Familia ni Kanisa dogo la nyumbani; ni shule ya tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu, kimaadili na kijamii. Familia ni Kanisa dogo la nyumbani; ni shule ya tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu, kimaadili na kijamii.   (@Vatican Media)

Sikukuu ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu: Kielelezo cha Familia Zote za Kikristo

Ni Familia Takatifu kwa sababu iliishi maisha Matakatifu, waliziishi fadhila zote za Kimungu, wakishiriki kikamilifu katika malezi na makuzi ya Bwana wetu Yesu Kristo. Hivyo Familia takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu ni “kielelezo cha Familia zote za Kikristo.” Inatufundisha kuwa familia bora ni msingi wa kanisa na taifa imara la Mungu na kitalu cha fadhila zote za Kimungu. Tumshukuru Mungu kwa zawadi ya Familia hii Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu inayotupa mfano bora!

Na Padre Bonaventura Maro, C.PP.S., -Kolleg St. Josef, Salzburg, Austria.

Utangulizi: Wapendwa Taifa la Mungu, leo ni Sikukuu ya FAMILIA TAKATIFU ya Yesu, Maria na Yosefu. Familia ni Kanisa dogo la nyumbani; ni shule ya tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu, kimaadili na kijamii. Familia ni tabernakulo ya Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; ni mahali pa kufundana umuhimu wa kumwilisha: huduma, upendo, ukarimu, msamaha na kuvumiliana. Hapa ni madhabahu ya sala, ibada, na tafakari ya Neno la Mungu; mambo msingi yanayowawezesha wanafamilia kujivika upendo, busara, rehema, utu wema, upole na unyenyekevu. Tupo bado katika Oktava ya Noeli tukisherehekea zawadi ya Upendo wa Mungu kuutwaa mwili na kukaa katika familia, katikati yetu ili kutuletea ukombozi. Ni Familia Takatifu kwa sababu iliishi maisha Matakatifu, waliziishi fadhila zote za Kimungu, wakishiriki kikamilifu katika malezi na makuzi ya Bwana wetu Yesu Kristo. Hivyo Familia takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu ni “kielelezo cha Familia zote za Kikristo.” Inatufundisha kuwa familia bora ni msingi wa kanisa na taifa imara la Mungu na kitalu cha fadhila zote za Kimungu. Katika Sikukuu hii ya Familia, tumshukuru Mungu kwa zawadi ya Familia hii Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu inayotupa mfano wa namna tunapaswa kuziishi fadhila za Kimungu katika familia zetu. Tuziombee familia zote ziishi kwa amani na upendo, kwa furaha na ushirikiano ili humo litoke kanisa na taifa imara la Mungu. Tuiombee pia dunia nzima ambayo sasa imegubikwa na mambo mengi ambayo yanaua msingi wa Familia kadiri ya mpango wa Mungu. Tuziombee pia familia zote zilizotawanyika, familia zisizo na amani na maelewano ili kwa ulinzi na usimamizi wa Familia Takatifu waishi kwa amani, furaha, Upendo na Mshikamano.  Tujiombee na sisi sote ili kila mmoja atekeleze kwa uaminifu wajibu wake katika familia, kanisa na taifa ili sote tupate tuzo ya Utakatifu kama ilivyokuwa familia Takatifu.

Watoto ni zawadi kutoka kwa Mungu
Watoto ni zawadi kutoka kwa Mungu   (@Vatican Media)

