Liturujia ya Neno la Mungu katika Dominika hii inatuongoza hatua kwa hatua katika kuelewa kwamba, “Mpango wa Mungu wa wokovu ni kwa watu wote” Liturujia ya Neno la Mungu katika Dominika hii inatuongoza hatua kwa hatua katika kuelewa kwamba, “Mpango wa Mungu wa wokovu ni kwa watu wote”   (@VATICAN MEDIA)

Tafakari Dominika ya Pili ya Mwaka A: Wokovu Ni Kwa Watu Wote!

Liturujia ya Neno la Mungu katika Dominika hii inatuongoza hatua kwa hatua katika kuelewa kwamba, “Mpango wa Mungu wa wokovu ni kwa watu wote” na unaanza kwanza kabisa na wito na jitihada za Mungu mwenyewe anayeanzisha safari hii katika maisha ya waamini wake; Pili ni namna ya kuitikia wito huu; Tatu ni mahali pa kuumwilisha wito huu ili uweze kuzaa matunda na kwamba, Kristo Yesu ndiye kilele cha safari ya ukombozi kwa njia ya Fumbo la Pasaka!

Na Padre Bonaventura Maro, C.PP.S., -Kolleg St. Josef, Salzburg, Austria.

Utangulizi: Wapendwa Taifa la Mungu, leo ni Dominika ya 2 ya Mwaka A wa Kanisa. Dominika iliyopita tuliadhimisha Sikukuu ya Ubatizo wa Bwana ambayo kimsingi ndio Dominika ya kwanza kabisa ya kipindi cha kawaida cha Mwaka wa Kanisa. Mama Kanisa anaanza Maadhimisho ya Juma la 60 la Kuombea Umoja wa Wakristo yaani kuanzia tarehe 18 Januari hadi tarehe 25 Januari 2026 Sikukuu ya Kuongoka kwa Mtakatifu Paulo Mtume na Mwalimu wa Mataifa, linanogeshwa na kauli mbiu: “Mwili mmoja, na Roho mmoja, kama na mlivyoitwa katika tumaini moja la wito wenu.” Efe 4:4. Tafakari ya Mwaka 2026 imeandaliwa na Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo pamoja na Kanisa la Kitume la Armenia linaloendelea kujitambulisha kuwa ni nguzo ya imani, umoja na mwendelezo wa Mapokeo ya Kikristo. Liturujia ya Neno la Mungu katika Dominika hii inatuongoza hatua kwa hatua katika kuelewa kwamba, “Mpango wa Mungu wa wokovu ni kwa watu wote” na unaanza kwanza kabisa na wito na jitihada za Mungu mwenyewe ambaye ndiye anayetuita kwa kuanzisha safari hiyo ndani mwetu, anayetukomboa, anayetuimarisha na kutushirikisha mpango wake wa ukombozi, kwa kutuweka kuwa nuru kati ya watu. Pili, ni namna sasa mwanadamu anavyopaswa kuitikia wito huu wa Mungu, yaani kwa utii, kwa unyenyekevu kwa uvumilivu na shukrani. Tatu, mahali tunapouishi wito wa Mungu na Imani yetu, yaani ndani ya kanisa, ndani ya jumuiya ya waamini, ndani ya familia zetu, na mwisho tukimtazama Kristo kama kilele cha safari ya ukombozi ya Mungu kwa wanadamu, kwa njia ya Fumbo la Pasaka.  Katika Dominika hii na kwa namna ya pekee tukiwa mwanzoni kabisa mwa mwaka, tumshukuru Mungu kwa mapendo yake makuu, aliyeamua kuanzisha tena upya mpango wa ukombozi kwa njia ya mwanaye wa pekee aliyetwaa mwili na kukaa katikati yetu. Tuombe neema ya Mungu ili sisi tulioshirikishwa Mpango wa Mungu wa ukombozi kwa njia ya ubatizo wetu, tuwe kweli mwanga kwa watu wote kwa njia ya ushuhuda wa maisha yetu yanayoakisi wito wetu wa kila siku wa kuwa watakatifu.

