Dominika ya Matawi Mwaka A:“Hosana kwa Mwana wa Daudi!”
Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.
Karibu mpenzi msilikizaji na msomaji wa tafakari ya Neno la Mungu kutoka hapa Vatican News. Leo Kanisa linaanza Juma Kuu kwa shangwe na unyenyekevu. Tunabeba matawi, tunaimba Hosana, na tunamkaribisha Yesu akiingia Yerusalemu. Lakini shangwe ya leo ina kivuli kizito: tunajua kwamba mji uleule ulimopokea kwa vigelegele, na shangwe baada ya siku chache utapaza sauti kusema “Msulubishe!”Dominika ya Matawi ni Dominika ya moyo unaoyumba: kati ya shangwe na mateso, kati ya matumaini na hofu, kati ya ushindi na msalaba. Ndani ya mvutano huu ndipo Neno la Mungu leo linatualika tujitazame sisi wenyewe. Yesu anaingia Yerusalemu si juu ya farasi wa vita, bali juu ya punda. Hii ni ishara ya wazi: Yesu si mfalme wa nguvu za kijeshi, bali Mfalme wa amani. Anatimiza unabii, lakini kwa namna isiyotarajiwa na wengi. Umati unashangilia, lakini wengi wanatarajia Yesu atawashinda Warumi, atabadilisha siasa, atawapa ushindi wa haraka.
Yesu, badala yake, anakuja kubadilisha mioyo.Katika dunia ya leo, bado tunatafuta waokozi wa haraka: viongozi, mifumo, teknolojia. Lakini Yesu anatukumbusha kwamba wokovu wa kweli huanza kwa unyenyekevu na toba, si kwa nguvu za nje. Ni mpole, naye amepanda punda, naam, mwanapunda mtoto wa punda.. ni nani huyu? Huyu ni yule nabii, Yesu, wa Nazareti ya Galilaya… ni nani huyu? Bwana mwenye nguvu hodari, Bwana hodari wa vita.. fungukeni enyi malango, fungukeni enyi malango ya milele, Mfalme mtukufu apate kuingia. Bwana wa majeshi, Yeye ndiye Mfalme wa utukufu (Zab 24:7-10)… ni Mtumishi mwaminifu na mteule wa Mungu, anamtumaini Bwana, amekaza uso wake kama gumegume kuelekea Yerusalemu (somo I, Isa 50:4-7), naam amekwisha kufika, nguo zimetandazwa, matawi yapepea, hosanna yarindima… hebu tuone atafanya nini akifika mjini.
Katika somo la kwanza, tunasikia sauti ya Mtumishi anayeteseka:“Sikuficha uso wangu nisipate fedheha na mate.” Huu ni utabiri wa wazi wa mateso ya Kristo. Yesu hakurudi nyuma alipodhalilishwa, hakujitetea alipopigwa. Kwa nini? Kwa sababu alitumainia Mungu. Katika dunia ya leo, mateso yanawagusa wengi: waliodhulumiwa, wakimbizi, wagonjwa, na wale wanaosimama upande wa ukweli. Yesu anaungana nao. Dominika ya Matawi inatukumbusha kwamba Mungu hayuko mbali na mateso ya wanadamu. Huyu ni Yesu, Mwana wa Maria, huyu ni Mfalme wako, tazama anakuja kwako jinsi hiyo… tujiweke basi mkao mwema wa kumpokea.. si tu kwa matawi ya mitende iharibikayo bali kwa matawi yasiyonyauka kutoka mti wa uzima, mti uzaao matunda wakati wote, matunda yanayodumu, matunda yastahiliyo uzima wa milele, yaani Kristo Mwenyewe aliye Edeni mpya na ya milele.. tujiunge na umati wa wayahudi kuimba “Hosanna Mwana wa Daudi..” si hosanna ya midomo bali hosanna ya moyo, yenye kumaanisha, hosanna ya utukufu.
UFAFANUZI
Tazama Mfalme wako anakuja kwako… huyo ni zao la upendo wa Baba kwetu, anatujia muda sahihi tunapomuhitaji zaidi, tumechoka hatuna hali, mnyukano na Ibilisi ni mkubwa mno kutuzidi, Mfalme wetu amekuja apate kutushindia.. mbele yake shetani anaanguka kama umeme na kwa hakika hainuki tena! jamii imepumbazika kwa mengi, ya udanganyifu na uozo, yasiyotazamika wala kugusika, uharibifu wa dhana ya ndoa, familia na ujinsia na wajibu za wanaume na wanawake. Kwa masikitiko makubwa, yale yahusuyo imani na maadili, uongozi na malezi, uadilifu na utu, fadhila na tunu, wengi tumeyaacha hayo na kukumbatia ulimwengu, kwa vigezo dhaifu vya uhuru na haki za binadamu.. tazama Mfalme wetu anakuja kwetu, apate kutusaidia, ‘Maranatha O Yesu!’... ‘njoo Bwana Yesu utuokoe twakusihi.
Mtume Paulo anatupa kiini cha imani yetu:“Alijifanya mtumwa… akajinyenyekeza hata mauti, naam, mauti ya msalaba.” Yesu alipanda chini ili atupandishe juu. Utukufu haukupitia njia ya kiburi, bali njia ya unyenyekevu na mateso. Katika dunia ya leo inayosifia ubinafsi, mashindano na nguvu, ujumbe huu ni kinyume kabisa. Lakini ni ukweli wa Injili: anayejinyenyekeza, atainuliwa. Mtakatifu Fransisko wa Assisi aliishi wimbo huu wa Paulo. Alimfuata Kristo mnyenyekevu na maskini, akakubali kudharauliwa, lakini maisha yake yakawa wimbo wa sifa kwa Mungu. Katika mwaka huu wa kumuenzi Mtakatifu Fransisko wa Assisi miaka 800 baada ya kifo chake, tunamkumbuka kama mtu ambaye hakusema Hosana kwa maneno tu, bali kwa maisha yake yote. Alimkaribisha Kristo:Kwa kuacha utajiri, Kwa kukumbatia maskini,Kwa kuheshimu uumbaji. Mt. Fransisko alitambua kwamba kumpokea Kristo kama Mfalme kunamaanisha kumfuata hadi msalabani, si kumpigia makofi tu njiani.
