Misa ya maandalizi ya Siku kuu ya Mtakatifu Vincent Pallotti (1795-1850). Misa ya maandalizi ya Siku kuu ya Mtakatifu Vincent Pallotti (1795-1850). 

Jubilei ya Miaka 230 ya Kuzaliwa kwa Mtakatifu Vincent Pallotti

Kumbukumbu ya Mwanzilishi wa Shirika la Umoja wa Utume Mkatoliki,Mtakatifu Vincent Pallotti(1795-1850),huadhimishwa kila ifikapo Januari 22.Maadhimisho ya mwaka 2026,yanakwenda sanjari na kumbukumbu ya miaka 230 tangu kuzaliwa kwake,miaka 200 ya Jubilei ya upadre wake,miaka 175 tangu kufariki kwake na miaka 190 tangu kuanzishwa rasmi kwa Umoja wa Utume Mkatoliki.

Na Sr Ernestina P. Lasway,SAC, – Vatican.

Wamisionari wa Shirika la Umoja wa Utume Mkatoliki (Wapallottini) duniani kote, walianza sala ya siku tatu kuanzia tarehe 19 Januari kwa ajili ya maandalizi ya sherehe ya kumbukumbu ya mwanzilishi wa Shirika hilo Mtakatifu Vincent Pallotti(1795-1850), aliyekuwa Padre wa mji wa Roma. Maadhimisho ya kumbukizi hii hufanyika ifikapo tarehe 22 Januari, ya kila mwaka ambapo mwaka 2026, yanakwenda sanjari na kumbukumbu ya miaka 230 tangu kuzaliwa Mtakati Vincent Pallotti, miaka 200 ya Jubilei ya upadre  wake, miaka 175 tangu kufariki kunako tarehe 22 Januari 1850, na miaka 190 tangu kuanzishwa rasmi kwa Umoja wa Utume Mkatoliki(SAC).

Misa ya maandalizi kwa siku tatu ya Siku Kuu ya Mtakatifu Vincent Pallotti
Misa ya maandalizi kwa siku tatu ya Siku Kuu ya Mtakatifu Vincent Pallotti

“Mradi tunaishi, bado kuna Tumaini”

Jubilei hii inaongozwa na kauli mbiu ya mafundisho ya Mtakatifu Vincent Pallotti aliyesema: “Mradi tunaishi, bado kuna Tumaini.” Maneno haya yanatualika kuimarisha moyo wa kimisionari na kupyaisha tumaini letu kwa Mungu, mwenye upendo usio na mipaka. Katika maadhimisho haya ambayo hufanyika Ulimwenguni kote, kuenzi mchango wa Mtakatifu Vincent Pallotti kwa kazi zake za kitume, kuanzisha shirika la Masista, Mapadre na Umoja wa Utume Mkatoliki, ni fursa kwa kila mbatizwa kutafakari nafasi yake kama mtume wa Baba wa milele. Mtakatifu Vincent Palllotti katika mafundisho yake alihimiza kuwa kila mbatizwa ni mtume na anaweza kushiriki kwa dhati katika kazi ya ukombozi, kuanzia ukombozi wa nafsi ya mtu binafsi na pia ya jirani zetu.

Maandalizi ya Siku Kuu ya Mtakatifu Vincent Pallotti
Maandalizi ya Siku Kuu ya Mtakatifu Vincent Pallotti

