Cuba:Wito wa mazungumzo,matumaini na Ulinzi wa Watu wa Cuba
Sr. Christine Masivo CPS, – Vatican.
Baba Mtakatifu Dominika tarehe 1 Februari 2026, mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, alionesha wasiwasi mkubwa kuhusu mvutano unaoongezeka kati ya mataifa jirani ya Cuba na Marekani, na akaungana na Maaskofu wa Cuba kuwasihi viongozi kuchagua njia za amani na kujenga.
Wito wa Papa wa amani
Akirudia msimamo thabiti wa Vatican, Papa alisisitiza kwamba migogoro, kulazimisha, na hatua zinazozidisha mateso haziwezi kamwe kuwa jibu. Badala yake, alitaka mazungumzo ya dhati na yenye ufanisi, akionya dhidi ya vitendo vinavyohatarisha kuongezeka kwa vurugu au kuzidisha hali chungu ambazo tayari zinavumiliwa na raia wa kawaida. Akikabidhi kisiwa hicho kwa utunzaji wa Mama Yetu wa Upendo wa El Cobre, aliomba ulinzi wake kwa watoto wote wa nchi hiyo pendwa.
Wito wa Maaskofu wa matumaini
Wito unaoendena na huo wa Papa, ni wa nguvu kutoka katika ujumbe wa hivi karibuni wa Baraza la Maaskofu katoliki Cuba kwa watu wote wenye nia njema. Kwa kuzingatia miongo kadhaa ya tafakari ya kichungaji, Maaskofu walithibitisha tena kwamba magumu yanayolikabili taifa hayawezi kushughulikiwa kwa njia ya uchambuzi au maelezo tu. Maaskofu hao walibainisha kuwa Nchini kote, mtu husikia kilio kile kile, ambacho mambo hayawezi kuendelea kama yalivyo, na maamuzi lazima yafanywe kwa manufaa ya taifa ili kurejesha matumaini.
Maaskofu walibainisha kwa huzuni kwamba hali imezidi kuwa mbaya. Maendeleo mapya hasa yale yanayoathiri upatikanaji wa rasilimali muhimu kama vile nishati ya umema, yamezidisha dhiki na kuongeza hatari ya kutokuwa na utulivu wa kijamii, hasa miongoni mwa walio katika mazingira magumu zaidi. Maaskofu hao aidha wanaonya kwamba uwezekano wa machafuko na vurugu miongoni mwa watu wale wale ni halisi, na kwamba hakuna Mkubwa mwenye nia njema anayeweza kufurahia matokeo kama hayo.
Mabadiliko ni muhimu
Ingawa wanatambua hitaji la dharura la mabadiliko makubwa ya kimuundo, kijamii, kiuchumi, na kisiasa, Maaskofu wako wazi. Cuba haihitaji uchungu zaidi, umwagaji damu, au maombolezo. Uzito wa mateso ambao tayari umebebwa na maskini, wazee, wagonjwa, na watoto haupaswi kuongezeka. Wakikumbuka maneno ya Mtakatifu Yohane Paulo II wakati wa ziara yake ya kihistoria nchini Cuba mwaka 1998, wanaukumbusha Ulimwengu kwamba kutengwa na shinikizo za nje zisizo na ubaguzi huwadhuru wanyonge zaidi, na kudhoofisha upatikanaji wa chakula, huduma ya afya, na elimu.
Dhamani ya mshikamano
Baba Mtakatifu na Maaskofu wa Cuba wanaakisi thamani ya kudumu ya mshikamano. Wanatoa shukrani kwa huruma iliyooneshwa na Jumuiya za ndani na za Kimataifa, Mashirika ya Kanisa, Serikali, na taasisi ambazo zimetoa msaada wakati wa majanga ya asili na uhaba. Ishara hizo, walithibitisha, zinaonesha kwamba udugu miongoni mwa watu unawezekana hata wakati wa shida kubwa. Katikati ya ujumbe huo kuna imani ya pamoja, kutokubaliana kati ya mataifa lazima kutatuliwe kupitia mazungumzo na diplomasia, si kupitia kulazimishwa au hatua zinazowaadhibu watu wote. Historia inaonesha kwamba kunapokuwa na nia njema, watu wanaweza kuzungumza, kuelewana, na kupata njia kuelekea ukweli, haki, upendo, na uhuru. Wakati huo huo, heshima kwa utu wa binadamu na uhuru wa msingi ndani ya taifa haiwezi kamwe kuwekewa masharti ya migogoro ya nje. Hakika, mazingira ya wingi na heshima ya pande zote ndani mara nyingi huwa daraja la mahusiano bora kimataifa.
Ushirikiano kwa kufunguka
Kwa kufafanua tena wito wa kudumu wa Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili, Kanisa linarudia tena himizo lake lililojaa matumain, ‘acha ulimwengu ufunguke kwa Cuba, na acha Cuba ifunguke kwa ulimwengu’ ili watu wake waweze kutembea katika njia ya amani, upyaisho, na mustakabali usio na kukata tamaa, bali kwa matumaini.
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata taarifa mpya kwa kujisajili kwenye jarida letu la kila siku: Just click here