Tafakari Neno la Mungu Mkesha wa Noeli: Yesu Ni Mwanga wa Mataifa
Na Padre Bonaventura Maro, C.PP.S., -Kolleg St. Josef, Salzburg, Austria.
Utangulizi: Wapendwa Taifa la Mungu, leo ni Sherehe ya kuzaliwa Bwana wetu Yesu Kristo. Ni siku ya furaha, ni usiku Mtakatifu wa kuzaliwa Bwana. Herini nyote kwa sherehe ya Noeli. Kadiri ya Mapokeo ya tangu zamani za kale Maadhimisho ya Fumbo la Umwilisho, yaani Noeli ya Bwana yanafanyika Usiku wa manane, ili kuwakumbusha waamini usiku ule mtakatifu utukufu wa Mungu ulipowang’aria wachungaji waliokuwa kondeni: “Na katika nchi ile ile walikuwako wachungaji wakikaa makondeni na kulinda kundi lao kwa zamu usiku. Malaika wa Bwana akawatokea ghafula, utukufu wa Bwana ukawang’aria pande zote, wakaingiwa na hofu kuu. Malaika akawaambia, Msiogope; kwa kuwa mimi ninawaletea habari njema ya furaha kuu itakayokuwa kwa watu wote; maana leo katika mji wa Daudi amezaliwa, kwa ajili yenu, Mwokozi, ndiye Kristo Bwana.” Lk 2: 8-11. Kama sehemu Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo yanayonogeshwa na kauli mbiu “Peregrinantes in spem” yaani: “Mahujaji wa Matumaini” na yanalenga pamoja na mambo mengine kuwahamasisha waamini kuishi kwa matumaini na hivyo kuendelea kuwa ni vyombo na mashuhuda wa fadhila ya matumaini inayokita mizizi yake katika imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Waamini wanahimizwa kujiandaa kuadhimisha Fumbo la Umwilisho kwa kumpokea Kristo Yesu anayezaliwa kwao kwa: Njia ya Neno la Mungu na Sakramenti za Kanisa katika Mkesha wa Sherehe ya Noeli, waamini kwa namna ya pekee wanampokea Kristo Yesu kama Kiini cha Injili ya Matumaini yasiyodanganya kamwe. Hii ni fursa ya kusikiliza, kutafakari na hatimaye, kumwilisha Neno la Mungu mintarafu uhalisia wa maisha na utume wa kila mwamini. Kitabu cha Orodha ya Majina ya Wafiadini wa Roma “Roman Martyrology” kinaonesha kwamba, Siku Nane Kabla ya Maadhimisho ya Mwaka Mpya Kadiri ya “Kalenda ya Januari” yaani tarehe 25 Desemba, Kristo Yesu anazaliwa na Bikira Maria kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Kwa hakika Kristo Yesu ni kitovu cha historia na Ulimwengu.
Liturujia ya Neno la Mungu katika Sherehe hii kubwa, usiku huu mtakatifu inatualika kufurahi na kushangilia kwa kuwa. “Mungu mwaminifu ametimiza ahadi yake kwa Taifa lake, ahadi ya kuwaletea ukombozi wa milele” Masiha aliyetabiriwa na manabii katika Agano la kale, anazaliwa katikati yetu, Immanuel yaani Mungu pamoja nasi. Mungu amewakumbuka watu wake, anawaletea amani, furaha, uhuru, anawaondolea hofu na mashaka, huzuni na utumwa wa giza la dhambi na kuwarejeshea matumaini mapya na mwanga wale wote waliokaa katika giza na na katika uvuli wa mauti. Ahadi hii ilikuwa kwa taifa la Israeli, lakini ni ahadi yetu sote ambao tulikua katika giza na katika utumwa wa dhambi. Tunafurahi kwa kuwa Mungu ametuleta Mkombozi ambaye kwa njia yake ulimwengu wote unapatanishwa tena na Mungu. Mungu wetu ni mwaminifu kwa ahadi zake kwetu, atatujibu wakati wake utakapowadia, kama ilivyokuwa kwa taifa la Israeli ambapo wakati utimilifu wa wakati ulipowadia, Mungu alitekeleza kile alichowaahidia (Gal 4:4-5.) Katika Sherehe hii ya kuzaliwa Bwana wetu Yesu Kristo, tumshukuru Mungu kwa kuwa ni mwaminifu kwa ahadi zake, ametimiza ahadi ya kuuletea ulimwengu mkombozi wa milele. Tuombe neema ya kumpokea kwa furaha Kristo anayezaliwa kwetu, tukubali akae ndani mwetu, Ufalme wake ukue na kuchanua ndani ya mioyo yetu na kupitia sisi, watu wengine wengi nao waweze kuuona mwanga wa Kristo.
