Tafakari Sherehe ya Noeli: Mwaliko wa Kutangaza na Kushuhudia Ukweli, Haki na Amani
Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.
UTANGULIZI: Karibu mpenzi msikilizaji na msomaji wa tafakari ya Neno la Mungu kutoka hapa Radio Vatican. Fumbo la Umwilisho ni kitovu na chemchemi ya furaha, amani, matumaini na mapendo yanayobubujika kutoka kwa Mwana wa Mungu aliyezaliwa mjini Bethlehemu ili kuvunjilia mbali nguvu za dhambi na mauti na hatimaye, kumrudishia tena mwanadamu utu na heshima yake, kwani ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Kristo Yesu anakuja kuwaletea waja wake amani na furaha ya kweli. Fumbo la Umwilisho ni tukio muhimu sana katika imani, tamaduni na sanaa ya Kikristo, kwani Neno wa Mungu amefanyika mwili na kuja kukaa kati ya waja wake. Noeli ni mwaliko wa kutangaza na kushuhudia amani, umoja, upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu na kwamba, hakuna mtu awaye yote anayeweza kutengwa na furaha ya ujio wa Mwana wa Baba wa milele. Leo ni furaha kuu mbinguni na duniani.. tunafurahi kwa sababu Mungu katika wema wake amewatazama watu wake kwa huruma, “… hakika nimeyaona mateso ya watu wangu walioko Misri, nami nimekisikia kilio chao kwa sababu ya wasimamizi wao, maana nayajua maumivu yao, nami nimeshuka ili niwaokoe na mikono ya Wamisri” (Kut 3:7 furaha yetu imetimia kwa sababu Mwana wa Mungu, Musa mpya na mkubwa zaidi, ameshuka katika mwili atuokoe na Misri kubwa zaidi.. dhambi na mauti. Nuru ya Yesu ni Nuru ya Haki, Nabii Isaya katika somo la kwanza anasema nira ya wanyonge itavunjwa, mzigo wa waliokandamizwa utaondolewa. Kwa hiyo, Noeli ni tangazo kwamba Mungu anapinga mifumo yote ya dhuluma: mifumo ya ufisadi, ubaguzi wa kikabila na kijinsia, ukosefu wa usawa wa kiuchumi, unyanyasaji wa watoto na wanawake, kukosekana kwa fursa za vijana. Yesu anazaliwa maskani ya wanyonge ili kutufundisha kuwa haki ya Mungu inaanzia katika mifereji midogo ya maisha ya watu rahisi.
Nuru ya Yesu ni Nuru ya Amani na Malaika waliimba: “Utukufu kwa Mungu juu mbinguni, na duniani amani kwa watu.” Amani si kutokuwepo kwa vita pekee; ni uwepo wa: heshima ya binadamu,kusikilizana, uwajibikaji, ukweli bila woga, msamaha wa kweli. Yesu anatualika kuwa wapatanishi, si wachochezi; wajenzi wa madaraja, si kuta; watu wa maneno ya upole, si hasira. Sherehe ya kuzaliwa Bwana Yesu yaani Noeli ya 2025 inaadhimishwa ndani ya muktadha muhimu wa Kanisa: Jubilei, yaani mwaka wa: neema, msamaha, kuanza upya, kuondoa mizigo ya kiuchumi, kijamii na kiroho. Katika Biblia, Jubilei ilikuwa wakati ambapo ardhi ilirudishwa, watumwa kuachiwa huru na madeni kufutwa. Katika mazingira ya leo yenye migogoro, ukosefu wa usawa, vita, umaskini, rushwa na ukosefu wa amani, Noeli inakuwa mwaliko wa kupokea Neno aliyefanyika mwili kama chemchemi ya ukombozi mpya. Noeli inakuwa ya kina tu pale tunapohama kutoka ibada za maneno kwenda maisha ya matendo. Tunapokaribia kuhitimsha mwaka 2025, tunaitwa Kuwa watenda haki na wapatanishi wa amani Katika dunia yenye vita na migawanyiko (kisiasa, kiukabila, kiuchumi), kuzaliwa kwa Mfalme wa Amani ni mwaliko wa, kusamehe, kuzungumza kwa hekima, kuondoa chuki na lugha za uchochezi, kujenga madaraja ya upendo. Kupigania hadhi ya kila mwanadamu. Kristo Yesu alipofanyika mwili, alithibitisha kwamba kila mwili una thamani, kupigania haki za watoto, wanawake, vijana wazee, wakimbizi, watu wenye ulemavu, kulinda maisha dhidi ya dhuluma, unyanyasaji, njaa, na mfumo usio sawa. Jubilei inataka madeni kupunguziwa watu, fursa za ajira zitengenezwe, mikataba ifanywe kwa uadilifu, na rasilimali za nchi zitumiwe kwa manufaa ya wengi na si wachache tu.