Mpango wa wokovu wa Mungu ni kwa ajili ya watu wote
Mpango wa wokovu wa Mungu ni kwa ajili ya watu wote   (@Vatican Media)

Somo la Kwanza: Ni kutoka katika Kitabu cha Nabii Isaya Isa 49:3, 5-6. Somo la kwanza tulilolisikia, kutoka katika kitabu cha Nabii Isaya ni wimbo wa pili (Isaiah 49:1-6) kati ya nyimbo nne za Mtumishi wa Mungu (Servant’s songs). Mazingira ya somo hili ni wakati taifa hili la Mungu walipokuwa utumwani Babiloni kuanzia mwaka 587 hadi mwaka 539/38 BC. Wakiwa utumwani waliteseka sana, waligundua kuwa walitoka nje ya njia ya Ahadi za Mungu. Ishara zote za Ahadi za Mungu zilipotea. Hekalu lilivunjwa vunjwa na kuharibiwa, waliondoshwa katika nchi yao na kupelekwa utumwani, walipoteza familia na ndugu zao, pamoja na mali zao zote. Wakiwa utumwani walidharauliwa na kudhihakiwa. Walinyanyaswa na kuteswa sana na watu wa Mataifa. Walijiona sio lolote si chochote tena. Waliona kama sio taifa teule tena la Mungu, na kama vile Mungu aliwaacha. Waliona kama Mungu wao hana nguvu tena na kwamba hana mpango nao tena. Kwa hiyo wengi wakawa wameanza kukata tamaa kabisa. Katika wakati huu ambapo waliona kabisa Mungu hawajali tena, wala hayupo pamoja nao tena, walipojisikia kabisa kwamba wao si wana wateule tena wa Mungu, walipojisikia si kitu tena, Nabii Isaya anakuja na huu wimbo wa pili wa Mtumishi wa Bwana, maneno mazito yenye kuamsha matumaini “Wewe u mtumishi wangu Israeli, ambaye katika wewe nitatukuzwa.”

Mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu ni chemchemi ya ukombozi
Mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu ni chemchemi ya ukombozi

Somo la Pili: Ni kutoka katika Waraka wa Mtakatifu Paulo 1 Kor 1:1-3. Mtume Paulo anawaandikia Wakorintho, jumuiya ambayo kimsingi hawakumpenda wala hawakumpokea sana. Walimtuhumu kwamba hakufahamu vyema jinsi ya kuongea. Lakini Paulo aliposikia changamoto bado katika kanisa la Korintho aliwaandikia waraka huu. Na anaanza waraka huu kwa namna ya pekee kidogo. Mwanzoni kabisa anaanza kwa kuutetea wito wake kama mmoja wa mitume wa Yesu. Anasema, “Paulo, aliyeitwa kuwa mtume wa Yesu Kristo kwa mapenzi ya Mungu, na Sosthenes ndugu yetu, kwa kanisa la Mungu lililoko Korintho” Wakoritho kama ilivyokuwa kwa jumuiya nyingine kama Galatia, hawakumtambua Paulo kama mmoja wa Mitume na ndio sababu yeye anaanza kwa kujitetea. Walisema, Paulo hakuwa mmoja wa mitume kumi na wawili wa Kristo. Je, mamlaka ya kuhubiri Injili kama mitume aliipata wapi?  Paulo aliyelitesa kanisa, Paulo aliyefanya kazi kubwa kuliumiza kanisa, leo anahubiri Injili ya Kristo. Hawakumkubali. Lakini tunamsikia tena hapa Sosthenes, huyu alikua mmoja watu waliomtesa na kumpeleka Paulo Kortini, bado Mungu alimtumia kuwa mshirika wa Paulo katika utume wake.

Mwenyezi Mungu ni chimbuko la miito na utume wa Kanisa
Mwenyezi Mungu ni chimbuko la miito na utume wa Kanisa   (ANSA)

