Papa Leo XIV: Waamini jengeni utamaduni wa kusoma, kutafakari na kulimwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa vipaumbepe vya maisha yenu! Papa Leo XIV: Waamini jengeni utamaduni wa kusoma, kutafakari na kulimwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa vipaumbepe vya maisha yenu!  (Vatican Media)

Dominika ya Tatu ya Mwaka A wa Kanisa; Dominika ya Saba ya Neno La Mungu 2026

Hati ya Kusikiliza kwa Uchaji Ufunuo wa Neno la Mungu “Dei verbum” inagusia kwa undani kuhusu: Ufunuo wenyewe; Urithishaji wa Ufunuo wa Kimungu; Uvuvio wa Kimungu na Ufafanuzi wa Maandiko Matakatifu; Agano la Kale, Agano Jipya; pamoja na Maandiko Matakatifu Katika Maisha ya Kanisa. Papa Leo XIV anasema, Mwenyezi Mungu kwa njia ya Kristo Yesu, Ufunuo wa Baba wa milele, anazungumza na wanadamu kama mtu anavyo zungumza na rafiki yake.

Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.

UTANGULIZI: Karibu mpenzi msikilizaji na msomaji wa tafakari ya Neno la Mungu kutoka hapa Radio Vatican. Dominika hii tunaendelea na safari ya mwanga tuliyoanza tangu Noeli, Epifania, na Dominika zilizopita. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Juma 59 la Kuombea Umoja wa Wakristo linalonogeshwa na kauli mbiu: “Mwili mmoja, na Roho mmoja, kama na mlivyoitwa katika tumaini moja la wito wenu.” Efe 4:4. Tafakari ya Mwaka 2026 imeandaliwa na Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo pamoja na Kanisa la Kitume la Armenia linaloendelea kujipambanua kuwa ni nguzo ya imani, umoja na mwendelezo wa Mapokeo ya Kikristo. Baba Mtakatifu Leo XIV anawahamasisha waamini wa Kanisa Katoliki kujibidiisha kusali kwa ajili ya kuombea Umoja wa Wakristo, ili umoja kamili na unaoonekana wa Wakristo wote uweze kupatikana. Hii ni dhamana na wajibu unaopaswa kujikita katika kutafuta na kudumisha haki na amani, sehemu mbalimbali za dunia. Hati ya Kusikiliza kwa Uchaji Ufunuo wa Neno la Mungu “Dei verbum” inagusia kwa undani kuhusu: Ufunuo wenyewe; Urithishaji wa Ufunuo wa Kimungu; Uvuvio wa Kimungu na Ufafanuzi wa Maandiko Matakatifu; Agano la Kale, Agano Jipya; pamoja na Maandiko Matakatifu Katika Maisha ya Kanisa. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Mwenyezi Mungu kwa njia ya Kristo Yesu, Ufunuo wa Baba wa milele, anazungumza na wanadamu kama mtu anavyo zungumza na rafiki yake. Huu ni mwaliko kwa waamini kujenga na kudumisha utamaduni wa kusoma, kulitafakari na hatimaye, kulimwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao pamoja na kujikita katika maisha ya sala!

Neno la Mungu liwe ni dira na mwongozo katika maisha.
Neno la Mungu liwe ni dira na mwongozo katika maisha.   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Kumbe, leo tunasherehekea Dominika ya Saba ya Neno la Mungu, siku ya kutukuza Neno la Mungu, ambalo linatufundisha, kutuongoza, na kutufanya kuwa wafuasi wa kweli wa Kristo. Katika dunia iliyojaa giza la migawanyiko, vita, na mateso, Neno la Mungu ni mwanga unaoangaza njia yetu. Kwa hivyo, tutapata nguvu ya kuishi maisha ya haki na amani kwa kufuata Neno la Mungu kila siku. ambayo ilianzishwa na Papa Francisko kwa mara ya kwanza mwaka 2019 ili kutukuza umuhimu wa Neno la Mungu katika maisha ya Wakristo. Inafanyika kila mwaka, katika Dominika ya Tatu ya Mwaka A, kuangazia umoja wetu na umuhimu wa kusikiliza, kufahamu na kutenda kulingana na Neno la Mungu. Masomo ya leo yanaunganishwa na wito wa Yesu, Mwanga wa Mataifa. Anatuambia: “Watu waliokaa gizani wameona mwanga mkuu.” (Is 9:2) Neno lake lina nguvu ya kuleta mwanga wa matumaini na amani katika maisha yetu. Sisi sote tumeitwa kuleta mwanga huo kwa dunia. Nabii Isaya katika somo la kwanza  anatabiri kuhusu watu waliokaa katika giza, lakini anasema kwamba watapata mwanga mkuu. Katika dunia ya leo, kuna giza kubwa, giza la chuki, vita, ukosefu wa haki, na maumivu. Hata hivyo, Neno la Mungu ni mwanga wa matumaini. Katika Neno lake, tunapata mwelekeo na faraja.

