Tafakari Dominika ya Pili Majilio Mwaka A: Imani, Toba na Haki!
Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.
UTANGULIZI: Karibu mpenzi msikilizaji na msomaji wa tafakari ya neno la Mungu kutoka hapa radio Vatikani. Tunaendelea na safari ya Majilio, kipindi cha kujiandaa kwa ujio wa Mwokozi wetu, Yesu Kristo. Wiki iliyopita tulialikwa kuamka katika tumaini; leo tunakaribishwa kukua katika tumaini, tumaini linalobadilisha mioyo, jamii, na dunia. tukijiandaa kuadhimisha fumbo la umwilisho Neno wa Mungu anapotwaa mwili na kuwa kati yetu, Emmanuel! tumuabudu Mungu wetu, tumshukuru Mkombozi wetu na tumuombe aliye Mwenyezi. Mwaka huu, tunasali na kutafakari katika mwanga wa Jubilei ya Tumaini 2025, iliyoasisiwa na Mama Kanisa Mtakatifu, akitualika kuwa watu wa matumaini hai: si matumaini ya maneno, bali ya matendo. Leo, kupitia maneno ya Nabii Isaya, Mtume Paulo, na Yohana Mbatizaji, tunasikia wito wa kina: tumaini linahitaji mizizi (imani), shina (toba), na matunda (matendo ya haki na huruma). Nabii Isaya leo (11:1-10) anatabiri chipukizi kutoka shina la Yese (baba ya Daudi) maana yake Mkombozi atazaliwa kutoka ukoo wa Daudi, naye Roho wa Bwana atakuwa juu yake. Katika aya hizi tunafafanuliwa zawadi au mapaji 7 ya Roho Mtakatifu; 6 katika Biblia ya Kiebrania na 7 katika Septuaginta (LXX) na Vulgata ikiongezwa ‘roho ya elimu.’ Roho wa Bwana ni nguvu ya Mungu wanayopewa watu fulani waliochaguliwa kwa kazi maalumu mfano waamuzi, wafalme, manabii, makuhani... Roho wa Bwana ana makazi ya kudumu katika Masiya atakayezaliwa.
Nabii anaendelea kusema Masiha ataleta mapinduzi, atajenga jumuiya ya haki na amani, upendo, utulivu na uhuru na dunia itakuwa shwari kiasi kwamba hata simba watakula majani na watoto watacheza na nyoka, ajabu kabisa. Ni picha ya tumaini linalochipua katikati ya giza.Mti uliokatwa haujakufa, mizizi bado ina uhai. Hivyo ndivyo alivyo Mungu wetu: Mungu wa fursa mpya, Mungu wa matumaini mapya.Katika ulimwengu wa leo, uliogubikwa na vita, umasikini, majanga, na woga, Kanisa linaitwa kuwa huo chipukizi cha tumaini. Tumaini ni zawadi ya Mungu inayotuwezesha kuona uwezekano wa amani hata pale ambapo dunia inasema haiwezekani. Tumaini hili linajikita katika Kristo, Yule anayekuja na roho ya hekima, uelewa, nguvu, na haki. Ni ufalme wa amani ambapo hata mbwa mwitu na mwana-kondoo wanaishi pamoja. Je, tunaweza kuamini kuwa dunia ya namna hii bado inawezekana? Ndiyo, ikiwa tunamruhusu Kristo kuanza utawala wake mioyoni mwetu. “Yote yaliyoandikwa zamani yaliandikwa kwa mafundisho yetu, ili tupate tumaini kwa faraja ya Maandiko.” Mtume Paulo anatukumbusha kwamba Neno la Mungu ni chemchemi ya tumaini. Anatuita kuwa na moyo wa uvumilivu na wa umoja “mpokee kila mmoja kama Kristo alivyowapokea.” Tumaini la Kikristo halina mipaka.Si la kundi moja tu, bali ni kwa wote, Wayahudina Mataifa, tajiri na maskini, vijana na wazee. Kwa hiyo, tumaini la Injili ni tumaini linalounga, si linalogawa.
UFAFANUZI: Katika Injili (Mt 3:1-12) tunamwona Yohane Mbatizaji aliye mtangazaji wa pambazuko la somo la la kwanza. Anajitambua kuwa ni mtangulizi wa Kristo hivi anatimiza wajibu wake huo kwa kutoa hamasa kuwa ufalme wa Mungu umekaribia na kwamba Masiya yupo karibu, tena amekwisha kufika hivi ‘tuitengeneze njia ya Bwana na kuyanyoosha mapito yake. Yohana Mbatizaji anaonekana jangwani, mahali pakavu, penye upweke. Lakini hapo ndipo sauti ya Mungu inasikika kwa nguvu.Ni sauti ya toba, sauti ya maandalizi, sauti ya ujasiri. Anasema: “Leteni matunda yanayostahili toba.” Hii inatukumbusha kwamba tumaini la kweli haliwezi kukua kwenye udongo wa dhambi. Kabla chipukizi jipya halijachipuka, lazima udongo utengenezwe. Baba Mtakatifu Leo XIV anaonya: “Kanisa lisipige tu mbiu ya tumaini, bali liwe tumaini lenyewe kwa dunia, kwa matendo, kwa huruma, kwa haki ni hivi ndio jamii yeyote ya wanadamu inapaswa kuwa.” Hivyo, Yohana Mbatizaji anatufundisha kuwa toba ndiyo njia ya kweli ya tumaini. Tumaini halijengwi juu ya udanganyifu, bali juu ya ukweli na uadilifu. Tunapohimizwa kuandaa njia tunao mfano hai wa mtu mwenye maandalizi ya ukweli, ndiye Yohane Mbatizaji. Yeye alibatiza kwa kufuata taratibu za Agano la Kale, ubatizo wake ulikuwa wa toba na maondoleo ya dhambi (Mk 1:4) kama maandalizi ya ubatizo mkubwa zaidi wa Kristo (Lk 3:16) aliyebatiza kwa Roho Mt. na moto, ubatizo halisi. Yohane ni nabii wa ajabu asiye na makuu, mtu mnyenyekevu (rej. mavazi, chakula, mahali pake pa kuishi, mafundisho yake bila woga.. hakunywa kileo wala chakula kizuri wakasema ana pepo, Yesu alikula na kunywa akaitwa mlevi na mlafi: kweli binadamu hana jema.)