Chimbuko la Sikukuu ya Familia Takatifu. Kiini na mwanzo wa Sikukuu hii ya familia Takatifu ni kunako mwaka 1921 ambapo Baba Mtakatifu Benedikto wa XV alitangaza kuwa, Jumapili katika Octava ya Noeli au tarehe 30 Disemba itakua ni Sikukuu ya Familia Takatifu. Mtakatifu Yohane Paulo wa pili katika kusherehekea Sherehe ya Bwana wetu Yesu Kristo Mfalme mwaka 1981, katika barua yake ya kitume “Familiaris Consortio” alieleza wajibu wa familia ya Kikristo kwa Kanisa la Ulimwengu akisisitiza umuhimu wa familia katika malezi ya watoto na ujenzi wa Kanisa na Taifa. Alisema, “Familia ni kitalu cha kanisa na taifa kwa ujumla”. Ili jamii na kanisa lifanikiwe ni lazima kuwe na msingi mzuri katika familia ambayo ndiyo inaathiri tabia, mwenendo na maisha ya jamii kwa ujumla. Hivyo familia ni kanisa la nyumbani, ni shule ya upendo, shule ya amani, shule ya utu, shule ya mshikamano na tunu zote Njema za Kikristo. Katika Hitimisho la Barua yake, Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa II aliziweka familia zote chini ya ulinzi wa na usimamizi wa Yesu, Maria na Yosefu. Lengo kuu la kuiadhimisha sikukuu hii ni kuombea familia zote zikue na kuishi kwa mshikamano zikimpendeza Mungu na zikidumu katika pendo lake, ziweze kujaa amani tele na Baraka za Mwenyezi Mungu.

Familia ni Kanisa Dogo la Nyumbani
Familia ni Kanisa Dogo la Nyumbani   (@Vatican Media)

Somo la Kwanza: Ni kutoka Katika Kitabu cha Ybs 3:2-6, 12-14. Katika tamaduni za kiyahudi, Familia ilikua ni taasisi muhimu sana si tu kijamii bali kiuchumi, kidini, kimaadili na kiimani. Kijamii, familia ilijumuisha si tu Baba na Mama na watoto, bali pia ndugu na jamaa, pamoja watumishi wote waliokuwemo nyumbani. Kidini, kiimani na kimaadili, familia ilikua ni shule ya Imani na maadili, ambapo Torati, desturi muhimu zilizohusu historia ya ukombozi wao na maadili vilifundishwa, kutoka kwa wazazi kwenda wa watoto (Deut 6:6-9). Hivyo Imani haikuhifadhiwa tu hekaluni, bali ilifundishwa nyumbani. Kiuchumi, kazi na majukumu yaligawanywa kulingana na umri na watoto walifundishwa majukumu mbalimbali. Lakini baadaye kuanzia karne ya 4 BC, ulianza kuenea utamaduni mpya wa kigiriki ambao uliathiri sana mamlaka ya wazazi. Kulitokea mfumo mpya wa elimu, uliohamisha elimu na malezi kutoka nyumbani kwenda shuleni yaani gymnasium, uliosisitiza kutafuta maarifa na busara za kidunia kuliko utiifu kwa Torati, ikapelekea kudhoofisha nafasi ya wazazi kama walimu wa kwanza wa maadili na Imani.  Falsafa ya Kiyunani ilisisitiza ubinafsi, kujitegemea na kutafuta heshima, lakini katika Israeli utambulisho wa mtu ulikua ni wa kijamii na Agano na si wa mtu binafsi. Ilisisitiza kupuuzwa kwa wazee na wategemezi, na hivyo wazee wakaonekana kama mzigo na si tena hazina ya hekima. Yoshua bin Sira anaandika kitabu hiki kuwakumbusha kurejelea tena misingi ya torati waliyokuwa wameipoteza. Wajibu wa wazazi, wajibu wa watoto na matokeo ya kuiishi kiaminifu Torati.

Wazazi wanawajibika katika malezi na makuzi ya watoto wao
Wazazi wanawajibika katika malezi na makuzi ya watoto wao   (@Vatican Media)

