Balozi Prof. Costa Rick Mahalu: Msomi, Mwanadiplomasia na Mwanafalsafa Amefariki!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Waamini wanahamasishwa kulitafakari Fumbo la kifo, kama sehemu ya matumaini ya Kikristo kwani, Kristo Yesu mwenyewe anasema, ndiye ufufuo na uzima na kwamba, yeyote anayemwamini ajapokufa atakuwa anaishi na kwamba, heri yao wale wote wanaokufa katika Kristo Yesu. Matumaini ya Kikristo yawasaidie waamini kukabiliana na Fumbo la kifo kwa imani na matumaini na kwamba, hata ustaarabu wa watu wa kale umepitia katika fumbo hili na kwa hakika, ibada ya kifo ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya binadamu. Mzaburi anasema, “Basi, utujulishe kuzihesababu siku zetu, tujipatie moyo wa hekima.” Haya ni maneno yanayowatia waamini matumaini badala ya kujisikia kuwa wanyonge wanapoyaona maisha yao yana yoyoma na kutoweka mara kama ndoto ya mchana. Kifo kinayaanika maisha ya binadamu na kumwondolea kiburi na kuwahimiza watu kujenga na kudumisha upendo, kutafuta na kuambata mambo msingi katika maisha, ili sadaka na majitoleo yao yaweze kuwapatia amani na utulivu wa ndani wanapokabiliana na Fumbo la Kifo! Kristo Yesu anapenda kuimarisha matumaini ya waja wake kwamba, Yeye ndiye ufufuo na uzima! Jambo la msingi ni wao kumwamini. Askofu Flavian Matindi Kassala wa Jimbo Katoliki la Geita, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino cha Tanzania, SAUT, anasikitika kutangaza kifo cha Makamu Mkuu wa Chuo Cha SAUT, Balozi Profesa Costa Ricky Mahalu, kilichotokea tarehe 9 Machi 2026 katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, “Jakaya Kikwete Cardiac Institute” (JKCI), iliyoko Jijini Dar Es Salaam.Amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 77. Askofu Kassala kwa niaba ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC na Baraza la Chuo Kikuu cha SAUT anapenda kutoa pole za dhati kwa familia ya Marehemu, Menejimenti na Jumuiya yote ya SAUT, Ndugu, Jamaa na Marafiki kwa msiba huu mkubwa. Anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuendelea kumwombea Marehemu Mahalu pumziko la amani.
Itakumbukwa kwamba, Balozi Profesa Costa Ricky Mahalu, Msomi, Mwanafalsafa na Mwanadiplomasia alizaliwa tarehe 9 Julai 1948 Kijijini Katunguru, Wilaya ya Sengerema mkoani Geita, Tanzania. Baada ya masomo yake ya Shule ya Msingi alijiunga na Shule ya Sekondari Kibaha na Mkwawa. Tangu mwanzo Prof. Mahalu alikuwa ni kichwa, mwigizaji hodari sana shuleni, kama wanavyoshuhudia waliosoma naye na kwamba, wajihi wake ulimbeba sana! Mwaka 1971 Profesa Mahalu alijiunga na Jeshi la Kujenga Taifa, JKT kwa mujibu wa sheria. Alihitimu Shahada ya Uzamili Chuo Kikuu cha Dar Es Saaam mwaka 1974 na Shahada ya Uzamivu mwaka 1979. Mwaka 1990 alikwenda nchini Ujerumani na kurejea UDSM na kuteuliwa kuwa Profesa wa Sheria. Kati ya Mwaka1992 hadi Mwaka 1996 aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Elimu ya Juu nchini Tanzania. Katika kipindi hiki cha uongozi wake, aliwasaidia wanafunzi wengi kwenda nje ya Tanzania kwa ajili ya masomo ya juu. Mwaka 1999 aliteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia na kuhudumu kati ya Mwaka 2000 hadi Mwaka 2006. Mwaka 2007 Balozi Profesa Costa Ricky Mahalu, alisweka ndani kwa tuhuma za ufisadi wakati akiwa Balozi wa Tanzania nchini Italia. Hayati Rais Benjamin William Mkapa tarehe 6 Mei 2012 “akatinga Mahakamani” kumtetea Prof. Mahalu kwa kusema kwamba, Mkapa akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndiye aliyeidhinisha malipo haya kwa kuzingatia Sheria na Kanuni za Italia, hatua ambayo ilipelekea Prof. Mahalu kuachiwa huru tarehe 9 Agosti 2012.
Itakumbukwa kwamba, Rais Mstaafu, Benjamin William Mkapa alipanda kizimbani Mei 06, 2012 kumtetea Prof. Costa Ricky Mahalu, na kuwa kiongozi wa kwanza wa juu kuwahi kufanya hivyo nchini Tanzania. Profesa Costa Mahalu na Grace Martin aliyekuwa Ofisa utawala wa Ubalozi, walishtakiwa mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakidaiwa kusababishia Serikali ya Tanzania hasara ya Shilingi bilioni 5. Hasara hiyo ya Euro 2,065,827.60 (Sh5 Bilioni) kama sehemu ya mchakato wa ununuzi wa Jengo Ubalozi wa Tanzania nchini Italia. Benjamin Mkapa alikuwa Rais wa Tanzania wakati hasara hiyo ikitokea. Rais Mkapa katika Kitabu chake cha “My Life, My Purpose” Yaani “Maisha Yangu, Kusudi Langu” alieleza kwamba alikubali kwenda kutoa ushahidi Mahakamani kwa kuwa alikuwa anafahamu ukweli wa jambo hilo. Balozi Costa Mahalu, alituhumiwa kwa kufanya malipo ya ununuzi wa Jengo hilo kinyume cha taratibu za Serikali kwa kufanya sehemu ya malipo katika benki ya Italia na benki nyingine. Mkapa alisema yeye ndiye alitoa idhini ya kufanya malipo kwa utaratibu huo baada ya kupewa maelezo na Balozi Costa Mahalu kwamba lilikuwa jambo la kawaida sana nchini Italia. Rais Benjamin Mkapa alisema hata Rais Jakaya Mrisho Kikwete kwa wakati huo aliposikia habari hizo alishangazwa na uamuzi wake wa kwenda Mahakamani kumtetea Balozi Profesa Costa Mahalu. “Ukweli utawaweka huru” Yn 8:32.
Baadaye, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania lilimteuwa kuwa Makamu Mkuu wa Chuo Cha SAUT. Askofu mkuu Gervas J. M. Nyaisonga, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC, wakati huo kwa madaraka aliyokuwa nayo kisheria kwa mujibu wa Katiba ya Chuo ya Mwaka 2010, akamteua Profesa Costa Ricky Mahalu kuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino cha Tanzania. Uteuzi huu ukaanza rasmi tarehe Mosi, Machi 2019. Profesa Mahalu, Balozi na Mwanasheria aliyebobea akachukua nafasi ya Padre Thadeo Mkamwa, ambaye alikwenda masomoni ili kuongeza ujuzi na maarifa zaidi. Nafasi hii kwa muda ilikuwa ikishikiliwa na Profesa Gabriel Mbaga. Katika uteuzi huu, Askofu mkuu Nyaisonga alifafanua kwamba, kabla ya uteuzi huu, Profesa Costa Rick Mahalu alikuwa ni miongoni mwa wakufunzi wa Chuo Kikuu cha SAUT kinachoendeshwa na kumilikiwa na Kanisa Katoliki nchini Tanzania! SAUT ni Chuo Mama kati ya Vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu zinazomilikiwa na kuendeshwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC.