2026.05.06 Maaskofu katika maandamano ya amani katika Jimbo la  Lira nchini Uganda. 2026.05.06 Maaskofu katika maandamano ya amani katika Jimbo la Lira nchini Uganda.  (©Diocese of Lira)

Maaskofu Kaskazini mwa Uganda watoa wito wa amani katika eneo hilo!

Maaskofu Katoliki wa Kaskazini mwa Uganda wamekusanyika katika Jimbo la Lira,kuanzia tarehe 3 Mei hadi 8,ili kuadhimisha kumbukumbu ya miaka 20 katika "Juma la Maombi na Amani,"mpango wa kichungaji uliozinduliwa mwaka 2006 kushughulikia changamoto za baada ya migogoro kufuatia uasi katika eneo hilo,ambao uliongozwa na Joseph Kony na waasi maarufu wa LRA.

Padre  Isaac Ojok – Jiji la Lira, Uganda.

Askofu Mkuu Raphael P’Mony Wokorach, MCCJ, wa Jimbo Kuu la Gulu; Askofu Mkuu Mstaafu John Baptist Odama; Askofu Sanctus Lino Wanok wa Jimbo la Lira; Askofu Sabino Ochan Odoki wa Jimbo la Arua; Askofu Constantine Rupiny wa Jimbo la Nebbi; Askofu Dominic Eibu wa Jimbo la Kotido; na Askofu Mstaafu Joseph Franzelli wa Jimbo la Lira, ni Maaskofu Katoliki wa Kaskazini mwa Uganda ambao walikusanyika katika Jimbo la Lira, tangu  tarehe 3 Mei hadi 8,ili kuadhimisha kumbukumbu ya miaka 20 katika muktadha wa  "Juma la Maombi na Amani," ambao ni mpango wa kichungaji wa kila mwaka uliozinduliwa mwaka 2006 kushughulikia changamoto za baada ya migogoro kufuatia uasi katika eneo hilo, ambao uliongozwa na Joseph Kony na waasi maarufu wa LRA.

Maaskofu wa Kaskazini mwa Uganda kushiriki Juma la Maombi kwa ajili ya amani
Maaskofu wa Kaskazini mwa Uganda kushiriki Juma la Maombi kwa ajili ya amani   (©Diocese of Lira)

Kuhamasisha upatanisho

Ukumbusho huo kuanzia tarehe 3 hadi tarehe 8, kwa njia hiyo huandaliwa kila mwaka katika Jimbo la Kikanisa la Gulu Kaskazini mwa Uganda.  Tukio hili la Juma nzima linahamasisha uponyaji, upatanisho, na amani ya kudumu kufuatia mzozo wa Jeshi la Upinzani la Lord’s Resistance Army (LRA)  uliongozwa na Joseph Kony na waasi maarufu wa LRA kunako 2006. Kaulimbiu ya mwaka 2026 ni : “Amani iwe nanyi” (Yh 20:19). Washiriki kutoka Majimbo ya Gulu, Arua, Nebbi, Lira, na Kotido, wakiwemo mapadre, viongozi wa kidini, mamlaka za kiraia, na waamini walei, wameshiriki katika maandamano ya amani kupitia Jiji la Lira, wakiashiria umoja na kujitolea kwa pamoja kwa upatanisho.

Msamaha na mazungumzo

Wakati wa kuadhimisha Misa Takatifu, Askofu Sanctus Lino Wanok, ambaye ni Askofu wa Jimbo la Lira, alisisitiza kwamba amani ni zawadi ndani ya kila mtu na aliwataka waamini kukumbatia uponyaji, msamaha, na mazungumzo. “Amani hustawi pale watu wanaposikilizwa, na hukua pale utu unapoheshimiwa,” alisema. Alizitaka jamii kushinda mgawanyiko, chuki, na kutoaminiana, huku pia akitoa wito wa uadilifu katika uongozi na kuhimiza kukataliwa kwa ukabila, ufisadi, na unyonyaji. Katika ujumbe wa pamoja, Maaskofu walizitaka jamii kuendelea kujitolea kukuza amani, wakipata msukumo kutoka kwa Mtakatifu Paulo katika Matendo ya Mitume, ambaye alibaki imara katika utume wake licha ya mateso.

Askofu Mkuu mstaafu Odama kuhamasisha mazungumzo

Askofu Dominic Eibu, MCCJ, wa Jimbo la Kotido, alimpongeza Askofu Mkuu Mstaafu John Baptist Odama kwa juhudi za kukuza amani Kaskazini mwa Uganda. Alikumbuka kujitolea kwa Askofu Mkuu kwa mazungumzo, ikiwa ni pamoja na kuwafikia kwa ujasiri viongozi wa Jeshi la Upinzani la Lord's Resistance. Aliwahimiza waamini kuiga kujitolea huko. Askofu Eibu aliwasihi wakristo kutafuta amani kikamilifu na kushiriki ushuhuda wa kibinafsi ambao unaweza kuwatia moyo wengine kuponya na kuishi kwa amani. Aliwataka washiriki kupeleka ujumbe wa amani kwa jamii zao. "Tunaporudi nyumbani, turudi na vitendo ambavyo vitaacha athari chanya katika maisha yetu na jamii zetu," alisema. Aliwapongeza zaidi watu wa Jimbo la Lira kwa ukarimu wao mwema kwa wageni kutoka majimbo mengune ya Kikanisa.

Mateso yanayodumu yaliyosababishwa na LRA

Jeshi la Upinzani la Lord's Resistance Army (LRA), uasi ulioongozwa na Joseph Kony, ulifikia kilele mwishoni mwa miaka ya 1980 kabla ya kuenea katika eneo lote la Afrika ya Kati. Kony na LRA walianzisha mzozo mbaya wa waasi Kaskazini mwa Uganda. Ingawa kundi hilo bado lipo, halitoi tena tishio kubwa kwa Uganda; linasalia kama kikosi dhaifu cha waasi katika nchi za Afrika ya Kati jirani na Uganda. Katika kilele cha vita vyake vya waasi, LRA ilisababisha mateso makubwa ya kibinadamu ambayo yanaendelea kuathiri watu wa Kaskazini mwa Uganda hadi leo hii. Wengi bado wanapona kutokana na kiwewe cha miaka hiyo. Kwa sababu hiyo, "Juma la Maombi na Amani" lina umuhimu mkubwa kwa sehemu hii ya Uganda. Joseph Kony ainaaminika kuwa bado yuko hai na kwa ujumla. Ameepuka kukamatwa kwa zaidi ya miongo miwili.

Imesasishwa Alhamisi tarehe 7 Aprili 2026, saa 5.11 asubuhi na Sr Christine Masivo

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here.

07 Mei 2026, 11:16