Tukio hili linautukuza ubinadamu unaofumbatwa katika Fumbo la Umwilisho linalopata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu! Tukio hili linautukuza ubinadamu unaofumbatwa katika Fumbo la Umwilisho linalopata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu!  

Tafakari Dominika ya Pili Kwaresima: Utukufu wa Fumbo la Pasaka

Mlimani Tabor, Kristo Yesu anaufunua utukufu na Umungu wake, mbele ya mashuhuda aliowateuwa mwenyewe ili kudhihirisha kwamba, kweli alikuwa ni Mwana mpendwa wa Mungu, Yeye kwa kuwa ni mng’ao wa utukufu wake na chapa ya Nafsi yake. Tukio hili linautukuza ubinadamu unaofumbatwa katika Fumbo la Umwilisho linalopata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu! Rej. Mk 8:31-34. Sanaa ya Kusikiliza!

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, Dominika ya pili ya Kipindi cha Kwaresima mwaka A wa Kanisa. Mtakatifu Paulo VI anasema, kitendo cha kung’ara kwa Kristo Yesu kunaangaza nuru ya ajabu katika maisha ya kila siku ya mwamini ili kufukuzia mbali giza la kifo linalosumbua akili ya mwanadamu. Mlimani Tabor, Kristo Yesu anaufunua utukufu na Umungu wake, mbele ya mashuhuda aliowateuwa mwenyewe ili kudhihirisha kwamba, kweli alikuwa ni Mwana mpendwa wa Mungu, Yeye kwa kuwa ni mng’ao wa utukufu wake na chapa ya Nafsi yake. Tukio hili linautukuza ubinadamu unaofumbatwa katika Fumbo la Umwilisho linalopata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu! Rej. Mk 8:31-34. Hapa Kristo Yesu anadhihirisha utukufu wa Fumbo la Pasaka, kielelezo makini cha sadaka na majitoleo yake kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti, ili hatimaye, aweze kustahilishwa kupokea sehemu ya urithi wa watakatifu katika nuru. Mwili uliotukuka mbele ya Mitume wa Kristo Yesu ni mwili wa Kristo na kwamba, hata mwili wa binadamu utapata urithi wa mwanga wa uzima wa milele, kwa kushiriki katika utukufu na kwa njia hii wapate kushiriki tabia ya Uungu kwa kuokolewa na uharibifu ulioko duniani kwa sababu ya tamaa. Tunaalikwa kupanda juu mlimani, kusali ili kuuona utukufu, yaani uzuri wa kuyashida majaribu ya Shetani, kutoka katika dhambi na kuingia katika utukufu wa Mungu, unaojidhihirisha kwa Yesu kugeuka sura. Tunaalikwa kuisikiliza na kuitii sauti ya Mungu kama Ibrahimu, Baba wa Imani, kwa kumsikiliza Kristo Yesu, Neno wa Mungu, mfano wa utii halisi. Katikisimu ya Kanisa Katoliki inatuelekeza hivi “kutii ni kujiweka kwa hiari chini ya neno lililosikilizwa kwa sababu ukweli wake umethibitishwa na Mungu aliye Ukweli wenyewe” (KKK 144). Ni katika muktadha huu wimbo wa mwanzo unasema hivi; “Moyo wangu umekuambia, Bwana, uso wako nitautafuta. Usinifiche uso wako” (Zab. 27:8-9). Ee Bwana, kumbuka rehema zako na fadhili zako, maana zimekuwako toka zamani. Adui zetu wasifurahi kwa kutushinda. Ee Mungu wa Israeli utukomboe katika taabu zetu zote (rej. Zab. 25:6, 3, 22). Na mama Kanisa katika sala ya mwanzo anatuombea akisali hivi; “Ee Mungu, umetuamuru tumsikie Mwanao wa pekee. Upende kutulisha neno lako ndani yetu. Nasi tukiisha takata, tufurahi kuuona utukufu wako.”