Somo hili linatuonesha Mungu anayefanya kazi kupitia mwanadamu licha ya udhaifu wao ili kufikia lengo kubwa zaidi kwa ajili ya wokovu wa watu wake. Jumuiya ya Korintho hali kadhalika kwa kuipokea imani, kwa kupoke Injili walikumbushwa wajibu wao si tu kama mtu mmoja mmoja bali kama jumuiya ya kuishi maisha matakatifu. Huenda kuna nyakati uliwahi kukutana matukio ya kukatisha tamaa na ya kuvunja moyo hata ukatamani kuacha kazi ya utume Mungu aliyokupa, katika familia au katika miito mingine pia. Nabii Yeremia alipokwenda kwa wafalme kupeleka ujumbe wa Mungu, hawakumpokea. Akakata tamaa na kusema, sitasema wala sitamtaja tena kwa jina lake. Lakini twapaswa kutambua kuwa Mungu atakwenda kukamilisha kupitia wewe pale utaposema, Bwana, licha ya yote yanayotokea katika maisha yangu na safari yangu ya wito, bado nipo tayari, mimi ni mtumishi wako, niko tayari kutenda kama mtumishi wako kweli katika kila kitu utakachonituma kutenda. Sitajali watu watasema nini kuhusu mimi. Ninakwenda kufanya kazi kwa ajili yako kwa kuwa ninataka kuwa mwanga kwa watu wote. Hili ndilo jibu letu kwa Mungu anayetuita bila mastahili yetu na kutustahilisha kuifanya kazi yake.

Yohane Mbatizaji anamshuhudia Kristo Yesu kuwa ni Mwanakondoo wa Mungu
Yohane Mbatizaji anamshuhudia Kristo Yesu kuwa ni Mwanakondoo wa Mungu   (@Vatican Media)

Somo la Injili: Ni Injili kama ilivyoandikwa na Yohane 1:29-34. Katika somo la Injili Takatifu, Yohane mbatizaji anamshuhudia kwetu Kristo Mwana Kondoo wa Mungu azichukuaye dhambi za ulimwengu. Yohane hamtambulishi kwetu Yesu kama Mfalme wa Ulimwengu, bali anamtambulisha kwetu kama Mwanakondoo wa Mungu.  Kwa nini anatambulishwa Yesu kama Mwanakondoo wa Mungu azichukuaye dhambi za ulimwengu? Picha hii ya Mwanakondoo tunapata katika kitabu cha kutoka katika ile sura ya 12. Ni katika pasaka ya wayahudi ambapo mwanakondoo alichinjwa na damu yake ilipakwa juu ya miimo ya mlango ili wasipate pigo lolote wakati malaika alivyopita na kuwaua wazaliwa wa kwanza wa Misri. Hivyo Yesu ni huyu Mwanakondoo wa Mungu ambaye amekuja kutuokoa sisi kutoka katika kifo na mauti kwa njia ya Amekuja kutulinda na kutukinga mambo yote yanayotaka kutudhuru. Sio Mfalme aliyekuja kufurahia maisha, bali anakuja kuteseka, ili sisi tuupate tena uhai na uzima. Ndiye mtumishi wa Bwana aliyezungumziwa na Nabii Isaya katika somo la kwanza, utabiri unaotimia katika Fumbo la Pasaka: mateso, kifo na ufufuko wake.

Kwa njia ya Ubatizo, Yesu alitambulishwa kwa njia Roho Mtakatifu
Kwa njia ya Ubatizo, Yesu alitambulishwa kwa njia Roho Mtakatifu

Ndugu zangu, katika masomo yote katika Dominika hii ya Pili ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa tuna mafundisho yafuatayo ya kujifunza. Kwanza: Mwenyezi Mungu anafufua matumaini mapya ndani mwetu hata katika mkato mkubwa wa tamaa. “Katika wewe nitatukuzwa”. Somo la kwanza limeeleza hali ya ta taifa hili la Israeli waliokuwa utumwani kwa muda mrefu. Katika hali ya mkato wa tamaa, Mwenyezi Mungu anadhihirisha ukuu na uweza wake, anaamsha upya matumaini yao. Walijiona hawana thamani yoyote tena machoni pa watu na machoni pa Mungu. Lakini ni katika hali hiyo hiyo, ni katika mazingira hayo hayo bado Mungu anaahidi kwamba katika wewe mimi nitatukuzwa. Ndugu mpendwa, kutukuzwa ndani ya mtu ambaye alikwisha kata tamaa kabisa ni jambo lisiloweza kuelezeka kwa urahisi sana. Mtu aliyekwisha hesabika si kitu, aliyeonekana hana thamani tena, hana future yoyote, anayeonekana tu kama mtumwa huko Babiloni, Mungu anakwenda kutukuzwa kupitia huyo huyo mtumishi wake, Israeli aliyedharauliwa. Ndugu mpendwa, Mwenyezi Mungu hasemi jambo na wewe katika Dominika hii kupitia somo hili? Je, katika hali uliyo nayo au uliyowahi kupitia, Je, humwoni Mungu anayenena nawe na kukupa tumaini jipya leo hii?