Yohane Mbatizaji hakutenda miujiza lakini amesifiwa na Kristo Yesu kuwa mkuu kuliko wote (Yn 10:41). Unyenyekevu wake ni fundisho kwetu, kujishusha kadiri ya vipaji na udhaifu tulio nao. Huenda tunadharauliana na kuwaona wengine si kitu, wengi tunajipa madaraka tusiyonayo au tunahangaika kufanya mambo yanayoshinda uwezo wetu… tujinyenyekeze kama Yohane tukijiweka mikononi mwa Mungu na kutegemea huruma yake, mazuri tunayofanya yawe ni kwa faida ya wote, sifa na utukufu kwa Mungu Baba. Katika dunia ya leo,Watu wengi wamepoteza matumaini kwa sababu ya vita, njaa, na ukosefu wa ajira. Familia nyingi zimevunjika moyo kwa magonjwa, migogoro, au ukosefu wa upendo. Vijana wengi wamekata tamaa kwa sababu hawana nafasi ya kesho bora. Katika hali hii, Kanisa linaitwa kuwa “chemchemi ya tumaini.” Tumaini si ndoto ya woga, bali ni chaguo la upendo. Ni kuamua kuamini kwamba Mungu bado anatenda kazi duniani.” Hiki ni kipindi cha ‘Majilio’, tujiandae vema Mwokozi azaliwe pazuri.. tujiandae kiroho kwa kuungama, kusoma na kutafakari Neno la Mungu katika semina, mafungo na vipindi vya dini. Sanjari na hilo, kutengeneza njia kwa ajili ya Masiya ni kuwatengenezea mazingira watu wake kwa sababu Kristo anaonekana katika wagonjwa, yatima, masikini, na walemavu wa viungo na wa akili watu wenye kipato duni nk... wapo katika jumuiya zetu na jamii zetu, tuitengeneze njia ya Bwana kwa kuwashughulikia watu aina hii. Maandalizi ya Noeli yawe ni shule kwa maisha yetu.
Tujifunze kuwa watu wa kujiandaa kimawazo na kisaikolojia kabla ya kusema au kutenda lolote, maana yake: tujiandae kwa kuwaza vizuri kabla ya kutenda, ukitenda kwa vionjo tu bila kutafakari athari za halafu basi utakuwa mtu wa kuudhi na kuumiza wenzio kila siku. Mfano tafakari kabla hujapeleka maneno popote kuwa athari yake itakuwa nini.. changamoto za wenzio unazitatuaje, kwa busara au la? tutengeneze njia ya Bwana kwa kufikiri kabla ya chochote. Kama tunavyojiandaa katika shughuli nyingine ikawe hivyo katika kumpokea Masiya. Mfano katika Familia au jamii nyingi duniani inapopata habari kuwa wakwe wanakuja labda kuleta posa au mahari basi hukosa raha na pengine kuingia madeni ili wageni wao wajisikie nyumbani, ni kawaida kwetu waafrika n. Wanafunzi makini hujiandaa vizuri kabla ya mtihani na tarehe inapofika huwa na amani na kufanya vizuri. Mapadre huandaliwa miaka mingi ili wabobee vema, matabibu kadhalika, ingekuwa heri leo wanandoa wangejiandaa na kuandaliwa vema.. walimu pia hupaswa kuandaa vipindi vyao, wanafunzi hung’amua mwanzoni tu mwa kipindi kuwa leo mwalimu hajajiandaa na kumpuuza.. Mama ajiandae kumpokea baba anaporudi kazini kwa chakula, mapokezi na maneno mazuri ya pole na pongezi ya kazi.. Akina baba tujiandae vema kwa maisha yetu kwa elimu, kazi, mahitaji na makuzi ya watoto na urembo wa wake zetu ili wabaki na uzuri wao, tusipoandaa hayo sasa tukumbuke wasemavyo waswahili ‘fainali ni ...” Ee Mungu wa haki na amani, tunaomba utupe roho ya toba na tumaini. Tufanye kama chipukizi jipya, tukue katika upendo wako na tufanye ulimwengu huu uwe bustani ya amani. Katika mwaka huu wa Jubilei ya Tumaini, tufanye kuwa vyombo vya faraja na upatanisho, ili dunia yote ifahamu kuwa Kristo ndiye Tumaini letu la kweli. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.