Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya Sita ya Kipindi cha B wa Kanisa: Roho Mtakatifu katika maisha na utume wa Kanisa Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya Sita ya Kipindi cha B wa Kanisa: Roho Mtakatifu katika maisha na utume wa Kanisa  (@VATICAN MEDIA)

Tafakari Dominika ya Sita Mwaka A wa Kanisa: Roho Mtakatifu Na Utume wa Kanisa

Ujumbe mkuu ni wa matumaini kwani Yesu anatuahadi zawadi ya msaidizi, Roho Mtakatifu, ndiye mleta uzima, Roho Muumbaji chanzo cha kila jema (Liturujia ya Kibizantino), Roho wa ukweli anayetuongoza katika kweli yote (KKK 291). Ni katika tumaini hili wimbo wa mwanzo unatualika kuuhubiri wokovu kwa sauti ya kuimba, ukisema; “Hubirini kwa sauti ya kuimba, tangazeni haya yatamkeni mpaka mwisho wa dunia, semeni, Bwana amelikomboa taifa lake!

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, Dominika ya 6 ya Kipindi cha Pasaka Mwaka A wa kiliturujia katika Kanisa. Ilikuwa ni tarehe 8 Mei 2025 Baba Mtakatifu Leo XIV alipokabidhiwa dhamana ya: Kuongoza, Kufundisha na Kuwatakatifuza watu wa Mungu kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, Siku ya Sala maalum kwa ajili ya Bikira Maria wa Pompei. Kumbe, hija hii ya kitume inapania pamoja na mambo mengine, kuiweka huduma na utume wa kichungaji unaotekelezwa naye kama Khalifa wa Mtakatifu Petro chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria wa Pompei na kwamba, katika maisha na utume wake, anaendelea kufuata nyayo za Papa Leo XIII, ambaye pamoja na mambo mengine, ni Kiongozi wa Kanisa aliyejibidiisha kuweka msingi wa Mamlaka fundishi ya Kanisa yaani “Magisterium” kuhusu Rozari Takatifu pamoja na yeye mwenyewe kumtangaza Mwenyeheri Bartolo Longo, Mtume wa Rozari Takatifu kuwa ni Mtakatifu.Ujumbe mkuu ni wa matumaini kwani Kristo Yesu anatuahadi zawadi ya msaidizi, Roho Mtakatifu, ndiye mleta uzima (Kanuni ya Nikea-Konstantinopoli), Roho Muumbaji (Uje Roho Muumbaji), chanzo cha kila jema (Liturujia ya Kibizantino), Roho wa ukweli anayetuongoza katika kweli yote (KKK 291). Ni katika tumaini hili wimbo wa mwanzo unatualika kuuhubiri wokovu kwa sauti ya kuimba, ukisema; “Hubirini kwa sauti ya kuimba, tangazeni haya yatamkeni mpaka mwisho wa dunia, semeni, Bwana amelikomboa taifa lake, aleluya (Isa. 48:20). Na Mama Kanisa katika sala ya mwanzo anasali; “Ee Mungu Mwenyezi, utuwezeshe kuadhimisha kwa bidii siku hizi za furaha, tunazozitumaini kwa heshima ya Bwana aliyefufuka. Na hayo tunayoyakumbuka sasa, tuyazingatie daima kwa matendo.”

Uwepo wa Roho Mtakatifu katika maisha na utume wa Kanisa
Uwepo wa Roho Mtakatifu katika maisha na utume wa Kanisa   (@Vatican Media)