Kwa nini tunashika matawi
Tazama Mfalme wako anakuja kwako.. ni kwa sababu hapo mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu lakini hakuona hilo kuwa jambo la kushikamana nalo akaacha utukufu, akawa mtii hata mauti naam, mauti ya msalaba… ni vema basi nayo ni haki kabisa kila goti lipigwe kwa Jina lake na kila ulimi ukiri ya kuwa Yesu Kristo ni Bwana kwa utukufu wa Mungu Baba. Pamoja na mema anayotuletea na sisi kufurahi tunaalikwa tutathmini uhalisia wa ufuasi wetu… kwa nini tumeshika matawi? Kwa nini tunaimba hosanna? Kwa nini tumo ndani ya maandamano? Je, tumo ndani ya umati wa watu tunaenda tu bila kujua tunalolifuata? kwa nini tunashangilia?
Historia ndefu ya mateso ya Kristo ilivyoimbwa au kusomwa leo vizuri kabisa kutoka Injili (Mt 26:14-27:66) inadhihirisha namna tunavyoweza kuwa wepesi na watupu katika imani na hivi kujikuta tu kwenye maandamano bila kujua tunachokifuata na tunachofanya… umati huu unamkaribisha Kristo kwa shangwe kuu, halafu siku sita tu baadaye umati huuhuu unapaza sauti mbele ya Pilato za kumkana Kristo na kumtaka muuaji, Baraba arudi tena mtaani aendelee kuwanyoosha hata leo hii tunashuhudia mahali pengi duniani tawala na mahakama hazitoi haki wengi wanabambikiziwa kesi na waharifu waachwa huru waendelee kuumiza watu hasa wanyonge na wapenda haki na ukweli! Sisi ndio umati huu wa watu, tunapokea Ekaristi kila siku, tumepokea Kipaimara, tumefunga Ndoa na pete za madini vidoleni zinashuhudia jambo hili jema, hata hivyo tumejifunga kwa kiasi gani na kumfuata Kristo mteseka? Watu walimkimbia Bwana dakika aliyowahitaji zaidi, hakukuwa na yeyote, Msalaba mzito ndio ulikuwa egemeo lake, kiti chake, na silaha yake pekee.. kwa Msalaba aliaibika na kwa Msalaba aliushindia ulimwengu ushindi usiosemeka… mimi na wewe, sisi, tumeitwa kwa Jina lake kwa mujibu wa ubatizo wetu, tuone basi tunakuwa faraja kwa mateso yake kwa kufanya japo kidogo na dada mkubwa.
Mtakatifu Veronika na Simoni wa Kirene
Mtakatifu Veronika kwa kuufuta uso wake uliochafuka kwa jasho na damu kadhalika kaka yetu Simoni wa Kirene kwa kutenda ipasavyo wajibu zetu, kuishi mapendo kamili, kuzishika amri, kupokea sakramenti na kusali, kudumu katika misingi ya utu na adabu njema, malezi bora ya watoto hasa wa kiume sababu katika nyakati zetu hizi hawa ni wahanga wakubwa zaidi wa unyanyasaji na uharibifu. Hii ni Dominika ya mateso ya Bwana, Siku kuu ya matawi inayomuonesha, kumdhihirisha na kumtangaza Kristo aliye Mfalme wa mbingu na ulimwengu, tazama anakuja kwetu… ni siku inayofungua mlango mkuu kuingia wiki kuu yenye kuibadili historia ya ulimwengu na kuunyanyua tena ubinadamu ulioanguka, kuuganga ubinadamu uliougua mahututi na kuunururisha upya ubinadamu uliochakaa…
Tujitahidi basi, japo kwa shida hivyohivyo kuitendea haki wiki hii kuu, ni siku hizi chache kabisa katika mwaka wote, tusitende dhambi, tufunge na tusali, tumshike mkono masikini mmoja au yatima, mjane na mzee, zaidi sana tuipe mioyo yetu nafasi kwa kuondoa yote yaliyoijaza ikiwamo chuki, hasira, kinyongo, hofu na mawazo kwa Sakramenti ya Upatanisho kusudi ipatikane nafasi ya kupokelea neema na baraka zinazotujia kutoka Kalvarini na nyingi zaidi kutoka bustani mle mnamong’aa kwa nuru kuu alfajiri ile njema ya siku ya kwanza ya Juma kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
Dominika ya Matawi inatuuliza kwa ukimya na tujibu kwa ukimya na unyoofu. Je, Hosana yetu ni ya kweli au ya msimu na mazoea? Je, tunamfuata Kristo anapotupeleka Golgota tupo nae au? Je, tuna ujasiri wa kufungua mioyo yetu kabisa? Tunapoingia Juma Kuu, tusiishie kwenye matawi mikononi, bali tumruhusu Kristo aingie mioyoni mwetu. Na tukimfuata kwa unyenyekevu, kama Mtakatifu Fransisko wa Assisi, basi hata baada ya msalaba, tutashuhudia ufufuko. Amina.