Somo la Kwanza ni kutoka katika Kitabu cha Nabii Isaya Isa 9:2-7. Somo la kwanza tulilolisikia kutoka katika kitabu cha Nabii Isaya ni utabiri wa Nabii Isaya juu ya ujio wa Masiha na matokeo makubwa ya ujio wake. Sehemu hii inatupa picha namna Mungu anavyotimiza ahadi yake kwa taifa lake, ahadi ambayo inatimia kwa kuzaliwa kwake Bwana wetu Yesu Kristo, Mungu anayeshuka, anatwaa mwili na kukaa katikati ya watu wake. Sehemu hii ya utabiri wa Nabii isaya inaturudisha nyuma kutafakari kipindi ambacho taifa la Israeli walikua katika mashaka na hofu kubwa (katika karne ya 8 BCE). Ni wakati wa hofu na mashaka kutokana na hali ya kisiasa iliyojitokeza wakati huo ambapo taifa la Waashuru (Assyrians) walianza kukua na kutawala kama taifa kubwa na matokeo yake wakaanza kuvamia na kuwachuka mateka mataifa yaliyokua dhaifu ili kujiimarisha zaidi, kiuchumi na kijeshi. Hofu na mashaka ni kinyume cha Imani na ujasiri kwamba Mungu wa Israeli bado yupo nao na kwamba angewapigania. Taifa la Israeli wakapoteza kabisa matumaini na wakawa katika mkato mkubwa wa tamaa, wakawa katika giza na mashaka ya kuwa wanakwenda kuwa watumwa kwa Waashuru. Ni katika hali hiyo ya hofu, mashaka na mkato mkubwa wa tamaa, Nabii Isaya anawapa matumaini tena kwamba Mungu anakwenda kuwakomboa, Mungu anakwenda kuingilia kati hali hiyo ya hofu na mashaka na mkato wa tamaa, sio kwa nguvu za Mfalme wa kidunia bali ni kwa nguvu na uweza wa Kimungu, anakuja Masiya ambaye atawatoa katika giza, hofu na mashaka ya kuwa watumwa.
Ndugu zangu katika somo hili la kwanza tuna mafundisho manne ya kujifunza. Kwanza: Yesu, Mwanga wa mataifa “Watu waliokwenda katika giza wameona nuru kuu (Isa 9:2)” Ndugu wapedwa, giza katika aya hii ya pili lamaanisha dhambi, mateso, hofu, mashaka na hali ya kutengwa na kuwa mbali na Mungu. Taifa la Israeli kwa nyakati mbalimbali waliingia katika hofu, mateso, mashaka na mahangaiko makubwa kwa sababu walimkataa Mungu kama Mfalme wao. Waposhindwa kutii amri na maagizo ya Mungu, walipokosa uaminifu kwa Agano walilofanya na Mungu, Mungu aliwaadhibu kwa kuinua taifa kubwa kuliko wao na kuwachukua mateka utumwani. Hii ilikuwa ni kuwakumbusha kuwa maisha yao daima yalipaswa kuongozwa na Mungu kama Bwana na Mfalme wao na kwamba, kuwa mbali na Mungu ni chanzo cha mateso, hofu, utumwa na mashaka. Ndugu zangu, mara kadhaa tunajitenga na Mungu kwa sababu ya dhambi. Tunapokosa uaminifu kwa amri za Mungu, tunapokosa uaminifu katika maagano mbalimbali tuliyofanya na Mungu kila mmoja kadiri ya wito wake, tunakuwa katika hofu na mashaka, tunakuwa utumwani mwa shetani, tunakuwa wafungwa wa vilema mbalimbali vya dhambi. Tunapokuwa mbali hivi na Mungu, ni rahisi sana kutikiswa na hofu na mashaka tunayokutana nayo katika maisha yetu ya kila siku. Tunakosa ujasiri wa kutumaini nguvu na uweza wa Mungu kwa kuwa tumemwacha. Tusipopokea Sakramenti za kanisa, tusiposoma Neno la Mungu, tunafanya Yesu akae mbali nasi na hivyo katika nyakati ngumu za hofu na mashaka, katika majaribu mbalimbali tunayokutana nayo, tutakosa ujasiri wa kukabiliana nayo na hivyo kuangushwa kirahisi na majaribu tunayokutana nayo. Ndugu zangu, Kristo anayezaliwa katika yetu, yeye aliye nuru, yeye aliye mwanga wa mataifa akae daima ndani mwetu. Atusaidie daima kuikataa dhambi inayotufanya tuwe gizani na kwenye mashaka na hofu ili tuishi daima kama watoto wa Nuru, watoto wa Mungu tuliowekwa huru kwa njia ya Yesu Kristo.