Somo la kwanza ni la kitabu cha Matendo ya Mitume (Mdo. 8: 5-8, 14-17). Linatueleza matokeo ya kifo dini cha Stefano, shemasi, kuwa madhulumu na mateso makali kwa wakristo yalishika kasi Yerusalemu. Hali hii iliwafanya wengine kukimbia na kwenda maeneo mbali mbali. Habari njema ni kuwa, popote walipofika waliendelea kuitangaza habari njema ya wokovu, kuwa Bwana amefufuka kweli aleluya. Filipo, mmoja wa mashemasi, alikimbilia Samaria akawahubiria wasamaria nao wakasikiliza maneno yake, na kuziona ishara alizozifanya, pepo wachafu kuwatoka waliopagawa wakilia kwa sauti kuu; na watu wengi waliopooza, na viwete, kuponywa. Ikawa furaha kubwa katika mji ule, wengi wakaipokea imani na kubatizwa. Habari hizi zilipowafika mitume Yerusalemu, waliwatuma Petro na Yohane kwenda kuwaimarisha wakristo wasamaria. Nao walipofika, waliwaombea na kuwawekea mikono nao wakampokea Roho Mtakatifu wakamsifu na kumtukuza Mungu kwa shangwe. Ni katika muktadha huu, Kateksimu ya Kanisa Katoliki namba 1241 na 1299 ikinukuu maandiko matakatifu inafundisha hivi; Katika adhimisho la Sakramenti ya kipaimara Askofu huweka mikono juu ya waimarishwa, kitendo ambacho tangu nyakati za mitume ni ishara ya kipaji cha Roho Mtakatifu, Roho mfariji, Roho wa hekima na akili, Roho wa ushauri na nguvu, Roho wa elimu na ibada, Roho wa uchaji kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

Roho Mtakatifu anatenda kazi ndani ya Kanisa
Roho Mtakatifu anatenda kazi ndani ya Kanisa   (@Vatican Media)

Na mpako wa Krisma Takatifu, mafuta yaliyotiwa manukato na kuwekwa wakfu na askofu, huashiria paji la Roho Mtakatifu kwa mbatizwa mpya kuwa amekuwa Mkristo, yaani mpakwa na Roho Mtakatifu, ameingizwa katika Kristo, ambaye amepakwa kama kuhani, nabii na mfalme. Hivyo “Ubatizo hautakasi tu dhambi, bali pia humfanya mbatizwa kiumbe kipya, humfanya mwana wa Mungu, aliyefanywa mshirika wa tabia ya uungu kiungo cha Kristo, mrithi pamoja na Kristo, hekalu la Roho Mtakatifu” (KKK 1265). Haya ndiyo makuu ya Mungu yanayoimbwa katika zaburi ya wimbo wa katikati ikisema; “Mpigieni Mungu kelele za shangwe, nchi yote. Imbeni utukufu wa jina lake, tukuzeni sifa zake. Mwambieni Mungu, Matendo yako yanatisha kama nini! Nchi yote itakusujudia na kukuimbia, naam, italiimbia jina lako. Njoni yatazameni matendo ya Mungu; Hutisha kwa mambo awatendayo wanadamu. Aligeuza bahari ikawa nchi kavu; katika mto walivuka kwa miguu; Huko ndiko tulikofurahia, atawala kwa uweza wake milele. Njoni, sikieni ninyi nyote mnaomcha Mungu, nami nitayatangaza aliyonitendea roho yangu. Na ahimidiwe Mungu asiyeyakataa maombi yangu, wala kuniondolea fadhili zake” (Zab. 66:1-7, 16, 20).

Roho Mtakatifu ni chanzo cha Umoja, Upendo na udugu wa kibinadamu
Roho Mtakatifu ni chanzo cha Umoja, Upendo na udugu wa kibinadamu   (@Vatican Media)

