Tafakari Neno la Mungu Dominika 5 ya Mwaka A wa Kanisa: “Iweni Chumvi na Mwanga: Teteeni Haki, Jengeni Amani, Toeni Matumaini kwa Dunia.” (Mt 5:13-16) Tafakari Neno la Mungu Dominika 5 ya Mwaka A wa Kanisa: “Iweni Chumvi na Mwanga: Teteeni Haki, Jengeni Amani, Toeni Matumaini kwa Dunia.” (Mt 5:13-16)  (AFP or licensors)

Tafakari Dominika 5 ya Mwaka A wa Kanisa: Mashuhuda wa Nuru na Chumvi ya Dunia

Mama Kanisa anawaita na kuwatuma watoto wake waliozaliwa kwa Maji na Roho Mtakatifu kuwa nuru ya Mataifa na chumvi ya dunia kwa njia ya ushuhuda wa maneno lakini zaidi kwa njia ya matendo yao adili na matakatifu yalete ladha ya maisha; yatunze, kulinda na kudumisha utakatifu wa maisha, unaopata chimbuko lake kutoka kwa Kristo Yesu, aliyezaliwa kwa Baba tangu milele yote, Mwanga kutoka kwa Mwanga, Mungu kweli kwa Mungu kweli! Yesu ni Nuru ya Kweli.

Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.

UTANGULIZI: Karibu mpezi na msomaji wa tafakari ya Neno la Mungu kutoka hapa Radio Vatican leo Dominika ya tano Mwaka A wa Kanisa. “Amani huanza na utu! Wito wa Kimataifa wa Kukomesha Biashara Haramu ya Binadamu” ndiyo kauli mbiu inayonogesha Maadhimisho ya Siku ya 12 ya Kimataifa ya Sala na Tafakari katika mapambano dhidi ya Biashara Haramu ya Binadamu pamoja na mifumo yote ya utumwa mamboleo! Kila mwaka ifikapo tarehe 8 Februari, Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Siku ya Kimataifa ya Sala na Tafakari ili kupambana na Biashara Haramu ya Binadamu na mifumo yote ya utumwa mamboleo. Leo tunasikia moja ya mafundisho mazito zaidi ya Yesu, kuwa chumvi ya dunia na mwanga wa ulimwengu. Yesu hatuambiwi tu “fanyeni mema,” bali anatufanya: chumvi inayotia ladha na kuhifadhi, na mwanga unaoangazia giza la dunia. Katika dunia inayovuja amani, inayotetemeka kwa ukosefu wa haki, migongano, umaskini na kukata tamaa, Yesu anatuita kuwa watu wanaoweza kuleta tofauti, watu wanaotenda, watu wanaojenga, watu wanaotoa matumaini. Masomo ya leo yote, kutoka Isaya 58, Zaburi 112, 1 Wakorintho 2 hadi Mathayo 5:13–16, yanatufundisha kwamba mwanga wa kweli unatoka katika haki, huruma na unyenyekevu, na chumvi ya kweli ni matendo ya upendo ya kila siku. Kwa ubatizo tunafanyika wajumbe wa kumpeleka Kristo kwa watu na kumfanya atambulikane kwao kwa njia ya matendo, mafundisho na mifano ya maisha yetu. Neno la Mungu linatukumbusha wajibu huu ambapo tunapasika kwa namna yoyote kuwa chumvi ya dunia na nuru ya ulimwengu.

Kristo Yesu ni Mwanga kwa Mwanga; Mungu kweli kwa Mungu kweli
Kristo Yesu ni Mwanga kwa Mwanga; Mungu kweli kwa Mungu kweli   (ANSA)