Neno la Mungu lipewe kipaumbele katika malezi na makuzi ya Kikasisi
Neno la Mungu lipewe kipaumbele katika malezi na makuzi ya Kikasisi   (Vatican Media)

Neno la Mungu ni mwanga wa wokovu, Yesu alikuja kutangaza Ufalme wa Mungu—ule ufalme unaosafisha, unaponya, na unaorodhesha haki kwa wote. Neno la Mungu linatusaidia kutambua ukweli na kutokubali kuishi katika giza la dhambi na kutokuelewa. Mwanga wa Neno hutufanya kuwa vyombo vya amani, Tunapoyapokea na kuyahifadhi Neno la Mungu, tunakuwa na amani katika mioyo yetu, na tutakuwa na amani kwa watu wetu. Mwanga ni nuru inayowezesha kuona njia, kufanya kazi, kuona aibu... Pia mwanga hueleza wazo au namna ya utendaji, mmoja atasema “nimepata mwanga namna ya kufanya ujasiriamali, kusoma, kuimba…” Mwanga unaletwa na jua na vifaa kama taa za umeme, mafuta, vibatari, tochi.. Mwanga una nguvu, mshumaa mdogo unaweza kupambana na giza kubwa na kulishinda. Kinyume cha mwanga ni giza, hilo si jema na wengi huliogopa, wengine huamini giza ni makao ya viumbe wabaya, gizani maovu hufanyika, wizi hutokea, ujambazi unatekelezeka na mipango ovu inawezekana. Hiyo ndiyo heri yetu tuliobatizwa, kwake giza halina nguvu, giza lililopofusha macho kwa vizazi vingi, lililomuinua shetani kwa miongo na karne na milenia, lililoficha ukweli halisi wa upendo wa Mungu na kusababisha tujigonge kwenye viambaza na milangoni kwa kutoona vizuri. Hili ni giza lililowapa watu wabaya nafasi ya kutenda wapendavyo. Tufurahi sababu Neno la Mungu linatupa faraja, kwamba enzi ya giza hilo imepita, sisi tuliokaa ng’ambo ya Yordani (mbali na Mungu), kwa ujio wa Kristo tumeona nuru kuu.. TU WANA WA NURU... amina.

Juma la 59 la Kuombea Umoja wa Wakristo
Juma la 59 la Kuombea Umoja wa Wakristo   (@Vatican Media)

