Papa akisali mbele ya Kaburi la Mtakatifu Charbel Makluf katika Monastero ya Mtakatifu Maroun huko Annaya wakati wa ziara yake ya kitume nchini Lebanon,Desemba 2025. Papa akisali mbele ya Kaburi la Mtakatifu Charbel Makluf katika Monastero ya Mtakatifu Maroun huko Annaya wakati wa ziara yake ya kitume nchini Lebanon,Desemba 2025.  (@Vatican Media)

Dominika ya 5 ya Kwaresima,Mwaka A:“Mimi ndimi Ufufuko na Uzima”

Leo,Kanisa linatualika kusimama mbele ya kaburi,mbele ya mauti,mbele ya kilio,hofu na harufu ya kifo.Injili ya leo si ya nadharia;ni Injili ya machozi,ya maumivu,lakini pia ya tumaini lisilokufa.Katika Ulimwengu mamboleo kifo kimekuwa karibu nasi:vita,magonjwa, majanga ya asili,uharibifu wa mazingira,na hata“vifo vya polepole”vya matumaini, imani na maadili.

Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.

Karibu mpenzi msilikizaji na msomaji wa tafakari ya Neno la Mungu kutoka hapa Vatican News. Dominika ya Tano ya Kwaresma inatuleta karibu sana na Pasaka. Leo, Kanisa linatualika kusimama mbele ya kaburi, mbele ya mauti, mbele ya kilio, hofu na harufu ya kifo. Injili ya leo si ya nadharia; ni Injili ya machozi, ya maumivu, lakini pia ya tumaini lisilokufa. Katika Ulimwengu mamboleo kifo kimekuwa karibu nasi: vita, magonjwa, majanga ya asili, uharibifu wa mazingira, na hata “vifo vya polepole” vya matumaini, imani na maadili. Ndani ya hali hii, Yesu anasimama mbele ya kaburi la Lazaro na kutamka maneno yanayotikisa historia: Tunaendelea kuandaa “tukio la Kristo” (Christ Event) lililo kiini cha ujio wake: mateso, kifo, ufufuko na kupaa kwake mbinguni.. Mbatizwa mwenzangu, mkristo mwenzangu na zaidi mkatoliki mwenzangu umefunga walau mara mbili au tatu? umesali zaidi? umetenda tendo la huruma kwa muhitaji japo mmoja? heri yako, unayo hazina mbele ya Mungu, kama hujafanya, neema ya Mungu ingalipo, tunazo Juma mbili kuadhimisha Pasaka... Neno la Mungu linatupa tumaini kuu kwamba kifo sio uharibifu kama ilivyokuwa kabla ya ujio wa Kristo ingawa ni fumbo lisilozoeleka na linaloumiza… wazo letu leo ni “kwa njia ya kifo tunahuishwa…”

Dominika ya 5 ya Kwaresima mwaka A
Dominika ya 5 ya Kwaresima mwaka A

Kabla ya tafakari yetu tunaona sanamu zimefunikwa, zitafunuliwa Jumamosi Kuu, tunakumbuka siku chache kabla ya mateso Yesu hakuwa akijitokeza waziwazi akikaa zaidi nje ya mji (Bethania) na mlima wa mizeituni faraghani na wanafunzi wake, hili linadhihirishwa na sehemu za Injili tutakazosikia hadi Ijumaa Kuu. Pili, wakati wa mchakato wa hukumu, mateso na kifo chake Kristo Yesu alificha Umungu wake akaonekana mnyonge na mdhaifu hadi alipoudhihirisha kwa utukufu alfajiri siku ya kwanza ya Juma. Halafu tunafunika sanamu ili kuonyesha mambo yapo tofauti na hivi kuwasha moto wa toba na hamu ya Pasaka ndani mwetu... na kuhusu picha za watakatifu ambao sio Yesu? Mkubwa akifichama watumishi wanajitokezaje? Kupitia nabii Ezekieli, Mungu anawaambia watu waliokuwa uhamishoni:
“Nitafungua makaburi yenu, nami nitawatoa makaburini mwenu, enyi watu wangu.” Hawa hawakuwa wamekufa kimwili tu; walikuwa wamekufa kiroho: wamekata tamaa, wamepoteza mwelekeo, hawana tena matumaini. Mungu anawaahidi si tu kuwarudisha nchini, bali kuwapa roho mpya.