Chumvi ni ‘kampaundi’ nyeupe zinazoyeyuka katika maji na huyeyuka kidogo sana katika pombe, hutia ladha chakula ili kilike na kifurahiwe.. hili linahusisha wanyama wote wenye damu moto, wao kwa silika tu hulamba mawe ya chumvi (maclik) na huwasaidia kujenga miili yao. Chumvi ina iodine inayozuia ugonjwa wa tezi shingoni.. hutunza vyakula visiharibike.. imo katika hamira ya mkate, katika mifumo ya majokofu, sabuni na dawa za kuondolea madoa.. dawa kwa vidonda.. bidhaa ya biashara hivi ni ajira.. hutengenezewa sabuni na vioo hasa lens na prisms.. ni ya muhimu, tukiikosa tunatumia magadi mradi tu ladha ya chumvi ipatikane.. mtu mzima atumie walau gramu 3-5 (kijiko cha chai) za chumvi kwa siku katika chakula.. sodium iliyo katika chumvi hupelekea shida ya moyo, “BP ya kupanda”.. kula chumvi nyingi kuna maana ya kuishi sana.. Kristo anasema sisi ni CHUMVI YA DUNIA.. tuna ladha hiyo? huenda tumechacha kitambo. Katika somo la kwanza Nabii Isaya anatupa picha ya ibada ambayo Mungu anaipenda: “Gawanya chakula chako na mwenye njaa, wapokee wasio na makazi, umvike aliye uchi, usimgeukie mjoli wako unayemdai.” Hapa tunaona kwamba: Huruma ndiyo msingi wa amani, Hakuna amani bila kushughulika na mateso ya jirani. Amani haiwezi kujengwa juu ya njaa, ukosefu wa makazi, ubaguzi au kupuuza maskini. Haki huangaza giza Isaya anasema: “Ndipo nuru yako itachomoza kama asubuhi.” Mwanga wa mtu unaanza pale anapogusa maisha ya wengine kwa huruma: anarisha wenye njaa, anapunguza mateso, anawaenzi wanyonge. Ibada bila haki ni giza Leo, dunia inazidi kujaa ibada nyingi, lakini haki inapungua. Kwa Mungu: matendo ya huruma ndiyo ibada iliyo ha Zaburi inasema: “Nuru humzuka mwenye haki.” “Hugawa, huwapa maskini; haki yake yakaa milele.” Zaburi hii inaunganisha heri tatu muhimu kuwa chumvi na mwanga:  Mwenye huruma → mwanga wake humulikia wengine, anagawa kwa maskini → anastawisha haki ya kijamii, Moyo wake hauna hofu → anachemsha matumaini kwa dunia Kwa kifupi: mtu mwema ni taa ya Mungu duniani.

Kristo Yesu ni Nuru ya Ulimwengu
Kristo Yesu ni Nuru ya Ulimwengu   (@Vatican Media)

UFAFANUZI: Chumvi na Mwanga vinachipuka katika unyenyekevu Mtume Paulo katika Somo la Pili anawaambia Wakorintho: “Sikuja kwenu kwa maneno ya hekima ya kibinadamu… bali kwa udhihirisho wa Roho na nguvu. “Hapa tunajifunza: Mosi Mwanga wa Mungu huangaza kupitia udhaifu wetu, Paulo hakujitegemea uwezo wake, bali nguvu ya Roho. Kwa hiyo sisi pia hatuitwi kuwa wakamilifu—tumeitwa tu kuwa waaminifu. Pili Ukristo si maonyesho, ni unyenyekevuChumvi inapoteza ladha inapochanganywa na majivuno; mwanga huzimika unapofunikwa na kiburi. tatuMatumaini ya dunia hayatoki kwa nguvu za kibinadamu, Lakini kutoka kwa watu wanaotegemea Munguhawa ndiyo chumvi na mwanga wa kweli. Nyumba yenye taa ilionesha uhai na kuzimika kwake kulimaanisha maafa/kifo kwa nyumba hiyo. kwa Wayahudi taa ilimaanisha Mungu (Zab 27:1, Isa 60:19, Yak 1:17, 1Yoh 1:5-7; 2:8-10). Neno la Mungu ni taa ya miguu yetu. ulinzi wa Mungu ni Taa, na wokovu wa Mungu ni Taa. Mwokozi ni Nuru, Kristo ni Taa, Daudi ni taa ya Israeli. Yohane Mbatizaji ni shuhuda wa nuru (Yn 1:6-9). Leo tunaitwa kuwa nuru na kuiangazia dunia ili watu waone vizuri safari yao sababu dunia imekosa dira katika nyakati zetu… je, taa yako inawaka? Dunia ya leo inahitaji chumvi na mwanga kuliko wakati mwingine wowote: Amani inadhoofika: Migogoro, vita, vitendo vya kigaidi, migawanyiko ya kikabila na kisiasa vinaongezeka. Haki imepungua. Wengi wanasema badala ya “haki,” tumesikia neno “rushwa,” “kuonewa,” “kubaguliwa.”  Matumaini yanavunjika: Hali ngumu ya kiuchumi, ukosefu wa ajira kwa vijana, kutokuwa na mwelekeo. Katika mazingira haya, Yesu anasema: “Wewe uwe chumvi. Wewe uwe mwanga.”

