Sheria ya Mungu ni chemchemi ya haki, amani na upendo; ni dira na mwongozo wa maisha adili na matakatifu. Sheria ya Mungu ni chemchemi ya haki, amani na upendo; ni dira na mwongozo wa maisha adili na matakatifu.  (@Vatican Media)

Tafakari Dominika ya 6 ya Mwaka A wa Kanisa: Sheria ya Mungu: Haki, Amani & Upendo

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya Sita ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa, inahimiza kwamba, Sheria ya Mungu ni chemchemi ya haki, amani na upendo kamili. Hiini Sheria ambayo imesimikwa katika sakafu ya moyo wa mwanadamu. Hii ni dira na mwongozo wa maisha adili na matakatifu na kwamba, Kristo Yesu Mpakwa wa Bwana amekuja kutimiliza Sheria na Manabii. Yeye ni Mwanzo na Mwisho; Alfa ya Omega, nyakati zote ni zake!

Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.

UTANGULIZI: Karibu Mpenzi msikilizaji na msomaji wa tafakari ya Neno la Mungu leo dominika ya sita Mwaka A. Dominika hii tunaliangazia Neno la Mungu linalotufundisha kwamba sheria ya Mungu si mzigo, si tishio, si kizuizi—bali ni njia ya upendo, njia ya amani, na njia ya haki. Katika ulimwengu unaotangatanga kwenye giza la machafuko, migogoro, rushwa, hofu na kukata tamaa, Yesu anatukumbusha kwamba sheria ya kweli ni upendo, na upendo huo ndio unaoweza kuponya dunia, kutengeneza familia, na kujenga jamii yenye haki. Wana wapendwa wa Baba wa milele, na tuzipokee baraka na neema za Dominika ya Sita ya Mwaka A wa Kanisa, na tuikaribie kwa ibada na unyofu wa moyo madhabahu takatifu kusudi tuadhimishe sadaka ya sifa na ya shukrani kwa Mungu Baba yetu... dhamira ya leo iwe ‘Kristo ndio ukamilifu wote’ kutoka neno lake, “Msidhani nalikuja kutangua torati hapana bali kutimiliza”. Katika Somo la Kwanza ni kutoka katika Kitabu cha Yoshua bin Sira anafundisha uhuru wa kuchagua njia ya upendo, Yoshua Bin Sira anatuambia: “Ameweka mbele yako moto na maji—uchague upendavyo.” Hii ni siri ya maisha ya mwanadamu, tunao uhuru wa kuchagua. Mungu hatulazimishi kumpenda, kutenda haki, au kujenga amani, lakini anatupa nafasi ya kuchagua mema. Kila siku tunachagua kati ya upendo na chuki, Upendo hujenga; chuki huharibu. Upendo huponya; hasira hushusha roho. Upendo hulinda utu; dhambi huharibu uhusiano. Uchaguzi wa upendo hutengeneza dunia yenye haki, Kila mara tunapochagua kutenda haki, kusaidia maskini, kuzuia maneno ya fitina, kuwa wakweli, tunaunda dunia bora. Mungu anajua uchaguzi wetu, Sira anasema: “Macho ya Bwana yako juu ya wale wamchao.” Hakuna wema unaopotea mbele ya Mungu. Hakuna uamuzi wa haki unaodharauliwa. Kwa hiyo: Uchaguzi wetu wa upendo una matokeo ya milele.

Sheria ya Mungu ni dira na mwongozo wa maisha
Sheria ya Mungu ni dira na mwongozo wa maisha   (@Vatican Media)

Mungu anapenda mwanadamu atende mema lakini hamlazimishi, anamwacha aamue mwenyewe, lakini kwa kumpenda anampa vitendea kazi yaani akili, utashi na uhuru wenye wajibu. Hata hivyo bado uchaguzi unakuwa mgumu tukitegemea hekima yetu wenyewe. Ndipo sasa katika somo II Mtakatifu Paulo (1Kor 2:6-10) anazungumzia hekima ya duniani na hekima itokayo mbinguni. Tunapochagua ubaya twaongozwa na hekima ya kidunia na tuchaguapo jema twaongozwa na hekima ya Mungu. tuchague leo hekima itokayo juu, ‘Aeterna Sapientia...’ Sheria na taratibu ni muhimu kwa ajili ya amani. Wayahudi walikuwa na Torati ambayo Yesu anaikamilisha. Torati (Torah) ni sheria na katika Biblia vitabu 5 vya Musa huchukuliwa kuwa vitabu vya sheria. Torah na Shemaah “Sikia ee Israel...” (Kumb 6:4-7) ndio mwongozo wa maisha ya kila siku ya Waisraeli. Sheria hizi zinafafanuliwa kwa muhtasari kama amri za Mungu nazo ni mapato ya Agano la Sinai. Ndilo Agano la milele lililowekwa kirafiki na Mungu na Abraham (Mwz 17), sasa linaratibiwa na kuwekwa katika maandishi na kuwa sheria, baadaye Agano hilohilo litarudiwa kwa Daudi na kukamilika katika Kristo kwa Damu yake ya Agano Jipya.

