Leo ni Noeli ya Bwana, yaani  Sherehe ya kuzaliwa Bwana wetu Yesu Kristo.  Leo ni Noeli ya Bwana, yaani Sherehe ya kuzaliwa Bwana wetu Yesu Kristo.  

Tafakari Sherehe ya Noeli: Mwaka A wa Kanisa: Fumbo la Umwilisho!

Leo ni Noeli ya Bwana, chemchemi ya haki, amani, upendo na msamaha wa kweli. Noeli ni Sherehe ya kuzaliwa Bwana wetu Yesu Kristo. Liturujia ya Neno la Mungu katika Sherehe hii kubwa ya kuzaliwa Masiha inatutafakarisha juu ya, “FUMBO LA UMWILISHO” Tunatafakari juu ya upendo mkubwa wa Mungu ambaye aliupenda hivi ulimwengu hata akamtoa Mwanaye wa pekee ili kila mtu amwaminiye asipotee bali awe na uzima wa milele (Yn 3:16).

Na Padre Bonaventura Maro, C.PP.S., -Kolleg St. Josef, Salzburg, Austria.

Utangulizi: Wapendwa Taifa la Mungu, leo ni Sherehe ya kuzaliwa Bwana wetu Yesu Kristo.  Liturujia ya Neno la Mungu katika Sherehe hii kubwa ya kuzaliwa Masiha inatutafakarisha juu ya, “FUMBO LA UMWILISHO” Tunatafakari juu ya upendo mkubwa wa Mungu ambaye aliupenda hivi ulimwengu hata akamtoa Mwanaye wa pekee ili kila mtu amwaminiye asipotee bali awe na uzima wa milele (Yn 3:16). Kwa kumtuma kwetu Neno wake, ambaye anatwaa mwili na kukaa kati yetu, Mwenyezi Mungu anajifunua kwetu, na anaufunua na kuukamilisha mpango wake wa ukombozi si tu kwa taifa la Israeli bali kwa watu wa mataifa yote. Katika Sherehe hii ya kuzaliwa Bwana wetu Yesu Kristo, tumshukuru Mungu kwa kuwa daima ni mwaminifu kwa ahadi zake, ametimiza ahadi ukombozi wa watu wake. Tuombe nasi neema ya kumpokea kwa furaha Kristo, Neno wa Mungu anayezaliwa kwetu, tufungue mioyo yetu, tukubali aingie na akae ndani mwetu, Ufalme wake ukue na kuchanua ndani ya mioyo yetu na kupitia sisi, mwanga wa Injili uenee kwa watu wa mataifa yote. Somo la Kwanza: Ni kutoka katika Kitabu cha Nabii Isaya Isa 52:7-10. Somo la kwanza tulilolisikia kutoka katika kitabu cha Nabii Isaya ni utabiri wa Nabii Isaya juu ya ujio wa Masiya na matokeo makubwa ya ujio wake. Sehemu hii inatupa picha namna Mungu anavyotimiza ahadi yake kwa taifa lake, ahadi ambayo inatimia kwa kuzaliwa kwake Bwana wetu Yesu Kristo, Mungu anayeshuka, anatwaa mwili na kukaa katikati ya watu wake. Somo hili ni sehemu ya Kitabu cha pili cha Nabii Isaya (40-55) ambapo taifa la Israeli walikua utumwani Babiloni kwa muda mrefu. Wakiwa huko, waliteseka sana. Walikua mbali na hekalu, walikua mbali na Mungu, walipoteza kila kitu, maisha yakawa ya taabu na mateso. Wakajiuliza maswali, “Je, Mungu yupo tena na sisi hata huku ugenini? Je, miungu ya watu wa mataifa (Madruck) ina nguvu kuliko Mungu wetu? Kama Mungu yupo nasi kwa nini atuadhibu vikali namna hii? Kwa nini atuache tuaibike, tuteseke na kuumia namna hii? Wakakata tamaa, wakapoteza matumaini. Ni katika mazingira hayo, Nabii Isaya anawapa tena ujumbe wa matumaini na faraja kwamba, mateso na adhabu yao sasa itakoma, anawatangazia tena uhuru na ukombozi kwamba watarejea tena katika nchi yao kutoka utumwani. Anawakumbusha juu ya ukuu wa Mungu (God’s sovereignity) na mpango wake wa tangu kale wa kuwaletea ukombozi watu wake. Kwa hivyo somo hili laeleza furaha ya habari hiyo njema ya Mungu kwa watu wake inayokamilishwa kwa ujio wa Masiha.