Pili: Mungu ni mwaminifu kwa ahadi zake “Umeliongeza taifa, umezidisha furaha yao (Isa 9:3)” Taifa la Israeli walisubiri masiya, Mkombozi kwa muda mrefu. Manabii wengi walitabiri juu ya ujio wa Masiya ambaye angetoka katika ukoo wa Daudi. Baada ya kusubiri muda mrefu, Mungu akatimiza ahadi hiyo kwa kuzaliwa kwake Kristo Mkombozi wetu. Ahadi ya Mungu kwa Daudi kwamba, kutoka kwake atazaliwa Mfalme na Masiha inatimia kwa kuzaliwa kwake Kristo kupitia Bikira Maria kama ilivyotabiriwa takribani miaka 720 kabla ya kuzaliwa Kristo. Wapendwa taifa la Mungu, Mwenyezi Mungu daima ni mwaminifu kwa ahadi zake kwetu. Aliyoahidi kwetu atatenda kwa wakati wake licha ya kwamba wakati mwingine kwa kuchelewa, lakini atatimiza. Taifa la Israeli walisubiri ahadi ya Mungu ya kuwaletea Masiya kwa muda mrefu na Mungu ametimiza ahadi yake. Ni dhahiri kwamba hata sisi tunaposali na kumwomba Mungu kwa matumaini na saburi, atatimiza ahadi zake kwetu kwa wakati ambapo anaona inafaa kwa ajili ya wokovu wetu. Tusikate tamaa tuonapo ahadi za Mungu zinachelewa kutimilika kwetu. Tunaposherehekea Noeli, tumwombe Mungu atusaidie ili furaha iliyo ndani mwetu kwa kuzaliwa Masiya iwe ni furaha ya kudumu. Tusikubali tena hofu na mashaka vitutawale wakati yupo Mungu katikati yetu anayekwenda pamoja nasi, anayesafiri nasi katika hali zote na katika hatua zote za maisha yetu mpaka tutakapopata utimilifu wa furaha yetu kwa kukutana naye mbinguni.
Tatu: Masiha ni chanzo cha ukombozi kwa taifa la Mungu “Kwa maana umeivunja nira ya mzigo wake na gongo la bega lake na fimbo yake yeye aliyemwonea kama katika siku za Midiani (Isa 9:4-5) Nabii Isaya anawapa ujumbe wa faraja na matumaini taifa la Mungu kwamba Masiya atakomesha kila aina ya utumwa, unyanyasaji na uonevu na kwa mkono wake wenye nguvu ataingilia kati na kuwapa watu wake ushindi, atavunja nira yaani atawatoa kabisa katika utumwa na kukomesha utawala wa watesi wao. Anawakumbusha namna Mungu kwa mkono wake wenye nguvu alivyotenda makuu katikati ya watu wake katika nyakati za waamuzi chini ya Gideoni (Amu 7). Ndugu zangu, mara kadhaa tunapitia katika nyakati ngumu, nyakati za shida na mateso, nyakati za mkato mkubwa sana wa tamaa kwa sababu nyingi. Yaweza kuwa ni matatizo ya familia zetu, yaweza kuwa ni migogoro jumuiya zetu, zaweza kuwa shida za kiuchumi, yaweza kuwa magonjwa na misiba, yapo mambo mengi yanayotutia hofu na mashaka. Mwenyezi Mungu kamwe hatuachi, anaingilia katika na kusimama nakutupigania. Tunaalikwa kumshirikisha Mungu hizo changamoto, hofu, mashaka na kukata tamaa kwetu. Mwombe Mungu asimame nawe, mwombe Mungu aingilie kati na kukupa msaada. Yesu anayezaliwa na aliye daima katikati yetu akaingilie katika nyakati ngumu unazopitia katika maisha, akakomeshe yale yote yanayotufanya kuwa na hofu na mashaka na kutupelekea kupoteza matumaini na imani thabiti kwake.
