Hali ya wakimbizi: Hali ya wakimbizi:  (AFP or licensors)

"Maaskofu Sudan na Sudan Kusini:Tufuate yale yanayoleta amani na kujengana sisi kwa sisi"

Katika taarifa iliyotolewa na Baraza la Maaskofu Katoliki la Sudan Kusini na Sudan(SSSCBC)ya tarehe 27 Januari imeelekezwa kwa:Serikali ya Umoja wa Kitaifa na Vikundi vya Upinzani katika Nchi:"Tufuate yale yanayoleta amani na kujengana sisi kwa sisi"(Rm 14:19).Katika kukabiliana na hali mbaya ya kisiasa,Usalama na kibinadamu nchini mwetu,tunalaani kwa nguvu mapigano mapya kati ya vikosi vya serikali,SPLA-IO na vikundi vingine vya upinzani."

Na Na Sr. Christine Masivo, CPS,- Vatican.

“Sisi Maaskofu Wakatoliki wa Kanda ya Sudan Kusini na  Sudan katika kukabiliana na hali mbaya ya kisiasa, Usalama na kibinadamu nchini mwetu, tunalaani kwa nguvu zaidi mapigano mapya kati ya vikosi vya serikali, SPLA-IO na vikundi vingine vya upinzani vyenye silaha, hasa katika Majimbo ya Jongle na Ikweta Mashariki. Ndivyo ilivyo katika taarifa iliyotolewa na Baraza la Maaskofu Katoliki la Sudan Kusini na Sudan (SSSCBC) iliyoandikwa tarehe 27 Jananuri 2026, ikielekezwa kwa “Serikali ya Umoja wa Kitaifa na Vikundi vya Upinzani katika Nchi yao pendwa kwa kauli mbiu: "Tufuate yale yanayoleta amani na kujengana sisi kwa sisi"(Rm14:19).

Kardinali Ameyu,Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Juba
Kardinali Ameyu,Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Juba

Wasiwasi wa Maaskofu kwa niaba ya watu wanaoteseka

Maaskofu wanabainisha:“Mwaka 2025, tulionesha wasiwasi mara mbili kwa niaba ya watu wanaoteseka wa Sudan Kusini kwa viongozi wa kisiasa. Tunakuja tena kwa dharura kurudia wito wetu wa mazungumzo, umoja, amani na maridhiano katika Jamhuri ya Sudan Kusini. Tena mnamo Julai 2025, tuliwataka viongozi wote wa kisiasa wasipuuze mazungumzo na tukasema "migogoro hii yote nchini inatokea kwa sababu mazungumzo ya kweli yanatengwa kimakusudi, huku hatua za kijeshi zikichukuliwa kimakosa kama suluhisho la kushughulikia tofauti za kisiasa na kijamii. Kwa hivyo, tuliuliza viongozi wetu wa serikali na upinzani: "je, mna nchi hii na watu wake mioyoni mwenu au mnajali na kuhangaika na kutafuta madaraka na utajiri tu?" Wakati wa mkutano wetu wa kila mwaka katika Jimbo Katoliki ya Malakal Novemba iliyopita, tuliwasihi pande zote za makubaliano ya amani kufanya kazi kwa manufaa ya watu wanaoteseka nchini Sudan Kusini wakati: "tunatoa wito wa utekelezaji kamili wa Mkataba wa Amani Uliohuishwa kwa Azimio la Mgogoro Sudan Kusini (R-ARCSS) na pande zote ili kujenga imani kwa watu na kushiriki katika mazungumzo ya dhati."

