Rais wa TEC:Askofu Mfumbusa alikuwa mwalimu wa vitendo na kuishi elimu kivitendo
Na Sr Ernestina Patrick Lasway – Dodoma/Kondoa
Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania(TEC), Mhasham Askofu Wolfgang Pisa na Askofu wa Jimbo la Lindi, Jumanne tarehe 21 Aprili 2026 jioni alihubiri Jimboni Kondoa, wakati wa misa, mara baada ya kufikishwa Mwili wa aliyekuwa Askofu wa Jimbo hilo, ambaye aliyaga dunia tarehe 14 Aprili 2026. Askofu Pisa alianza kutoa pole kwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dodoma, Askofu Msaidizi, Maaskofu, wazazi, ndugu, jamaa na marafiki waliokuwapo na kumwombea pumziko la Milele.
"Wapeni ninyi chakula"
“Wapeni Ninyi Chakula”, Askofu Pisa alitumia neno hili la Mungu kuonesha jinsi gani Askofu Bernadin Mfumbusa "alivyowapatia watu chakula" kwa kazi kubwa aliyofanya katika kulianzisha na kuliendeleza Jimbo Katoliki la Kondoa, kwa kuanzisha kiwanda cha divai, Kanisa kuu, ukumbi, na miradi mingine ya maendeleo jimboni Kondoa. Katika utume wake, Askofu Mfumbusa daima alipenda kusema: "haya mambo yanawezekana," alibainisha Askofu Pisa katika ngazi ya Jimbo na hata katika Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC)wakati wa kupanga mambo ya maendeleo ya Kanisa.
Askofu Mfumbusa alitokomeza adui Ujinga
"Askofu Mfumbusa alikuwa mwalimu kwa vitendo na kuishi elimu kwa vitendo. Mfumbusa ni mdau mkubwa wa elimu kwa kiwango cha kimataifa,” alibanisha Askofu Pisa. Alipenda kusoma na kuandika, na kuhimiza wanafunzi wake wasome kwa bidii na kuandika. Baadhi ya Wanafunzi wake, wameandika vitabu hata kingine juu ya Askofu Mfumbusa mwenyewe. Kunako mwaka 2013, Shirika la Wafransiskani Wakapuchini walimtumia kama mhamasishaji wa shirika lao, alitoa ushuhuda.
Uchungaji ni kutoa watu katika Nyika la dhambi
Askofu Mfumbusa alitamani kuwatoa watu katika nyika la dhambi, taaluma, maadili ya habari. Alikuwa na lengo la kuwainua watu kitaaluma kama njia ya kuwatoa katika nyika. Askofu Mfumbusa alitafuta wastaafu kusimamia Taaluma katika Chuo Kikuu cha CUEA na kusimamia rasilimali Pesa za Chuo hicho. Akihamasisha umuhimu wa Taasisi kujisimamia (self-sustainability). Ili kuwatoa watu nyikani pia alikuwa na ujuzi mkubwa katika kutafuta ufumbuzi wa matatizo katika nyanja zote. Alikazia umuhimu wa kujitegemeza wenyewe badala ya kutegemea wafadhili.
Uchungaji wa Askofu na kazi nyingine zaambatanishwa
Katika kulitegemeza Kanisa, Askofu Mfumbusa ni mmoja kati ya Maaskofu walio wachache waliofanya kazi za kichungaji sambamba na kufundisha Seminari na Vyuo Vikuu vya Kanisa, aliongeza Askofu Pisa. Alikuwa “Msikilizaji mzuri katika mikutano na kufuata Sera katika utendaji. Ili kuendeleza Taasisi, lazima kujenga Sera kwa utendaji wa ufanisi,” aliongeza. Kwa njia hiyo maisha ya Askofu Mfumbusa ni matokeo ya utafiti, na hakufanya chochote bila kufanya utafiti. Alikuwa makini katika kusahihisha kazi za taalum alipopatiwa.