Noeli ni Sherehe ya Fumbo la Umwilisho
Noeli ni Sherehe ya Fumbo la Umwilisho   (ANSA)

Ndugu zangu katika somo hili la kwanza tuna mafundisho matatu ya kujifunza. Kwanza: Mungu anawakumbuka watu wake walio utumwani (Divine faithfulness). Taifa la Israeli walikua utumwani Babeli kwa muda mrefu, takribani miaka 70. Ni kusema kwamba walikua utumwani na katika mateso kwa kipindi cha kutosha. Wakiwa utumwani wanajiuliza maswali mengi juu ya uwepo, nguvu na uweza wa Mungu katikati yao katika mateso na magumu wakiwa utumwani Babeli. Wanatishwa na nguvu za wababiloni na miungu yao lakini Nabii Isaya anawapa matumaini kwamba Mungu wao hajawasahau, Mungu wao anawakumbuka kwa kuwa amewaandika katika viganja vya mikono yake (Isaiah 49:15). Ndugu wapendwa, sherehe hii ya Noeli inatukumbusha kuwa Mungu anatukumbuka katika mahangaiko na taabu zetu. Kwa sababu ya dhambi, na changamoto mbalimbali tunazopitia katika safari yetu ya maisha, mara kadhaa tunakuwa mbali na Mungu, tunapoteza furaha, amani, Imani na matumaini. Katika nyakati hizi tunaweza kujiuliza maswali mengi kwamba, Je, Mungu bado yupo nami katika nyakati hizi ngumu ninazopitia? Je, Mungu ananiona? Ananisikia sala zangu? Je, Mungu hana nguvu, Mungu hana uwezo wa kunitoa katika mateso na mahangaiko ninayopitia? Tunaweza kupoteza Imani kwa Mungu na kushawishika kutafuta majibu ya maswali yetu sehemu nyingine. Ndugu wapendwa, tuwe na matumaini kwamba Mungu anatukumbuka na ujio wa mwanaye unaleta kwetu matumaini mapya ndani mwetu. Mungu amekuachora katika viganja vya mikono yake, hawezi kukusahau, hawezi kukuacha. Kristo mjumbe wa habari njema anasema na Moyo wako kama alivyosema na mioyo ya wana wa Israeli kwamba, “Mungu wako anamiliki “Mungu wako ana nguvu na uweza. Mungu anatukumbuka pia sisi tuliokuwa katika utumwa wa dhambi na mauti na anatuletea mkombozi anayetuweka tena huru. Kwa njia yake sisi sote tunapatanishwa tena na Mungu nasi tunakua huru kabisa.

Fumbo la Umwilisho linapata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka
Fumbo la Umwilisho linapata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka   (AFP or licensors)

