Tafakari Dominika ya Nne ya Kipindi Cha Kwaresima Mwaka A wa Kanisa: Yule Kipofu tangu kuzaliwa anamkiri Kristo Yesu kuwa ni: Nabii, Bwana na Masiha na anamwabudu Mungu Mkombozi. Tafakari Dominika ya Nne ya Kipindi Cha Kwaresima Mwaka A wa Kanisa: Yule Kipofu tangu kuzaliwa anamkiri Kristo Yesu kuwa ni: Nabii, Bwana na Masiha na anamwabudu Mungu Mkombozi.  (@Vatican Media)

Tafakari Dominika ya Nne ya Kipindi Cha Kwaresima Mwaka A: Kipofu: Kiri ya Imani!

Kipofu ndiye aliyezaliwa kipofu sasa anayo furaha ya kuona, amekuwa huru: kiroho na kimwili na anamshuhudia Yesu si tena kama “Mtu yule; Nabii, bali sasa kwake ni Masiha, Bwana na Mtakatifu wa Mungu akamsujudia! Imani imemwezesha kuwa jasiri na kwake Kristo Yesu amekuwa ni chemchemi ya: Imani, mapendo na matumaini mapya, kwa kumrejeshea tena utu na heshima yake, siku ya Sabato na sasa kwa jeuri anamtolea ushuhuda wa nguvu.

Na Padre Bonaventura Maro, C.PP.S., -Kolleg St. Josef, Salzburg, Austria.

Utangulizi. Wapendwa Taifa la Mungu, ni Dominika ya 4 ya Kwaresima, mwaka A wa Kanisa. Dominika ya nne ya Kwaresima hujulikana kama, “Domica Laetare” yaani Dominika ya Furaha. Ulemavu katika Agano la Kale ulihesabiwa kuwa ni kielelezo cha dhambi, kiasi hata cha kutengwa na kusukumizwa pembezoni mwa jamii. Walitengwa na kuwekwa nje ya Hekalu, huku wakiendelea kuomba kila siku ya maisha yao! Yule mtu aliyezaliwa kipofu bila kupepesapepesa macho akakiri na kutangaza wazi kwamba, ndiye yeye aliyezaliwa kipofu sasa anayo furaha ya kuona, amekuwa huru: kiroho na kimwili na anamshuhudia Kristo Yesu si tena kama “Mtu yule; Nabii, bali sasa kwake ni Masiha, Bwana na Mtakatifu wa Mungu wala hana tena woga ndani mwake akamsujudia! Imani imemwezesha kuwa jasiri na kwake Kristo Yesu amekuwa ni chemchemi ya: Imani, mapendo na matumaini mapya, kwa kumrejeshea tena utu na heshima yake, siku ya Sabato na sasa kwa jeuri anamtolea ushuhuda wa nguvu. Mtu aliyezaliwa kipofu ni changamoto ya kuangalia mambo kwa jicho la imani, ili kuondokana na giza na hivyo kuanza kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka. Hii ni changamoto ya toba na wongofu wa ndani. Kipofu akabahatika kuona, kuelewa na hatimaye kuamini: “Nina amini Bwana.” Tunafurahi kwa kuwa tumekaribia kuiona nuru ya Kristo Mfufuka, katika Fumbo Takatifu la Pasaka. Liturujia ya Neno la Mungu inatutafakarisha kuwa, “Kristo Yesu ni Nuru ya Ulimwengu.” Katika Dominika ya 3, Kristo Yesu alijifunua kwetu kama Maji ya Uzima, Mungu anayetuliza kiu ya wote wanaomtafuta wa moyo mnyofu. Dominika hii ya 4, Mwinjili Yohane anamtambulisha kwetu tena Kristo kama Nuru ya ulimwengu. Kwa dhambi sisi sote tulikuwa gizani. Yeye alifika duniani kututoa katika giza na kutuonesha njia iendayo kwa Mungu kwenye uzima na Heri. Si kwa mastahili yetu Mungu anatushirikisha neema hii, bali ni kwa sababu ya upendo wake, anatuita kila mmoja kwa njia ya ubatizo na kutushirikisha neema mpya ya kuwa watoto wa nuru, watoto wa Mungu. Tuendelee kuwaombea Wakatekumeni ambao wanaitafuta nuru na njia iendayo kwa Mungu kwa njia ya ubatizo. Tujiombee na sisi sote ili daima tuishi katika nuru ya Kristo, kwa kuachana na mambo yote yanayotufanya kila mara kurudi katika maisha ya kale, maisha ya giza la dhambi.

