Tafakari Neno la Mungu Noeli Misa ya Mchana: Neno wa Mungu
Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.
Tafakari ya Neno la Mungu, masomo ya Misa ya mchana, katika Liturujia ya Sherehe ya kuzaliwa Bwana wetu Yesu Kristo, Imanueli, Mungu pamoja nasi, Mama Kanisa anatufundisha kwamba, Kristo Yesu amezaliwa mnyenyekevu zizini, katika familia maskini. Wachungaji wa kawaida ndiyo mashuhuda wa kwanza wa tukio hili kubwa. Katika umaskini huo, utukufu wa mbinguni ulionekana. Mama Kanisa hachoki kuimba utukufu wa usiku wa Noeli. Rej. KKK 525. Hii ni sherehe ya Fumbo la Umwilisho, Neno wa Mungu kutwaa mwili, kuwa mwanadamu na kukaa kwetu. Fumbo hili la umwilisho ni ishara wazi ya upendo wa Mungu wa kutaka kuturudishia sura na mfano wake aliotuumba nao, ulioharibiwa kwa dhambi na kutufanya tupoteze uhusiano mwema naye. Lakini kwa upendo na huruma yake, Mungu alianza mara moja mpango wa kuturudisha kwake na kutufanya upya watoto wake wapendwa kwa kuliteua taifa la Israeli ili kwalo, mataifa yote yapate kukombolewa kutoka utumwa wa dhambi na mauti. Na wakati ulipowadia, Mungu katika Nafsi yake ya pili, Mungu mwana alichukua ubinadmu wetu akakaa nasi ili kutufundisha namna tunavyopaswa kuhusiana na Mungu, katika Utatu Mtakatifu. Tukio la kuzaliwa kwake Yesu Kristo ni mwanzo wa kuanza kutimia kwa ahadi ya ukombozi wa mwanadamu ambao utimilifu wake ni katika fumbo la Pasaka. Ni katika muktadha huu maneno ya wimbo wa mwanzo yanasema; “Kwa ajili yetu mtoto amezaliwa, tumepewa mtoto mwanamume, na uweza wa kifalme utakuwa begani mwake, naye ataitwa jina lake Mshauri wa ajabu” (Isa.9:6). Na mama Kanisa katika sala ya mwanzo anasali hivi; “Ee Mungu, ulimweka mwanadamu katika cheo cha ajabu, na tena ukamtengeneza upya kwa namna ya ajabu zaidi. Tunakuomba utujalie kushiriki umungu wake, Yeye aliyekubali kushiriki ubinadamu wetu."
Katika somo la kwanza kutoka katika Kitabu cha Nabii Isaya (Isa. 52:7-10). Katika somo hili Mungu anaahidi kuwarudisha Waisraeli tena Yerusalemu kutoka utumwani Babeli. Utumwa wao ni mfano wa hali ya dhambi, na ukombozi wao ni mfano wa ukombozi wa mataifa yote kutoka dhambini. Waisraeli wanapewa ujumbe huu wakiwa wanateseka utumwani Babeli. Ni ujumbe wa matumaini kuwa amani imefika, vita sasa vimekwisha, utumwa umekwisha. Nabii Isaya anawaalika wafurahi akisema; “Pigeni kelele za furaha, imbeni pamoja, enyi mahali pa Yerusalemu palipokuwa ukiwa”, kwa sababu mda sasa umewadia wa Mungu kutimiza ahadi yake ya kuwakomboa na ncha zote za dunia zitauona wokovu wa Mungu. Ujumbe huu ni utabiri wa ukombozi wa binadamu wote kutoka utumwa wa dhambi ambao nasi tunafurahia kuupata kwa kusherehekea kuzaliwa kwake Yesu Kristo, Emanueli-Mungu pamoja nasi. Ni katika muktadha huu zaburi ya wimbo wa katikati inasema hivi; “Mwimbieni Bwana wimbo mpya, kwa maana ametenda mambo ya ajabu. Mkono wa kuume wake mwenyewe, mkono wake mtakatifu umemtendea wokovu. Bwana ameufunua wokovu wake, machoni pa mataifa amedhihirisha haki yake, amezikumbuka rehema zake, na uaminifu wake kwa nyumba ya Israeli. Miisho yote ya dunia imeuona Wokovu wa Mungu wetu. Mshangilieni Bwana, nchi yote, inueni sauti, imbeni kwa furaha, imbeni zaburi. Mwimbieni Bwana zaburi kwa kinubi, kwa kinubi na sauti za zaburi. Kwa panda na sauti ya baragumu, shangilieni mbele za Mfalme, Bwana” (Zab. 98: 1-6).