Dominika ya PIli Kipindi cha Kwaresma
Dominika ya PIli Kipindi cha Kwaresma   (@VATICAN MEDIA)

Somo la kwanza ni la kitabu cha Mwanzo (Mwa.12:1- 4a). Ni wito wa Ibrahimu baba wa Imani. Katekismu ya Kanisa Katoliki inatueleza hivi kuhusu jambo hili; “Kwa imani Ibrahimu alipoitwa atoke aende mahali pale atakapopapata kuwa urithi aliitika; akatoka asijue aendako. Kwa imani aliishi kama mgeni na mhujaji katika nchi aliyoahidiwa. Hatimaye, kwa imani Ibrahimu alimtoa sadaka mwanawe wa pekee” (KKK 145). Hivyo, Ibrahimu amekuwa baba wa imani kwa kuishi kile kilichoandikwa katika waraka kwa Waebrania: “Imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, na bayana ya mambo yasiyoonekana”. Na kwa sababu ya imani hiyo amekuwa “Baba wa wale wote wenye kusadiki” (KKK 146).  Katika Biblia, sura mbili za mwanzo zinatuonesha uzuri wa kazi ya Mungu ya uumbaji (Mw. 1:1-2:25). Sura ya tatu hadi ya kumi na moja zinasimulia matokeo ya dhambi, anguko la mwanadamu, kujitenga kwake na Mungu (Mw. 3:1-5:32), habari za Nuhu na gharika kuu (Mw. 6:1-9:29), na kutawanywa kwa mataifa kwa kile kinachofahamika kama mnara wa Babeli (Mw. 10:1-11:32). Sura hizi zinaonesha kuwa mwanadamu baada ya kutenda dhambi hakuweza tena kurudi kwa Mungu kwa jitihada zake mwenyewe. Sura ya kumi na mbili inafungua ukurasa mpya wa mahusiano kati ya Mungu na mwanadamu kwa kuitwa kwa Ibrahamu. Hii akawa ni hatua ya kwanza ya mpango wa ukombozi, ambapo Mungu kwa upendo na huruma yake aliamua kushuka, na kuongea na mwandamu, ili kumuongoza aweze kurudi kwake. Katekisimu ya Kanisa Katoliki inafafanua ikisema hivi; “Ili kuwakusanya wanadamu waliotawanyika, Mungu alimwita Abramu “atoke nje ya nchi yake, na nje ya nyumba ya baba yake ili kumfanya awe Ibrahimu, yaani, “baba wa mataifa mengi” (KKK 2570). “Mungu alimchagua Ibrahimu na kufanya agano pamoja naye na uzao wake. Amefanya taifa lake ambalo alilifunulia sheria yake kwa njia ya Musa. Alilitayarisha kwa njia ya manabii kupokea wokovu uliokusudiwa kwa ajili ya binadamu wote” (KKK 72).

Jengeni utamaduni wa kusoma, kusikiliza na kulimwilisha katika maisha
Jengeni utamaduni wa kusoma, kusikiliza na kulimwilisha katika maisha   (@Vatican Media)