Mungu anamteuwa Daudi kuwa Mfalme wa Israeli, mwanzo mpya
Mungu anamteuwa Daudi kuwa Mfalme wa Israeli, mwanzo mpya   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Somo la Kwanza ni kutoka katika Kitabu cha 1 Sam 16:1b, 6-7, 10-13a. Somo la kwanza kutoka katika kitabu hiki cha kwanza cha Samweli ni simulizi la kuchaguliwa kwa Daudi kuwa Mfalme wa Israeli. Kwa kumchagua Daudi, Mwenyezi Mungu alianzisha kipindi kipya katika historia ya wokovu. Kutoka katika ukoo wa Daudi atazaliwa Masiya, ambaye kwa njia yake Historia nzima ya ukombozi wa taifa jipya la Mungu na utilimilifu wa Ahadi zake vinatimia. Ningependa tutafakari somo hili kwa kuangazia mambo manne muhimu yafuatayo: Jambo la kwanza: Katika udhaifu, katika dhambi na kushindwa, Mungu hawaachi kamwe watu wake, anaonesha bado njia. Katika historia ya taifa la Israeli wakiwa ndani ya Nchi ya Ahadi, Mfalme Sauli ndiye aliyepakwa mafuta kuwa Mfalme wa kwanza. Ni Mungu mwenyewe aliyemteua na Nabii Samweli akampaka mafuta. Hata hivyo, Sauli hakutenda kadiri ya mapenzi ya Mungu, na Mungu anamkataa kama Mfalme. Samweli alikuwa amewekeza nguvu nyingi katika kumwandaa Sauli kuwa Mfalme. Kuona mradi wake unashindwa na Mungu anajuta kumtawaza Sauli, kulimfanya Samweli alie mbele za Mungu usiku kucha (1 Sam 15:11). Samweli alihuzunika kuona mwanadamu mwenye uwezo mkubwa akishindwa kutokana na kiburi na kutotii maagizo ya Mungu, jambo lililopelekea Roho wa Bwana kumwacha. Licha ya udhaifu huo, ambao kimsingi tunauona tangu hata kwa Adamu na Eva, Mungu hawaachi watu wake, habadili mpango na hatma yao. Ndugu mpendwa, Mwenyezi Mungu anatukumbusha kuwa kila wakati anatuwazia yaliyo mema licha ya dhambi, kushindwa na udhaifu wetu. Licha ya kushindwa hatupaswi kubaki hapo, bali kutazama mbele na kuendelea na safari. Mungu alimuuliza Samweli, "Hata lini utamlilia Sauli, ikiwa mimi nimemkataa...?" (1 Samweli 16:1). Hii inatufundisha kuwa ingawa ni sawa kuhuzunika baada ya kushindwa au kupoteza kitu, mipango, malengo, hatma, na ndoto zetu, kukatishwa tamaa na kurudishwa nyuma na kufa moyo wakati fulani, huzuni hii haipaswi kutuzuia kuendelea mbele. Samweli alikuwa amekwama kwenye "jana" akihuzunikia kukataliwa kwa Sauli, wakati Mungu alikuwa tayari anashughulikia "leo na kesho" akimwandaa Daudi kwa mpango wake mkubwa zaidi. Mungu anakuandalia kesho iliyo bora zaidi hata kama leo inaonekana yenye matumaini hafifu, ya kukatisha tamaa, ya kuhuzunisha, ya kuvunja moyo. Waza kesho yako iliyo njema pamoja na Mungu.