Tunashangazwa na kupuuzwa kwa utekelezaji wa amani

Maaskofu hao wanabainisha kwamba, kama Wachungaji na viongozi katika nchi hii, tunashtushwa na kushangazwa na kupuuzwa kabisa kwa utekelezaji kamili wa makubaliano ya amani yaliyohuishwa. Mzozo unaoongezeka ndani ya Serikali ya Umoja, mashambulizi ya kukabiliana kati ya pande zinazopigana. Katika sehemu nyingi za nchi unaenea kwa kasi na kusababisha watu kuhama makazi yao, njaa, na hali nyingine nyingi zisizo za kibinadamu. Kuna ongezeko la kutisha la wizi wa kutumia silaha wa madereva na watu wa kawaida hata katika jiji la Juba na sehemu zingine za nchi. Tuna wasiwasi pia na utoaji wa maneno makali katika mitandao ya kijamii, ambayo huongeza hotuba za chuki, taarifa potofu na za kugushi. Sehemu mbaya zaidi ya aina hii ya mawasiliano katika mitandao ya kijamii ni kukuza hisia za kikabila na uchochezi. Maaskofu Wakatoliki wa Sudan Kusini wanalaani hasa, hotuba inayodaiwa ya Jenerali Johnson Olony, Naibu Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi vya Sudan Kusini (SSPDF) kwa Uhamasishaji na Upokonyaji Silaha, akitaka vurugu zisizo na ubaguzi dhidi ya raia katika Jimbo la Jonglei. Kuelekeza vikosi "kutoacha maisha" ni wito wa moja kwa moja kwa mauaji ya kimbari. Tunatoa wito kwa vikosi vyote vya mapigano kutotii agizo lolote linalohatarisha kuwatesa raia wasio na hatia na kugombanisha jamii dhidi ya kila mmoja."

Tunawasihi viongozi wa Serikali ya Umoja kutia saini ya kukomesha vita

Maaskofu wanaendelea kutoa rai kwamba: "Tunawasihi nyote viongozi katika Serikali ya Umoja na wale ambao hawajatia saini Mkataba wa Amani Uliohuishwa kukomesha vita na kukumbatia mazungumzo, kusikilizana na watu mnaodai kuwapigania. Raia si mali, ni wanadamu na itakuwa vizuri kujua maumivu yao, njaa ya amani, na hamu yao ya kuishi kwa uhuru. Kwa jina la Mungu tunawaita "tufuate kile kinachoongoza kwenye amani na kujengana sisi kwa sisi" (Rm 14:19). Hatutachoka kunukuu maneno ya Baba Mtakatifu Francisko ambaye kutoka mbinguni bado anawaambia kama viongozi wa watu huko Sudan Kusini "hakuna vita tena, "Hakuna umwagaji damu tena, hakuna migogoro tena, hakuna vurugu tena na shutuma za pande zote kuhusu ni nani anayehusika nayo, hakuna kuwaacha watu wenu kiu ya amani tena. Hakuna uharibifu tena: Ni wakati wa kujenga! Acha wakati wa vita na wakati wa amani uje" (Ujumbe wa Papa Francisko kwa watu wa Sudan Kusini 2023).

Papa Francisko wakati wa Ziara yake ya Kitume nchini Sudan Kusini
Papa Francisko wakati wa Ziara yake ya Kitume nchini Sudan Kusini   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Watu wote wapenda amani wasipoteze tumaini kwa Mungu

Mababa wa Kanisa hili la Sudan na Sudan Kusini wanasisitiza kwamba, "tunawaomba watu wote wapenda amani wasipoteze tumaini kwa Mungu "tumaini ambalo halikatishi tamaa, kwa sababu upendo wa Mungu umemiminwa mioyoni mwetu na Roho Mtakatifu ambaye tumepewa."Tushikilie maombi kwa ajili ya nchi hii. Nchi hii ni zaidi ya matamanio yoyote ya kibinadamu, ni makazi ya vizazi elfu vijavyo. Tuitunze na tujilinde na hasa tumuombe Mungu atupe siku mpya. Hatuna Sudan Kusini nyingine ya kuhamia, kwa hivyo tufanye kazi kwa kile kinachotuunganisha. Kwa washirika wetu wote, mashirika ya kikanda na jumuiya ya kimataifa, watu wa Sudan Kusini wanafahamu mchango wenu muhimu. Ninyi ni marafiki zetu kwa vitendo na tunawasihi kwa niaba ya watu wanaoteseka wa nchi yetu msichoke kutenda yaliyo mema kwao. Tunawaomba mapadre  wetu, wanaume na wanawake wa kidini na watu wote wenye mapenzi mema kutenga muda huu kwa ajili ya maombi maalum kwa ajili ya amani katika nchi yetu. Maria Mama yetu na Malkia wa Amani atuombee.

Papa Francisko alitembelea Kusini Sudan 2023
Papa Francisko alitembelea Kusini Sudan 2023   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Ujumbe umetiwa saini na Kwa niaba ya Maaskofu Wakatoliki nchini  Sudan Kusini na Kardinali Stephen Ameyu Martin Mulla, Askofu Mkuu wa Juba na  Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki wa Sudan na Sudan Kusini (SSSCBC)

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata taarifa mpya kwa kujisajili kwenye jarida letu la kila siku: Just click here

29 Januari 2026, 17:30