Kardinali Kardinali  

Asia ya Kati:Maaskofu wa wamuunga mkono Papa Leo XIV

Maaskofu wa Asia ya Kati wameonyesha mshikamano imara na Papa Leo XIV wakati wa Mkutano wao Mkuu huko Tashkent,wakithibitisha umoja katikati ya mivutano ya kimataifa.Mkutano huo ulimalizika kwa kuchaguliwa kwa Kardinali Giorgio Marengo kuwa Rais wa Baraza la Maaskofu na kupyaisha ushirikiano wa kichungaji.Maaskofu pia waliakisi kuimarisha amani,mazungumzo kati ya dini na uwajibikaji wa pamoja kwa utume wa Kanisa lote katika eneo hilo.

Na Sr. Christine Masivo, CPS – Vatican.

Baraza la Maaskofu Katoliki wa Asia ya Kati, liliandaa Mkutano Mkuu wao huko Tashkent, Uzbekistan, kuanzia tarehe 15 hadi 19 Aprili 2026, na kwa kauli moja walimuunga mkono Papa Leo XIV kwa ajili ya utume wake hasa kwa sababu ya miito ya amani na utunzaji wa kichungaji, wakibainisha kuwafikia wale wanaoteseka kutokana na vita na dhuluma. Tamko lao lilikuja baada ya ukosoaji wa maneno ulioelekezwa kwa Papa na Rais wa Marekani Bwana Donald Trump. Katika kujibu, Maaskofu walionesha ukaribu wa kidugu na Papa, wakisisitiza umoja ndani ya Kanisa la Ulimwengu na kuthibitisha uaminifu wao kwa uongozi wake.

Uongozi mpya kwenye Baraza

Wakati muhimu wa Mkutano ulikuwa uchaguzi wa uongozi mpya mnamo Aprili 17. Kardinali Giorgio Marengo alichaguliwa kuwa Rais wa Baraza la Maaskofu wa Asia ya Kati, ambaye kutokana na kazi yake ya kichungaji ya kufanya utume wa kimisionari huko Mongolia, hili lilibainishwa na Shirika la Kipapa la Habari za Kimisionari Fides, kwamba atashirikiana na Askofu José Luis Mumbiela Sierra kama Makamu wake na Askofu Yevgeniy Zinkovskiy,  kama Katibu Mkuu. Timu hii ya uongozi imepewa jukumu la kuongoza Kanisa katika eneo lililo na utofauti, jumuiya ndogo ya Wakatoliki, na mahitaji ya kichungaji yanayobadilika.

Kushiriki changamoto na matumaini

Mkutano huo uliwaleta pamoja Maaskofu na Mapadre kutoka Uzbekistan, Kazakhstan, Kyrgyzstan, Tajikistan, Turkmenistan, Mongolia, na Azerbaijan. Kwa ushirikiano, walibadilishana uzoefu wa utume wao wa kichungaji na kujadili hali halisi zinazowakabili jamii zao. Walitafakari ugumu na ishara za matumaini zilizopo katika Makanisa mahalia, wakisisitiza umuhimu wa umoja na ushirikiano. Maaskofu waliangazia dhamira na wajibu wao wa pamoja wa kuwaongoza waamini wa kikatoliki ambao ni wachache, huku wakiimarisha ushuhuda wa Kanisa katika jamii.

Kujitolea kwa amani na mazungumzo

Mada kuu katika mkutano huo ulikuwa amani. Maaskofu walitoa sala za dhati kwa ajili ya wote walioathiriwa na migogoro na dhuluma, wakiwakabidhi kwa maombezi ya Bikira Maria, Malkia wa Amani. Waliwataka waamini kujiunga katika maombi kwa ajili ya amani ya haki na ya kudumu duniani kote. Mnamo Aprili 18, maaskofu walitembelea Kituo cha Ustaarabu wa Kiislamu huko Tashkent, ishara ya kuashiria uwazi na heshima ya pande zote. Ziara hiyo ilisisitiza kujitolea kwao kwa mazungumzo ya kidini, jambo muhimu katika kukuza maelewano katika eneo lenye Waislamu wengi.

Kuimarisha Kanisa

Mkutano huo ulitajirishwa na michango kutoka kwa wawakilishi wa Kanisa. Askofu Mkuu George Panamthundil, Balozi wa Vatican nchini Kazakhstan, Kyrgyzstan, na Tajikistan, alishiriki katika vikao vya ufunguzi, huku Askofu Mkuu Giovanni D’Aniello, Balozi wa Vatican nchini Uzbekistan na Urusi, akituma ujumbe kwa mkutano huo. Kuhusika kwao kulionyesha uhusiano wa karibu kati ya Vatican na Makanisa ya Asia ya Kati. Mkutano huo ulimalizika kwa umoja mpya, mwelekeo wazi wa kichungaji, na kujitolea kwa pamoja kwa amani, mazungumzo, na huduma ya uaminifu.

MAASKOFU WA ASIA YA KATI

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwenye jarida letu la kila siku. Just click here.

23 Aprili 2026, 11:12