Kenya:Katika jimbo la jangwani la Lodwar,Injili bado inapata ardhi yenye rutuba
Na Rose Achiego Ande – Lodwar, Kenya.
Katika Eneo la Kanisa lililoenea karibu kilomita za mraba 77,000 za ardhi ukame na nusu ukame huko Lodwar, Askofu John Mbinda, Jimbo hilo lililoko Kaunti ya Turkana, linapakana na Sudan Kusini, Ethiopia na Uganda, alijitambulisha na kuelezea hali halisi ya kijiongrafia na hali ya kichungaji. Katika maelezo yake Askofu alisema kuwa “Wanaoishi hapa ni watu wa Turkana, eneo hilo pia ni makao ya watumishi wa umma, wamisionari na wanaume na wanawake wa kidini kutoka sehemu zingine za Kenya. Kwa pamoja, huunda uwepo mdogo lakini wenye dhamira ya Kikatoliki katika kile ambacho Askofu Mbinda, mwana shirika wa Spiritan Fathers, alielezea kama "eneo la uinjilishaji wa kwanza."
Utume wa uwepo
Jimbo la Lodwar lina Parokia 33, nyingi ziko katika maeneo ya mbali sana. Hata hivyo, hizi si jumuiya zinazojitegemea. Sadaka ya Dominika katika Parokia kadhaa haitoshi hata gharama ya mafuta yanayohitajika kwa ajili ya ufanya utume. "Tuliunda Parokia hizi ili kuhakikisha kwamba Neno la Mungu linakaribia watu," Askofu alielezea. "Padre na Katekista lazima wawe karibu." Katika nchi ambapo jamii huhama kutafuta maji na malisho, Jimbo Katoliki pia limewafunza makatekista wahamaji ambao husindikizana na familia kwenye safari, wakipeleka Injili katika midundo ya maisha ya wachungaji. Hata hivyo, kazi hiyo ina gharama kubwa. Makatekista wanahitaji malezi na malipo ya kawaida. Mikutano inahitaji usaidizi wa usafiri katika njia ndefu na ambazo mara nyingi hazipitiki. Nje ya barabara kuu iliyopangwa lami hivi karibuni kutoka Kitale kuelekea mpaka wa Sudan Kusini, barabara nyingi zinabaki kuwa ngumu. Ufadhili wa huduma ya wachungaji, Askofu Mbinda alibainisha, unazidi kuwa mdogo. "Wachache wanataka kusaidia magari kwa ajili ya uinjilishaji au mafunzo kwa viongozi wa kawaida," alisema, akitoa wito kwa Makanisa yenye rasilimali bora kusaidia maeneo ya utume ambapo imani ni changa na dhaifu.
Njaa na furaha ya Ekaristi
Upungufu wa mali ni sehemu ya uhalisia wa kila siku. Halijoto huongezeka mara kwa mara zaidi ya nyuzi joto 37 Selsiasi. Upatikanaji wa maji, huduma za afya na huduma za msingi bado ni mdogo katika maeneo mengi. Askofu alisimulia nyakati zinazoonyesha ugumu na neema. Wakati wa sherehe ya Kipaimara katika parokia ya mbali, wanawake na watoto kadhaa walizimia, si kwasababu ya ugonjwa bali, walikuwa hawajala kwa siku mbili au tatu, alielezea. Alizidi kusema kwamba, “furaha ambayo wanayo wanapopokea neno la Mungu, na tabasamu zao hata katika shida, ndizo zinazotufanya tuendelee." Licha ya njaa na umaskini, Ekaristi inaadhimishwa kwa ari kubwa. Katika jumuiya hizi za jangwa, imani si nyongeza bali ni riziki.
Afya, maji na hadhi ya binadamu
Ikiwa imeongozwa na Wito wa Injili ya Mathayo 25, Jimbo la Lodwar linachanganya uinjilishaji na matendo halisi ya Upendo. Kupitia miundo yake ya Caritas na shughuli za kichungaji, jimbo linaendesha zaidi ya vituo 18 vya afya katika maeneo ya mbali, mara nyingi ambapo uwepo wa serikali ni mdogo. Hata hivyo, mabadiliko ya hivi karibuni katika mfumo wa bima ya afya wa Kenya, ikiwa ni pamoja na mabadiliko kutoka NHIF hadi mfumo mpya wa Bima ya Afya ya Jamii, yameacha vituo vingi vinavyoendeshwa na Kanisa vikipata shida. Kuchelewa kwa malipo kumefanya iwe vigumu kuwalipa wafanyakazi na kudumisha vifaa muhimu vya matibabu, na hivyo kuweka baadhi ya vituo katika hatari ya kufungwa. Zaidi ya huduma ya afya, maji ni muhimu kwa maisha. Jimbo linaendesha mojawapo ya programu imara zaidi za maji katika kaunti, kuchimba na kudumisha visima katika jamii za jangwa. "Maji ni mojawapo ya zawadi kubwa zaidi unazoweza kuwapa watu wanaoishi katika hali hizi," Askofu Mbinda alisema. Utunzaji wa mazingira pia ni sehemu ya dhamira. Jamii zinahimizwa kupanda na kutunza miti karibu na vituo vya maji, kukuza ustahimilivu katika hali mbaya ya hewa.
Kuhudumia wakimbizi huko Kakuma
Ndani ya Jimbo kuna moja ya makazi makubwa zaidi ya wakimbizi barani Afrika, Kambi ya Wakimbizi ya Kakuma, ambayo inahifadhi wakimbizi zaidi ya 250,000. Kanisa linashirikiana kwa karibu na washirika, ikiwa ni pamoja na UNHCR, kusaidia watu waliokimbia makazi yao. Makanisa ya Watawa, miongoni mwao Wasalesian wa Don Bosco, hutoa mafunzo ya kiufundi na elimu. watawa hutoa mafunzo ya ujuzi, kama vile ushonaji, ili kukuza kujitegemea. Kupunguzwa kwa ufadhili wa hivi karibuni duniani kumeathiri mgao na huduma za chakula kambini, na kuongeza mvutano. Hata hivyo Kanisa linabaki pale, likitembea na wakimbizi na kutetea utu wao.
Nchi yenye uwezo mkubwa
Licha ya changamoto kubwa, Askofu Mbinda aliona ahadi kubwa. "Uwezo mkubwa zaidi," alisema, "ni hamu ya watu kupata habari njema ya Mungu.” Katika eneo kavu la Turkana, udongo unaweza kuwa mgumu, lakini mioyo inabaki wazi. Jimbo la Lodwar linaendelea kupanda mbegu ya imani, mara nyingi kwa rasilimali chache lakini ikitegemezwa na furaha ya watu na imani tulivu kwamba utume, katika kiini chake, ni uwepo. Jangwani, Injili bado inapata ardhi yenye rutuba.