Chumvi na nuru ushuhuda wa Wakristo Ulimwenguni
Chumvi na nuru ushuhuda wa Wakristo Ulimwenguni   (@Vatican Media)

Maana yake: Usiongeze giza kwa maneno ya chuki, Usiongeze uchungu kwa woga Usiongeze uvundo kwa rushwa, Usiongeze mgawanyiko kwa kiburi. Badala yake: ongeza ladha ya upendo, ongeza mwanga wa ukweli, ongeza tumaini la Kristo. Bila bahati, mara si haba tumekiuka agizo la kuwa nuru na chumvi, tumekumbatia giza.. giza ni shetani wa kuepukwa. Katika Kigiriki pepo ‘diabolos’ ni kitu kidogo lakini kinachosumbua, ki-kokoto/ki-jiwe kwenye kiatu kinamsumbua na kumnyima raha mvaaji, wapo wanaojitahidi kuingia kwenye viatu vya wenzao, wanafanana 100% na tumawe kwenye viatu na tujiwe hutu tunaleta karaha kweli, unashindwa kukanyaga na kupiga hatua vizuri, ni heri kutembea peku kuliko kuvaa kiatu chenye ‘dayabolosi. ibilisi au mwovu’. Chumvi inatunza, kwa imani na ufuasi wetu tunaitwa kuitunza jamii na kuikoa kutoka mifumo isiyo sawa ya kijamii, kiuchumi na kisiasa, kuinusuru na sera za kitaifa na kimataifa zinazomtoa mwanadamu kwenye lengo halisi la uumbaji wake na kumfanya aonekane kiumbe asiye na chochote na hivi kumuondolea hadhi yake kama mtawala wa dunia mahali pa Mungu. Dunia yetu inapendekeza mengi yanaonekana mazuri machoni na ya kupendeza moyoni lakini yana hila ndani yake, tumakinike, tusipoteze lengo. Kristo kasema ‘nuru yenu ni lazima iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni’Je, matendo yako ni mema? yanamtukuza Baba wa mbinguni? tuchangamke! tusimuinue shetani.

Waamini wawe ni nuru ya maisha adili na matakatifu kwa walimwengu
Waamini wawe ni nuru ya maisha adili na matakatifu kwa walimwengu   (@Vatican Media)

Kila mmoja wetu anaweza kuwa chumvi na mwanga kwa namna zifuatazo: Tenda haki katika familia na jamii, Toa chakula, usaidizi au faraja kwa wasiokuwa na kitu, Simama na ukweli hata ikiumiza, Punguza maneno ya chuki, ongeza upole, Wekea vijana matumaini, sio kukata tamaa. Ombea amani ya nchi na ulimwengu, Kuishi kwa unyenyekevu kama Paulo, Kuangazia dunia kwa matendo kama Isaya 58 na Zaburi 112, Kwa kufanya hayo, tunakuwa: chumvi inayotia ladha mwanga unaoangazia na wajenzi wa amani na matumaini kwa dunia. Wakati wenzetu wenye mapenzi mema wanahimiza kutibu dalili kuliko kusubiri ugonjwa kwa kutatua matatizo na migongano kwa uwazi, ukweli na unyofu wa moyo, wengi wetu tumetamani kubaki katika minyukano na malumbano. Zaidi ya hilo, tumekuwa tukiunda mitandao/network ya watu wenye roho kama zetu wanaounga mkono maneno na matendo yetu na hivi maisha ya giza na yaliyokosa ladha ya chumvi yanasambaa kwa wengi na kuivuruga jamii... tusimpe shetani nafasi (Efe 4:27). Kuwa chumvi ya dunia na mwanga wa ulimwengu si rahisi, kuna kuchacha kwa hapa na pale na kuishiwa mafuta ya taa. Tunahitaji neema ya Mungu asemavyo Mt Paulo katika Somo II (1Kor 2:1-5).. tusali ili kupata nguvu hiyo na kuwa wakarimu asemavyo Isaya katika somo I (58:7-10).. Mama Bikira Maria na watakatifu wote wa mbinguni watuombee ili nia zetu njema zizae matunda na kwamba katika sisi, INJILI YA KRISTO na UFALME WA MUNGU vionekane katika giza la maisha ya watu ili mwishoni tuyastahili ayasemayo Mt. Yohane katika Ufunuo wake (22:4-5) kwamba “watauona uso wake na Jina lake litaandikwa juu ya mapaji ya nyuso zao. Usiku hautakuwako tena wala hawatahitaji mwanga wa taa au wa jua, maana Bwana Mungu atawaangazia nao watatawala milele na milele. Tuombe neema ya kuangaza bila kuchoka, kuhifadhi bila kuchakaa, kutia ladha bila kuchoka, tukiwa wajumbe wa amani, haki na matumaini mwaka huu wa 2026. Amina.

Liturujia D 5 Mwaka A
05 Februari 2026, 15:39