Nne: Kwa ajili yetu mtoto amezaliwa, Mungu katikati ya watu wake. Mtoto anayetajwa katika utabiri huu wa Nabii Isaya ndiye Bwana wetu Yesu Kristo ambaye leo tunamsherehekea ulimwenguni kote. Ni masiya, Immanuel yaani Mungu katikati ya watu wake, ambaye utawala wake ni wa mbinguni, utawala wa milele, utawala wa haki. Mtoto huyu anapewa majina mengi ambayo yote yanaakisi asili yake na utume ambao alikuja kuufanya. Ataitwa mshauri wa ajabu, maana yake Yesu anawaongoza na kuwafariji watu wake, ataitwa Mungu mwenye nguvu, maana yake yeye ni Mungu, mwenye uwezo wa kuokoa na kutuweka huru kabisa, ataitwa Baba wa milele, jina hili laakisi mapendo yake ya kibaba, ulinzi na uwepo wake wa daima kati ya watu wake na mwisho anaitwa Mfalme wa amani, ikimaanisha kuwa ujio wake utaleta amani tena kati ya Mungu na watu wake. Ndugu wapendwa, tuna furaha kubwa kwa sababu ya zawadi ya Mungu ya kumtoa mwanaye wa pekee kwa ajili yetu sisi wanadamu. Tunaalikwa kumtambua kama Mshauri wa ajabu, anayetuongoza na kufariji na kututia nguvu kila tunaporudi nyuma na kuchoka katika kumfuasa. Tuaalikwa kumtambua kama Mungu mwenye nguvu ambaye yu juu ya vitu vyote, ndiye mwenye nguvu na uwezo wa kutupa sisi uhuru na uzima wa kweli. Tunaalikwa kumtambua kama Baba wa milele ambaye kwa mapendo yake ya kibaba na uwepo wake wa daima anatusaidia katika mahitaji yetu ya kiroho na kimwili na anatembea nasi daima katika safari yetu. Tumtambue kama Mfalme wa amani, tuwe kweli watu wa haki na amani, tuwe mabalozi wa upatanisho kwa wale wasio na amani lakini pia kukumbuka kujipatanisha sisi na Mungu.
Somo la Injili: Ni Injili ya Lk. 2:1-14. Katika somo la Injili Takatifu tumesikia habari za kuzaliwa Kristo Mkombozi na Mfalme wa ulimwengu aliyetabiriwa na Manabii. Mwinjili Luka anaelezea tukio hili kihistoria na kijiografia kuonesha kuwa kuzaliwa kwake Kristo sio habari za kutungwa bali ni tukio kweli lililotokea katika historia. Yesu alizaliwa katika mji wa Daudi, Bethlehemu ambapo wakati wa kuzaliwa kwake haukuwa tena mji mkubwa bali ilijulikana kama kijiji cha wakulima. Kuzaliwa kwa Kristo Yesu mjini Bethlehemu kunatimiza utabiri wa Manabii kwamba Masiha atazaliwa katika mji wa Daudi na atatoka katika ukoo wa Daudi. Katika somo hili la Injili dominika ya leo tuna mafundisho manne ya kujifunza. Kwanza: Kristo Yesu ni Masiha aliyetabiriwa na Manabii. Taifa la Israeli walimngojea Masiha kwa muda mrefu sana. Kama tulivyosikia katika kipindi chote cha majilio, Manabii mbalimbali wa Agano la kale walitabiri juu ya ujio wa Mkombozi, atakayewakombo watu kutoka katika utumwa wa dhambi na mauti. Yohane mbatizaji akiwaalika watu wote kuandaa ujio wa huyu masiya kwa kuitengeneza njia ya Bwana. Utabiri huu umetimia kwa kuzaliwa kwake Bwana wetu Yesu Kristo. Ahadi iliyosubiriwa kwa muda mrefu sasa imetimia na Mungu amekuja kukaa pamoja nasi, ndiye Imanueli ambaye leo tunamshangilia. Wapendwa taifa la Mungu, Mwenyezi Mungu daima ni mwaminifu kwa ahadi zake kwetu. Aliyoahidi kwetu atatenda kwa wakati wake licha ya kwamba wakati mwingine kwa kuchelewa, lakini atatimiza. Taifa la Israeli walisubiri ahadi ya Mungu ya kuwaletea Masiha kwa muda mrefu takribani miaka 720 na Mungu ametimiza ahadi yake. Ni dhahiri kwamba hata sisi tunaposali na kumwomba Mungu kwa matumaini na saburi, atatimiza ahadi zake kwetu kwa wakati ambapo anaona inafaa kwa ajili ya wokovu wetu. Tusikate tamaa tuonapo ahadi za Mungu zinachelewa kutimilika kwetu.