Ndugu zangu katika somo hili la kwanza tuna mafundisho manne ya kujifunza. Kwanza: Muundo wa familia una msingi wa kimungu (Family structure as divinely instituted). Katika somo la kwanza, mwandishi anatuonesha kuwa muundo wa familia una msingi wa kimungu, ambapo baba na mama wanapewa mamlaka na Mwenyezi Mungu mwenyewe juu ya Watoto wao anaposema, “Bwana amempa Baba utukufu mintarafu wana na kuithibitisha haki ya Mama mintarafu Watoto (Ybs 3:2). Kumbe wazazi wana mamlaka makubwa juu Watoto wao na ni kutoka kwa Mungu mwenyewe. Wapendwa sana wazazi, ninyi mmepewa mamlaka (Authority) juu ya watoto ambao Mungu amewapa kama zawadi. Lengo ni kuwasaidia waweze kukua katika fadhila za kimungu, wampende Mungu, wawapende na kuwaheshimu watu wote, wakue katika fadhila za kimungu na za kiutu, wafahamu wajibu wao kwenu ninyi wazazi, wajibu wao kwa Mungu, wajibu wao kwa kanisa, na wajibu wako kwa jamii ambapo wanaishi. Kila mzazi ajiulize, nina mamlaka juu ya Watoto wangu? Tuna mamlaka juu ya Watoto wetu?  Ni ajabu kwamba siku hizi imekua kinyume chake, kwamba watoto ndio wana mamlaka juu ya wazazi wao, tumewakuza katika mfumo ambao wao ndio wanapanga kila kitu na sio sisi tena. Tunakua na hofu hata ya kuwaadhibu watoto wetu kwamba watatuchukia, watatuona wabaya na hatuna mapendo ya kweli, watatuona katili na wenye roho mbaya. Matokeo yake watoto wanakua na nguvu kuliko sisi na hatuna uwezo tena wa kuwakemea na pindi wanapokuja kuwa watu wazima tunasema, wakaharibika na kupotoka tunaishia kusema “Watoto wametushinda tabia” Nawasihi wazazi, tumieni mamlaka yenu mliyopewa na Mungu katika kuwalea watoto wenu. Si mamlaka ya kutumia nguvu na mabavu bali kuwajibika kwa upendo, kwa kujali na kuwa na huruma.

Watoto wafundishwe imani, maadili na utu wema
Watoto wafundishwe imani, maadili na utu wema   (@Vatican Media)

Pili: Kuna thawabu kwa anayewaheshimu wazazi wake (Honoring parents as atonement and treasure). Mwandishi Yoshua bin Sira anatuambia kuwa, “Anayemheshimu baba yake atafanya malipizi ya dhambi, naye anayemtukuza mama yake huweka akiba iliyo azizi” (Ybs 3:3-4). Kuheshimu baba na mama kunaonekana kuwa ni tendo la haki na lenye thamani na thawabu kubwa. Kumbe kuwaheshimu wazazi sio tut endo la kijamii bali lina maana kubwa sana pia kiroho. Ndugu zangu wapendwa, kila mmoja wetu hapa amezaliwa na wazazi, wengine wapo hai, wengine walikwishatangulia mbele za haki. Kila mmoja ajiulize leo katika maisha yake alishawahi kufanya nini kwa ajili ya wazazi wake? Je, nimewapenda? Nimewaheshimu? Nimewasadia wakati wote walipokuwa hai? Ninawasidia hata sasa wakati bado wanaishi? Ninawasikiliza wazazi wangu au ndo sikio la kufa? Leo tunakumbushwa kuwa wazazi wana thamani kubwa, na kwamba kuwaheshimu ni chanzo cha baraka kwetu. Usisubiri mpaka usikie baba na au mama amelazwa hospitali ndio uanze kuhangaika kumhudumia. Msaidie mzazi wakati bado akiwa na nguvu. Kama kuna yeyote ana tofauti yoyote na mzazi wake, leo rudi haraka ukamalize tofauti yako na mzazi. Mzazi anaweza kushikilia baraka yako maana ni agizo kutoka kwa Mungu kwamba tukiwasaidia tunapata baraka na kinyume chake pia ni sawa, kwamba tusipowasadia na kuwaheshimu tunajitafutia laana. Tafakari na uchukue hatua haraka.