Daudi Kijana anapakwa mafuta kuwa Mfalme wa Israeli: Upendeleo!
Daudi Kijana anapakwa mafuta kuwa Mfalme wa Israeli: Upendeleo!   (Vatican Media)

Jambo la pili: Kuteuliwa kwa Daudi kuwa Mfalme ni tendo la upendeleo wa Kimungu, kupitia yeye Mungu anatimiza kusudio lake. Sehemu hii tuliyosoma leo, Mwenyezi Mungu anamwagiza Samweli, acha kulia, “Ijaze pembe yako mafuta, uende, nami nitakupeleka kwa Yese maana nimejipatia Mfalme katika wanawe” Kama vile Mungu alivyomwita na kumchagua Abramu, ni kwa upendeleo huo huo Mwenyezi Mungu anajichagulia Daudi Mtumishi wake. Si kwa sababu Daudi alikua na jina kubwa, sio kwa sababu alikua na nguvu, sio kwa sababu alikuwa maarufu, bali kwa sababu ni Mungu mwenyewe alimpendelea, ili kupitia yeye Ahadi aliyonena na Ibrahimu, Ahadi ya Mkombozi itimie. Ndugu mpendwa, Mwenyezi Mungu kwa njia ya sakramenti ya ubatizo ametupendelea. Hatukustahili kuitwa tena watoto wa Mungu, lakini Mungu mwenyewe kwa upendo wake, kwa uhuru wake mwenyewe, anatutafuta tena, anatupaka mafuta na kutuweka wakfu. Anafutanya kuwa wafalme, manabii na makuhani ili tumtumikie yeye. Sambamba na wito wetu huo wa kwanza, Mwenyezi Mungu bado amemwinua kila mmoja wetu katika njia yake ili awe baraka.  Mwenyezi Mungu ameahidi baraka kupitia maisha yako katika familia, Mungu ameahidi baraka kupitia maisha yangu kama Padre, kila mmoja anaishi ndani ya mpango wa Mungu ulio mwema na mkamilifu. Ishi kusudio la Mungu, Mungu anataka akutumie wewe kutimiza mpango wake, anataka akutumie kama chombo cha kusambaza neema na baraka zake, anataka akutumie kama alama ya ushuda wa wema na neema yake ya bure hata pasipo mastahili yetu.

Mungu huwatayarisha na kuwakamilisha wale anao wachagua kwa utume
Mungu huwatayarisha na kuwakamilisha wale anao wachagua kwa utume   (@Vatican Media)

Jambo la tatu: Mwenyezi Mungu anawachagua wale walio wanyofu wa Moyo: Vigezo vya kimungu dhidi ya vigezo vya kibinadamu. Nabii Samweli anapofika kwa Yese, anapowaona wanawe tayari alikua na picha kwamba Mfalme alikua ni mtu mwenye mwonekano wa namna gani, ndio maana anapomwona mwana wa kwanza wa Yese (Eliabu), anafikiri moja kwa moja kwamba Mungu angelimchagua huyo. Hali kadhalika Yese naye alikuwa na mtazamo wake ndio maana hakuwaza kamwe kama Daudi aweza kuwa mteule wa Bwana. Samweli kwa haraka anatazama vigezo vya nje, lakini Mungu hatazami hayo. Mwenyezi Mungu anamwambia, “Usimtazame uso wake, wala urefu wa kimo chake, kwa maana mimi nimemkataa. Bwana haangalii kama binadamu aangaliavyo” Yese akawapitisha wanawe saba, lakini Bwana hakuwachagua hawa. Mwishoni anamchagua Daudi na kumpaka mafuta kuwa Mfalme. Ndugu mpendwa mara kadhaa twaweza kujiona tupo dhaifu mbele za watu, hata twaweza kuonekana hivyo pia. Lakini mbele za Mungu sisi tu wenye thamani kubwa sana machoni pake. Twaweza kukataliwa kwa vigezo vya kibinadamu, kwa sababu ya unyonge, umaskini, udhaifu, kwa sababu hatujulikani, hatuna wa kutuunganisha, lakini kwa Mungu sisi ni wateule wake. Twaweza kukataliwa hata na watu wetu wa karibu kabisa kama Daudi alivyokataliwa hata na Baba yake na ndugu zake, alionekana hana umuhimu sana, hana thamani, hana sifa huyu ya kuwa Mfalme, hana umbo la kifalme, kijana mdogo tu, mchunga kondoo, aliyekuwa wa mwisho katika umuhimu. Samweli anatuma watu wakamlete. Wanadamu hutazama sura ya nje, Mungu anatazama unyofu wa ndani. Mwenyezi Mungu anamwambia Samweli, “Ondoka ukamtie Mafuta, maana huyu ndiye.” Wakati wanadamu tunavutiwa na elimu, muonekano, au mali, Mungu anatafuta utii na usafi wa moyo. Hii inatukumbusha kuwa thamani yetu haitokani na kile watu wanachoona, bali kile tulicho mbele za Mungu. Daudi alikuwa mdogo kuliko wote na alikuwa machungani akichunga kondoo (kazi ya hali ya chini). Hii inatufundisha kuwa hakuna aliye mdogo sana mbele za Mungu. Mungu hutumia “vinyonge vya dunia ili kuviaibisha vyenye nguvu” (1 Kor 1:27). Mungu anamwandaa kwa siri katika mambo makubwa, na ndivyo ilivyo hata kwetu. Mipango ya Mungu hufanyika katika ukimya, akituandaa kwa ajili ya kusudi lake kubwa zaidi.