Hivyo “matayarisho ya mbali ya kusanyiko la Taifa la Mungu, yanaanza na wito wa Ibrahimu, ambaye Mungu anamwahidi kuwa baba wa taifa kubwa” (KKK 762). Utimilifu wa ahadi hii ya Mungu kwa Ibrahimu iliyongojewa kwa mda mrefu uko katika Kristo Yesu. Katekismu inafafanua hivi; Baada ya kuharibika sura kwa dhambi na kwa mauti, mwanadamu anabaki “mfano wa Mungu,” mfano wa Mwana, lakini amepungukiwa na “utukufu wa Mungu,” wa “kufanana” naye. Ahadi iliyofanywa kwa Ibrahimu yaanzisha mpango wa wokovu, ambao kilele chake Mwana mwenyewe atachukua “mfano” na atautengeneza “ufanane” na Baba, akiupa utukufu, Roho “aletaye uzima” (KKK 705). Hivyo “kutahiriwa kwa Yesu, siku nane baada ya kuzaliwa, ni ishara ya kujifanya kwake mmoja wa ukoo wa Ibrahimu katika taifa la agano; ni ishara ya utii wake kwa sheria; ni ishara ya kuwa mjumbe kwa ibada ya Israeli ambayo ataishiriki maisha yake yote” na kutahiriwa kwa Kristo, ni ishara ya ubatizo wetu, unaotushirikia agano hili. (KKK 527).Ni katika muktadha huu tunakutana na Mzaburi alipoutafakari uaminifu wa Mungu kwa ahadi zake aliimba zaburi hii ya wimbo wa katikati akisema; “Ee Bwana, fadhili zako zikae nasi, kama vile tulivyokungoja Wewe.  Kwa kuwa Neno la Bwana lina adili, na kazi yake yote huitenda kwa uaminifu. Huzipenda haki na hukumu, Nchi imejaa fadhili za Bwana. Tazama, jicho la Bwana li kwao wamchao, wazingojeao fadhili zake. Yeye huwaponya nafsi zao na mauti, na kuwahuisha wakati wa njaa. Nafsi zetu zinamngoja Bwana; Yeye ndiye msaada wetu na ngao yetu” (Zab. 33:4-5, 18-20, 22). Nasi tunaitwa tutoke katika maisha ya ukale, maisha ya dhambi, tuitii sauti ya Mungu, ili fadhili zake zikae nasi, zitufanye tuwe warithi wa ufalme wake.

Fumbo la Umwilisho linapata utimilifu katika Fumbo la Pasaka
Fumbo la Umwilisho linapata utimilifu katika Fumbo la Pasaka   (@VATICAN MEDIA)

Somo la pili ni kutoka katika Waraka wa Pili wa Mtume Paulo kwa Timoteo (2Tim. 1:8b-10). Ni mashauri na mausia ya Paulo kwa Timoteo, Askofu wa Efeso, aliyeitwa na kupewa neema ya Mungu kwa kuwekewa mikono na Paulo mwenyewe, akimtia nguvu na kumtaka asikate tamaa katika utume wake kwa sababu yoyote ile hata kama ikimbidi kuteseka na kuhangaika kwa taabu zozote zile, bali avumilie akizitumia nguvu alizojaliwa na Mungu kwa ajili ya Injili. Nasi tuliokombolewa, si kwa kadiri ya matendo yetu, bali kwa makusudi na neema zake Mungu, tunaitwa kuishuhudia imani yetu kwa neema tuliyoipokea kutoka kwa Kristo Yesu kwa njia ya ubatizo, ambapo umauti wetu ulibatilishwa na tukafunuliwa uzima usioharibika. Injili ni kama ilivyoandikwa na Mathayo (Mt. 17:1-9). Ni simulizi la kugeuka sura kwa Yesu. Tukio hili lilifunua umungu wake na kuonesha kuwa Yeye ni ukamilifu wa sheria na manabii kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake. Ni katika mukatdha huu sala ya utangulizi wa dominika hii inasema hivi; “Yeye aliwaambia mapema wafuasi wake kwamba atauawa; na pale katika mlima mtakatifu aliwaonyesha utukufu wake, akaonyesha kwamba kama ilivyoandikwa katika Torati na Manabii, atapata utukufu wa ufufuko kwa kuteswa”. Hivyo tukio hili la Yesu kugeuka sura limebeba mafundisho mazito juu ya fumbo la ukombozi wetu. Katekisimu ya Kanisa Katoliki inafafanua hivi; “Kugeuka sura kwa Yesu kuna lengo la kuimarisha imani ya Mitume kwa kutazamia mateso yake: kupanda juu ya mlima mrefu kunatayarisha kupanda juu ya Kalvari. Kristo, kichwa cha Kanisa, anaonesha kile alicho nacho na anachotoa, mwili wake katika Sakramenti, tumaini la utukufu” (KKK 568). Tukio hili lililenga kuwaimarisha mitume wake walioanza kukata tamaa. Ni kwa sababu, baada ya Petro kuungama kwamba Yesu ni Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai (Mt. 16:13-15). Yesu alianza kuwaambia wazi wazi wafuasi wake kwamba ilimpasa kwenda Yerusalemu, na kupata mateso mengi na kuuawa, na siku ya tatu kufufuka (Mt. 16:21-22). Petro alipinga tangazo hili na wengine hawakulielewa kabisa. Katika hali hiyo Yesu aliwachukua wanafunzi wake watatu, Petro, Yakobo na Yohane, akapanda nao mlimani, na katika kusali akageuka sura, mbele yao ili wawe mashahidi kwa ambayo yangetokea Yerusalemu (rej. KKK 554).

