2025.03.30 Gesù in Croce

Dominika V Kwaresima Mwaka A:Nasadiki:Yesu Kristo ni Ufufuo na uzima wa milele

Kwanza,kadiri ya utamaduni na mapokeo ya Kanisa,Dominika hii ya V misalaba inafunikwa,mpaka Ijumaa kuu wakati wa adhimisha la mateso ya Kristo na sanamu zinafunikwa,mpaka wakati wa maaadhimisho ya vijilia vya Pasaka.Pili,ni adhimisho la takaso la tatu na la mwisho kwa wakatekumeni watakaobatizwa mkesha wa Pasaka.

Na Padre Paschal Ighondo –Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, domenika ya tano ya kwaresima mwaka A wa kiliturujia katika Kanisa. Katika domenika hii kuna mambo makuu mawili ya kuzingatia. Kwanza, kadiri ya utamaduni na mapokeo ya Kanisa, Dominika hii misalaba inafunikwa, mpaka Ijumaa kuu wakati wa adhimisha la mateso ya Kristo na sanamu zinafunikwa, mpaka wakati wa maaadhimisho ya vijilia vya Pasaka. Pili, ni adhimisho la takaso la tatu na la mwisho kwa wakatekumeni watakaobatizwa mkesha wa Pasaka. Na fundisho kuu ni kuwa kwa ubatizo tunakufa kuhusu dhambi na kufufuka pamoja na Kristo kama inavyofundisha Katekisimu ya Kanisa Katoliki ikisema; “Ubatizo ni sakramenti ya kwanza ya msingi ya ondoleo la dhambi, inayotuunganisha na Kristo aliyekufa kwa ajili ya dhambi zetu, aliyefufuliwa tupate kuhesabiwa haki, kusudi vivyo hivyo na sisi tuenende katika upya wa maisha” (KKK 977).

Hivyo ni kwa ubatizo tunapata uzima wa kiroho ndani mwetu, na kuokolewa kutoka utumwa na hila za Ibilisi. Ni katika muktadha huu zaburi ya wimbo wa mwanzo inasema hivi; “Ee Bwana, unihukumu, unitetee kwa taifa lisilo haki, uniokoe na mtu wa hila asiye haki. Kwa kuwa wewe Mungu ndiye uliye nguvu zangu” (Zab.  43:1-2). Na mama Kanisa katika sala ya mwanzo anasali hivi akituombea; “Ee Bwana Mungu wetu, tunakuomba utusaidie tuwe na mapendo kama ya Mwanao, aliyeipenda dunia hata akajitoa auawe”.

Msalaba ulitukomboa
Msalaba ulitukomboa   (Vatican Media)

Somo la kwanza ni la kitabu cha Nabii Ezekieli (Eze. 37:12-14). Nabii Ezekieli anauelezea uhamisho wa Babeli kwa waisraeli kama kifo na maziko ya Taifa teule kwa dhambi zao. Lakini kule kutambua makosa yao, kuyatubu na kumlilia Mungu wakiomba huruma yake, Mungu kwa huruma na upendo wake alisikia kilio chao, akawasamehe maovu yao, na kuwapa habari ya matumaini ya kutolewa katika makaburi yao, kutolewa utumwani na kurudishwa tena katika nchi yao. Utumwa na ukombozi wa Israeli ukawa ni fundisho kwetu kuwa, tunapotenda dhambi, tunakuwa kama wafu ndani ya makaburi, kwani dhamiri na nafsi zetu zinakuwa chafu mfano wa uchafu ulio ndani ya kaburi. Kutubu dhambi zetu ni sawa na kufufuliwa na kuvalishwa utu mpya.

Ni katika mukatdha huu zaburi ya wimbo wa katikati inasema hivi; “Ee Bwana, toka vilindini nimekulilia,  Bwana, usikie sauti yangu. Masikio yako na yaisikilize sauti ya dua zangu. Bwana, kama Wewe ungehesabu maovu, Ee Bwana, nani angesimama? Lakini kwako kuna msamaha, ili Wewe uogopwe. Nimemngoja Bwana, roho yangu imengoja, na neno lake nimelitumaini. Nafsi yangu inamngoja Bwana, kuliko walinzi waingojavyo asubuhi. Ee Israeli, umtarajie Bwana. Maana kwa Bwana kuna fadhili, na kwake kuna ukombozi mwingi. Yeye atamkomboa Israeli, na maovu yake yote” (Zab. 130).

Kisima cha ubatizo na kuzaliwa upya
Kisima cha ubatizo na kuzaliwa upya   (@Vatican Media)

Somo la pili la waraka wa Mtume Paulo kwa warumi (Rum. 8:8-11). Ujumbe ni huu; shauku ya dhambi hutokana na mwili, na matendo mema yanayompendeza Mungu hutokana na Roho Mtakatifu tuliyempokea kwa njia ya Ubatizo. Basi tumfuate Roho huyo ili tumpendeze Mungu, tupate kustahilishwa utukufu wa ufufuko siku ya mwisho, tukiwa watu wapya. Na ikitokea tumetenda dhambi, tuikimbilie mara moja na haraka sakramenti ya kitubio kuomba msamaha. Ni katika muktadha huu Mababa wa kanisa wanaiita sakramenti hii “ubatizo wa taabu” wakisema kuwa; “Kwa ajili ya wale walioanguka dhambini baada ya ubatizo, sakraamenti ya kitubio ni ya lazima kwa wokovu, kama ulivyo ubatizo wenyewe kwa ajili ya wale ambao hawajabatizwa mara ya pili” (KKK 980).

Injili ni ilivyoandikwa na Yohane (Yn 11:1-45). Ni simulizi la kufufuliwa kwa Lazaro. Tukio hili limebeba uhalisia wa mambo tunayokumbana nayo katika maisha ya kila siku; Urafiki wa kweli unaojidhihirisha katika urafiki wa Yesu kwa Maria, Martha na Lazaro, thamani ya uhai wa mwanadamu katika hali zote ikiwemo ugonjwa na kifo, uchungu, huzuni, na kilio sababu ya magonjwa na kifo, maziko na maombolezo ya wapendwa wetu wanapokufa, kiri ya imani kuhusu ufufuko na maisha ya uzima wa milele, na nguvu ya sala ya mtu mwenye imani thabiti. Licha ya kuwa kifo kinatisha na kuogopesha, kwa kutunyang’anya uhai, tunu aliyotujalia mwenyezi Mungu. Lakini kwa imani tunasaidiki kuwa kifo si mwisho wa maisha, bali ni daraja la kuelekea uzima wa milele kwa njia ya Kristo Yesu aliye “ufufuo na uzima”.

Katekisimu ya Kanisa Katoliki inafafanua hivi hili fundisho la kiimani kuwa Kanuni ya imani ya kikristo “huhitimishwa na tangazo la ufufuko wa wafu siku ya mwisho na katika uzima wa milele” (KKK 988). “Tunasadiki kwa uthabiti, na pia tunatumaini kwamba kama vile Kristo alivyofufuka kweli kutoka wafu na anaishi daima, vivyo hivyo wenye haki, baada ya kifo chao, wataishi daima na Kristo Mfufuka, naye atawafufua siku ya mwisho” (KKK 989). Lakini licha ya kuwa “mbele ya kifo fumbo la hali ya kibinadamu linakuwa kubwa sana. Kwa namna moja kifo cha mwili ni kawaida, lakini kwa imani, kifo ni mshahara wa dhambi” (KKK 1006). Kwa dhambi ya asili, dhambi ya Adamu na Eva kukosa utii kwa Mungu, kifo kiliingilia maisha kama adhabu (rej. KKK 1008).

