Tanzania,Uzinduzi wa Jimbo jipya la Bariadi:Sala,huduma na Amani kuwaongoza!
Na Sr. Ernestina Patrick Lasway, SAC - Vatican.
Kanisa la Tanzania, linamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuzidi kukua kama wana wa Mungu, na kupata Jimbo Jipya lililozinduliwa na kusimikwa kwa Askofu wake mpya, siku ambayo Mama Kanisa anasheherekea Mtakatifu Yosefu, Mlinzi wa Familia Takatifu ya Nazareth, tarehe 19 Machi 2026. Kabla ya maadhimisho haya ya kitaifa, yalitanguliwa na masifu ya jioni tarehe 18 Machi 2026, katika Kanisa la Mtakatifu Luka Mwinjili Jimboni hapo. Aliyeongoza tafakari hiyo ya masifu ya jioni alikuwa ni Mhashamu Askofu Simon Masondole wa Jimbo la Bunda, na mhusika mkuu wa Idara ya Liturujia, ya Baraza la Maaskofu Tanzania(TEC), ambapo alimtakia Askofu wa Jimbo jipya mwanzo mwema na utendaji mwema anapoanza kulistawisha jimbo hilo.
Majimbo yana jukumu muhimu katika utume wa Kanisa
Katika Sherehe hiyo ya Mkatifu Yosefu, Askofu wa kwanza wa Jimbo jipya la Bariadi alisimikwa rasmi. Aliyeongoza Misa Takatifu alikuwa ni Askofu huyo wa Bariadi na mhubiri alikuwa ni Mhasham Severine Niwemugizi, Askofu wa Jimbo la Rulenge - Ngara, ambapo katika mahubiri yake alianisha umuhimu wa kuanzishwa kwa jimbo jipya la Bariadi kama ishara ya kukua na kustawi kwa imani Katoliki nchini Tanzania.″Kuanzishwa kwa jimbo jipya ni alama ya kukua kwa Kanisa, kukua kwa Imani Katoliki iliyo msingi wa matumaini yetu. Ni alama ya ongezeko la waamini, ishara ya kukua kwa Imani. Majimbo yana jukumu muhimu katika utume wa Kanisa, utawala wa Kanisa, uongozi wa kiroho, elimu na malezi ya kikuhani, huduma za afya, utetezi wa haki na utu wa watu wote, pamoja na kuunganisha imani ndani ya tamaduni mbalimbali,″ alibainisha. Kuanzisha kwa jimbo jipya kunasogeza huduma za Kanisa karibu na ushirikishwaji wa jamii katika jimbo, aliendelea kusema Askofu Niwemugizi kwa kutumia jina la Askofu Prosper kama kielelezo cha kuleta maendeleo katika Kanisa la Bariadi, kwani jina hili ni kielelezo cha mafanikio."
Kwa utii anakwenda kutimiza mapenzi ya Mungu Jimboni Bariadi
Adhimisho la kusimikwa Askofu mpya katika Sherehe ya Mtakatifu Yoseph, Baba mlishi wa Yesu ni kielelezo cha utii na utayari kufanya kazi ya Mungu. Mtakatifu Yosefu alikuwa mtii kwa mapenzi ya Mungu, kwa kupokea habari za ujauzito wa Maria na kukubali kupokea majukumu makubwa. Kwa askofu Prosper Baltazary Lyimo kukubali kupokea majukumu ya kuliongoza Jimbo jipya, ni hatua muhimu katika utii kwa Mungu, kama alivyofanya Mtakatifu Yoseph. Kwa utii anakwenda kutimiza mapenzi ya Mungu jimboni Bariadi, kwa kuongozwa na maisha ya utii ya Mtakatifu Yosefu, aliyeishi maisha ya haki, upole na unyenyekevu ambazo pia ni fadhila za Askofu Prosper."
Askofu Mpya wa Jimbo Jipya ni mlezi
Askofu Niwemungizi alimsihi Askofu mpya kumtumaini Mungu, kama mchungaji mkuu wa jimbo la Bariadi katika kufundisha ukweli kwa kuongoza na 1Thes 2: 3-4. "Umetumwa kufanya kazi ya ukweli katika jimbo la Bariadi. Kwa kuwa Askofu wa kwanza ni mlezi wa kwanza anayapaswa kulea na kufanya yote kwa ajili ya Bwana. Karama za kujenga mwili wa Kristo kwa kushirikiana na mapadre, watawa na walei jimboni humo ni msingi wa mafanikio. ″Kama Yosefu, wewe ni mlinzi wa Jimbo lako na unaitwa kujali mahitaji ya kiroho ya watu wako. Ulete faraja na matumaini miongoni mwa watu na kukazia umuhimu wa familia kama Mtakatifu Yoseph alivyofanya kwa familia,″ alihimiza Askofu Niwemuguzi.
