2026.02.13 Kardinali Ambongo, Rais wa SECAM na Balozi Bankole Adeoye,Kamishna wa Masuala ya Siasa,Amani na Usalama(PAPS) wa Tume ya Umoja wa Afrika baada ya kutia saini Mkataba. 2026.02.13 Kardinali Ambongo, Rais wa SECAM na Balozi Bankole Adeoye,Kamishna wa Masuala ya Siasa,Amani na Usalama(PAPS) wa Tume ya Umoja wa Afrika baada ya kutia saini Mkataba. 

SECAM na Umoja wa Afrika wapyaisha Mkataba wa Maelewano,Addis Ababa!

SECAM na UA wasaini Mkataba Upya wa Maelewano katika Makao Makuu ya Tume ya UA,Addis Ababa,Februari 13.Saini ilitiwa siku moja tu kabla ya Kikao cha 39 cha Kawaida cha Baraza la Wakuu wa Nchi na Serikali la Umoja wa Afrika,kilichopangwa kuanzia Februari 14–15.Mfululizo wa matukio“unaakisi uimarishaji wa ushirikiano wa kitaasisi kati ya Umoja wa Afrika na SECAM na unasisitiza kujitolea kwa Kanisa Katoliki kuendelea kuchangia maana ya vipaumbele vya Afrika.”

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu wa Afrika na Madagascar (SECAM) na Umoja wa Afrika (UA) walisaini Mkataba kwa upya wa Maelewano(MOU) Ijumaa, tarehe 13 Februari 2026 saa 7:00 mchana katika Makao Makuu ya Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) huko Addis Ababa nchini Ethiopia. Mkataba huo (MOU) ulisainiwa kwa niaba ya SECAM na Kardinali Fridolin Ambongo Besungu, OFMCap, Askofu Mkuu wa Kanisa Kuu la Kinshasa,Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, na Rais wa SECAM, na kwa niaba ya Umoja wa Afrika alikuwa Mhe. Balozi Bankole Adeoye, Kamishna wa Masuala ya Siasa, Amani na Usalama (PAPS) wa Tume ya Umoja wa Afrika(UA.)

Secam na Umoja wa Afrika watia saini ya maelewano
Secam na Umoja wa Afrika watia saini ya maelewano

Makubaliano mapya yanaendeja na maagizo mapya na mfumo wa Tume ya UA

Kwa mujibu wa Taarifa kutoka SECAM, Utiaji saini huu umefanyika muongo mmoja baada ya MOU ya kwanza kuhitimishwa tarehe 19 Agosti 2015 katika Tume ya Umoja wa Afrika. Makubaliano mapya yanaendana na maagizo mapya na mifumo ya kitaasisi iliyotolewa na Tume ya Umoja wa Afrika, na kuimarisha ushirikiano uliopangwa kati ya UA na washirika wake.

Mkutano wa SECAM na UA
Mkutano wa SECAM na UA

Kuimarisha juhudi za pamoja katika kushughulika migogoro ya kibinadamu

MOU unalenga kuimarisha ushirikiano katika kukuza na kulinda haki za binadamu na watu, kuendeleza utawala bora, demokrasia, na utawala wa sheria, pamoja na uimarishaji wa ujenzi wa amani, maridhiano, na mshikamano wa kijamii kote barani. Pia unalenga kuimarisha juhudi za pamoja katika kushughulikia migogoro ya kibinadamu, kuwalinda watu waliokimbia makazi yao na watu walio katika mazingira magumu, kukabiliana na mabadiliko ya hali yatabianchi kupitia usimamizi endelevu wa maliasili, na kukuza maendeleo fungamani ya binadamu kulingana na Ajenda ya 2063: Afrika Tunayoitaka. Kama ilivyoelezwa katika maandishi yaliyosainiwa, ushirikiano huo umejikita katika maono ya pamoja ya Ajenda ya 2063: "Afrika iliyounganishwa, yenye ustawi na amani, inayoendeshwa na raia wake."

Mkutano wa SECAM na UA
Mkutano wa SECAM na UA

Mkutano wa SECAM kuhusu Uendelevu wa Maji na Usafi wa Mazingira,Februari 7

Muda wa kusainiwa upya ulikuwa ni muhimu sana. Imekuja siku sita baada ya SECAM kuandaa tukio la upande wa ngazi ya juu kwa ushirikiano na Umoja wa Afrika kuhusu Uendelevu wa Maji na Usafi wa Mazingira mnamo tarehe 7 Februari 2026 huko Addis Ababa, ambalo liliwaleta pamoja washirika muhimu wa bara na kimataifa, ikiwemo Kiti Kitakatifu kupitia Baraza la Kipapa la Kuhamasisha  Maendeleo Fungamani ya Binadamu. Pia ulifanyika siku moja tu kabla ya Kikao cha 39 cha Kawaida cha Baraza la Wakuu wa Nchi na Serikali la Umoja wa Afrika, kilichopangwa kufanyika tarehe 14–15 Februari 2026. Katika taarifa yake iliyotolewa kutoka Ofisi ya SECAM,  inabainisha kwamba “Mfululizo huu wa matukio unaakisi uimarishaji wa ushirikiano wa kitaasisi kati ya Umoja wa Afrika na SECAM na unasisitiza kujitolea kwa Kanisa Katoliki kuendelea kuchangia kwa maana vipaumbele vya Afrika.”

Mkutano wa SECAM na UA
Mkutano wa SECAM na UA

“Ushirikiano unawakilisha kanuni ya suluhisho za kiafrika kwa matatizo ya Kiafrika”

MOU mpya inaonesha imani ya pamoja kwamba ushirikiano mzuri wa pande nyingi ni muhimu na kwamba ushirikiano kati ya mashirika ya kimataifa, serikali, asasi za kiraia, na taasisi zenye msingi wa imani ni muhimu kwa ajili ya kuendeleza haki, amani, na maendeleo fungamani ya binadamu. SECAM aidha inabainisha kwamba “Wakati ambapo ushiriki mpya wa pande nyingi unazidi kuwa muhimu, ushirikiano huu unawakilisha kanuni ya suluhisho za Kiafrika kwa matatizo ya Kiafrika, zenye msingi wa mshikamano, uwajibikaji wa pamoja, na maono ya pamoja kwa mustakabali wa bara.”

Mkutano wa SECAM na UA huko Ethiopia
Mkutano wa SECAM na UA huko Ethiopia

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata taarifa mpya kwa kujisajili kwenye jarida letu la kila siku: Just click here.

14 Februari 2026, 09:53