Dominika ya Matawi Mwaka A:Kristo Yesu kuingia kwa shangwe Yerusalemu
Na Padre Paschal Ighondo –Vatican.
Tafakari ya Neno la Mungu, Dominika ya matawi mwaka A wa kiliturujia katika Kanisa. Ni siku ya kuadhimisha mambo makuu mawili. Kwanza ni Yesu kuingia Yerusalemu kwa shangwe kama mfalme siku sita kabla ya Pasaka. Katekisimu ya Kanisa Katoliki ikinukuu maandiko matakatifu inafundisha hivi; Yeye ambaye siku zote alikataza juhudi za watu za kutaka kumfanya mfalme, muda ulipowadia aliingia katika mji wa Daudi, Yerusalemu, kama Masiha, Mfalme wa utukufu, akipanda punda, akishangiliwa kama Mwana wa Daudi, anayeleta wokovu, sio kwa hila, wala kwa nguvu, bali kwa unyenyekevu na amani, wokovu ambao ataukamilisha katika Pasaka ya kifo chake na ufufuko wake (rej. KKK 569, 570).
Hivyo adhimisho la sehemu hii linapambwa na maandamano yetu sisi tukikumbuka tukio hili, na kumuungama Kristo Yesu kuwa ni mfalme wetu hapa duniani na katika Yerusalemu mpya, yaani mbinguni, kama sala ya kubariki matawi inavyosema: “Ee Mungu Mwenyezi wa milele, uyatakase matawi haya kwa baraka yako. Nasi tunaomfuata Kristo Mfalme kwa shangwe, utujalie tufike Yerusalemu ya milele kwa jina lake”. Maandamano haya yanapaswa kupambwa kwa nyimbo za furaha za kumsifu Mungu, na kumshangilia Kristo Yesu “mbarikiwa Mfalme ajaye kwa jina la Bwana; amani na utukufu juu mbinguni”. Yesu anaonya tusipoimba sisi au tukinyamaza “mawe yatapiga kelele”.
Sehemu ya pili ni adhimisho la mateso ya Yesu yanayotuingiza katika Juma Kuu, kiini cha mwaka mzima wa kiliturujia. Katika Katekisimu ya Kanisa Katoliki, mama Kanisa anatufundisha kuwa, Dominika ya Matawi ni mwanzo wa Juma Takatifu, kipindi cha kuyatafakari mateso makali aliyoyapata Kristo, na mapato yake, ushindi dhidi ya dhambi na mauti, ushindi unaodhihirishwa na utukufu wa ufufuko wake. Yeye alipanda Yerusalemu tayari kufa, kwani ni mara tatu alishatangaza juu ya mateso yake na kifo chake. Naye akikumbuka kifo dini cha manabii waliouawa Yerusalemu alisema: haimkini nabii afe nje ya Yerusalemu. Naye alipouona mji wa Yerusalemu, aliulilia akisema; Laiti ungalijua, hata wewe katika siku hii, yapasayo amani. Lakini sasa yamefichwa machoni pako (rej. KKK 557-560).
Fumbo la Pasaka,Msalaba na Ufufuko ni Kiini cha Habari Njema
Hivyo Fumbo la Pasaka, Msalaba na Ufufuko wa Kristo ni kiini cha Habari Njema ya mpango wa wokovu wa Mungu uliotimilika “mara moja tu kwa kifo cha ukombozi cha Mwanae Yesu Kristo” (KKK 571). Ni katika tumaini hili mama Kanisa katika sala ya mwanzo anasali hivi; “Ee Mungu Mwenyezi wa milele, ulitaka Mwokozi wetu atwae mwili na kuteswa msalabani ili wanadamu wapate kufuata mfano wa unyenyekevu wake. Utujalie kwa wema wako tuweze kuwa na uvumilivu kama yeye, na kustahili kuishi mateso yake ambayo tunaweza kuyafahamu vizuri tu, tukiyatazama pamoja na ufufuko wake”. Na hili ndilo tumaini letu.
Masomo yanayosomwa katika liturujia ya Neno dominika hii ni haya: Katika sehemu ya kwanza ni Injili ya Matayo 21:1-11, ikisimulia kuingia kwa Yesu Yerusalemu kwa shangwe. Na katika sehemu ya pili: I. Isa 50:4-7, II. Flp 2:6-11, III. Mt. 26:14-27:66. Nayo kwa ujumla wake yanamwonesha Yesu Kristo kuwa ni Masiha na Mfalme wa amani, mpole, mnyenyekevu, mvumilivu na hana makuu. Haya yote yanajidhihirisha kwa kuingia kwake Yerusalemu kwa shangwe akiwa juu ya mwanapunda na sio juu ya farasi kama wafalme wa nyakati hizo.
Kadiri ya mapokeo, mwanapunda ambaye hajatumiwa bado kwa kazi yoyote, alitumika kwa mambo matakatifu. Hivyo Yesu kupanda mwanapunda ni ishara ya utakatifu wake na ya kuwa anayoenda kuyafanya ni matakatifu. Tukio hili linatimiza utabiri wa nabii Zekaria unaosema; “Furahi sana Ee binti Sayuni, piga kelele ee binti Yerusalemu! Tazama Mfalme wako anakuja kwako. Ni mwenye haki, naye ana wokovu, ni mnyenyekevu amepanda punda, naam, mwana punda, mtoto wa punda” (Zek.9:9).