Ubatizo ni mlango wa maisha ya uzima
Ubatizo ni mlango wa maisha ya uzima   (@Vatican Media)

Wewe ambaye wakati fulani umeonekana hufai kwa lolote lile. Kila ulichojaribu katika maisha hakikufanikiwa. Jamii imeshakuchukulia kwamba hufai kitu, familia imeshakuchukulia kwamba hufai kwa lotote, rafiki zako hali kadhalika. Huenda kwa sababu ya hali ya maisha unayopitia kwa sasa. Huenda kwa kuwa hujabahatika kupata ajira, huenda hukufanikiwa kufaulu vizuri masomo, huenda hauna uwezo kifedha, hauna ushawishi wala jina katika jamii. Huhusishwi hata kwenye vikao vya familia, maamuzi ya jumuiya kwa kuwa huna cha kuchangia wewe, hujulishwi hata baadhi ya mipango kwa kuwa huna msaada. Huitwi popote, hufuatwi kwa lolote, hupigiwi simu wala kujuliwa hali. Huenda umepitia hata changamoto nyingine za maisha, magonjwa, changamoto za kifamilia, na vyote hivyo vinakufanya ujione kabisa huna thamani tena mbele ya watu na mbele za Mungu, haoni tumaini tena, unaona kama dunia yote imekuelemea, na Mungu kama vile anakuadhibu. Hata sasa Mungu anasema nawe kama alivyosema na Taifa la Israeli waliokuwa kwenye hali ngumu kuliko hata ile ambayo tunaweza kuwa tunapitia kwa sasa, “Wewe u mtumishi wangu ambaye katika wewe nitatukuzwa. Unaweza kuwaza kwamba wewe hufai kitu machoni pa watu lakini machoni pa Mungu wewe ni chombo chake kiteule ambacho yeye mwenye anakwenda kutimiza mpango wake kupitia wewe. Machoni pa Mungu una thamani kubwa sana, kwa kuwa alijua mpango wake kwako hata kabla hajakuumba.

Mwenyezi Mungu ni chemchemi ya miito tote: Utakatifu
Mwenyezi Mungu ni chemchemi ya miito tote: Utakatifu   (@Vatican Media)

Pili: Wito unatoka kwa Mungu, Mwenyezi Mungu anakuinua na kukuimarisha ili uwe mwanga na taa inayoangaza. Taifa la Israeli walijiona kabisa hawana tena thamani. Walijisikia wako mbali na uso wa Mungu na hata kukata tamaa juu ya hadhi yao kama taifa teule la Mungu ambao Mungu tangu mwanzo aliwachagua ili wawe mwanga kwa mataifa. Lakini bado Mungu anaahidi kuwaimarisha tena na kuwafanya kuwa mwanga, kuwa chanzo ha ukombozi kwa watu wa mataifa yote. Kumbe, ni mpango wa Mungu kuwainua watu wake apendavyo ili kupitia hao alete mwanga na wokovu kwa watu wa mataifa yote. Paulo aliinuliwa Mungu licha ya udhaifu wake ili awe chanzo mwanga wa Injili kwa watu wa mataifa. Hali kadhalika wakoritho waliitwa, walishirikishwa Nuru ya Kristo na kuitwa kuwa watakatifu. Ndugu mpendwa, Mwenyezi Mungu ndiye anayemwinua kila mtu anavyopenda yeye, kisha kumwimarisha ili kupitia yeye watu wengine waione nuru. Sisi tumepata bahati ya kubatizwa, tumeitwa kwa nafasi ya kwanza, tumeinuliwa kutoka mavumbini, kutoka katika giza na bonde la dhambi na uvuli wa mauti na kukabidhiwa mwanga wa imani. Tumeimarishwa kwa roho Mtakatifu ili tuweze kuwaangazia watu wote wakaao gizani. Kwa ubatizo wetu tumekuwa vyombo vya wokovu wa Mungu. Katika kipindi hiki cha kawaida cha mwaka wa Kanisa ni muda wa kukua na kuimarika katika imani, matumaini na mapendo, na kwa njia hiyo tunakuwa daima tayari Mwenyezi Mungu atutumie kwa ajli ya kuleta nuru na mwanga kwa watu wengine. Yeye mwenyewe anasema, ni neno dogo sana wewe kuwa mtumishi wangu. Anatuahidi kwamba anakwenda kutubadilisha, na kutufanya vyombo vyake vya wokovu. Na wokovu huu ni kwa watu wa mataifa yote. Kumbe jibu letu kwa Mungu ni utayari wetu, kusema, tazama, nimekuja Bwana kuyafanya mapenzi yako kama tunavyotafakarishwa na Zaburi ya 40.