Sheria ya Mungu imeandikwa kwenye sakafu ya moyo wa mwanadamu
Sheria ya Mungu imeandikwa kwenye sakafu ya moyo wa mwanadamu   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

UFAFANUZI: Zaburi ya leo ni kilio cha mtu anayetaka kutembea katika amri za Mungu: “Nifumbue macho yangu nione mambo ya ajabu katika sheria yako.” Sheria ya Mungu ni nuru, si kifungo. Zaburi inatuambia sheria ya Mungu inaleta: mwanga, furaha, amani, mwelekeo, uadilifu. Sheria ya Kristo ya upendo inatufunulia jinsi ya kuishi kama watoto wa Mungu. Amani ya kweli hutoka kwa moyo mtiifu. Mtu anayekubali kufuata Neno la Mungu huwa mtu wa amani, mtu wa tabasamu, mtu wa kusamehe, mtu wa kusaidia—huyu ndiye husimamisha haki na upatanisho katika jamii. Amri hizo 10 za Mungu zilinyumbuliwa na marabi kufikia 613 na Waisraeli walipaswa kuzivaa katika panda za uso, mikononi na kwenye mavazi yao. Nyingi zilikuwa ni mzigo kwa watu wa kawaida, ziliwapendelea wakubwa na zilifuata mapokeo ya mila na desturi mf. kunawa mikono, kutawadha, vyakula, unajisi wa mama, sabato nk. Ni katika mambo hayo ndiyo Kristo anasema Yeye ni ukamilifu wa sheria, anazirekebisha zimsaidie mtu katika kufuata maisha ya uadilifu na haki na siyo kuwa sababu ya mahangaiko, kukosa raha na kukosekana kwa amani.  Amri 3 za kwanza zinamuhusu Mungu (uaminifu kwake, kutoabudu miungu, heshima kwa Jina lake na ibada kwake) na amri 7 zinahusu maisha ya jamii (umoja wa familia, heshima kwa uhai, kwa viapo vya ndoa, kwa vitu/mali, ukweli wa kauli na mtazamo chanya wa wenzetu na mali zao). Amri 8 ni hasi/makatazo rej. Usi... na 2 tu ndizo chanya/maagizo rej. Shika kitakatifu na waheshimu baba yako na mama yako... hizi ni amri sio majadiliano au mapendekezo, zimebeba mamlaka, zinadai utii na utekelezaji tu sababu chanzo chake ni Mungu Mwenyewe. Mtume Paulo anasema tunanena hekima ya Mungu iliyo ya rohoni, si ya kibinadamu. Hekima hii ya Mungu ni: hekima ya unyenyekevu, hekima ya msamaha, hekima ya kujitoa, hekima ya kutotukanisha, hekima ya kupenda bila masharti.  Dunia hailinganii hekima hii, Dunia leo hupima: nguvu kwa pesa, maendeleo kwa teknolojia, heshima kwa cheo, umuhimu kwa umaarufu. Lakini Mungu hupima maisha kwa upendo tulioishi. Ndiyo maana Paulo anasema: “Macho hayajawahi kuona mambo aliyowaandalia wampendao.” Kwa hiyo: Hekima ya Mungu ni upendo unaofanya kazi.

Sheria ya Mungu ni upendo wa Kristo kwa wanadamu
Sheria ya Mungu ni upendo wa Kristo kwa wanadamu   (Vatican Media)

