Shughuli za Wanashirika wa Mtakatifu Vincent Pallotti. Shughuli za Wanashirika wa Mtakatifu Vincent Pallotti.  #SistersProject

Tanzania:Urithi wa Masista Wapallottini,kuwawezesha wanawake kupitia elimu

Kile kilichoanza kama utume mdogo huko Singida,leo kimekuwa chanzo cha matumaini ya kudumu kwa vizazi vyote. Kwa miongo kadhaa, masista wapallottini wameitetea elimu kama chombo cha kuwawezesha wanawake na kubadili jamii.Utendaji huu umekuwa chachu ya mabadiliko makubwa katika maisha ya jamii na kuboresha fursa na maisha ya familia.

Na Sr. Ernestina Patrick Lasway SAC,- Vatican.

Masista Wapallottini waliwasili katika Jimbo la Singida mnamo mwaka 1990 kutoka Uingereza,wakiitika mwaliko wa mapadre wamisionari Wapallottini ambao walikuwa wakifanya utume nchini Tanzania tangu miaka ya 1940. Walikaribishwa katika parokia ya Mtakatifu Leo Mkuu huko Makiungu na kujikita katika utume wa kufundisha katekesi parokiani na kujifunza Kiswahili.

Watoto katika mafunzo ya Kompyuta( Sr.Agripina Mmassy SAC)

Kwa kuongozwa na askofu wa Jimbo, marehemu Askofu Bernard Mabula, masista waling’amua hitaji la haraka kwa eneo hili: elimu kwa wasichana haikuwa kipaumbele katika jamii nyingi za wafugaji Singida. Kwa kujibu hitaji hilo, masista walihamia kijiji jirani cha Siuyu mwaka 1994, na baadaye kuanzisha shule ya wasichana Pallotti wakiwa na dhamira ya dhati kuwainua wasichana wa kijiji kupata elimu bora.

Masista Wamisionari wa Umoja wa Utume Mkatoliki (Sr.Agripina Mmassy SAC)

Elimu kwa Wasichana Wahitaji

Kwa miaka kadhaa shule hii iliweka kipaumbele cha kusomesha wasichana wanaotoka kwenye familia duni, ikitoa elimu bila malipo kwa wale waliokuwa na hamu kubwa ya kujifunza. Mkakati huu ulifungua milango kwa wasichana wengi kuendelea na elimu ya sekondari katika mazingira salama. Leo, wahitimu wengi kutoka Sekondari ya Pallotti wameendelea kuwa vinara katika taaluma ya uuguzi,biashara, uongozi bora wenye kuleta chachu ya mabadiliko chanya katika ya taasisi ndani na nje ya Tanzania.

Mafanikio na Ushuhuda

“Kama mhitimu naweza kushuhudia kuwa, kama isingekuwa uwepo wa masista Wapallottini na kupata elimu ya sekondari bure katika shule ya wasichana Pallotti, nisingekuwa nilivyo leo, wala kufanya kazi kama mkunga na muuguzi katika hospital bora nchini Tanzania. Kupitia masista hatukufaidi tu kwa taaluma, bali pia tunapata majiundo ya kimaadili na malezi ya kikristo, ambayo hutusaidia kuhusiana vizuri kazini na watu wengine, tukitambua kuwa sisi sote ni watoto wa Mungu,” alisema Magdalena Vitali. Aliongeza kuwa, shule ya bweni kwa wasichana Singida, imemsaidia sana mtoto wa kijiji na kupunguza ndoa za utoto. Magdalena anashuhudia kuwa elimu aliyopata kupitia Pallotti, imekuwa chachu ya kubadilisha maisha na kuongeza fursa katika maisha yake, familia na jumuiya kwa ujumla.

Mary Joan Msonza anahudumu kama Mkurugenzi Mtendaji wa IDEON Limited nchini Tanzania, kampuni inayojishughulisha na huduma za kituo cha mawasiliano kwa njia ya kuajiriwa nje ya nchi, uendeshaji wa mauzo kwa njia ya simu, suluhisho za rasilimali watu, pamoja na usaidizi wa michakato ya biashara. Pia ni Mkurugenzi wa Joyfort Intertrade Company Limited, kampuni inayojikita katika biashara, usambazaji na huduma mbalimbali za kibiashara. Kupitia kampuni hizi, amepata fursa ya kuunda ajira kwa zaidi ya watu 1,300. Akiwa anashuhudia, alisema: “Naamini kwa dhati kwamba msingi nilioupata katika Shule ya wasichana Pallotti unaendelea kunisaidia katika uongozi, muundo na ukuaji wa taasisi ninayoiongoza, na ninabaki na shukrani za dhati kwa nafasi ambayo Masista walichangia katika kunilea na kunifanya nilivyo leo.” Aliongeza kuwa, “Malezi ya Kipallottine yaliimarisha nidhamu yangu, uadilifu wangu, na mtindo wangu wa uongozi unaozingatia maadili.”

Wito wa kuwekeza katika Elimu kwa mwanamke

Shirika la Masista Wapallottini lililoanzishwa mwaka 1838 na Mtakatifu Vincenti Palloti huko Roma, bado wanaendelea kuishi karama ya kufufua imani na kuamsha upendo kwa matendo katika maisha ya kila siku. Nchini Tanzania wanafanya utume katika nyanja mbalimbali kuwa njia ya kutoa elimu, huduma za afya, huduma za kijamii na kichungaji na kuhakikisha kuwa elimu inabaki kuwa chanzo cha kudumu cha matumaini, heshima na mafanikio kwa vizazi vyote. Pamoja na changamoto zilizopo, hasa kwa wasichana wanaotoka katika jamii za pembezoni,elimu sawa na kwa wote, bado ni jambo msingi ili kujenga taifa lenye wataalamu na uzalishaji yakinifu. Kwa muktadha huu, utume na kazi za masista wapallottini bado zina umuhimu mkubwa kwa jamii.

Sr. Juliana Quaras amekuwa Mwalimu Mkuu katika shule ya wasichana Pallotti kwa miaka kadhaa,anajivunia juhudi na bidii ya wanafunzi pamoja na walimu katika kuhakikisha kwamba ndoto za vijana waliokabidhiwa kwao zinakuwa halisi. Anatoa wito kwa watu wenye mapenzi mema kuunga mkono juhudi yakuwawezesha wasichana hasa wale wanaotoka kwenye mazingira magumu kupata elimu bora kwa kuwafadhili.

Kufikia mwaka 2026, shule ya wasichana Pallotti ina wanafunzi wapatao 500 wa bweni, na kujivunia wahitimu zaidi ya 5000 kwa miaka iliyopita. Sr. Juliana anasisitiza kuendeleza karama ya kuwasomesha wasichana, hasa wanaotoka kwenye familia duni kiuchumi, tukitambua kwamba “kumwelimisha mtoto wa kike, ni kuelimisha jamii nzima.”

Elimu kwa wanawake Tanzania

Asante kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku. Just click here

02 Machi 2026, 12:49