Pili: Kristo Yesu anayezaliwa kwetu ni Mkate wa Mbinguni atakayejisadaka kwa ajili ya uzima wetu. Yesu anazaliwa Bethlehemu ya uyahudi. Kutoka katika lugha ya Kiebrania, “Beth” maana yake ni nyumba na “Lehem” ni mkate. Kristo anazaliwa Bethlehemu ambapo kwa tafsiri yake ni “Nyumba ya Mkate”. Kristo anashuka kwetu kama mkate wa Mbinguni. Anajishusha na kuja kukaa kati yetu sisi. Anajitoa mwili wake na damu yake kama sadaka kwa ajili ya uzima wa ulimwengu mzima. Ni upendo mkubwa wa Mungu kujitoa kama sadaka kwa ajili ya sisi rafiki zake. Kuzaliwa kwake Kristo kutukumbushe na sisi kuishi maisha ya kiekaristia. Maisha ya shukrani daima kwa Mungu kwa zawadi ya Mwanaye Yesu Kristo aliyejitoa kwetu kama sadaka kwa ajili ya kutukomboa sisi. Anatualika kila siku kumpokea tukiwa na mioyo safi na kwa mastahili ili tufaidike na neema za uwepo wake ndani ya mioyo yetu. Kuzaliwa kwa Kristo kutukumbushe pia wajibu wetu wa kujitoa sadaka kwa ajili ya wengine. Kuwa tayari kujimega, kujivunja sisi wenyewe ili kuwanufaisha wengine. Kristo alikua tayari kujimega kwa ajili yetu sisi, tuombe neema ya Mungu ili nasi daima tuweze kujitoa sadaka kwa ajili ya uzima wa kimwili na kiroho wa Ndugu zetu.
Tatu: Kristo anazaliwa katika mazingira duni na anadhihirishwa kwa watu duni akitukumbusha kuwa wanyenyekevu. Yesu anazaliwa katika mji wa Bethlehemu katika hori ya kulishia wanyama. Anatufundisha jinsi Mungu alivyojishusha akaja akakaa kati yetu katika unyonge na udhaifu wetu ili atupatanishe sisi na Mungu na kutupatia zawadi na utajiri wa uzima wa milele. Kristo hakuzaliwa katika nyumba ya kifahari, hakuzaliwa katika kasri ya mfalme bali anazaliwa katika hali duni. Vile vile watu wa kwanza kupewa habari ya kuzaliwa kwake hawakua wafalme bali walikuwa ni wachungaji, watu ambao walidharauliwa na walionekana kama watu duni na wasiokuwa na thamani. Ndugu zangu, Kristo Yesu anazaliwa ili atutoe sote katika hali duni, hali iliyosababishwa na dhambi ya wazazi wetu wa kwanza. Kuzaliwa kwake kunaleta ukombozi kwa wale wote waliokuwa hawana thamani katika jamii, maskini, wajane, wakoma, viwete, yatima nk. Injili ya Kristo inakua chanzo cha furaha, haki, faraja, upendo, uponyaji na amani. Kristo kujidhihirishwa kwanza kwa wachungaji inatufundisha kuwa Mwenyezi Mungu anajidhihirisha kwanza kwa wale walio wanyenyekevu na wanyofu wa moyo. Masiya hakujidhihirisha kwanza kwa wafalme na watu maarufu bali alijidhihirisha kwa wachungaji na kuwaletea habari Njema, habari ya ukombozi kupitia ujumbe wa malaika. Tunapokubali kuwa wanyenyekevu, Mungu atajidhihirisha kwetu. Kristo Yesu alikosa nafasi katika nyumba za kulala wageni kule Bethlehemu, alikosa nafasi ya kuzaliwa katika mazingira mazuri. Hii yatukumbusha kuwa mara kadhaa tunaweza kumkosesha nafasi Kristo kuzaliwa katika maisha yangu. Katika kipindi cha Majilio tulialikwa kuandaa njia kwa ajili ya masiya ili apate nafasi ndani ya mioyo yetu. Ni wakati wa kuondoa mambo yote ndani ya mioyo yetu ambayo yanamkosesha nafasi Yesu ndani mwangu.