Familia ni Tabernakulo ya Neno la Mungu
Familia ni Tabernakulo ya Neno la Mungu   (@Vatican Media)

Tatu: Familia ni shule ya imani, maadili na tamaduni njema. Katika tamaduni za kiyahudi, familia ilikua ni taasisi muhimu kama nilivyotangulia kusema hapo mwanzo. Humo watoto walifundishwa torati, waifahamu kwa moyo na kuiishi kiaminifu. Walifundishwa kuwa utambulisho wao upo katika familia, na uaminifu katika Imani na Agano kwa Mungu. Ndugu mpendwa, familia ni shule ya Imani. Ndipo sehemu ya kwanza ambao mtoto anajifunza Imani kutoka kwa wazazi na kukuzwa katika misingi ya Imani hiyo. Sikukuu hii ya Familia Takatifu itukumbushe wajibu wetu wa kuwalea na kuwakuza Watoto katika misingi ya Imani na maadili. Kimsingi mambo haya wanajifunza kwa mara ya kwanza kutoka kwa wazazi wao. Kama wazazi wamesimama imara katika Imani, katika maadili, ni wazi kabisa Watoto watatembea katika njia hiyo hiyo ikiwa watarithishwa tunu hizo njema katika familia. Mara kadhaa tunafikiri tunawaonea huruma Watoto wetu, tunaona kama tutawachosha, tunapotakiwa kuwakumbusha nyajibu zao. Mara kadhaa tunakwenda kusali, katika jumuiya au Ibada ya misa na kuwaacha Watoto wamelala ndani, tunawaacha wapumzike, wamechoka na Masomo magumu. Matokeo yake, tunatengeza waregevu dini wa kutosha mapema kabisa katika familia zetu kwa mikono yetu sisi wenyewe. Ewe mzazi unayemdekeza mtoto katika mambo ya msingi, amka sasa, Yoshua bin sira ana jambo lake nawe. Watoto katika familia wanafundishwa kazi na majukumu mbalimbali yanayowapasa. Wafundishwe kazi za mikono, kufua, kusafisha mazingira, kulima, kupika, usafi binafsi nk. waelekezwe mambo mbalimbali ya kijamii, wafundishwe heshima na utu, wafundishwe uwajibikaji katika ukweli. Mara kadhaa wazazi tumekua wazito katika mambo ya Imani na maadili, hatusali, hatuhudhurii kanisani, hatuwafundishi na kuonesha kwa mfano kujali, uadilifu na utu, ukweli na uwazi, uwajibikaji na tunawajumuisha Watoto katika migogoro yetu ambayo inawaachia majeraha na picha mbaya. Watoto wanaiga tunu mbaya badala ya maadili na tamaduni njema. Je, familia yangu ni shule ya Imani na maadili?

Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu ni mfano bora wa kuigwa
Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu ni mfano bora wa kuigwa   (@Vatican Media)

Tatu: Athari za mifumo ya kisasa katika Familia zetu. Yoshua bin Sira anaandika kitabu hiki kama jibu kwa athari mbambali zilizokumba mfumo wa familia kadiri ya Tamaduni za Kiyahudi, ulioathiriwa na tamaduni mpya za kigeni za kigiriki au kiyunani. Alisisitiza kurudi katika misingi ya Torati ya Musa ambayo ndiyo ilikua mwongozo wa maisha ya kila myahudi. Anasisitiza wajibu wa kila mmoja katika familia na matokeo yake. Matokeo ya maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia pamoja na utandawazi ndugu mpendwa ni makubwa ajabu. Hayaelezeki. Athari zake tunaziona wazi kabisa katika familia zetu. Mifumo ya elimu na kijamii imetufanya nasi wazazi kuona kama tumerahisishiwa kazi ya malezi. Muda mwingi sana hatupo na watoto wetu. Malezi yamehama kutoka nyumbani kwenda mashuleni. Asilimia zaidi ya 90% ya muda wa mtoto hayupo na wazazi wake. Ni kweli, ni mfumo wa kijamii, tutasema ni kazi, majukumu yanatubana. Lakini tukumbuke kuwa jukumu la malezi lilikua ni jukumu letu la kwanza kabla ya hayo yote. Ni huzuni mzazi kusikia mtoto ameharibika na huna taarifa kwa kuwa huna muda naye. Hujui tabia yake, hufahamu mienendo yake, unakuja kukutana na suprise muda ambapo samaki hafai tena kumkunja. Simu, mitandao, internet imeharibu watoto wetu kwa asilimia kubwa sana. Muda mwingi wa kufanya mambo ya msingi unatumika kwa ajili ya mitandao, ambayo pia imejaa mambo mengi yasiyo mazuri. Tuna mifumo ya kijamii inayosisitiza haki hata kama zinapingana na mapenzi ya Mungu vyote vikiwekwa chini ya mwamvuli wa haki za binadamu. Wazazi turudi kwenye misingi ya Imani na tamaduni zetu. Tusimpe shetani nafasi kwa kushirikiana naye pale tunapokwepa na kushinda kutimiza nyajibu zetu muhimu. Tuziweke pia familia zetu katika maongozi ya Mungu, tukiwaomba Yesu Maria na Yosefu ulinzi wao.