Tazama Nimekuja Kuyafanya Mapenzi Yako
Tazama Nimekuja Kuyafanya Mapenzi Yako   (@Vatican Media)

Tatu: Sisi tunaomfuata Kristo Mwanakondoo wa Mungu, hatuna budi kujitoa sadaka kikamilifu kwa ajili ya Mungu. Katika somo la Injili Takatifu, Yohane mbatizaji anamtambulisha kwetu mwanakondoo wa Mungu. Hamtambulishi kwetu Kristo kama mfalme anayekuja kufurahia maisha, la hasha, bali ni Mwanakondoo wa Mungu aneyekuja kutoa uhai wake kwa ajili ya uzima wetu. Atateseka, atakufa na kufufuka ili kuikamilisha kazi ya ukombozi wetu sisi wanadamu wote. Ndugu mpendwa, tukimwelewa Kristo kama mwanakondoo wa Mungu, basi tutamwelewa yeye tunayemfuata. Tunamfuata mwanakondoo wa Mungu, ni mwanakondoo wa kafara, na kama ninamfuata mwanakondoo wa kafara, ni lazima na sisi katika maisha yetu tuwe watu wa kujitoa daima sadaka. Ninapaswa kuwa mtu wa kuamsha matumaini mapya kati ya watu, kuwasha moto wa imani kati ya watu na kuushi upendo wa kweli kati ya watu. Kama tunamfuata mwanakondoo wa Mungu tunapaswa na sisi pia kuwa kondoo kwa ajili ya wengine. Tutaondoa daima ubinafsi, katika nyanja zote za maisha yetu. Hatuwezi kumfuata Mwanakondoo wa Mungu huku tunakua waporaji na wadhulumishi wa haki za wengine, hatuwezi kusema tunamfuata mwanakondoo huku tunakua chanzo cha maumivu na vilio kwa wengine, hatuwezi kusema tunamfuata mwanakondoo wa Mungu huku tunaogopa kusema ukweli na kusimamia haki.  kama wazazi katika familia zetu tunaalikwa kujitoa sadaka kwa ajili ya familia zetu, kwa ajli ya kukaa na watoto wetu, kwa ajili ya kusali pamoja, kula pamoja. Ninaitwa kuwa mwanakondoo, kusahau kujifikiria zaidi mimi na kuwaza kuhusu wengine.

Mwanakondoo wa Mungu aondoaye dhambi za walimwengu
Mwanakondoo wa Mungu aondoaye dhambi za walimwengu   (@Vatican Media)

Hitimisho: Katika Dominika hii na kwa namna ya pekee, tukiwa mwanzoni kabisa mwa mwaka, tumshukuru Mungu kwa mapendo yake makuu, aliyeamua kuanzisha tena upya mpango wa ukombozi kwa njia ya mwanaye wa pekee aliyetwaa mwili na kukaa katikati yetu. Tuombe neema ya Mungu ili sisi tulioshirikishwa Mpango wa Mungu wa ukombozi kwa njia ya ubatizo wetu, tuwe kweli mwanga kwa watu wote kwa njia ya ushuhuda wa maisha yetu yanayoakisi wito wetu wa kila siku wa kuwa watakatifu.

Dominika ya Pili Mwaka A

 

17 Januari 2026, 09:44