Baada ya kuwekwa wakfu wanatumwa kutangaza Injili
Baada ya kuwekwa wakfu wanatumwa kutangaza Injili   (@Vatican Media)

Jambo la nne: Mwenyezi Mungu anamwimarisha kila anayemwita. Samweli mara baada ya kumpaka mafuta Daudi kuwa Mfalme, tunaambiwa Roho ya Bwana ikamjia Daudi kwa nguvu tangu siku ile. Tendo la kupakwa mafuta halikuwa ishara tu; ulikuwa ni uhamisho wa nguvu. Daudi hakuachwa na uwezo wake wa kibinadamu kama mchungaji, bali alipewa uwezo wa Kimungu ili kutimiza majukumu makubwa ya kifalme yaliyokuwa mbele yake. Kumbe tangu siku ile, Daudi hakuwa tena “yule kijana mchungaji” tu, bali alikuwa Mpakwa Mafuta wa Bwana (Messiah kwa Kiebrania). Hii ilimpa nguvu, hekima na ujasiri (kama alioutumia alipompiga Goliath) na zaidi ya yote moyo wa unyenyekevu na utii kwa amri na maagizo ya Mungu. Ndugu mpendwa, nasi sote tunapokabidhiwa majukumu na wajibu wowote kutoka kwa Mungu, amekwisha tupatia pia nguvu ya kuweza kuyatekeleza. Mungu hakuwaita wala hawaiti watu walio tayari wakamilifu, bali huwatayarisha na kuwakamilisha wale anaowaita. Tunapopewa jukumu lolote na Mungu (kama mzazi, kama Padre, kama Mtawa, kama kiongozi, au mfanyakazi), hatufanyi kwa akili zetu tu bali Roho Mtakatifu anatupatia vifaa au zana za kufanikisha jukumu hilo. Hii inatukumbusha nguvu ya Ubatizo na Kipaimara. Kama ilivyokuwa kwa Daudi, u nasi tulipopakwa mafuta ya Krisma katika ubatizo na kipaimara, tulipokea Roho yuleyule anayetupa ujasiri wa kushinda "Magoliathi" wa maisha yetu (dhambi, hofu, na majaribu) tutakayokutana nayo katika miito yetu.

Kiri ya Imani ya yule Kipofu: Nabii, Bwana na Masiha
Kiri ya Imani ya yule Kipofu: Nabii, Bwana na Masiha   (@Vatican Media)

