Siku ya Tatu Afrika:Kutoka Algeria hadi Cameroon
Na Claudia Torres – Yaoundé, Cameroon.
Papa Leo XIV alihitimisha awamu ya kwanza ya Ziara ya Kitume ya nchi nne kwa hafla ya kuaga katika Uwanja wa Ndege huko Algiers Jumatano asubuhi, tarehe 15 Aprili 2026. Ndani ya ndege ya Papa akiwa njiani kuelekea Cameroon, alielezea kukaa kwake katika nchi ya Mtakatifu Agostino kama "baraka maalum," na alitoa shukrani kwa "fursa nzuri ya kuendelea kujenga madaraja na kukuza mazungumzo."
Makaribisho mema
Baada ya masaa tano, Baba Mtakatifu aliwasili Yaoundé, mji mkuu wa Cameroon, ambapo utofauti mkubwa wa kiutamaduni na lugha ya taifa hilo la Afrika ya Kati ulikuwa wazi. Umati mkubwa wa watu ulimsubiri uwanjani, wakipunga bendera za Vatican na Cameroon na kupaza sauti kwa maneno ya kumkaribisha Papa kwa Kiingereza, Kifaransa na wakati mwingine 'Buonasera' katika lugha ya Kiitaliano ilisikika.
Watu walikusanyika kando ya sehemu kubwa ya barabara, wakimkaribisha Baba Mtakatifu kutoka uwanja wa ndege hadi ikulu ya rais, mavazi yao ya rangi yakipendeza na mandhari ya kijani kibichi ya jiji hilo lenye rutuba. Walishangilia, wakiimba, na kucheza kwa sauti za mdundo wa vyombo vya ngoma na shaba, wakionesha furaha yao kubwa ya kuridhisha na kupunguza uchovu baada ya safari ndefu ya kuchosha.
Kukutana na mamlaka
Nguvu hiyo ilikuwa dhahiri vile vile katika Ikulu ya Rais, ambapo Baba Mtakatifu alikutana faragha na Rais wa nchi hiyo, Paul Biya, kabla ya kuhutubia mamlaka ya nchi, wajumbe wa asasi za kiraia, na kikosi cha kidiplomasia. Walipiga makofi mara kadhaa wakati wa hotuba ya Papa Leo XIV. Alitetea haki za wanawake na kutoa wito wa amani "isiyo na silaha" ambayo "haitegemei hofu, vitisho, au silaha."
Ziara ya Kituo cha Yatima cha Ngal Zamba
Baada ya mkutano wake na mamlaka, Baba Mtakatifu alitembelea Kituo cha Yatima cha Ngal Zamba, kinachosimamiwa na Shirika la Mabinti wa Maria. Watoto na watawa walifurahi sana kuwa pamoja na Papa, naye pia alitabasamu kwa furaha. Walimkaribisha kwa nyimbo na shangwe, watoto walikuwa wamevaa mavazi ya bluu yenye nembo ya ziara ya Papa nchini Cameroon. Wakati ulipofika wa Papa kuondoka kwenye chumba kidogo, watawa na watoto walimzunguka na kumtembeza nje wakiimba na kupiga makofi bila kukoma.
Mkutano wa faragha na Maaskofu
Mwisho wa mkutano huo wa furaha, Papa alisafiri hadi makao makuu ya Baraza la Kitaifa la Maaskofu kwa mkutano wa faragha na Maaskofu wa Cameroon, na kuhitimisha siku yake ya tatu barani Afrika.
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwenye jarida letu la kila siku. Just click here