Leo hii, kuna “makaburi” mengi: Kaburi la chuki,Kaburi la umaskini, Kaburi la kukata tamaa, Kaburi la dhambi. Lakini Mungu anasema wazi: hali yoyote ya kifo si ya mwisho mbele yake. Kwa njia ya kifo tunahuishwa!” ... Nabii Ezekieli katika somo I (37:12-14) anatoa unabii wa kupandishwa wana na binti za Yakobo kwa mfano wa kufunua makaburi na kuwatoa waliozikwa.. ni mfano wa ufufuko wa miili yetu siku ya mwisho... Mt. Paulo katika somo II (Rum 8:8-11) anafundisha kuwa kila anayetenda dhambi anachangia kuenea uovu na kuharibu uhusiano na Mungu, ili kurudisha uhusiano huo tunahitaji toba ya dhati ambayo kwayo Mungu ‘ataihuisha miili yetu’ iliyo katika hali ya kufa.

Masalia ya Mtakatifu Francis wa Assisi
Masalia ya Mtakatifu Francis wa Assisi

Katika mwaka huu wa kumuenzi Mt. Fransisko wa Assisi, miaka 800 baada ya kifo chake, tunamkumbuka mtu aliyekubali “kufa” kwa dunia ili aishi kwa Mungu. Mt. Fransisko: Alikufa kwa anasa, Alikufa kwa tamaa ya utajiri, Alikufa kwa ubinafsi. Lakini kutoka katika “kifo” hicho, alizaliwa maisha mapya ya furaha, amani na upendo. Aliishi Injili kwa undani kiasi kwamba maisha yake yalikuwa ushuhuda wa ufufuko unaoanza hapa duniani. Katika dunia ya leo inayokumbwa na uharibifu wa mazingira na dharau kwa maskini, Mtakatifu Francisko wa Assisi Mwinjili Yohane amesimulia kufufuliwa kwa Lazaro, kaka ya Martha na Maria... kwa nini Yesu hakwenda haraka kumponya? alikaa siku 2 nzima! na hata baada ya Lazaro kufariki bado alikawia akafika siku ya nne... Kadiri ya Wayahudi roho ya marehemu ilibaki kuzunguka mwili siku 3 na katika siku hizo mwili wa marehemu ulipakwa mafuta kila alfajiri, siku ya 4 roho iliondoka na marehemu alianza kuharibika... Yesu anafika siku ya 4 wasije watu wakadai Lazaro hakuwa amekufa kweli, roho yake ilikuwa bado ‘around’.. Yesu alikawia kwa malengo: kumpa Mungu Baba utukufu, kuelezea umisionari ambao Yeye alikuwa amekuja kuufanya, kuufunua Umungu wake machoni mwa binadamu, kuthibitisha umasiha wake kwa watu, kuzindua rasmi ulimwengu mpya kwa mateso, kifo na ufufuko wake, kuimarisha imani ya waliokuwepo, kuonyesha kuwa wakati wa Mungu ni wakati sahihi, kwake hakuna kuwahi au kukawia na kubwa zaidi kutupatia uelewa mpya kuwa YEYE ndiye Bwana wa uzima, minyororo ya mauti na hofu ya kifo zisiwasumbue watu tena bali imani kwa Mungu katika Kristo Mfufuka itatupa ushindi dhidi ya mauti na umilele wa kimbingu, ndio maana tunasema, ‘kwa njia ya kifo tunahuishwa..