Katika mahubiri hayo aliendelea akibainisha kuwa, "familia ni kiungo muhimu katika katika ustawi wa Kanisa. Familia inaakisi upendo wa jamii, hivyo Askofu analo jukumu la kukuza Imani katika familia na kuwa mtumishi wa familia kwa kuwa mtumishi asiyekuwa na faida." Askofu aidha "analo jukumu la kufundisha na kutakatifuza malimwengu kwa kufanya yote kwa ajili ya Kristo. Tuigeuzie mioyo yetu kwa maombezi ya Mtakatifu Yosefu na Mama Bikira Maria na kwa maombezi yao kufanikiwa katika utume," alihitimisha.
Balozi wa Vatican anawaalika mapadre, watawa na waamini waleo kushirikana na Askofu mpya
Wakati wa sherehe hiyo naye Balozi Vatican nchini Tanzania Askofu Mkuu Angelo Accattino, akiwasilisha salamu za Baba Mtakatifu Leo XIV, akishukuru Askofu wa Jimbo la Shinyanga kwa kukubaliwa kutwaa sehemu ya mamlaka yake na jimbo lake kwa jimbo la Bariadi. Yeye alivutiwa na kaulimbiu, inayomuongoza Askofu katika kumtumikia Mungu. Tangu alipoitika wito na kuendelea na ufuasi mpaka kufika Bariadi kuwatumikia watu wa Mungu. Kwa njia hiyo Askofu Mkuu Accattino aliwaalika "waamini kufuata njia ya amani ambayo kila mtu anahitaji katika maisha yetu ya kila siku. Vile vile, aliwaalika mapadre, watawa na waamini walei kushirikiana na Askofu mpya katika kulijenga jimbo jipya la Bariadi. Kauli mbiu ya Askofu wa jimbo jipya inaonyesha jinsi alivyounganisha Imani na Utume wa Kanisa na adhimisho la Ekaristi Takatifu, kwani Yesu anatualika tuhudumiane,"alibanisha.
Rais wa TEC awaalika wakristo kuitangulia dunia na kuiongoza dunia
Kwa upande wake Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania,(TEC) Askofu Wolfugang Pizza, wa Jimbo la Lindi, alisema kuwa "historia ya Kanisa la Tanzania imebadilika na kukua kwa kuanzishwa kwa jimbo jipya ya Bariadi, ambalo linafanya Kanisa la Tanzania kuwa na majimbo Katoliki 37." Askofu Pizza aliwaalika wakristo kuitangulia dunia na kuiongoza dunia, kwa kuiacha roho ya dunia na kuiongoza dunia. Kwa maombezi ya Mtakatifu Yosefu aliye mwombezi wa Kanisa, alilinde Kanisa la Bariadi na Kanisa la ulimwengu." Rais wa Baraza la Maaskofu wa Tanzania aidha aliwasihi mapadre, watawa na waamini walei kumpatia ushirikiano Askofu: ″Mkifanya naye kazi vizuri, mtaliendeleza jimbo hili,″ alisisitiza. Alimpongeza Askofu wa Jimbo Katoliki Shinyanga kwa wazo hilo na ushirikiano na wazo la kuanzishwa kwa jimbo jipya.
Askofu Prosper awashukuru wana Bariadi kwa mapokezi
Kwa Mhasham Askofu Prosper Baltazari Lyimo, wa Jimbo Jipya la Bariadi wakati wa kutoa neno lake alianza kwa kuwashukuru wana Bariadi kwa mapokezi mazuri na kuongozwa na neno la Mungu kutoka (1Thesꓽ5, 16-24)"Furahi siku zote, tusali bila kuchoka na kuwa watu wa shukrani," akiwashukuru familia na walezi wote waliomsaidia kuwa jinsi alivyo. Aliwaomba mapadre, watawa na waamini kumpa ushirikiano kama Askofu mpya wa jimbo kwa kutambua utume wao na nafasi yao katika Kanisa. Aliwahakikishia mapadre kuwa atashirikiana nao bila mashaka wala wasiwasi, wakati huo huo kuwaomba wakristo, watawa wa kike na kiume kutokuwa na hofu kwani kwa pamoja wataifanya kazi ya Kristo. "Moyo wa sala, shukrani na upendo uwaongoze wanabariadi katika utume na kufanya yote kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mungu, kwa kuongozwa na kauli mbiu ya Sala, Huduma na Amani.
Jimbo jipya la Bariadi limezinduliwa rasmi tarehe 19 Machi 2026, likiwa na idadi ya mapadre 34, mashemasi 3, mapadre wa shirika 5, watawa 20 pamoja na mafrateri 46. Hii ni ishara ya uhai wa Kanisa ambao unapaswa kupaliliwa na kustawisha na Kanisa mahalia kwa kuongozwa na Askofu mpya wa Jimbo hili.
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku bonyeza hapa: Just click here.