Somo la Pili ni kutoka katika Waraka kwa Waebrania (Ebr. 1:1-6). Somo hili linaweka wazi kuwa utabiri wa kale umetimia katika Yesu Kristo. Katika Yeye utukufu wa Mungu umefunuliwa na ni katika Yeye tu Mungu anaongea nasi katika nyakati zetu. Tunasoma hivi; “Mungu, ambaye alisema zamani na baba zetu katika manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia nyingi, mwisho wa siku hizi amesema na sisi katika Mwanaye, aliyemweka kuwa mrithi wa yote, tena kwa Yeye aliufanya ulimwengu…Yeye kwa kuwa ni mng’ao wa utukufu wake na chapa ya nafsi yake, akivichukua vyote kwa amri ya uweza wake, akiisha kufanya utakaso wa dhambi aliketi mkono wa kuume wa ukuu huko juu”. Mtoto Yesu ndiye chapa ya Mungu, nasi tunafurahia kuzaliwa kwake. Injili ni kama ilivyoandikwa na Yohane (Yn. 1:1-18). Sehemu hii ya Injili inaelezea kile alichokuwa Yesu kabla ya fumbo la umwilisho, yaani asili yake ya kuwa ni Mungu mwenyewe, naye ni Mungu kwa asili. Ni katika Yeye na kwa njia yake vitu vyote viliumbwa. Yeye ni Mwanga halisi naye aliyekuja kulishinda giza na kutujalia nuru, kutufanya tuuone Mwanga wa Mungu na kuufuata kikamilifu. Neema zote zimekuja kwa mkono wake, naye ndiye aliyemfunua Mungu kwetu. Yeye amekuja ili kwa njia yake tuweze kusamehewe dhambi zetu. Amekuja ili kutufuta machozi yetu. Amekuja ili kutusafisha mioyo yetu, kutununua toka utumwa wa shetani kwa gharama ya uhai wake. Yeye yupo nasi katika kila hali ya maisha yetu. Yeye ni Emanueli “Mungu pamoja nasi.”
Noeli ni Sherehe ya Fumbo la umwilisho, Mungu kuchukua mwili na hali ya kibinadamu. Kama Mungu amethamini utu wetu na kutwaa mwili kama sisi, nasi tunapaswa kujithamini na kuuthamini ubinadamu wetu na kuiheshimu miili yetu. Tusiudhalilishe ubinadamu wetu au kuwadhalilisha wengine. Mtu ana thamani, ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na Mungu amejiunga naye katika ubinadamu wake. Kwa hiyo, tuondoe yale yote yanayodhalilisha utu wa mwanadamu. Tuthamini miili yetu kwa kuitunza vizuri kwa heshima. Hivyo katika shamrashamra, nderemo na vifijo vya kumshangilia mkombozi aliyezaliwa, tusijiingize katika dhambi na kupoteza baraka na neema tulizojichotea katika kipindi cha majilio na hivyo kupoteza maana ya kusherekea Noeli. Huko ni kuikata Nuru na kuendelea kuishi katika giza kama anavyoonya Yohane katika Injili akisema: “Mwanga umekuja ulimwenguni, lakini watu wakapenda giza kuliko mwanga, kwani matendo yao ni maovu. Kila mtu atendaye maovu anachukia mwanga, wala haji kwenye mwanga, maana hapendi matendo yake maovu yamulikwe. Lakini mwenye kuuzingatia ukweli huja kwenye mwanga, ili matendo yake yaonekane yametendwa kwa kumtii Mungu” (Yn.3:19-21).
Tuipokee basi Nuru iliyokuja ulimwenguni, ituangazie tusiifanye Krismasi kuwa msimu wa kutenda maovu. Tukumbuke kwa majuma manne tulijiandaa kusherekea Noeli kwa kufanya toba na malipizi kwa dhambi zetu. Tusisahau maazimio tuliyoweka. Ni katika tumaini hili mama Kanisa katika sala ya kuombea dhabihu anasali hivi; “Ee Bwana, ikupendeze sadaka ya sikukuu hii ya leo. Sadaka hii ndiyo fidia kamilifu ya kutupatanisha nawe, na pia ibada timilifu ya kukutolea wewe, ee Mungu”. Na katika sala baada ya komunyo anatuombea akisali hivi; “Ee Mungu mwenye huruma, tunaomba huyo Mwokozi wa dunia aliyezaliwa akatufanye watoto wako, atujalie pia uzima wa milele”. Tumuenzi Masiha aliyezaliwa kwa kutenda mema na kuepuka nafasi za dhambi na Mungu atatujaza baraka na neema zake. Heri na baraka tele kwa sikukuu ya kuzaliwa Mwokozi wetu Yesu Kristo, Imanueli, Mungu pamoja nasi. Tumsifu Yesu Kristo!