'Hakika Huyu alikuwa mwana wa Mungu'...
Masimulizi ya maandiko matakatifu yanasema kuwa watu waliochukua matawi, ishara ya ushindi na matumaini, walitandika nguo zao huku wakiimba nyimbo za furaha, na kuufanya mji wa Yerusalemu utikisike kwa kelele za shangwe, hivyo kuamsha hasira za wakuu wa Makuhani, Mafarisayo na Waandishi, hata wakaanza mikakati ya kumkamata. Hivyo nyakati za usiku walimkamata akiwa bustani ya Gethsemane akisali. Kesho yake alihukumiwa bila hatia, akapigwa mijeledi, akavikwa taji ya miiba, akadhihakiwa, akatemewa mate, akabebeshwa msalaba, akashika njia kuelekea Golgota. Ni safari ya mateso makali. Alipofikika Golgota, alisulibiwa, hatimaye akafa kifo kama cha mtu aliyelaaniwa, kwani maandiko matakatifu, katika kitabu cha Kumbukumbu la Torati 21:22-23 yanasema hivi: “Ikiwa mtu ametenda dhambi ipasayo kufa, nawe ukamtundika juu ya mti, mzoga wake usikae usiku kucha juu ya mti; lazima utazikwa siku hiyo hiyo. Kwani aliyetundikwa amelaaniwa na Mungu, asije akatia unajisi katika nchi yako akupayo Bwana Mungu wako iwe urithi wako”. Lakini jinsi kifo chake kilivyokuwa cha pekee, kiliwafanya walioshuhudia wasadiki uaguzi wa manabii na kusema; “Hakika huyu alikuwa mwana wa Mungu”.
Haya yote aliyotendewa Yesu, yanatufundisha kuwa hakuna utukufu pasipo mateso. Mateso na mahangaiko ya maisha yetu hapa duniani yanaakisi tu mateso yake kwa ajili ya dhambi zetu. Ni katika tumaini hili mama Kanisa anatuhimiza kuyavumilia mateso yanayotupata katika kuikiri na kuishuhudia imani yetu kwa Kristo, ili tuufikie utukufu wake na kuingia katika ufalme wa mbinguni, kama tukiyapokea kwa imani. Tukiwa na mtazamo huu kamwe mateso hayatakuwa kikwazo kwa imani yetu. Lakini mateso yatokanayo na dhambi zetu wenyewe, tusipotubu, kuomba msamaha na kubadilika, hayatuletei wokovu, bali yanatupeleka katika “moto wa milele aliotayarishiwa ibilisi na malaika zake”.
Kwa kutotimiza wajibu wetu kwa Kristo tunamkana Kristo
Katika simulizi la mateso ya Yesu, umati wa watu walipiga makelele wakisema Mwondoshe! Mwondoshe! Msulubishe! Msulubishe! Nasi kwa mawazo, maneno, na matendo yetu maovu, kwa kutokutimiza nyajibu zetu za kikristo, tunamkana Kristo na kunatoa mlio na makelele kama hayo tukisema, mwondoshe, mwondoshe, msulubishe, msulubishe. Petro alijaribu kupambana na nguvu za giza kwa upanga, na mara tatu alimkana Kristo. Je, sisi nasi hatuna fikra kama za Petro za kupambana na nguvu za shetani kwa ubanga na mambo ya giza, maseng’enyo, malumbano, mapigano, visasi na fitina? Tukumbuke kuwa Kristo Yesu amemshinda shetani na hila zake kwa uvumilivu, unyenyekevu, upole na utii wake kwa Mungu Baba. Nasi hatupaswi kumpigania kwa nguvu za kibinadamu na kishetani, bali kwa ushuhuda wa maisha mema. Jogoo amekwisha kuwika mara ya tatu, tulipokosea tujirudi, tujiweke chini ya msalaba, kwani hatuna tumaini lingine; “Japo kwao wanaopotea ni kikwazo na upuuzi”, kwetu sisi ni nguvu ya Mungu, alama ya ushindi, tukiutazama kwa imani na moyo wa toba.
Tumwombe Mungu atujalie moyo thabiti na wa ujasiri wa kuyapokea mateso na mahangaiko kwa uvumilivu na imani kama Kristo, hata tukisikia hatumjui mtu huyu! Mwondoshe! Mwondoshe! Msulubishe! Msulubishe! Tusikatike tamaa na kurudi nyuma, bali tupate nguvu na kujivika ujasiri zaidi, ili mwisho wa yote tukamsifu Mungu pamoja na malaika mbinguni milele yote. Nabii Isaya anasema; “Bwana Mungu amenizibua sikio langu, wala sikuwa mkaidi…huniamsha sikio langu lipate kusikia kama watu wafundishwao”. Tuombe neema ya kuwa wasikivu na watii. Tukubali kufundishwa na kuelekezwa. Tuingie Juma Kuu kwa moyo wa majuto. Tujipatanishe na Mungu, ili tuweze kuifurahia siku ya Pasaka na tunuie kutorudi nyuma mpaka tutakapoingia katika furaha ya milele katika Pasaka ya Mbinguni.