UFAFANUZI: Haki ya mazingira (ecological justice) Uumbaji mzima “unashangilia” katika Zaburi 96. Noeli inatuita: kulinda misitu na rasilimali zote amabazo nchi imejaliwa, mito na vyanzo vya maji, kupinga uchafuzi, kutumia nishati kwa uangalifu, kupinga ulaji kupita kiasi unaoharibu mazingira. Kwa nafasi hii tuwe na utulivu, tusikie mafundisho kutoka kiti kitakatifu, anayehubiri leo ni Wakili wa Kristo na Halifa wa Mtakatifu Petro, Mwalimu wetu Papa Leo XIV, anatufundisha akisema “…leo Mwokozi amezaliwa, tufurahi na kushangilia. Huzuni, mashaka na majonzi havina nafasi tunaposherehekea “birthday” ya uzima wetu, hofu ya kifo imemezwa na uzima unatupa furaha ya milele. Tufurahi kwa sababu hakuna anayebaki nyuma katika “surprise” hii ya wokovu wetu, wema na wafurahie ushindi huu, wakosefu na wafurahie msamaha na wapagani wapokee uzima. Tendo hili linaupa ubinadamu hadhi kubwa, kwa hiyo mkristo tambua cheo chako, usirudie dhambi, mkumbuke Kristo aliye kichwa chako na usisahau kuwa umeokolewa kutoka nguvu za giza na umeletwa katika nuru ya Bwana…” (sermon 1, Nativity 1-3). Mtoto Yesu ameupatia ubinadamu wetu hadhi kubwa, amekuwa mtu ili mtu awe mungu (Mt. Anselimo), amekuja ili afe na kwa kifo hicho sisi tuwe na uzima kisha tuwe nao tele (Yn 10:10), tutunze basi neema hii. Kristo Yesu amekuwa HAKI yetu, utakaso wetu, ukombozi wetu na hivi tumpe Mungu utukufu na sifa. UKWELI umechipuka katika nchi, Kristo (Njia, Ukweli na Uzima) amezaliwa na Bikira. HAKI imechungulia toka mbinguni sababu imani katika Mtoto wa Bethlehemu inatoka kwa Mungu juu. UKWELI umechipuka katika nchi, NENO amefanyika mwili. HAKI imechungulia toka mbinguni sababu zawadi zote zilizo kamili zatoka juu.
UKWELI umechipuka katika nchi, mwili na damu kutoka Bikira Maria. HAKI imechungulia toka mbinguni kwa vile mwanadamu hana kitu asipopokea toka mbinguni… Leo HAKI na AMANI vimekumbatiana na kubusiana katika Mtoto Yesu aliyezaliwa. Hakuwezi kuwa na AMANI duniani hadi UKWELI (KRISTO) uchipuke katika nchi, HAKI ichungulie toka mbinguni, Yesu (Mungu) anapotwaa mwili. Huyo ndiye amani yetu kusudi sisi nasi tupokee neema ya kufanyika wana wa Mungu, tuliofanywa kwa kifungo cha umoja na upendo.”Yesu ni Mwanga unaofukuza Hofu, Dunia ya sasa imejaa hofu: vijana wana hofu ya ajira, wazazi wana hofu ya usalama wa watoto wao, wazee wana hofu ya kutengwa, jamii inahofia mgawanyiko na vita. Lakini Injili inatuambia: “Msiogope.” Yesu anazaliwa ili hofu zetu zipate majibu. Kama alfajiri inavyofungua giza la usiku, Yesu anafungua njia mpya ya matumaini. Zaburi yasema: “Mwimbieni Bwana wimbo mpya.” Sio tu wimbo wa midomo, bali wa maisha, wimbo wa kutenda haki, wimbo wa kuwa waaminifu, wimbo wa kusamehe, wimbo wa kuwalinda wanyonge, wimbo wa kutumia vizuri mali ya umma na mali binafsi. Huu ndio wimbo wa mwanga. Tupokee kwa mapendo na shukrani zawadi hii ya Mtoto wa Bethlehem, anakuja atuletee ukweli, atupitishe katika haki na kutuinua katika cheo chetu halisi… letu ni moja tu, kumpokea kwa moyo wote na kutenda anayotutarajia tuyatende… kuvaa vizuri, chakula maalumu na sherehe viende bega kwa bega na hali mpya ya ndani ya moyo… huenda tunalaumu hatujanunuliwa nguo au viatu vipya vya sikukuu lakini hatujaungama Majilio hii, hatujasali.
Tumesali Novena ya Noeli, lakini bado tuna hali ya kinyongo, hasira na moyo wa kisasi, katika mazingira haya Noeli ni siku tu kama jana na juzi na majuzi.. tumuombe Mtoto Yesu atusaidie, nao Maria na Yosefu watuombee ili Noeli hii ikawe majira mapya, mbegu bora inayoota na kumea na kustawi na hatimaye kuzaa matunda mema.. Noeli isibaki kuwa tukio la siku moja bali iwe ni maisha yanayoongozwa na nuru ya Kristo Bwana na Mkombozi wetu aliyezaliwa leo, amina. Katika roho ya Jubilei, Sherehe hii tunaambia: Simama upya kama familia, acha chuki za zamani. Simama upya kama mtu binafsi, acha dhambi za kukuvunja moyo. Simama upya kama jamii, acha ubaguzi, chocheo cha chuki na maneno ya udhalilishaji. Yesu wa alfajiri anazaliwa ili kutangaza mwanzo mpya—kwetu na kwa jamii nzima. Leo, nuru ya Bethlehemu iingie nyumbani kwako, kazini kwako, moyoni mwako. Yesu azaliwe ndani yako ili uwe mwanga wa haki, mtetezi wa amani, na shuhuda wa upendo wa Mungu katika dunia yenye kiu ya nuru. Amani ya Kristo ijazwe ndani yenu katika usiku huu mtakatifu. Amina.