Somo la pili ni kutoka katika Waraka wa Mtume Petro kwa Watu Wote (1Pet. 3:15-18). Ni ujumbe wa kuwatia moyo wakristo waliokuwa katika mateso na madhulumu kwa sababu ya imani yao akiwaasa watambue kuwa Kristo yupo pamoja nao, yupo ndani yao kwa njia ya roho wake akiwaimarisha. Zaidi sana madhulumu haya hayaelekezwi kwao tu bali pia kwa Kristo mwenyewe. Hivyo wanapaswa kuyapokea kwa imani kwa ajili ya Kristo ili yawe njia ya kuupata utukufu. Zaidi sana wasilipe ovu kwa ovu bali wawatendee wema watesi wao kwa upole na upendo, kwa uweza wa Roho Mtakatifu. Mtume Petro anasema hivi; “Muwe tayari siku zote kumjibu kila mtu awaulizaye habari za tumaini lililo ndani yenu, kwa upole na kwa hofu. Nanyi muwe na dhamiri njema, ili katika neno lile mnalosingiziwa, watahayarishwe wale wautukanao mwenendo wenu mwema katika Kristo. Maana ni afadhali kuteswa kwa kutenda mema, ikiwa ndiyo mapenzi ya Mungu, kuliko kwa kutenda mabaya. Kwa maana Kristo naye aliteswa mara moja kwa ajili ya dhambi, mwenye haki kwa ajili yao wasio haki, ili atulete kwa Mungu; mwili wake akauawa, bali roho yake akahuishwa”. Ujumbe kwetu, tutoe ushuhuda wa imani na wa matumaini kwa njia ya maisha mema na ukarimu kwa watu wote hata kwa adui zetu, hata kwa wanaotudhulumu. Hii itawasaidia nao wautambue ukweli wa Injili ili nao waweze kumpokea Kristo na kuongoka. Zaidi sana kuchukulia mateso kwa ajili ya Yesu kama baraka; kukubali kuteseka kwa ajili ya haki kama alivyoteseka Yeye kwa ajili yetu. Maana tukishiriki mateso yake tutashiriki pia utukufu wake.

Roho Mtakatofu ni chanzo cha mema yote
Roho Mtakatofu ni chanzo cha mema yote   (@Vatican Media)

Injili ni ilivyoandikwa na Yohane (Yn. 14:15-21). Ni wosia wa Yesu kwa wanafunzi wake katika karamu ya mwisho, Alhamisi Kuu, kabla ya kukamatwa, kuhukumiwa, kuteswa na kufa Msalabani. Kwanza kabisa ni mwaliko wa kumpenda Yeye na kuzishika amri zake. Matunda ya kumpenda Yesu na kuzishika amri zake ni Yeye kumwomba Mungu Baba atupe Msaidizi mwingine, Roho Mtakatifu ili akae nasi, Roho wa kweli ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea. Sisi tunampokea na kumtambua, kwa maana anakaa ndani kwetu, kwa kuwa kwa ubatizo tumekubali kuwa wana wa Mungu na hekalu la Roho Mtakatifu. Katekisimu ya Kanisa Katoliki inatufundisha hivi; “Kristo ni hekalu la kweli la Mungu, mahali ambapo hukaa utukufu wake; kwa njia ya neema ya Mungu hata Wakristo huwa hekalu la Roho Mtakatifu, mawe hai ambayo kwayo hujengwa Kanisa” (KKK 1197). Kristo Yesu anatufariji na kututia moyo wa matumaini akisema; “Mioyo yenu isifadhaike”, “sitawaacha yatima, naja kwenu”. Kristo yupo pamoja nasi katika Neno lake na sakramenti zake kwa njia ya Roho Mtakatifu, nasi tunamuona kwa macho ya kiimani tukiwa ndani yake, naye ndani yetu.

Muujiza wa nguvu ya upendo
Muujiza wa nguvu ya upendo   (@Vatican Media)

Huu ndio muujiza wa nguvu ya upendo kwa maana Kristo anasema; “Naye anipendaye atapendwa na Baba yangu, nami nitampenda na kujidhihirisha kwake”. Ndiyo maana Katekismu ya Kanisa Katoliki inafundisha hivi; “Kanisa haliachi kumpa Baba matoleo ya zawadi zake na kumsihi amlete Roho Mtakatifu juu ya matoleo, juu yake lenyewe, juu ya waamini wake na juu ya ulimwengu wote, ili, kwa kushiriki kifo na ufufuko wa Kristo Kuhani, na kwa nguvu ya Roho Mtakatifu, baraka hizi za kimungu zilete matunda ya uzima wa milele kwa sifa na utukufu wa neema yake” (KKK 1083). Ni katika tumaini hili mama Kanisa katika sala baada ya komunyo anasali; “Ee Mungu Mwenyezi wa milele, wewe watuponya kwa kufufuka kwake Kristo ili tupate uzima wa milele. Utuzidishie neema za fumbo la Paska, na kutujaza mioyoni mwetu nguvu ya chakula hiki cha wokovu”. Tumsifu Yesu Kristo. 

Tafakari D6 Pasaka
09 Mei 2026, 16:17