Familia ni kitovu cha uinjilishaji
Familia ni kitovu cha uinjilishaji   (@Vatican Media)

Tatu: Matokeo ya utii kwa wazazi ni Baraka tele (Blessings of obedience). Yoshua bin Sira anatuambia kuwa, “Anayewaheshimu wazazi atawafurahia watoto wake mwenyewe na siku ya kuomba dua atakasikiwa” (Ybs 3:5-6). Anayewaheshimu wazazi anajijengea msingi wa baraka na neema hata kwa uzao wake ujao. Pia anatuambia kuwa akisali sala zake na dua zake zitasikiwa. Ndugu wapendwa, katika amri zote kumi za Mungu, amri ya nne tu ndio amri inayoambatana na baraka kwamba, “Waheshimu baba na mama upate miaka mingi na heri duniani” maisha marefu na yenye heri ni baraka zitokazo kwa Mungu kwa anayewaheshimu wazazi. Zaidi ya hayo, tunaambiwa kuwa uzao wetu pia utabarikiwa. Hivyo tuwafundishe na kuwalea watoto wetu kwa misingi kwamba watakua katika kutuheshimu sisi wazazi. Watambue kuwa wana wajibu wa kuwapenda, kuwaheshimu, kuwajali na kuwasadia wazazi wao. Tusiwajengee watoto mazingira ya kuja kutukosea heshima wajapo kuwa watu wazima. Wazazu na walezi jitahidi kuishi maisha maadilifu, ugomvi wenu msihamishie kwa watoto, msiwaumize watoto bila sababu na kuwajengea maumivu na hali ya kutaka kulipiza kisasi.

Familia ni Kanisa Dogo la Nyumba, shule ya sala, haki na amani
Familia ni Kanisa Dogo la Nyumba, shule ya sala, haki na amani   (@VATICAN MEDIA)

Somo la Injili: Ni Injili kama ilivyoandikwa na Mathayo 2:13-15, 19-20. Somo la Injili katika Sikukuu hii ya Familia Takatifu laelezea tukio la Familia Takatifu kukimbilia Misri, kumlinda mtoto Yesu dhidi ya hatari ya kuuwawa na Herode na kisha baadaye wanarejea tena Galilaya baada ya Herode kufariki. Tendo hili kiteolojia linatukumbusha kuwa, kuzaliwa kwa Kristo Mkombozi ni mwanzo wa taifa teule jipya mfano wa taifa la Israeli. Kristo kama mwana pekee wa Mungu, vile kama ilivyokuwa Israeli taifa teule la Mungu, kwa kukimbilia Misri anaturudisha kutafakari juu ya mwanzo wa safari ya ukombozi kutoka utumwani Misri kwenda nchi ya Ahadi. Ni kwa njia ya Kristo safari hii ya ukombozi itatimia. Pili tunaona wajibu wa wazazi walioisikia daima sauti ya Mungu na kuishi kadiri ya maongozi yake, wanavyotimiza wajibu wao katika hatua zote za malezi na makuzi ya Bwana wetu Yesu Kristo. Katika somo hili la Injili dominika ya leo tuna mafundisho matano ya kujifunza. Kwanza: Utii na unyenyekevu katika familia Takatifu. Katika somo la Injili, tunaambiwa kuwa “Wazee wake Yesu huenda Yerusalemu kila mwaka wakati wa sikukuu ya Pasaka” (Lk 2:41-42). Yosefu na Maria licha ya kuwa wazazi wa Mungu, bado walikua watii na wanyenyekevu katika jamii yao, walifuata sheria na taratibu zote zilizowahusu kuhusiana na mtoto Yesu. Wapendwa familia ya Mungu, familia hii takatifu inatufundisha kuwa wanyenyekevu. Mwenyezi Mungu aliwainua Yosefu na Maria kuwa wazazi wa Yesu lakini hakujikweza wala hawakupungukiwa kuwa wanyenyekevu na watii. Sisi mara kadhaa Mungu anapotuinua tu kidogo tunasahau na kukosa unyenyekevu na utii kwa Mungu aliyetuinua na kwa wenzetu pia. Anapotupa mali na utajiri tunaona kama ni kwa nguvu na juhudi zetu na hata hatumtumikii tena vile inavyopaswa. Hatushiriki kwa lolote kwa kanisa na kwa jamii kwa kisingizio kwamba “Kazi hizo haziendani na hadhi yetu”. Hatujitoi kwa kazi za kanisa, kwa jumuiya ndogondogo wala kwa nyajibu zingine kwa jamii zetu. Tuwe wanyenyekevu hata pale Mungu anapotuinua juu.

