Tafakari Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya Nne Kipindi cha Kwaresima: Wanafunzi wake wakamuuliza Kristo Yesu ni nani aliyekuwa ametenda dhambi kiasi cha mtu yule kuzaliwa kipofu? Tafakari Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya Nne Kipindi cha Kwaresima: Wanafunzi wake wakamuuliza Kristo Yesu ni nani aliyekuwa ametenda dhambi kiasi cha mtu yule kuzaliwa kipofu?   (@Vatican Media)

Tafakari Dominika ya Nne Kwaresima Mwaka A: Kipofu: Ufunuo wa Huruma Ya Mungu!

Yule mtu aliyezaliwa kipofu bila kupepesapepesa macho akakiri kwamba, ndiye yeye aliyezaliwa kipofu sasa anayo furaha ya kuona, amekuwa huru: kiroho na kimwili na anamshuhudia Yesu kuwa kweli ni Nabii wala hana tena woga ndani mwake! Imani imemwezesha kuwa jasiri na kwake Kristo Yesu amekuwa ni chemchemi ya: Imani, mapendo na matumaini mapya, kwa kumrejeshea tena utu na heshima yake, siku ya Sabato na sasa kwa jeuri anamtolea ushuhuda wa nguvu.

Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.

UTANGULIZI: Karibu mpenzi msikilizaji na msomaji, wa tafakari ya Neno la Mungu kutoka hapa Vatican News. Dominika ya Nne ya Kipindi cha Kwaresima, "Domenica Laetare" ni Dominika ya mwanga na furaha ya ndani. Katikati ya safari ya toba, wongofu wa ndani na kujinyima, Kanisa linatualika tusimame kidogo, tuone mwanga unaoanza kung’aa, na tujitie moyo kwamba Mungu yuko kazini ndani ya historia yetu. Wanafunzi wake wakamuuliza Kristo Yesu ni nani aliyekuwa ametenda dhambi kiasi cha mtu yule kuzaliwa kipofu? Ulemavu ulihesabiwa kuwa ni kielelezo cha dhambi, kiasi hata cha kutengwa na kusukumizwa pembezoni mwa jamii. Walitengwa na kuwekwa nje ya Hekalu, huku wakiendelea kuomba kila siku ya maisha yao! Yule mtu aliyezaliwa kipofu bila kupepesapepesa macho akakiri na kutangaza wazi kwamba, ndiye yeye aliyezaliwa kipofu sasa anayo furaha ya kuona, amekuwa huru: kiroho na kimwili na anamshuhudia Kristo Yesu kuwa kweli ni Nabii wala hana tena woga ndani mwake! Imani imemwezesha kuwa jasiri na kwake Kristo Yesu amekuwa ni chemchemi ya: Imani, mapendo na matumaini mapya, kwa kumrejeshea tena utu na heshima yake, siku ya Sabato na sasa kwa jeuri anamtolea ushuhuda wa nguvu. Mtu aliyezaliwa kipofu ni changamoto ya kuangalia mambo kwa jicho la imani, ili kuondokana na giza na hivyo kuanza kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka. Hii ni changamoto ya toba na wongofu wa ndani. Kipofu akabahatika kuona, kuelewa na hatimaye kuamini: “Nina amini Bwana.”

Wakati mwingine mateso ni ufunuo wa huruma ya Mungu
Wakati mwingine mateso ni ufunuo wa huruma ya Mungu   (@Vatican Media)

Dominikai ya furaha;  tunafurahia nusu ya safari ya mfungo.. tuna ‘jibrekisha’ kidogo na ala za muziki kukusanya nguvu za kuendelea.. Wazo letu leo ni maisha ya nuru, kuwa watu tunaoona na kung’amua. Swali la mafarisayo kwa Yesu ‘Je, sisi nasi tu vipofu?’ linaongoza tafakari yetu. Dunia ya leo ina teknolojia kubwa, maarifa mengi, lakini bado tunaona upofu mkubwa wa kiroho: vita visivyoisha, chuki kati ya mataifa, dhuluma kwa maskini, uharibifu wa mazingira, na kupotea kwa dhamiri. Watu wanaona kwa macho ya mwili, lakini wanashindwa kuona kwa macho ya moyo. Ndiyo maana Neno la Mungu leo linatualika kutoka gizani kwenda nuruni. Lakini furaha ya leo si furaha ya juu juu. Ni furaha ya mtu anayepata kuona. Ndiyo maana Injili ya leo inatuweka mbele ya swali gumu lakini la wokovu:“Je, sisi nasi tu vipofu?” Hili ndilo swali la Mafarisayo, lakini pia ni swali la kila Mkristo katika safari ya Kwaresma. Injili ya leo inatuletea simulizi ya mtu aliyekuwa kipofu tangu kuzaliwa. Watu walidhani tatizo lake ni dhambi. Lakini Yesu anaweka wazi jambo muhimu: si kila mateso ni adhabu; wakati mwingine ni nafasi ya kazi za Mungu kudhihirika.

