvunjika moyo, kusingiziwa mabaya nk, somo hili linatufundisha daima kutokukata tamaa. Mungu anaweza kuwa anatumia misukosuko na nyakati hizo ngumu katika maisha yetu kutupeleka mahali ambapo tunahitajika zaidi. Badala ya kulia, kalaumu, kujilaani, na kunung’unika, simama kwa nguvu ya Roho Mtakatifu, na mshukuru Mungu kwamba amependa akuchague ili uwe ushuhuda wa uwepo wake kati ya watu.

Imani ni zawadi kutoka kwa Mungu
Imani ni zawadi kutoka kwa Mungu   (@Vatican Media)

Fundisho la tano: Mwenyezi Mungu anaithibitisha zawadi ya imani ndani mwetu ili maisha yetu yawe chachu ya kuleta uponyaji na furaha katika maisha ya wengine. Katika somo hili tumemsikia Filipo anafanya ishara zilezile alizofanya Yesu, kutoa pepo na kuponya viwete (Mdo 8:7). Hii inaonyesha kuwa Roho Mtakatifu aliendelea kufanya kazi ndani ya Filipo kwa uwezo ule ule wa Yesu. Wasamaria walikuwa wamebatizwa (muungano wa nje), lakini walihitaji kupokea Roho (muungano wa ndani kabisa). Kupitia Petro na Yohane, muungano huo unakamilika, na Wasamaria wanakuwa sehemu kamili ya mwili wa Kristo, licha ya kwamba hapo mwazo walikua hawachangamani kabisa na wayahudi. Matokeo ya kuhubiriwa kwa Kristo na ujio wa Roho huko Samaria ni furaha kuu katika mji ule (Mdo 8:8). Furaha hii ni uthibitisho kwamba uwepo wa Msaidizi huondoa huzuni na upweke wa uyatima na kuleta uzima mpya. Je, Mimi nikifika mahali ninaleta furaha au ninaleta migogoro? Kazini kwangu, kwenye jumuiya yangu, kanisani, kwenye biashara zangu, ninaihubirije Injili kwa njia ya matendo yangu? Mitume hawa wanatenda miujiza mikubwa kwa njia ya nguvu ya Kristo iliyokuwa ndani mwao. Kama nilivyotangulia kusema, Kristo anatenda kazi kubwa katika maisha ya wengine kupitia Roho Mtakatifu aliye ndani mwetu. Roho Mtakatifu anatupa nguvu ya kupenda, anatupa nguvu ya kuhurumia, anatupa nguvu ya kufariji wengine, anatupa nguvu ya kusamehe, anatupa nguvu ya kujali. Pengine tunaweza kuwaza miujiza mikubwa kama hii waliofanya mitume, na kusahau kuwa hata tendo dogo lolote tunalolitenda kwa upendo mkubwa ni muujiza mkubwa sana kwa wengine. Wapo watu wenye shida nyingi kati kati yetu, maskini, yatima, walemavu, wajane, watoto wa mitaani nk. Tunapowasadia hao tumetenda muujiza mkubwa sana kwao. Maisha ya kila siku pale nilipo yanatufundisha kuwa mkristo wa kweli ni yule anayesaidia kupunguza mizigo ya wengine (kama Filipo alivyoponya viwete) na kuacha tabasamu mioyoni mwa watu. Tumwombe Mungu atupe nguvu ya kuwa sehemu na sababu ya amani na furaha kwa wengine, na tusishiriki hata mara moja kuwa chanzo cha vilio na maombolezo kwa wengine, kwa maneno, kwa mawazo au hata kwa matendo yetu. Tuwe sehemu ya kuleta mapatano na amani, palipo na ugomvi chuki.

Waamini wanaitwa na kutumwa kuwa ni mashuhuda wa Kristo Yesu
Waamini wanaitwa na kutumwa kuwa ni mashuhuda wa Kristo Yesu   (@Vatican Media)

Somo la Pili: Ni Waraka 1 Pet 3:15-18. Fundisho la sita: Roho Mtakatifu anatusaidia kuishuhudia imani katika upole na busara. Katika somo hili la pili, mtume Petro anatueleza kuwa kuna ugumu mwingi katika kumfuata Yesu. Tukumbuke barua hii Mtume Petro aliiandika kwa Wakristo waliokuwa wakipitia mateso na madhulumu katika mazingira ya kikatili ya dola ya Kirumi, ambapo imani yao ilionekana kama usaliti na ujinga. Watu walikuwa wakiwahoji na kuwacheka Wakristo hawa hasa kuhusu tumaini lao la uzima wa milele na Kristo aliyesulubiwa. Licha ya hayo, Mtume Petro anawasihi kutokurudi nyuma, kwa kuwa hayo ndiyo mapenzi ya Mungu. Zaidi sana walipaswa kuwa tayari daima kumjibu kila mtu awalizaye habari za tumaini hilo kubwa lililokuwa ndani mwao. Ndugu mpendwa, Mtume Petro anaongea nasi tulio wafuasi wa Kristo katika ulimwengu wa leo. Tunaishi kwenye jamii ambapo watu waweza kutucheka na kutudhihaki kwa sababu ya misingi ya imani yetu. Tunaishi kwenye ulimwengu ambapo, uovu mwingi umehalalishwa na pengine watu waweza kuwashangaa wale ambao wanaenda kinyume na mitazamo hiyo ya kidunia kwa sababu inapingana na misingi ya imani yao. Je, ni mara ngapi nimesimama kwenye msingi wa imani yangu hata pale nilipodhihakiwa? Mara kadhaa tunaweza kuulizwa maswali magumu yahusuyo imani yetu, twapaswa kufahamu undani wa mafundisho yetu, na sababu kwa nini tunaamini. Tunapaswa kusimama imara kuilinda, kuithamini na kuitetea imani yetu, sio kwa mabishano na mashindano bali kwa ushuhuda wa maisha. Wakristo hawa walikua wakiteseka lakini watu walishangaa kwa nini waliendelea bado kubaki katika tumaini, ingawa pia wapo wengine waliorudi nyuma. Kumbe na sisi tunapaswa kuishi maisha ya mfano, maisha ya ufuasi wa kweli kwa Kristo, na kwa njia hiyo tutauthibitishia ulimwengu tumaini thabiti lililo ndani mwetu, yaani Kristo Mfufuka. Hitimisho. Katika Dominika hii, tunaalikwa kufungua mioyo yetu ili Roho huyo wa Kweli atufanye kuwa mashahidi hodari wa Kristo aliyefufuka, kama anavyotuambia mtume Petro, “kuwa tayari siku zote kumjibu kila mtu atuulizaye Habari la tumaini hilo la ufufuko wa Kristo lililo ndani mwetu, kwa upole na kwa hofu.”

Tafakari D6 Pasaka Mwaka A
09 Mei 2026, 17:39