Kuitwa kufanya kazi ya Mungu
Katika utendaji wake, “Askofu Mfumbusa aliisikiliza na kuitii sauti ya Mungu. Yote aliyafanya kama mapenzi ya Mungu katika maisha yake,” aliongoza Askofu Pisa. Tunaitwa kuwa wakamilifu katika kuifanya kazi ya Mungu, Ayubu alisema: "Najua ya kuwa mtetezi wangu yu hai!" Tumwombee Huruma ya Mungu Askofu Mfumbusa kwani yeye si Ayubu, Mungu amjalie raha ya milele Mbinguni. Askofu Pisa alihitimisha kwa kuwaomba wanakondoa wasikimbie Kondoa kama wanafunzi wa Emau, bali waangalie Msalaba wa Kristo kama njia ya kumwelekea zaidi Mungu. Aliwaalika “Wakristo wa Kondoa kudumu katika umoja, sala na kuomba Mungu awapatie mchungaji mwenye roho mara mbili ya Askofu Bernadin Mfumbusa,”
Misa ya kumuaga Askofu Bernardin Mfumbusa huko Dodoma
Na katika Ibada ya Misa ya kumuaga Askofu Bernardin Mfumbusa iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Paulo wa Msalaba Jimboni Dodoma, Tanzania asubuhi tarehe 21 Aprili 2026 kabla ya kusafirisha mwili kuupelekwa jimboni kwake, Askofu Wilbroad Henry Kibozi, Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki, Dodoma katika mahubiri yake alikazia juu ya kuyapokea Mapenzi ya Mungu kwa njia ya kifo, kama tunavyosali katika sala ya Baba Yetu, Mapenzi yako yatimizwe." Ni katika mazingira ya Gethseman tunamuona Yesu Kristo akipokea Mapenzi ya Baba yake, ingawa haikuwa kazi rahisi.
“Wanafunzi waliomsindikiza, walishindwa kukesha pamoja naye. Mara tatu katika Injili hii tunaambiwa walilala. Tunaalikwa kukesha tukiomba tunapoomba mapenzi ya Mungu yatimie. Askofu Bernadin Mfumbusa katika nyakati za mwisho wa maisha yake alikipokea na kukinywea kikombe cha mateso. Mateso ni ushuhuda na ushindi dhidi ya dhambi, kama anavyokinywea Bwana wetu Yesu Kristo pale Gethseman kwa ajili ya wokovu wa mwanadamu,” alisisitiza Askofu Kibozi.
Mwanadamu hupitia fumbo la mateso
Katika hali ya kawaida kila mwanadamu hupitia fumbo hili la Mateso. Tunapokumbana na mateso tusirudi nyuma wala tusikate tamaa, bali tumtazame Kristo, asisitiza Askofu Kibozi. Tuunganishe mateso na shida zetu na fumbo la ukombozi, alikazia.
Kuzungumza mengi kuhusu Hayati Mfumbusa
Katika kumsindikiza Hayati Bernadin Mfumbusa, “tuna mambo mengi ya kuzungumzia juu ya utu wake kama Mkristo, aliyetambua wito wake kama mkristo aliyoing'amua na kuitendea kazi. Kama mwalimu alifundisha kwa ufanisi, kama Padre na kama Askofu.” Kazi alizozifanya kwa taifa la Tanzania na nje ya mipaka ya Tanzania, alifanikiwa kuunganisha elimu na hali ya kawaida ya maisha ya kawaida na kuleta maendeleo chanya katika jamii, alibainisha Askofu Kibozi.
Hayati Askofu Mfumbusa aliunganisha watu wa rika na umri mbalimbali, pamoja na dini nyingine na muumba wao. Uongozi wake imara ulijenga mahusiano mema katika jamii hasa ya Kondoa alipohudumu kama askofu wa kwanza.
Kuenzi yale aliyofundisha na kuishi Askofu Mfumbusa
Pamoja na shughulu zake kama Askofu, alijitolea kuwafundisha Maaskofu juu ya kilimo bora kwa vitendo, ambapo mafunzo haya yameanza kuzaa matunda kati yetu. Mfumbusa anaendelea kuishi ndani yetu kwa kuenzi yale mema aliyofundisha na kuishi Askofu Mfumbusa. Tumwombee Mungu ampokee na kumpatia zawadi ya uzima wa milele. Raha ya milele umpe ee Bwana.
Mazishi ya Askofu Mfumbusa huko Kondoa Aprili 22
Askofu Mfumbusa anatarajiwa kuzikwa Jumatano tarehe 22 Aprili 2026 Jimboni Kondoa. Hivi karibuni tarehe 9 Aprili 2026, Baba Mtakatifu Leo XIV alikuwa amemteua Askofu Bernardin Francis Mfumbusa, kuwa Rais wa Kamati ya Mawasiliano ya Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Afrika na Madagascar, CEPACS,” na wakati huo huo alikuwa ameteuliwa siku chache kuwa Mjumbe wa Bodi ya Baraza la Kipapa la Mawasilianiano.
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwenye jarida letu la kila siku. Just click here.