Lakini kwa mateso, kifo na ufufuko wa Kristo, kifo sio tena adhabu, bali ni njia ya kuufikia uzima wa milele. “Utii wa Yesu uliigeuza laana ya kifo kuwa baraka” (KKK 1009). “Kwa sababu ya Kristo, kifo cha kikristo kimepata maana nzuri. Ndiyo maana Mtume Paulo anasema; kwangu mimi kuishi ni Kristo na kufa ni faida” (Flp. 1:21). Hili “ni neno la kuaminiwa: kwa maana tukifa pamoja naye tutaishi pamoja naye pia” (2Tim 2:11). Upya huu wa kifo cha kikristo umejikita katika sakramenti ya ubatizo. Kwa ubatizo, mkristo tayari amekufa pamoja na Kristo kisakramenti, ili kuishi maisha mapya, na kama tunakufa katika neema ya Kristo, kifo cha mwili hutimiliza kufa pamoja na Kristo, na hivyo hukamilisha kuingizwa kwetu ndani yake katika tendo la ukombozi” (KKK 1010). Hivyo “kwa wale wanaokufa katika neema ya Kikristo kifo ni ushirika katika kifo cha Bwana, ili kuweza kushiriki pia ufufuko wake” (KKK 1006). Hili ni fundisho la kiimani nasi “tunasadiki kwa ufufuko wa kweli wa mwili huu ambao tunao sasa kuwa hupadwa kaburini mwili wa uharibifu, hufufuka katika kutokuharibika mwili wa roho” (KKK 1017).

Msalaba wa Yesu ulitukomboa
Msalaba wa Yesu ulitukomboa

Ni katika tumaini hili; “Mkristo anayeunganisha kifo chake na kifo cha Yesu anakiangalia kifo kama safari ya kumwendea Yeye na kuingia maisha ya milele. Ndiyo maana Kanisa linapotamka kwa mara ya mwisho maneno ya msamaha wa maondoleo ya dhambi, kwa mkristo anayekufa, likimpaka kwa mara ya mwisho mpako wenye kutia nguvu, na kumpa Kristo – Ekaristi –, ushirika mtakatifu wa kufani kama chakula cha safari, linatamka maneno haya ya matumaini likisema: Ondoka, roho ya kikristo, kutoka ulimwengu huu, kwa jina la Mungu Baba Mwenyezi aliyekuumba, kwa jina la Yesu Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai, aliyekufa msalabani kwa ajili yako, kwa jina la Roho Mtakatifu aliyemiminwa ndani yako. Chukua nafasi yako leo kwa amani, na uyaweke makao pamoja na Mungu ndani ya Sayuni takatifu, pamoja na Bikira Maria, Mama wa Mungu, pamoja na Mtakatifu Yosefu, malaika na watakatifu wote wa Mungu. Urudi kwa Muumba wako aliyekutengeneza kutoka vumbi za dunia. Wewe ambaye roho yako itatoka mwilini mwako, Maria Mtakatifu, malaika na watakatifu wote waje kukulaki. Nawe ujaliwe kumwona Mkombozi wako uso kwa uso. Amina” (KKK 1020).

Tukiwa na tumaini hili, tunapokaribia kuadhimisha fumbo la ukombozi wetu, tumruhusu Yesu aingie na tumpatie nafasi akae ndani mwetu kwa neno lake, na sakramenti zake, tujenge unafiki naye katika taabu na raha. Tuthamini maisha yetu na ya wengine, tuone uchungu pale tunapoona mwenzetu ananyimwa haki ya kuishi kwa namna yoyote ile na kumtetea. Tutumie vema muda uliobaki kabla ya Pasaka tumlilie Mungu kwa huzuni kuu, tuone uchungu wa dhambi zetu, atutakase na uovu wetu, ili tuweze kuisherehekea Pasaka kwa moyo safi. Ni katika tumaini hili mama Kanisa katika sala ya kuombea dhabihu anasali hivi; “Ee Mungu Mwenyezi, utusikilize sisi watumishi wako uliotujalia kujua dini ya kikristo. Ututakase kwa nguvu ya sadaka hii”. Na katika sala baada ya Komunyo anasali; “Ee Mungu Mwenyezi, tunakuomba tuwe tumeugana naye daima Yeye ambaye tunashiriki Mwili na Damu yake”. Na hili ndilo tumaini letu.

Tumsifu Yesu Kristo.

Tafakari Dominika V ya Kwaresima
20 Machi 2026, 10:20