 Pili: Kristo Yesu ni Mjumbe wa Habari Njema, nasi tunapaswa kuwa vyombo na wajumbe wa utume na uinjilishaji. Nabii Isaya anaimba utenzi huu wa sifa kwa Mungu kwa kuwa amemtuma mjumbe wa habari njema kwetu, ndiye Masiha, Bwana wetu Yesu Kristo. Ni habari za amani na wokovu. Mjumbe wa Habari Njema atauambia mji sayuni kwamba Mungu wako anamiliki. Utabiri huu unakamilishwa kwa ujio wa masiya Bwana wetu Yesu Kristo anaetuleta habari njema ya ukombozi. Ndugu wapendwa, Bwana wetu Yesu Kristo ametushirikisha kazi hii ya kuwa wajumbe wa habari njema ya wokovu kwa wengine kwa njia ya ubatizo. Kila mmoja ajiulieze miguu yangu inapeleka habari za furaha, matumaini, upatanisho, haki, amani, wema na huruma kwa watu wengine? Kuwa kwangu Mkristo Mkatoliki, kunaleta tofauti gani katika maisha ya kawaida kabisa ya watu wengine? Je, nimekua chanzo cha kupeleka habari njema au chanzo cha kusambaza habari mbaya, kusema mabaya ya wengine, kusengenya na kuwasemea vibaya wengine, kukatisha wengine tamaa, kutokutambua mazuri ya wengine, kueneza chuki na uchocheza kati ya watu? Tumwombe Yesu atusaidie, maneno na Matendo yetu visaidie katika kueneza habari njema ya Kristo aliyezaliwa katikati ya watu wake, tusambaze upendo, tusambaze furaha, tusambaze msamaha na huruma ya Mungu kwa watu wote. Tatu: Kristo ni chanzo cha ukombozi kwa mataifa yote. Nabii Isaya anatabiri kuwa ukombozi utawahusisha watu wa mataifa yote, kwamba Mwenyezi Mungu hamwachi hata mmoja nje ya mpango wake wa ukombozi. Ndugu wapendwa, ni mpango wa Mungu kwamba watu wote waokoke. Masiha anayezaliwa kwetu analeta ukombozi kwa watu wote. Lakini Mungu hatulazimishi katika kuupokea huo mpango wake wa ukombozi kwetu. Ametupatia kila neema tunayohitaji ili tunufaike na ukombozi utokao kwake. Kila mmoja wetu ajiulize, niliposikia tangazo la Habari Njema inayohubiriwa kwangu, nimekua tayari kuipokea? Ni mara ngapi nafanya jitihada katika kuwasaidia watu wengine kuikumbatia neema ya ukombozi tunayoshirikishwa na Mungu? Noeli hii ikawe chanzo cha mabadiliko ya kweli ndani mwangu. Pale ambapo nimekataa neema za Mungu zinazoletwa kwangu bure kabisa kwa njia ya Kanisa nianze upya ili niwe mmoja wa wanufaika wa mpango wa Mungu wa ukombozi.

Kristo Yesu ni Mwanga wa Mataifa
Kristo Yesu ni Mwanga wa Mataifa   (ANSA)

Somo la Injili: Ni Injili kama ilivyoandikwa na Yohane 1:1-18. Katika somo la Injili Takatifu kutoka katika Injili ya Yohane, tumesikia habari za Neno wa Mungu (Divine Logos), ndiye Bwana wetu Yesu Kristo aliyetwaa mwili akaa kati yetu. Ni Mungu kwa Neno Lake aliumba vitu vyote na neno hilo la uzima ndio mwanga wetu unaoondoa na kufukuza giza la dhambi ulimwenguni. Mungu ametwaa hali ya kibinadamu ili akae nasi na kutushirikisha tena uzima wa Kimungu. Kumbe Krismasi tunasherehekea sherehe ya Upendo wa Mungu aliyetwaa mwili na kukaa katikati ya watu wake ili kuwaletea ukombozi. Sehemu hii ya Injili ya Yohane huitwa dibaji (Prologue) ambayo inaweka mbele yetu dhima muhimu kuhusu utambulisho wa Yesu kama Neno (Logos), umwilisho wake, nafasi ya Yohane Mbatizaji kama mtangulizi wa Masiya na zawadi ya neema na ukweli kupitia Neno wa Mungu. Katika somo hili la Injili katika Sherehe ya Noeli Misa ya Mchana tuna mafundisho manne ya kujifunza. Kwanza: Kristo Neno wa Baba wa milele (Christ as Eternal Word). Dibaji hii ya Yohane inaanza na, “Hapo mwanzo kulikuwako Neno (Yn 1:1-3)” ikiturudisha nyuma kabisa katika kitabu cha mwanzo 1:1. Aya hii yatukumbusha kwamba Yesu alikuwako kwa Baba tangu milele yote, alikua pamoja na Mungu naye alikua Mungu. Na kwa njia yake huyo Neno vitu vyote vilifanyika. Neno huyu ndiye Bwana wetu Yesu Kristo.   Ndugu wapendwa, wakati Mwinjili Yohane anaandika Injili hii, kulikuwepo na wazushi wengi sana waliopinga kuhusu Umungu wa Kristo na ndio sababu Yohane anaandika kusisitiza juu ya kuwako Neno wa Mungu tangu kuumbwa kwa ulimwengu. Sisi mara kadhaa tunaweza kuwa na shaka juu ya uwepo wa Yesu katikati yetu. Kila mara tunakiri katika Imani yetu lakini tunakuwa tena wazito kuamini katika uwepo wake katika yetu. Wapo watu wengi wasioamini juu ya Ekaristi takatifu, uwepo halisi wa Yesu Neno wa Mungu katikati yetu. Tumwombe Yesu anayezaliwa kwetu leo atuongezee Imani ili tumkiri Yeye kama Mungu aliye daima katikati yetu.