Ushauri wa Mtakatifu Vincent Pallotti

Kuna ushauri mwingi wa Mtakatifu Vincent Pallotti kama alivyoandika kwenye  Katiba  ya Shirika, kuwa: "Kila Mkristo hufurahia wazo la kumwiga Bwana wetu Yesu Kristo: lakini ni wachache wanaojitahidi kila mara na kiukweli kumwiga, kwa sababu ni wachache wanaofikiria hilo. Miongoni mwa hawa ni wachache ambao ni wa Utume wa Kikatoliki." Na zaidi anabainisha kuwa:  "Mungu wangu... Sio akili, bali Mungu, si utashi, bali Mungu... sio roho, bali Mungu, si kuona, bali Mungu, si sikio, bali Mungu, si harufu, bali Mungu, si ladha na usemi, bali Mungu, si pumzi, bali Mungu, si mguso, bali Mungu, si moyo, bali Mungu, si mwili, bali Mungu, si hewa, bali Mungu, si chakula na kinywaji, bali Mungu, si mavazi, bali Mungu, si kitanda, bali Mungu, si vitu vya muda, bali Mungu, si utajiri, bali Mungu, si heshima, bali Mungu, si tofauti za kidunia, bali Mungu, si heshima, bali Mungu, si vyeo, ​​bali Mungu, si kupandishwa cheo, bali Mungu, Mungu katika mambo yote na siku zote." "Yesu Kristo alikuwa akikua. Sasa wale wote walio na watakaokuwa katika Shirika... lazima wawe na sifa zao za kutofautisha,  za kusonga mbele kila wakati na kukua katika utakatifu na ukamilifu wa kiinjili ili kushirikiana vyema katika kazi za utukufu mkuu wa Mungu na wokovu wa roho.” Katika maandiko yake aidha anabainisha kuwa  “Nafsi inayomwamini Yesu Kristo na kujitahidi kumwiga kwa unyenyekevu na uaminifu, ni kwamba inapata Yesu Kristo ambaye  huharibu kila ulemavu na kutokamilika ndani yake; Yesu Kristo huingia ndani ya nafsi hiyo, anaishi ndani yake na kuipatia sifa ya kazi zake takatifu zaidi."

Maandalizi ya Siku Kuu ya Mtakatifu Vincent Pallotti
Maandalizi ya Siku Kuu ya Mtakatifu Vincent Pallotti

Maandalizi ya Kumbukumbu kwa Tridium

Katika kuenzi  Jubilie hii, Mjini Vatican, katika Kanisa  ambalo umelala  mwili wake  Mtakatifu Vincent Pallotti la Mtakatifu Salvatore, jijini Roma siku tatu za sala ya maandalizi ilianza tangu tarehe 19 Januari  jioni  na kuwa na ushiriki mkubwa wa Mapadre, Masista, Wana Umoja wa Utume Mkatoliki na waamini wengine walei.  Tridium au  Siku tatu za sala ya Maandalizi ni kipindi cha neema na baraka, ambacho tunasali, tunamwabudu Yesu wa Ekaristi na kupata baraka. Kilele cha maadhimisho haya ni tarehe 22 Januari  2026 ambapo mjini Roma na katika Kanisa mahalia au mahali popote walipo wamisionari Masista,  Mapadre na Wanaumoja wa Utume Mkatoliki ambao wanamuenzi Mwanzilishi wao,  inaadhimisha kumbukizi hii.

Maandalizi ya Siku Kuu ya Mtakatifu Vincent Pallotti
Maandalizi ya Siku Kuu ya Mtakatifu Vincent Pallotti

Upendo wa Kristo unatubidisha (2Kor 5:14)

Katika Mahubiri ya Siku ya Kwanza kati ya Tatu ya maandalizi iliyofanyika katika Kanisa la Mtakatifu Salvatore jijini  Roma, kwa kuongozwa na Padre Luciano Alimandi, alijikita na  taswira ya “Divai mpya na Viriba vya zamani” kutoka Injili ya Marko(Mk.2:18-22). Taswira hii inaonesha asili yenye mwendo wa utakatifu hasa katika maisha ya mkristo anayeuchuchumilia utakatifu katika maisha ya kila siku. Padre huyo alisema, “Utakatifu ni divai mpya, ni uhalisia mpya unaokuwa na kupanuka kila siku, unatolewa kwa neema na si kitu kilichoganda au kujitosheleza chenyewe.” Mtakatifu Vincent Pallotti  kwa njia hiyo alitambua undani wa ukweli huu  na kusema “Upendo wa Kristo unatuchochea kusonga mbele.” Huu ndiyo wito  wa Shirika la Wapallottini  kuwa“Upendo wa Kristo Watubidiisha” (2Kor 5:14). Upendo huu unatuchochea kusonga mbele, si upendo wa kukaa kimya tu, unamsukuma mwamini kuvuka daraja la hofu, na kujijali mwenyewe,alisisitiza Padre Almandi. Kwa kuwa upendo wa Kristo unatusukuma kusonga mbele, utakatifu hauwezi kubaki kuwa jambo la faragha au ndani tu, bali ni jambo la imani linalopaswa kujifunua katika maisha ya kila siku kwa maneno na matendo yetu. Kwa kufanya hivyo, viriba vilivyopyaishwa vinaruhusu upendo wa Kristo kuendelea kulisukuma Kanisa mbele kwa maisha ya utakatifu.