Somo la Injili Ni Injili kama ilivyoandikwa na Yohane 9:1-41. Somo la Injili Takatifu kutoka katika Injili ya Yohane ni simulizi refu la kuponywa kwa mtu aliyekuwa kipofu tangu kuzaliwa kwake. Muujiza huu wamfunua Kristo kama nuru ya ulimwengu, ambaye alifika duniani ili kuondoa upofu wetu kwa sababu ya dhambi na kutuonesha njia iendayo kwa Mungu kwenye uzima wa milele. Katika somo hili ningependa tutafakari kwa kina mambo manne yafuatayo ambayo ni msingi sana katika kuelewa ujumbe wa Injili hii ya leo, na kuona ni jinsi gani yanatugusa sisi pia katika maisha yetu ya kila siku, hususani katika safari yetu kuelekea Fumbo la Pasaka. Jambo la kwanza: Safari kutoka kwenye giza/upofu kwenda kwenye nuru yahitaji unyenyekevu na utayari wa moyo. Bwana wetu Yesu Kristo alipokuwa akipita alimwona mtu huyu aliyekuwa kipofu tangu kuzaliwa. Mtu huyu alikua ni kipofu wa mwili lakini roho yake ilikua tayari kumpokea Kristo, na kumwamini kama masiya, anahama kutoka kutokuamini mpaka kumkiri Kristo kama Masiya. Tukio hili lilitokea katika siku ya Sabato, na hili linaleta mgogoro kila mara kati ya Yesu na Mafarisayo. Mafarisayo ambao ijapokuwa kimwili walikua wanaona, kiroho walikua ni vipofu kwa kuwa hawakuwa tayari kumpokea Kristo, wala kuona ukuu na utukufu wa Mungu ndani ya Kristo. Walikua na majivuno na kiburi kwa cha sheria, hivyo hawakumwamini Kristo wala wahakuziamini kazi zake. Hawa ndio walikua vipofu kweli kweli. Ndugu mpendwa sisi pia kwa sababu ya dhambi tulikua vipofu gizani. Kristo kwa njia ya ubatizo ameanzisha safari mpya ndani mwetu, safari ya kutoka kwenye giza kwenda kwenye nuru. Ni safari endelevu inayotudai kubaki daima katika katika Mwanga wa Kristo na kutokubali kamwe kurudi tena gizani. Tunapokubali mapungufu yetu na dhambi zetu mbele za Mungu, tunafungua mlango wa muujiza. Kipofu alitii agizo la Yesu la kwenda kunawa Siloamu bila kubisha, kwa sababu alijua hana ufumbuzi wa tatizo lake isipokuwa kwa Yesu. Kumbe nasi tunapaswa kujinyenyekesha na kukiri hitaji letu la nuru ya Mungu katika giza la maisha yetu. Mafarisayo walijifungia katika “boksi la sheria,” kwamba wao ni wana wa Abrahamu, ni taifa teule, wataalamu wa sheria na maandiko, wakifikiri kuwa walijua kila kitu. Sisi pia elimu, akili, fedha, mali, vyeo, vipaji, vyaweza kututia upofu tusiione nafasi ya Mungu katika maisha yetu, tukaona kana kwamba tunajua kila kitu, tukawa wepesi kuona madhaifu na kuwahukumu wengine bila kuona undani wa maisha yetu, tukaona kana kwamba tunajitosheleza sisi wenyewe kama hawa mafarisayo. Tumwombe Kristo atuondolee kiburi na majivuno ili tumtambue na kumkiri yeye kama nuru halisi katika giza la maisha yetu, na tutambue pia nafasi ya wengine.

Ukuu na Utukufu wa Mungu umedhihirishwa kwa njia ya Kipofu
Ukuu na Utukufu wa Mungu umedhihirishwa kwa njia ya Kipofu   (@Vatican Media)

