Maaskofu wa Zimbabwe waonya marekebisho ya Katiba yanatishia misingi ya kidemokrasia
Na Sr. Christine Masivo, CPS -Vatican.
Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Zimbabwe umekosoa vikali Muswada wa Marekebisho ya Katiba ya Zimbabwe kufungu Namba 3 cha 2026,huku likionya kwamba kuna hatari ya kudhoofisha kanuni za kidemokrasia zinazosimamia utawala wa taifa. Katika taarifa iliyotolewa mnamo tarehe 19 Machi 2026, maaskofu walionya kwamba rasimu ya sheria "inapinga msingi wa maisha yetu ya pamoja," ikizua wasiwasi mkubwa kuhusu utawala, uaminifu wa umma, na manufaa ya wote.
Wasiwasi wa kujilimbikizia madaraka
Marekebisho yaliyopendekezwa yangeongeza muda wa urais na bunge kutoka miaka mitano hadi saba na yanaweza kumruhusu Rais wa sasa Emmerson Mnangagwa, mwenye umri wa miaka 84, kubaki madarakani hadi 2030. Pia inapendekeza kubadilisha uchaguzi wa moja kwa moja wa rais na mchakato wa uteuzi wa bunge na kuhamisha mamlaka ya utendaji miongoni mwa taasisi muhimu za serikali. Maaskofu walionya kwamba hatua kama hizo zinahatarisha kuhamisha madaraka kutoka kwa raia na kudhoofisha uwajibikaji wa kidemokrasia. "Mamlaka yote halali hutoka kwa watu," walisisitiza, wakibainisha kuwa Wazimbabwe waliwapa viongozi wao muhula wa miaka mitano katika uchaguzi wa 2023, uliopangwa kukamilika mwaka wa 2028.
Kulinda Taasisi na Uadilifu wa Kidemokrasia
Taarifa hiyo ilionyesha umuhimu wa Katiba ya 2013, iliyopitishwa baada ya miongo kadhaa ya utawala wa hayati rais Robert Mugabe, ambayo ilianzisha mipaka ya mihula na kuimarisha udhibiti na mizania ya kitaasisi. Mageuzi haya yalibuniwa ili kukabiliana na utawala wa chama tawala cha Zimbabwe African National Union-Patriotic Front na kuhakikisha uhuru mkubwa wa mahakama na uwazi wa uchaguzi. Maaskofu walisisitiza kwamba kudhoofisha mifumo kama vile tume huru na vyombo vya usimamizi wa uchaguzi kunaweza kuharibu imani ya umma na kuongeza mgawanyiko wa kitaifa. Walielekeza taasisi kama Tume ya Uchaguzi ya Zimbabwe na Tume ya Amani na Maridhiano ya Kitaifa kama nguzo muhimu za demokrasia. Wakihitimisha ujumbe wao, maaskofu walisisitiza kwamba amani ya kudumu inategemea haki, uwazi, na uhuru wa kitaasisi. Walihitimisha wakisema kwamba, "amani haidumu kwa nguvu, bali kupitia utawala wa haki na uwajibikaji unaomtumikia kila raia sawa."
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku bonyeza hapa: Just click here.