UFAFANUZI:Mtume Paulo anawaalika Wakristo wa Korintho kuwa na umoyo mmoja na mawazo moja, kuepuka mgawanyiko. Neno la Mungu ni kile kinachotufanya kuwa na umoja katika Kristo. Tunapokuwa na Neno la Mungu, tunaunganishwa na mafundisho yake na tutakuwa wamoja katika imani. Umoja katika Kristo, kupitia Neno, Dunia yetu inagawanyika kwa misingi ya kidini, kisiasa, na kijamii. Lakini Kanisa linatufundisha kuwa Neno la Mungu linatufanya kuwa watu wa umoja. Hatuwezi kusema "mimi ni wa Paulo" au "mimi ni wa Apolo". Sisi ni wa Kristo. Mwanga wa Neno unapoingia ndani yetu, hutufanya kuwa wamoja. Neno la Mungu linatufanya kuwa vyombo vya haki, Paulo anasema: "Kristo alitupatia wokovu", hii ni haki ya Mungu iliyozungumziwa katika Neno lake. Haki ya Mungu haikuji kwa njia ya majivuno au upendeleo, bali kwa upendo na ukweli. Neno la Mungu linatufundisha kutoa haki kwa wote bila ubaguzi. Hii ni Dominika ya Neno la Mungu lililo moja ya nguzo muhimu ya ukristo, Neno hilo ni jema, linatupa wokovu, basi na tulifurahie. Ni katika Neno tunakutana na Kristo, tunapata ufunuo wa kimungu na kuyajua mapenzi yake. Neno hilo ni taa ya kutuongoza na mwanga wa miguu yetu. Ni sauti ya Mungu mwenyewe, linaimarisha imani, linakuza matumaini na kueneza mapendo. Kwa njia ya Neno tunasali, tunatukuza na kubarikiana, tunajipatia neema na nguvu ya kuendelea mbele katika hija yetu hapa duniani. Basi na tulisome, tulitafakari na kuliweka katika utendaji stahiki… Neno la Mungu ndiye Kristo Bwana aliye nuru ya ulimwengu, kwa njia yake sisi TU WANA WA NURU, kuishi nuruni kunaendana na kuishi na kutenda kadiri inavyowapasa wana wa Mwanga, matendo yetu yawe mazuri, bila kificho, ndio tabia ya mwanga. Tunaitwa pamoja na mitume Simoni Petro na Andrea nduguye, Yakobo wa Zebedayo na Yohane nduguye kuwa wavuvi wa watu, yaani kuwapelekea mwanga wa neno la Mungu wenzetu wote, popote, katika hali zote. Mitume wanamfuata bila kusita nasi tumuitikie mara, tujitoe bila kujibakiza kwa huduma ya neno na ya meza kwa mapendo kamili naye Kristo nuru yetu atatuangaza.

Juma la 59 la Kuombea Umoja wa Wakristo: Mwili Mmoja, Roho Moja, Tumaini..
Juma la 59 la Kuombea Umoja wa Wakristo: Mwili Mmoja, Roho Moja, Tumaini..   (@Vatican Media)

Katika Injili ya leo, Yesu anatangaza Ufalme wa Mungu kwa kuanza huduma yake Galilaya, akisema, “Tubuni, kwa maana Ufalme wa Mbinguni umekaribia.” Yesu anawaita wafuasi wake kuwa wavuvi wa watu, wakiwa tayari kusikiliza, kufuata, na kutangaza Neno la Mungu. Yesu anaita watu wa kawaida kuwa wafuasi wake, Petro na Andrea walikuwa wavuvi, lakini walikubali wito wa Yesu na waligeuka kuwa wafuasi wa Neno la Mungu. Hatutakiwi kuwa wajasiri au wakamilifu ili kupokea Neno la Mungu. Neno la Mungu linawaita watu wa kawaida, na linawawezesha kuwa vyombo vya mabadiliko. Neno la Mungu linatufundisha utume wa kuleta amani. Wafuasi wa Kristo, kama Petro na Andrea, walijua kwamba Neno la Mungu linahusisha utume wa kuleta amani. Kama wavuvi wa watu, tunaitwa kueneza Neno la amani, upendo na haki, kupitia matendo yetu ya kila siku. Katika dunia ya leo, giza linaendelea kutawala: Migogoro ya kijamii, Ukosefu wa haki, Hali ngumu ya kiuchumi, Watu wanaokata tamaa na kushindwa kuona mwelekeo wa maisha. Lakini Neno la Mungu linakuja kama mwanga unaoangaza kila giza. Kristo anasema leo, “Nimekuja ili mwanga uwepo duniani, ili kila anayeamini kuwa na nuru ya uzima.” (Yn 12:46) Tunapoendelea na mwaka huu mpya, tusikie wito wa Neno la Mungu. Neno la Mungu ni mwanga wa dunia yetu, na sisi ni vyombo vya mwanga huo. Tumeitwa,  Pokea Neno la Mungu katika maisha yako.  Jenga umoja na amani kupitia Neno la Mungu.  Weka haki mbele ya migawanyiko ya kijamii na kisiasa.  Tangaza matumaini kwa dunia inayohitaji mwanga wa Neno. Katika Dominika ya Neno la Mungu, tunapohudhuria ibada na kutafakari Neno lake, tunajua kuwa Neno la Mungu linatufanya kuwa watu wa umoja, haki na amani. Tunaalikwa kufuata Neno la Kristo, ambaye anasema: “Nifuateni, na nitawafanya wavuvi wa watu.” Utukufu na shukrani zetu ziende kwa Baba ambaye ametupa Neno lake kama mwanga wa maisha yetu. Amina.

Dominika ya Tatu ya Mwaka A
23 Januari 2026, 16:24