Noeli: Neno wa Mungu amefanyika mwili
Noeli: Neno wa Mungu amefanyika mwili   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Pili: Yesu ni uzima na Mwanga wa Ulimwengu. Mwinjili Yohane anatuambia, “Ndani mwake ndimo ulimokuwa uzima” (Yn 1:4-5). Yesu ni chanzo cha uhai na uzima, uzima wa kiroho na uzima wa kimwili. Na anapokuja kati yetu anaondoa na kufukuza giza la dhambi nasi sote tunakuwa Watoto wa nuru. Ndugu wapendwa, Noeli hii itukumbushe kwamba chanzo cha uhai na uzima wetu ni Yesu. Yesu amejitoa kwetu kama chakula cha uzima ili tule tuupate uzima wa milele. Sisi tu wasafiri hapa duniani kuelekea makazi yetu ya kudumu mbinguni. Maisha yetu bila Yesu si kitu. Tukitembea peke yetu bila kuongozwa na Neno lake hatuwezi kuona njia, tutatembea daima gizani na hivyo kupoteza lengo la maisha yetu hapa duniani. Tusiposhibishwa kwa Neno lake na sakramenti zake, tutachoka katika safari yetu na kupoteza matumani. Yesu akatupe uzima mpya ndani mwetu, maisha yetu yakaongozwe naye daima. Tatu: Ushuhuda wa Yohane Mbatizaji, nami nimshuhudie Kristo kwa maisha yangu. Yohane mbatizaji katika dibaji hii anatambulishwa na mwinjili Yohane. Sote tunatambua kazi kubwa aliyoifanya Yohane Mbatizaji kama mtangulizi wa Masiha. Yeye alisema wazi kwamba si Masiha bali masiha yu aja ambaye yeye hastahili hata kulegeza Kamba za viatu vyake. Aliwaandaa watu ili kumpokea Masiya akihubiri juu ya ubatizo wa toba na maondoleo ya dhambi. Alimwandalia masiya njia. Ndugu wapendwa, krismasi itukumbushe tena kila siku kwamba tunapaswa kuwa mashuhuda wa masiya. Tunampomsikia katika Neno lake na kumpokea katika sakramenti tunatumwa kila siku kwenda kuwa mashuhuda wake kwa watu wote. Yesu atusaidie maisha yetu yawe Injili hai katika familia zetu, katika ndoa zetu, katika maeneo yetu ya kazi, katika jumuiya zetu. Tumtambulishe Kristo kwa watu wengine. Wapo ndugu zetu wengi ambao bado hawajamtambua Masiya au wengine wamekata tamaa na kurudi nyuma katika Imani. Krismas hii ikawe nafasi ya kila mmoja kumdhihirisha tena Kristo Yesu aliye daima katikati ya watu wake ili kuwaletea ukombozi wa milele.

Kristo Yesu ni ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu
Kristo Yesu ni ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

 Nne: Licha ya kwamba Kristo mwanga na nuru ya ulimwengu yu kati yetu, bado mara kadhaa tunarudi tena gizani (Yoh 1:9-13). Mwinjili Yohane anatuambia kwamba, “Yesu nuru halisi alikuwako ulimwenguni, hata kwa yeye ulimwengu ulipata kuwako wala ulimwengu haukumtambua” Licha ya kwamba alikuwa Mungu na kushiriki katika kazi ya uumbaji, bado ulimwengu haukumtambua. Ndugu wapendwa, tunaishi katika ulimwengu uliojaa mambo mengi ya giza, vita, visasi, utengano, ubaguzi, unyanyasaji, dhuluma, mmomonyoko mkubwa sana wa maadili, ni kwa sababu tumekataa wakati fulani kumpokea Yesu kama nuru. Tunaishi katika ulimwengu ambapo kila mmoja anataka kuwa huru, hata kama uhuru wenyewe upo kinyume na mapenzi ya Mungu. Tuanishi katika ulimwengu ambao kila mtu anataka vyeo na madaraka hata kwa kuutoa uhai wa watu wengine. tunaishi katika ulimwengu ambao familia nyingi zinatengana kwa sababu mbalimbali. Tumwombe Yesu atupe nguvu ya kuishi ndani ya mwanga wake, atubadilishe nasi tuwe wapya tena.

