Askofu Berardi:Lazima tuombe tusije tukazama katika mzunguko huu
Na Olivier Bonnel – Vatican.
Akizungumza kutoka vikaria huko Awali, Bahrain, Askofu Aldo Berardi, Msimamizi wa Kitume wa Arabia Kaskazini, hafichi wasiwasi wake, kwani vita vimevuka kizingiti kipya katika eneo hilo. Israel na Marekani zimefanya mashambulizi ya mabomu nchini Iran, na Jamhuri ya Kiislamu imejibu, ikirusha makombora katika nchi kadhaa za Ghuba, ambapo pia kuna kambi za kijeshi za Marekani. Katika siku ya kwanza ya mashambulizi ya mabomu Jumamosi, Februari 28, alituma taarifa kwa mapadre wote na watawa wa kiume na kike, ya Vikarieti yake, ambayo inashughulikia nchi nne za Ghuba ya Arabia: Kuwait, Saudi Arabia, Bahrain, na Qatar. Alisisitiza kwamba huu ni "wakati wa kutokuwa na uhakika" na kuwaomba kila mtu kujificha, kubaki pamoja katika maombi, na kufuata maagizo ya usalama ya mamlaka za mitaa.
Baada ya Papa Leo XIV kutoa wito wa amani wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana Dominika tarehe Mosi Machi 2026, Askofu Berardi alizungumza na Vatican News katika mahojiano ambayo alianza kusema kuwa: "Bila shaka, tulikuwa tukitarajia kuingilia kati kutoka kwa Papa Dominika hii, kwa sababu hali ni ngumu sana kwa sababu ya siasa za kijiografia na athari zake za kiuchumi, na sasa, kwa uingiliaji kati huu wa Israeli na Amerika, hali imezorota zaidi kiasi ambacho hatukutarajia. Kwa upande mwingine, tulikuwa tukijiambia kwamba Iran inaweza kujibu kwa njia isiyozuilika, kwani ilipigwa katikati ya jamii yake; hii imeibua chuki zaidi na kulipiza kisasi. Tumeshikwa na mantiki ya "unanipiga, na mimi ninakupiga; unanishambulia, na mimi ninakushambulia."
Miji mingi ya Ghuba imepigwa makombora kama kisasi. Hali ikoje sasa ulipo Bahrain, na katika nchi zingine za eneo hilo?
Muda mfupi uliopita, (karibu saa saba mchana za Roma), kombora lilipita juu ya makaazi ya Askofu hapa, na vifusi vilizuiliwa na Bahrain; vilianguka karibu na kanisa kuu. Tulikuwa na moto karibu na jengo. Hilo limetushtua sana, haswa kwa kuwa kanisa kuu ni jipya. Kumekuwa na uzinduzi wa makombora tangu jana. Kwa hivyo, tumefunga makanisa yote ili kuepuka matatizo. Sio makanisa yenyewe yanayolengwa moja kwa moja, lakini vifusi na milipuko vinaweza kuharibu majengo na, zaidi ya yote, kuwadhuru watu.
Inaendelea: kuna kengele za kawaida, na kwa hivyo kila mtu anabaki nyumbani. Hatuendi nje kwa sababu za usalama. Maisha yamepungua kwa njia fulani, na makanisa yetu yamefungwa. Mapadre husherehekea Misa pamoja jioni kwa sababu ya amani; hivi ndivyo nilivyoomba katika kila parokia, kwamba makuhani wote kwa pamoja washerehekee Misa kwa sababu ya amani. Hii inafanywa kwa video, kwa Manama na kwa Kuwait. Watu waliomba waweze kushiriki, lakini hatutaki kuchukua hatari hiyo. Kwa mfano, huko Qatar, kanisa lilifungwa na polisi; eneo lote la kidini lilifungwa—hakuna anayeingia, hakuna anayetoka—na pia kulikuwa na vifusi karibu na majengo ya kidini. Kila mtu anaomba, na tunasubiri mambo yatulie.
Papa alizungumzia wajibu wa kimaadili wa viongozi wa kuzuia mzunguko wa vurugu kabla haujawa “dimbwi lisiloweza kurekebishwa.” Je, hiyo ni hatari unayohisi ulipo?
Ndiyo, kwa sababu, kama unavyojua, katika sehemu hii ya dunia, malalamiko yana mizizi mirefu na yamepitwa na karne nyingi. Kwa hivyo, vurugu kubwa kama hiyo inapokusanywa, wakati heshima na kujiheshimu kwa watu vinapopigwa, na wakati mashambulizi yanapofanywa kwa nguvu, majibu huwa ya vurugu vile vile. Bila shaka, tunaingia kwenye dimbwi, na hatujui mahali ambapo inaweza kutupeleka. Kuna hatari kwamba tutavutwa kwenye mzunguko wa kisasi na vurugu za kurudishana ambazo zinaweza kutuangamiza. Lazima tuombe kwamba amani irejeshwe na kwamba tusipoteze mwelekeo katika mzunguko huu. Ikiwa kila upande utaingia vitani kwa sababu unahisi kushambuliwa, kuna hatari kwamba eneo lote litalipuka.
Asante kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku. Just click here