Kristo Yesu ni nuru na mwanga wa Mataifa
Kristo Yesu ni nuru na mwanga wa Mataifa   (ANSA)

UFAFANUZI: Wayahudi waliamini dhambi hulipwa na Mungu, au baada ya kifo au hapahapa duniani.. pia anaweza akakuacha na kumuadhibu mwanao aliyepo au ambaye hajazaliwa bado.. anaweza kumsubiri hata mjukuu au kitukuu na huyo atazaliwa na tatizo sababu ya dhambi za baba, babu, bibi. Katika Kut 20:5 tunasoma ‘kwa kuwa mimi Mungu wako ni Mungu mwenye wivu, nawapatiliza wana maovu ya baba zao hata kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao..’ Ndio sababu wanafunzi wa Kristo wanapomuona kipofu wanamuuliza ‘Rabi, ni yupi aliyetenda dhambi…hasa ukichukulia kwamba huyu ni kipofu tangu kuzaliwa?’ Yesu anaondoa dhana ya urithi wa adhabu ya dhambi za wazee.. ‘usiseme baba amekula zabibu mbichi na watoto wamekufa ganzi meno’ (Eze 18:1-4, 25-32), kila mtu atauchukua mzigo wake mwenyewe, upandacho ndicho uvunacho (Gal 6:5,7b). Kipofu huyu ameponywa kipekee.. anapakwa tope za mate na kuamriwa kunawa kisimani Siloam.. ‘Siloamu’ maana yake “aliyetumwa/aliyepelekwa”, kilikuwa kisima kilichopelekwa ndani ya mji na mfalme Hezekia ili kuingiza maji mjini wakati wa vita kwa njia ya bomba la upana wa 6m na urefu 583m ndio maana kiliitwa Siloam.. Kristo naye ni “Siloam” sababu alipelekwa na Baba.. kipofu naye ni “siloam” sababu amepelekwa na Yesu akanawe.. anapona sababu Yesu anayo maji yaliyo hai alivyomwambia mama Msamaria Dominika iliyopita (Yn 4:5-52).

Hii ni Dominika ya Furaha
Hii ni Dominika ya Furaha   (@Vatican Media)

Kwa nini Kristo Yesu alitumia mate na udongo? Wayahudi waliamini mate ya mtu ni dawa.. mara kadhaa ameyatumia kuwaponya vipofu.. ‘akamshika mkono yule kipofu akamleta nje ya kijiji akamtemea mate ya macho, akamwekea mikono yake akamuliza unaona kitu?.. naona watu kama miti inayotembea…’ (Mk. 8:23). Wayahudi waliamini pia roho imo kwenye mate na hivi kumtemea mtu mate sio dharau ila ni ishara ya roho ya baraka, kunuizia nk hivyo kwa tope la mate Yesu anamuumba upya kipofu kutoka asili yake sababu Adam aliumbwa kwa udongo.. Halafu mate na udongo, vitu vinavyoonekana, ni ishara ya Sakramenti za Kanisa ambazo ni alama wazi zinazoonekana ila zimebeba maana ya ndani iliyofichika.. Ubatizo (maji), Ekaristi (mkate na divai), Kipaimara (mikono/mafuta), Mpako wa wagonjwa (mafuta), Kitubio (dhambi), Upadre (mikono) na Ndoa (wachumba). Upofu wa kiroho ni dhambi, maisha ya giza. Somo II (Efe 5:8-14) linaeleza ‘zamani ninyi mlikuwa katika giza, bali sasa mmekuwa nuru katika Bwana..’ Kwamba, kabla ya ubatizo tulikuwa gizani, kwa huo tumewekwa katika mwanga kwa kumfahamu Bwana na kuishi kama wana na binti wa nuru.. hili ni suala endelevu, si tukio la siku moja bali kila siku tunahitaji kuona zaidi na zaidi na hivi kukua katika kumuelewa na kumfuata Kristo. Katika muujiza wa leo tunaweza kuwagawa watu makundi manne: Kundi lisilojua, halijui kama halijui.. ni la wapumbavu wasiotaka kuelimishwa... mafarisayo!.. Kundi lisilojua lakini linajua kutojua.. ni wajinga, wanyenyekevu walio tayari kujifunza.. yumo kipofu wa Injili.. hoja zake kwa mafarisayo zinadhihirisha Roho wa Bwana alikuwa ndani mwake.

Yule Mtu aliyezaliwa kipofu, akakiri kwamba, Yesu ni Masiha
Yule Mtu aliyezaliwa kipofu, akakiri kwamba, Yesu ni Masiha   (@Vatican Media)

Kundi linalojua lakini halijui kuwa linajua.. Ngugi wa Thiongo anawaita ‘Simba waliolala’, wanahitaji kuamshwa.. wamo wazazi na ndugu wa yule kipofu, wanajua shida za mwenzao lakini hawazishughulikii, hayawahusu.. hata kupona kwake waliona kero.. huenda ndio sababu aliamua kuwa ombaomba.. na kundi linalojua na linajua kwamba linajua.. werevu wenye busara, tunaalikwa kuwafuata.. ni Kristo.. kipofu anamfuata Huyo anayejua na anajua kwamba anajua. Katika makundi haya kila mmoja wetu anafahamu mwenyewe anaingia wapi.. wito ni kutenda kama kipofu anayekiri kutojua akihitaji kujulishwa, tusiwe mafarisayo wasiojua na hawajui kuwa hawajui.. ‘alikuwa haoni na alijua wazi kabisa kuwa hakuwa anaona, mwisho anaona na waliodhani wanaona kumbe wao ndio vipofu kabisa..’ Je, sisi nasi tu vipofu? Katika familia, jumuiya kuna watu tuna viatu jozi nyingi.. lakini jirani au watoto wake wanashinda pekua, hatuoni wala hatuwasaidii japo jozi moja.. Je! Sisi nasi tu vipofu? Kipindi hiki cha Kwaresima na masika kuna familia wamekosa chakula, wanalala na kuamka hivihivi tu, si kwa kupenda ila ugumu wa hali.. tupo wenye kila kitu na kusaza, tumekaza mioyo.. Je sisi nasi tu vipofu?

Kristo Yesu ni Nuru ya Ulimwengu
Kristo Yesu ni Nuru ya Ulimwengu   (@Vatican Media)

Kila mmoja wetu anaalikwa akubali kwamba haoni na anahitaji uponyaji.. kipofu hana uhuru wa mambo yake.. Kristo pekee na sio mwingine yeyote anaweza kutusaidia sababu Yeye ni Nuru ya ulimwengu.. kipofu hawezi kumuongoza kipofu (Lk 6:39). Mungu hana likizo, anatutunza nyakati zote.. tukubali hilo ili Kristo atuondolee upofu tupate kuona kwa kuwa katika Jina lake lilo kuu sana vipofu wanaona, viwete wanatembea na wafu wanafufuliwa. tumuombe aingie katika maisha yetu, aponye majeraha ya mioyo iliyovunjika na kupondeka, atupe macho ya imani tuone utukufu wake na kwa nguvu na neema yake tuudhihirishe utukufu wake katika yote tunayosema na tunayotenda.Dominika ya Laetare inatualika tufurahi kwa sababu: Kristo ni nuru ya dunia, Upofu si wa milele, Macho ya moyo yanaweza kufunguliwa. Tukubali leo kusimama mbele ya Yesu na kusema kwa unyenyekevu: “Bwana, nataka kuona.” Na tukiona, tutaishi kama watoto wa nuru, tukishuhudia kwa matendo yetu kwamba furaha ya kweli ni kuona ukweli na kuishi ndani yake. Tukubali leo kusimama mbele ya Yesu na kusema kwa unyenyekevu: “Bwana, nataka kuona.” Na tukiona, tutaishi kama watoto wa nuru, tukishuhudia kwa matendo yetu kwamba furaha ya kweli ni kuona ukweli na kuishi ndani yake.

Liturujia D4 Kwaresima
12 Machi 2026, 15:51