Ethiopia:Maaskofu wamewasihi Waethiopia kupinga chuki na kukataa mgawanyiko
Na Sr. Christine Masivo, CPS - Vatican.
Mkutano wa Maaskofu Wakatoliki wa Ethiopia (CBCE) umelaani wimbi la hivi karibuni la vurugu zinazowalenga raia nchini kote hasa mauaji katika Eneo la Arsi la Oromia. Maaskofu walionesha huzuni wao mkubwa katika taarifa iliyotolewa tarehe 9 Machi 2026, kuhusu ukatili na uharibifu unaowakabili watu wasio na hatia. Kulingana na Shirika la Kipapa la habari za Kimisionari la Fides, linabainisha :"Vurugu kama hizo dhidi ya watu wasio na ulinzi haziwezi kuhalalishwa na mafundisho yoyote ya kidini, utamaduni au sababu za kisiasa," Maaskofu walisema. Taarifa hiyo ilisainiwa na Kardinali Berhaneyesus Demerew Souraphiel, CM; Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Addis Ababa na Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Ethiopia(CBCE.) Maskofu walisema kwamba "mauaji na uharibifu huo si wa kibinadamu, na mashambulizi haya ya mara kwa mara yameleta hofu na mateso mengi miongoni mwa wenyeji. Kanisa linalaani vitendo hivyo na linatoa wito wa hatua za haraka za kuwalinda raia."
Mgogoro wa kibinadamu
Hali ya usalama inazidi kuwa mbaya katika maeneo ya Aris, ambapo wilaya kama vile Shirka, Merti, Guna, na Holonto zimekuwa vituo vya vurugu kali. Wengi wanakabiliwa na kunyongwa, majeraha, uharibifu wa mali na kulazimishwa kuhama. Ripoti iliyotolewa na Tume ya Haki za Binadamu (EHRC) mnamo Machi 2026 ilirekodi mashambulizi ya kimfumo katika eneo hilo yakihimiza uingiliaji kati wa haraka na mamlaka za shirikisho na za kikanda.
Mauaji
Kulingana na takwimu zilizopatikana Wakristo 34 wa Waorthodox waliuawa hivi karibuni, wakiwemo 26 Shurka na 4 Merti, na kufikisha idadi ya waathiriwa huko Shirka pekee hadi 164 tangu mwanzo wa mwaka. Vurugu hizi ziliwaacha watu 8 hospitalini, na wengine 8 hawajulikani walipo na wawili wakitekwa nyara. Mashuhuda walielezea familia zinazokimbia nyumba zao kwa hofu huku maelfu ya wakazi wakipoteza makazi yao huku hofu ikienea na uchumi wa eneo hilo ukiporomoka kutokana na msongo wa mawazo unaoendelea. Mashambulizi ya hivi karibuni yanakuja wakati wa mzozo wa mpaka wa Ormaia ulioanza mwaka 2025, mgogoro ambao tayari umesababisha vifo vya raia zaidi ya 1,244, hasa katika maeneo ya Ars na Ars Magharibi.
Wito wa umoja na mshikamano
Maaskofu walionesha wasiwasi wao kwa Wakristo wa Kiorthodox waliolengwa katika mashambulizi mwishoni mwa Februari, wakisisitiza umuhimu wa mshikamano wa kidini mbele ya vurugu. Mnamo Februari 26, watu wenye msimamo mkali waliripotiwa kuvamia soko huko Arsi Mashariki, eneo lenye amani kati ya Waislamu na Wakristo wa Waorthodox, na kuwafyatulia risasi wakazi. Wakristo ishirini wa Kiorthodox na mlinzi mmoja Muislamu, waliuawa huku wengine kadhaa wakiripotiwa kupotea na wanaaminika kutekwa nyara. Walioshuhudia walisema kwamba washambuliaji baadaye waliingia kanisani wakiimba nyimbo za kidini kabla ya kuwafyatulia risasi wale waliokuwa ndani.
Miongoni mwa waathiriwa alikuwa Padre. Nyumba na mazao yalichomwa moto, na wakazi wengi walikimbia nyumba zao hadi mji wa karibu kwa ajili ya usalama. Shambulio lingine lilifanyika tarehe 28 Februari 2026 katika eneo hilo hilo na kusababisha vifo zaidi ndani ya Kanisa. “Tunawasihi Waethiopia wasiwe na chuki,” Maaskofu walisema. “Msifuate njia ya matukio haya ya kusikitisha na mkatae majaribio yoyote ya kuunda mgawanyiko katika jamii yetu.”
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata taarifa mpya kwa kujisajili kwenye jarida letu la kila siku. Just click here.