Nne: Msiogope, ninawaletea Habari Njema. Haya ni maneno ya malaika kwa wachungaji waliokuwa wakikaa makondeni na kulinda kundi lao kwa zamu ya usiku. Ni habari njema ya kuzaliwa Mtoto Yesu, mwokozi, Kristo Bwana. Ujio wake unaleta furaha, unaleta uhuru, unaleta msamaha, unaleta mwanga ulimwenguni, unaleta upatanisho kati ya Mungu na watu wake. Tunapaswa kufurahi kwa kuwa Mungu amewakumbuka watu wake. Ndugu mpendwa, tunaposherehekea sherehe hii kubwa ya Noeli ni wakati kila mmoja wetu kujiuliza, Kristo anayezaliwa leo analeta nini ndani mwangu? Je bado nipo na hofu na mashaka kwa sababu ya maisha? Je, nipo bado na chuki na visasi kati yangu mimi na majirani, mwenzangu wa ndoa, mwanajumuiya mwezangu, mfanyakazi mwenzangu nk? Yesu anatuletea leo habari njema, iingie ndani mwetu, pale nilipo na hofu na mashaka aniondolee mashaka, pale ninaposhindwa kusamehe anisaidie niweze kusamehe na kuachilia kama mimi nilivyosamehewa, pale ninaposumbuliwa na misukosuko ya maisha niwe tayari kuyakabidhi yote kwa Kristo na kumwomba atembee nami na anisaidie kuchukua msalaba wangu. Usiogope, Yesu anakuletea leo Habari njema.
Somo la Pili: Ni Waraka wa Mtume Paulo kwa Tito 2:11-14. Katika somo la pili Mtume Paulo anatuambia, Neema ya Mungu wetu inayowaokoa watu wote imefunuliwa. Ni zawadi ya bure kutoka kwa Mungu ambayo sisi hatukustahili lakini kwa kustahilishwa na Mungu tumeshikishwa neema hiyo kwa fumbo la umwilisho, maisha, mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo. Neema hii matokeo yake ndani mwetu ni kukataa ubaya na tamaa za kidunia ili itupate kuishi maisha ya fadhila yanayompendeza Mungu. Kristo Yesu aliyezaliwa kwetu anatupa neema ya kuwa Watoto wa nuru. Hatuko tena utumwani mwa dhambi, hatuko tena katika giza na uvuli w amauti. Hivyo tunamshukuru Mungu kwa zawadi ya Bwana wetu Yesu Kristo ambaye kwa njia yake sisi sote tumepokea tena neema ya kuwa Watoto wa Mungu na warithi wa ahadi za Mungu pamoja naye. Hitimisho: Katika Sherehe hii ya kuzaliwa Bwana wetu Yesu Kristo, tumshukuru Mungu kwa kuwa ni mwaminifu kwa ahadi zake, ametimiza ahadi ya kuuletea ulimwengu mkombozi wa milele. Tuombe neema ya kumpokea kwa furaha Kristo anayezaliwa kwetu, tukubali akae ndani mwetu, Ufalme wake ukue na kuchanua ndani ya mioyo yetu na kupitia sisi, watu wengine wengi nao waweze kuuona mwanga wa Kristo Yesu.