Kufufuliwa kwa Lazzaro
Kufufuliwa kwa Lazzaro

Kufufuliwa Lazaro ni ishara kwamba tukiunganika na Kristo atatufufua na sisi. Hii ni Habari Njema (Injili) kuwa kifo sio mwisho wa historia bali ni njia ya kuunganika na Kristo katika uzima wa milele, ni daraja linalotuvusha ng’ambo ya 2 kuelekea maisha halisi, ni sura mpya ya kitabu cha uhai wetu... kifo cha Kristo kiliua hofu ya kifo cha kale na kuitiisha kuzimu... Shetani anatutishia kifo lakini silaha yetu ibaki kuwa. Msalaba wa Kristo... hatukimbii silaha bali tunaibeba vema, tusiukimbie msalaba, tuubebe na kumfuata Kristo kama wafuasi kamili... Tuombe neema ya kifo chema na ujasiri wa kustahimili dakika ile ngumu itakapowadia na matumaini ya umilele wa kimbingu.  Ee Yesu, Maria na Yosefu, mtujie saa ya kuzimia roho zetu, tufe mikononi mwenu, amina!

Wengi tunadhani tunayo afya njema, lakini kiuhalisia tumekufa, tumo kaburini siku 4, tunanuka kama Lazaro. Kifo kimetupiga, tupo chini kabisa, tumekakamaa kama samaki wakavu, shetani ametushika hatutikisiki. Tazama maisha ya familia yako utaona hakuna uhai, mahusiano ni ya wasiwasi sana, baba na mama hatuaminiani, hatuna mipango ya pamoja, hatujui mshahara unapoingia na unapoisha, ni watu tunaopishana kauli, hakuna mwenye ujasiri wa kusema ‘yaishe’ na kuomba radhi, wote tupo juu, wote tunaongea, unatawala uvumilivu kuliko upendo.. nyumba ya hivi imo kaburini siku 4. Kristo anapoita ‘lazarus, njoo huku nje!’ awaite na wa nyumbani humu ili uwepo tena uhai, ajalie mabadiliko ya ndani ya nafsi, aguse mioyo, ajalie toba ili wakati utakapofika afufuke ndani ya nafsi zilizojiandaa.

Vijana wengi tumo kaburini na Lazaro, ikiwa huzingatii maonyo ya waliokuzidi umri na mang’amuzi, utasema unaishi? wengine hawapendi kazi, wanakaba na kuiba.. wengine hawapendi mambo ya Kanisa na ibada.. hawataki kusoma wala kutumia vema vipaji walivyojaliwa... wanavutiwa zaidi na pombe, klabu za kukesha, sigara, anasa na starehe… hili ni kaburi la siku 4.

Tunapoacha maadili ya kazi kwa kukosa uaminifu, kuiba, kudanganya, kughushi, tunapokuwa wabinafsi, kukosa upendo na kutojali, tunajiweka kaburini na tunanuka. Tunapochelewa Kanisani, likizo za muda wote, kutoshiriki JNNK, kutoshiriki Njia ya Msalaba, kuzembea kitubio na kutokukomunika Ekaristi, kusingizia hiki na kile tumekufa sie, tumo kaburini sasa ni siku 4... Tumuombe Mungu, kwa maombezi ya Bikira Maria Msaada wa Wakristo, atuletee Yesu nje ya hayo makaburi yetu kusudi kama alivyoita “LAZARO, NJOO HUKU NJE!” atuambie na sisi “NJOONI HUKU NJE..” tutatoka na sanda zetu kama Lazaro lakini tutakuwa wazima, atatufungua na kuturuhusu twende tukiwa huru.

Atukuzwe Mungu Baba ya Bwana wetu Yesu Kristo, aliyetubariki kwa baraka zote za rohoni, katika ulimwengu wa roho, ndani yake Kristo… ili tuwe watakatifu, watu wasio na hatia mbele zake katika Pendo » (Efe 1 :3-4), na hivi tupate kuishi, tusife na kupotea milele. Tunapokaribia Pasaka, Kanisa linatualika tuishi Kwaresma hii kwa matumaini. Yesu hakuepuka kaburi; aliingia humo ili kutufungulia njia ya uzima. Tukiungana naye, kama Mt. Fransisko wa Assisi, basi hata katika dunia iliyojaa mauti, tutakuwa mashahidi wa ufufuko na uzima. Amina

DOMINIKA YA 5 YA KWARESIMA MWAKA A
21 Machi 2026, 15:04