Kristo Yesu ni Mwanga wa Mataifa
Kristo Yesu ni Mwanga wa Mataifa   (Vatican Media)

Tano: Fumbo la Umwilisho, Ufunuo kamili wa Baba wa milele na kiini cha Sherehe ya Noeli (Yoh 1:14). Kiini cha sherehe ya Noeli ni Fumbo Takatifu sana la Umwilisho ambapo Mungu katika Nafsi ya Pili anatwaa mwili wa kibinadamu na kuingia katika historia ya mwanadamu, historia ya dhambi ili aigeuze iwe historia mpya ya wokovu. Anashiriki ubinadamu wetu ili atushirikishe Umungu wake. Kristo ni ufunuo wa Mungu, yeye na baba ni wamoja na hivyo aliyemwona Yesu, amemwona Baba. Ni utimilifu wa ufunuo wa Mungu kwa mwanadamu. Ujio wake umeleta kwetu neema juu ya neema (Yn 1:16-17) kwa kuanzisha nyakati mpya za neema ambayo inapita sheria. Ni neema bure iliyoshushwa kwetu bila kipimo kwa njia ya umwilisho wa mwana pekee wa Mungu. Ndugu wapendwa, sherehe hii kubwa ya Noeli itukumbushe nasi pia wajibu wetu wa kumwilishwa katika maisha ya watu wengine. Kristo aliacha enzi na utukufu mbinguni na akaja duniani, akaingia katika historia yetu ya dhambi ili atuletee uzima, ili atuinue tena na kutupeleka mbinguni. Hivyo nasi kila mmoja wetu awe tayati kuona na kuguswa na shida na matatizo ya wengine, kuwa tayari kuwapokea wengine licha ya udhaifu wao, kuwashirikisha wengine furaha kwa njia ya karama na vipaji vyetu mbalimbali kwa kadiri Mungu alivyotukirimia. Pia neema ya Mungu ambayo ni bure kabisa kwetu imeletwa kwetu kwa njia ya Yesu Kristo. Noeli ya mwaka huu ikawe chanzo cha neema zaidi ndani mwa kila mmoja wetu. Anapotushushia Yesu neema na baraka zake, nasi tukazisambaze neema na baraka hizo kwa wengine bila kujibakisha. Kwa kufanya hivyo nasi tutashiriki katika kumdhihirisha Mungu kwa watu wengine.

Noeli ni sherehe ya upendo, haki na mshikamano
Noeli ni sherehe ya upendo, haki na mshikamano   (Vatican Media)

Somo la pili ni kutoka katika Waraka kwa Waebrania 1:1-6. Somo la pili kutoka Waraka kwa Waebrania, linaeleza jinsi Mungu alivyojidhihirisha kwetu waziwazi kwa njia ya mwanaye Bwana wetu Yesu Kristo, Imanueli, Mungu pamoja nasi. Katika Agano la kale, Mungu alionekana kuwa mbali na watu wake, hakujidhihirisha waziwazi kwa watu wote bali alijidhihirisha kwa manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia nyingi. Mungu kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, sasa anasema nasi katika mwanaye mpendwa, anasema nasi mubashara kwa njia ya Kristo. Na hivyo ametufanya sisi sote kuwa warithi pamoja na Kristo ambaye kwa ujio wake hakuona haya kutuita sisi ndugu zake. Tunamshukuru Mungu kwa zawadi ya mwanaye Yesu Kristo na tumwombe akae nasi daima. Hitimisho: Katika Sherehe hii ya kuzaliwa Bwana wetu Yesu Kristo, tumshukuru Mungu kwa kuwa ni mwaminifu kwa ahadi zake, ametimiza ahadi ya kuuletea ulimwengu mkombozi wa milele. Tuombe neema ya kumpokea kwa furaha Kristo anayezaliwa kwetu, tukubali akae ndani mwetu, Ufalme wake ukue na kuchanua ndani ya mioyo yetu na kupitia sisi, watu wengine wengi nao waweze kuuona mwanga wa Kristo Yesu. 

 

24 Desemba 2025, 16:46