Yesu anatupeleka katika sheria ya moyo—Sheria Ya Upendo, Katika Injili, Yesu anasema: “Sikuja kuitangua sheria, bali kutimiliza.” Na anaiongeza kwa undani: Sheria si maneno tu—ni moyo wake unavyotenda upendo. Kuhusu Hasira: Upendo hupatanisha, Yesu anasema: “Hata ukimwonea nduguyo hasira, uko hatarini.” Hasira ni moto unaounguza amani. Upendo hupatanisha bila kuchelewa. Kuhusu Tamaa: Upendo unaheshimu utu Yesu anaonyesha kwamba tamaa moyoni ni chanzo cha dhambi. Upendo wa kweli haupati mtu mwingine kama kitu cha kutumiwa, bali kama mtu wa kutunza, Kuhusu Ndoa: Upendo ni uaminifu Yesu anatukumbusha utakatifu wa familia. Upendo haukimbii wakati mgumu; unavumilia, unasamehe, unajenga. Kuhusu Maneno: Upendo hunena ukweli “Neno lenu na liwe ‘Ndiyo ndiyo, Hapana hapana.’” Uongo umeharibu nchi nyingi. Maneno ya kweli ni msingi wa haki na amani. Jamii pia inaongozwa na amri/sheria. Kimsingi sheria zote ni kwa ajili ya ufalme wa Mungu hata kama ni za taasisi, siasa au serikali kwani zote zimelenga watu kutendeana haki na kuishi uadilifu. Sheria sharti ilete uhusiano mwema baina ya mtu na mtu na mtu na Mungu, “Sheria isiyowafaidia wanaoifuata na hivi kutokuwa na manufaa kwao ifutwe mara” (Mt. Tomaso wa Akwino).  Kristo anakamilisha mambo manne kutoka sheria ya kale: kuhusu kuua, kuzini, talaka na kuapa. Kristo anaboresha pia sheria ya talaka. Ndoa ina sheria zake, mmoja anapoingia agano la ndoa atambue kuwa anajifunga na sheria hizo. Ndoa ni ‘umoja na umilele’ ambayo ni mapato ya ‘kuondoka nyumbani na kuambatana wawili’ (Mwz 2:24), talaka haina nafasi hata ikiwa mmoja yu taabani (Mt 19:3kk). Inafaa kuwa waangalifu kabla ya kuamua kujifunga na kifungo hiki na tukishakuwa kwenye ndoa tutunze ndoa hizo kwa kuzinogesha na kuzifanya mpya kila siku ili kuepusha hali ya kuchokana na kutoka nje, wanandoa wadumishe upendo, maelewano, ukweli, uaminifu na msamaha.

Sheria ya Mungu imeandikwa katika sakafu ya maisha ya mtu
Sheria ya Mungu imeandikwa katika sakafu ya maisha ya mtu   (@Vatican Media)

Yesu anatambua dhambi haianzi kwenye tendo lenyewe bali akilini na kusukumwa na utashi, wazo hutengenezwa ndani na baadaye kutekelezwa kwa kitendo cha nje kama ni kuua, kunyima haki, kuzini, kuiba, kumbe dhambi ni ukamilifu wa mchakato uliotamaniwa moyoni, kichwa kikaratibu, miguu ikaifuata, mikono ikashughulikia na tendo kutendeka. Yesu ameongeza uzito wa dhambi ili kutusaidia kutambua dhambi ni nini. Na wale waliokuwa wanapenda au kukusudia kutenda lakini mazingira yaliwazuia kwa maelezo ya Yesu ni wametenda na ni wakosaji mbele za Mungu.  Labda unatamani mahusiano na mama fulani lakini unaogopa mumewe mwanajeshi, umeishafanya dhambi hiyo. unatamani kuiba lakini kuna watu hupati nafasi, dhambi yako i tayari. Unatamani kunipiga lakini unaogopa Polisi au huna nguvu ndio ushanipiga tayari moyoni mwako, simo moyoni mwako, huoni matatizo yangu, umenifuta kichwani mwako, hapo umefanya dhambi ya kuua, kuna mtu amekosa furaha kwa sababu yako, umemzungumzia kwa ubaya jirani yako, umebeba chuki moyoni, hukutumia lugha ya staha, umemuhukumu jirani yako, umemnyanyapaa kwa jinsi alivyo na mapungufu yake, ndugu yangu umeua. Hakuna anayesalimika na kwa vile sote tumepungukiwa utukufu wa Mungu, basi tusinyanyapaliane bali tusaidiane vile iwapasavyo wana wa Mungu naye atatunusuru.

Kristo Yesu ni utimilifu wa Sheria na Unabii
Kristo Yesu ni utimilifu wa Sheria na Unabii   (Vatican Media)

Yesu hakuja kutangua sheria bali kutimiliza, na amri zote ameziweka katika amri moja muhimu... kumpenda Mungu na kumpenda jirani. Twaweza kufanya mengi na tukasifika lakini hayatakuwa na faida kama hayaongozwi na hekima ya Mungu na hayana roho ya upendo... Basi wapendwa, “Mungu anayetupatia amani awafanye ninyi watakatifu kwa kila namna na kuzilinda nafsi zenu: roho, mioyo na miili yenu mbali na hatia yoyote, wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo” (1Tes 5:23). Leo dunia inakosa amani kwa sababu tunakosa upendo wa kweli: Migogoro ya kisiasa na vita, rushwa inayosambaa kama ugonjwa, Familia zinazovunjika Vijana wanaokatishwa tamaa Ubinafsi unaowatupa maskini pembeni, Maneno ya chuki, mitandaoni na majumbani. Msingi wa haya ni moja: tumeacha sheria ya upendo wa Kristo. Na ndiyo maana leo Yesu anatuita kwa sauti kuu: “Rudini kwenye upendo, rudini kwenye amani.” Masomo ya leo yanatuambia kwa sauti moja: Sheria ya Kristo ni Upendo. Upendo ndio unaotengeneza haki. Upendo ndio unaotengeneza amani. Upendo ndio unaotengeneza familia, taifa na ulimwengu.

Liturujia D 6 Mwaka A
13 Februari 2026, 14:54