Baada ya misa ya maandalizi ya Siku Kuu ya Mtakatifu Vincent Pallotti
Baada ya misa ya maandalizi ya Siku Kuu ya Mtakatifu Vincent Pallotti

Mungu huwachagua wale awapendao,bila kuangalia aliye na nguvu au mvuto wa nje”

Naye Padre Wixin Masih, Gombera wa Chuo Kikuu Urbaniana, ili kuutafari vyema wito wa Mtakatifu  Vincent Pallotti, tafakari yake ilijikita kwenye wito wa Daudi.  “Nimemkuta Daudi Mtumishi Wangu,” ni maneno yanayodhihirisha kuwa Mungu huwachagua wale awapendao, bila kuangalia aliye na nguvu au mvuto wa nje. “Mungu huwachagua walio wake kwa kuangalia utu wa ndani, unyenyekevu na ukimya”, aliongeza. Daudi alikuwa chaguo la Mungu, japo hakuwa mzaliwa wa kwanza au mwenye kuthaminiwa sana na familia yake,vivyo hivyo Mungu huwaita awapendao katika nyakati zetu hata kama kwa macho ya kibinadamu hatuwezi kuona. Kwa namna kama hiyo Mungu alimwita Mtakatifu Vincent Pallotti na kujenga kazi yake juu ya mamlaka na Imani isiyo na mipaka kwa Mungu na juu ya heshima ya ubatizo. Kama Daudi alivyochaguliwa kwa kuwa na moyo wa kusikiliza, kuamini na kubadilika, vivyo hivyo Mtakatifu Vincent Pallotti aliwaka moto wa upendo na utume katika wito wake. Padre Wixin Masih alisisitiza kuwa, wito haumfanyi mtu awe juu ya wengine, bali humfanya awe mwajibikaji mkubwa kwa watu anaotumwa kwao. Kwa kumwadhimisha Mtakatifu Vincent Pallotti, tunaongozwa na roho wa Mungu kuendeleza kazi alizozianzisha, alihimiza.

Masalia ya Mwili wa Mtakatifu Vincent Pallotti
Masalia ya Mwili wa Mtakatifu Vincent Pallotti

Maadhimisho ya Jubilei nchini Tanzania

Katika kuadhimisha Jubilei hii ya Wapallottini  Ulimwenguni, hata nchini Tanzania, wanashirika walijiandaa kwa hija katika Parokia ya Bikira Maria Mama wa Mateso Gallapo, Jimbo Katoliki la Mbulu, kwa kuhitimisha na kufunga mwaka wa Jubilei tarehe 22 Januari 2026. Mkuu wa Shirika la Mapadre Wapallottini,  Kanda ya Afrika Mashariki, Padre John Onna,(SAC,) akiwaalika Mapadre, Watawa na Waamini Walei kushiriki vyema katika kilele cha hija hiyo  alibainisha kuwa, “Jubilei ni wakati Mtakatifu kwa Familia nzima ya Wapallottini Ulimwenguni, inaadhimishwa sanjari na Jubilei ya Kanisa Ulimwenguni na inatualika kutafakari mwanga wa miaka 190 ya maono ya Mtakatifu  Vincent Pallotti, kuhamasisha ushiriakiano kati ya Walei, Watawa na Mapadre uliolenga kufufua Imani, kuamsha upendo na kulea utume kwa wote.”

Washiriki wa Maandalizi ya Siku Kuu ya Mtakatifu Vincent Pallotti
Washiriki wa Maandalizi ya Siku Kuu ya Mtakatifu Vincent Pallotti

Kipindi hiki cha maadhimisho ya Jubilei kanisa pia kinatoa fursa  ya kupokea Rehema Kamili. Wakati mjini Roma Wanashirika wataadhimisha siku hii adhimu kwenye Kanisa la Mtakatifu Salvatore(Salvatoris in Unda,) Nchini Tanzania, Mahujaji kutoka Ukanda wa Afrika Mashariki, watakwenda Gallapo huko Mbulu kwa sababu ndipo kitovu cha kihistoria kwa uwepo wa Wapallottini Afrika Mashariki, kilipo tangu mwaka 1940.

22 JANUARI SIKU KUU MTAKATIFU PALLOTTI

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here

 

21 Januari 2026, 15:20