Jambo la pili: Mateso si Ishara ya kuadhibiwa na Mungu bali ni njia Mungu anayodhihirisha kazi yake. Mitume wa Yesu wanamuuliza Yesu swali wanapokutana na kipofu huyu kwamba, “Rabi, ni yupi aliyetenda dhambi, mtu huyu au wazazi wake hata azaliwe kipofu?”  Katika Agano la Kale watu waliamini kuwa kulikua na uhusiano kati ya mateso mtu aliyopitia na dhambi, au zake au za wazazi wake, ndio maana wanafunzi hawa wanauliza swali hili. Yesu anasema upofu wa yule mtu haukutokana na laana au dhambi ya wazazi wake, bali ilikuwa fursa ya kazi za Mungu kuonekana. Yesu anatuambia kuwa si kila tatizo ni matokeo ya dhambi. Kwa kukataa nadharia ya laana, Yesu anampa yule kipofu (na sisi pia) utu na heshima, kwamba, Mateso yetu hayamaanishi kuwa Mungu ametukataa. Ndugu mpendwa, Kristo akiisha kutoa fundisho hilo kwa wanafunzi wake, alitema mate chini, akafanya tope kwa yale mate. Akampaka huyu kipofu tope za macho, akamtuma akanawe katika birika la ya Siloamu naye akarudi anaona. Kupitia kipofu huyu utukufu wa Mungu, nguvu ya Mungu imedhihiria, kama Masiya. Mara kadhaa nasi tunapopitia mateso hujiuliza maswali, “kwa nini mimi?”  Hii hutupelekea kuwaza na kutafuta pengine sababu za nyuma zilizotupelekea kuwa katika shida na changamoto hizi. Kristo leo anatualika tubadili mtazamo, swali letu kila mara tunapopitia mateso twapaswa kujiuliza, “Mungu anataka kusema nini nami katika hali hii?” Kumbe hata katika mapito magumu ya sasa, Mungu anaweza kuwa anajenga ushuhuda ambao utawatia moyo wengine hapo baadaye. Hii inaonyesha kuwa Mungu anaweza kutumia vitu duni (udongo) na hali mbaya (upofu) kuanzisha uumbaji mpya. Mateso yako yanaweza kuwa malighafi ambayo Mungu anatumia kutengeneza kitu kipya na bora zaidi ndani ya roho yako. Kumbe nasi tunapoteseka tunashiriki katika mateso ya Kristo, kama anavyotuambia Mtume Paulo, “Sasa nayafurahia mateso niliyo nayo kwa ajili yenu, tena nayatimiliza katika mwili wangu yale yaliyopungua katika mateso ya Kristo, kwa ajili ya mwili wake, yaani, kanisa (1:24). Leo tunaalikwa, badala ya kulaumu hatima (destiny) au kutafuta mchawi tunapokwama, tunaitwa kutulia na kumuuliza Mungu, “Bwana, dhihirisha utukufu wako katika udhaifu wangu huu.” Bwana, nipe nguvu ya kukuona wewe hata katika msalaba wangu.

Utukufu na Ukuu wa Mungu Unadhihirishwa hata kwa njia ya mateso
Utukufu na Ukuu wa Mungu Unadhihirishwa hata kwa njia ya mateso   (@Vatican Media)

Jambo la Tatu: Safari ya Imani ni mchakato, sio jambo la haraka na la mara moja. Kuponywa kwa kipofu huyu kunaonyesha jinsi imani inavyokua. Kipofu anaanza kwa kumwita Yesu “mtu yule” Hapa anamwona Yesu kama mwanadamu wa kawaida tu anayefanya mambo ya ajabu. Ni hatua ya kwanza ambapo mtu anajua habari za Kristo Yesu (historical Jesus) lakini bado hana uhusiano wa kiroho naye. Kisha “Nabii” Hapa imani yake imekua. Anaanza kuelewa kuwa Yesu ana nguvu inayotoka kwa Mungu. Hapo ndipo anapoanza kuitetea imani yake mbele ya maadui, Mafarisayo waliokuwa wakimsumbua kwa maswali mengi. Hii ni hatua ya kutambua kuwa Yesu ana nafasi maalumu katika mpango wa Mungu, na mwishowe anamwabudu kama “Bwana” Hapa ndipo kilele cha imani. Haishii tu kumpa sifa (nabii), bali anampa ibada (anamwabudu). Anamtambua Yesu kama Mungu na Mwokozi wake binafsi. Dominika hizi tatu za Kwaresima yani 3,4 na ya 5 ni wakati wa maandalizi kwa Wakatekumeni ambao watabatizwa katika mkesha wa Pasaka. Masomo haya yanatupa nafasi ya kutafakari hasa juu ya ubatizo wetu, namna tulivyopokea Imani na hatua kwa hatu inakua ndani mwetu. Tunakumbushwa katika domika ya leo kwamba tunapaswa kusaidiana katika kukua katika Imani. Wapo ambao ndio kwanza wamemjua Kristo, watoto waliobatizwa, hata wakatekumeni ambao wapo bado kwenye mchakato wa kumjua na kumwamini Kristo. Tunapaswa kuwasaidia si tu kwa maneno bali hata kwa mifano ya maisha yetu, ili wazidi kuimarika, Imani ikue na kushika mizizi katika mioyo yao. Je, Watoto wetu tunawakuza katika mchakato huu wa Imani? Tunapowapeleka mashuleni, tuna uhakika wataendelea kukuzwa katika misingi ile ile ya Imani walimobatizwa? Tusikae mbali na wale walioimarishwa. Yesu hayupo mbali na wale aliowaimarisha. Tunaona namna anavyomtafuta huyu aliyeponywa hata baada ya kufukuzwa na mafarisayo kutoka hekaluni. Mungu hachezi mbali na sisi; tunapopiga hatua moja ya imani, Yeye anakuja kutupa nuru zaidi ya kumtambua.