Utafuteni Uso wa Mungu
Utafuteni Uso wa Mungu   (Vatican Media)

Kristo Yesu kuonesha utukufu wake wa kimungu, alithibitisha ungamo la Petro, akaweka wazi ufunuo wa kuwa ili kuingia katika utukufu wake anapaswa kwenda njia katika ya Msalaba. Mtakatifu Thomaso wa Akwino anasema hivi; “Wewe uligeuka sura mlimani, na kadiri walivyoweza wafuasi wako, walitafakari utukufu wako ee Kristo Mungu, ili watakapokuona umesulubiwa waelewe kwamba mateso yako yalikuwa ya hiari, na watangaze duniani kwamba, Wewe ni kweli mng’aro wa Baba” (KKK 555; STh III, 45, 4, ad. 2). Kumbe “kung’ara sura kunatupa limbuko la ujio mtukufu wa Kristo, atakaye ubadili mwili wetu wa unyonge, upate kufanana na mwili wake wa utukufu. Lakini tukumbuke pia, kwamba imetupasa kuingia katika ufalme wa Mungu kwa njia ya dhiki nyingi” (KKK 556). Haya yote tutayaweza tukidumu katika sala, ndiyo maana mazingira ya kutokea tukio hili ni wakati Yesu akiwa katika sala. Hii inatuonesha thamani na nguvu ya sala. Sala ina nguvu ya kuzifungua mbingu na kumfanya Mungu ashuke na kusema nasi. Ndiyo maana mababa wa Kanisa wanatufundisha kuwa sala ni kuongea na Mungu. Sala ni kuinua akili na roho mbele za Mungu. Sala ni mawasiliano kati ya Mungu na Mwanadamu. “Sala ni kuinua moyo kwa Mungu au maombi ya mambo mema kwa Mungu” (KKK 2559). Ndiyo maana moja ya nguzo kuu ya kipindi hiki cha Kwaresima ni kusali kwa bidii tena bila unafiki. Hitimisho la tukio hili ni sauti ilitoka katika wingu, ishara ya uwepo wa Mungu na utukufu wake (rej. Kut.13:21; 24:16-18; 40:34), iliyotoa agizo la kumsikiliza Yesu ikisema; “Huyu ni Mwanangu, mteule; Msikilizeni yeye.” Nyakati zetu Yesu anaongea nasi Neno la Mungu linaposomwa. Hivyo tunapaswa kulisikiliza na kuliishi na kuwa tayari kuyapokea mateso yatokanayo na kuliishi Neno la Mungu ili mwisho wa maisha ya hapa duniani tukaufurahie utukufu wake mbinguni, utukufu tunaoanza kuuonja katika sherehe ya Pasaka. Ni katika tumaini hili mama Kanisa katika sala ya kuombea dhabihu anasali hivi; “Ee Bwana, tunakuomba sadaka hii ifute dhambi zetu na kuwatakasa waamini wako mwili na roho, wapate kuadhimisha sikukuu ya Paska”. Na katika sala baada ya komunyo anasali; “Ee Bwana, baada ya kupokea mafumbo yako matakatifu, tunakushukuru, kwa maana ingawa tuko bado hapa duniani watushirikisha ya mbinguni."

Tafakari D 2 Kwaresima
26 Februari 2026, 11:19