Kenya kuwa mwenyeji wa Mkutano Mkuu wa 21 wa AMECEA
Rose Achiego Ande–Nairobi na Sr. Christine Masivo, CPS – Vatican.
Mkutano Mkuu wa XXI wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki (AMECEA), unaotarajiwa kufanyika Nairobi, Kenya kuanzia tarehe 17 hadi 26 Julai 2026, ukiwakutanisha washiriki kutoka nchi wanachama wa AMECEA ambao ni: Sudan, Sudan Kusini, Ethiopia, Eritrea, Uganda, Kenya, Tanzania, Malawi, na Zambia pamoja na wawakilishi kutoka maeneo washirika ikiwa ni pamoja na Djibouti na Somalia.
Kujenga madaraja ya ushirika
Katika ujumbe ulioshirikishwa na Vatican News, Askofu Mkuu Maurice Muhatia Makumba, Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu Wakatoliki wa Kenya, alielezea tukio hilo kama "wakati wa neema" kwa Kanisa nchini Kenya na eneo pana la Afrika Mashariki. "Ni heshima kwa nchi na kwa Kanisa mahalia kuwa mwenyeji wa mkutano mkuu," Askofu Mkuu Muhatia alisema. "Unawaleta pamoja watu wa Mungu wa pande zote katika eneo letu ili kutafakari hali halisi ya kichungaji kwetu na kuimarisha dhamira yetu ya pamoja ya uinjilishaji."
Mkutano Mkuu wa 2026 utafanyika chini ya mada: "Kujenga Madaraja ya Ushirika, Matumaini, Haki, na Utawala Bora." Kulingana na Rais wa AMECEA, Askofu Charles Kasonde wa Zambia, mada hii inaonyesha kujitolea kwa Kanisa la kikanda kushughulikia masuala ya kichungaji na kijamii katika roho ya sinodi. "Mkutano huu Mkuu ni fursa kwetu kuungana kama Kanisa kutafakari, kusikiliza, na kutambua jinsi tunavyoweza kuhudumia jamii zetu vyema," Askofu Kasonde alisema. "Pia ni wakati wa kujibu matarajio ya watu wetu, haswa vijana, ambao wanadai haki, uwajibikaji, na matumaini." Mkutano Mkuu unatarajiwa kuleta pamoja uwakilishi mpana wa Maaskofu, Viongozi wengine wa Kanisa, mapadre, watawa wa kike na kiume, pamoja na wajumbe wa vijana na wataalamu kutoka taasisi za Kikatoliki.
Kuwashirikisha vijana katika AMECEA
Msisitizo maalum utawekwa kwenye nafasi ya vijana katika maisha ya Kanisa. Askofu Mkuu Muhatia alisisitiza umuhimu wa kuwashirikisha vijana katika uenezaji wa imani na katika kuunda sasa na mustakabali wa Kanisa. "Vijana si mustakabali wa Kanisa tu; wao ni sasa," alisema, akitaka ushirikishwaji mkubwa na ushiriki wa vijana katika michakato ya Kanisa.
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwenye jarida letu la kila siku. Just click here