Hii ni Dominika ya Furaha: Fumbo la Pasaka Liko Karibu
Hii ni Dominika ya Furaha: Fumbo la Pasaka Liko Karibu   (@Vatican Media)

Jambo la nne: Katika ubatizo tunapewa nuru na kutumwa kumshuhudia Kristo. Baada ya Yesu kumpaka yule kipofu tope za macho alimwambia, “Nenda kanawe katika Birika ya Siloamu. “Siloamu maana yake “Aliyetumwa” Basi akaenda na kunawa, naye akarudi anaona. Ndugu mpendwa, dhambi ni kama tope linalotuzuia macho yetu kuweza kuiona nuru ya kweli. Tendo la kipofu huyu kujiosha katika Birika la Siloamu ni Ishara ya Ubatizo wetu unaoondoa upofu, unaoondoa tope katika roho zetu ili tuweze kuiona nuru ya kweli, Kristo Masiha aliyetumwa na Baba kuja ulimwenguni. Kipofu anaponawa katika maji ya Siloamu, anajizamisha katika mamlaka ya Kristo aliyetumwa na Mungu. Nasi pia kwa Ubatizo tunajizamisha katika mamlaka ya Kristo. Tunakuwa Watoto wa Mungu na Watoto wa Mama Kanisa Mtakatifu. Birika hili pia linaashiria Kanisa, ambalo limetumwa na Kristo kuwafundisha, kuwabatiza watu na kuwafungua macho ya mioyo yao. Neno “Siloamu” (Aliyetumwa) linatukumbusha kuwa baada ya sisi "kuoshwa" na "kufumbuliwa macho" katika Ubatizo, sisi pia tunatumwa. Kama Kristo alivyotumwa na Baba, nasi kwa ubatizo wetu tunashirikishwa kazi hiyo ya umisionari, kwa kupewa ofisi tatu za Kristo yaani, Ukuhani, Ufalme na Unabii. Kipofu anakua mmisionari kwa wazazi wake na kwa mafarisayo. Nasi hatupaswi kubaki na neema ya Ubatizo sisi wenyewe, tunaalikwa kudhihirisha upya wa maisha yetu kwa kuishi kweli kiaminifu Ahadi zetu za ubatizo na kwa kumshuhudia Kristo bila woga na bila kuchoka. Kuwa nuru, kusimamia haki, kusema ukweli, kupenda, kusamehe, kuhurumia, kama Ujumbe wa Kwaresima kutoka katika Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC unavyotuasa, kamwe tusiochoke kutenda mema!

Kwa Maji na Roho Mtakatifu waamini wanazaliwa upya!
Kwa Maji na Roho Mtakatifu waamini wanazaliwa upya!   (@Vatican Media)

Somo la Pili ni kutoka katika Waraka wa Mtume Paulo kwa Efe 5:8-14. Katika somo hili la pili, Mtume Paulo anatufundisha kuwa ni kwa njia ya Ubatizo sisi sote tumeingia katika mwanga wa Kristo. Hivyo mwanga huu unatualika katika upya wa maisha kwa kuwa daima wana wa nuru. Hatupaswi tena kuchanganya mwenendo mpya wa Kikristo na mwenendo na matendo ya kale ya giza kama anavyotufundisha sehemu nyingine Mtume Paulo kwamba, “Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita tazama! Yamekuwa mapya” (2 Kor 5:17). Tumwombe Kristo atusaidie ili tuishi kweli upya wa maisha katika nuru ya ufufuko wake. Hitimisho: Katika Dominika ya leo, tuombe neema ya Mungu na tujiombee sisi sote ili daima tuishi katika nuru, yaani kuchuchumilia kila wakati upya wa maisha katika utakatifu.

Tafakari D4 Kwaresima
13 Machi 2026, 10:23