Familia ni Kanisa Dogo la Nyumba, shule ya sala, haki na amani
Familia ni Kanisa Dogo la Nyumba, shule ya sala, haki na amani   (@Vatican Media)

Pili: Uwajibikaji wa pamoja katika familia Takatifu (Collective responsibility). Mwinjili Luka anatueleza kuwa Yosefu na Maria walipotambua kuwa mtoto Yesu hakua pamoja nao, walianza mara moja harakati za kumtafuta mtoto Yesu. Walitembea mwendo wa kutwa nzima wakimtafuta kwa jamaa zao na wenzao na walipomkosa wakaanza safari tena kurudi Yerusalemu, kwa sasa ni takribani kilometa 146 (Mwendo takribani masaa 33 kwa miguu). Ikawa baada ya siku tatu wakamkuta hekaluni. Ndugu wapendwa, familia Takatifu inatukumbusha juu ya uwajibikaji wa pamoja katika majukumu ya malezi. Mara kadhaa tunakwepa wajibu wa pamoja katika kuwalea watoto wetu kwa kisingizio kwamba tupo bize na kazi na majukumu mengi kwa hiyo kazi ya kulea tunawaachia wafanyakazi. Na hata matatizo yanapotokea katika malezi huwa tunaishia kutupiana lawama kwamba mama wewe ndio umesababisha huyu mtoto kuharibika, au baba wewe ndo umechangia huyu mtoto/hawa watoto kuharibika. Hatuko tayari kukaa chini na kutafuta suluhu ya pamoja jinsi gani ya kuwajibika katika malezi na makuzi ya watoto wetu. Kuna mahali flani mzani hauko sawa. Wanandoa, kaeni chini liangalieni upya jambo hili ili tuweze kupata suluhu sahihi kwa wakati pindi changamoto ya malezi inapotokea.

Changamoto za maisha ya ndoa na familia zichukuliwa kwa utulivu
Changamoto za maisha ya ndoa na familia zichukuliwa kwa utulivu   (@VATICAN MEDIA)

Tatu: Utulivu katika kutatua changamoto katika familia zetu. Yosefu na Maria hakuna sehemu tunaambiwa walianza kulaumiana na kufokeana wala hakuna popote katika maandiko matakatifu tunaambiwa walianza kurushiana maneno licha ya uchovu walioupata katika kumtafuta mtoto wao Yesu. Ni Bikira Maria tu anasikikia akimuuliza Yesu, “Mwanangu, mbona umetutenda hivi? Tazama baba yako na mimi tulikua tukikutafuta kwa huzuni” Yosefu hakusema neno lolote. Hizi ni Fadhila za kimungu walizokuwa nazo zilizowasadia kutatua changamoto zao kwa utulivu mkubwa. Ndugu wapendwa, mara kadhaa tunakutana na changamoto mbalimbali katika familia zetu. Tujiulize kila mmoja ni kwa jinsi gani tuna utulivu katika kuzitatua? Ni mara ngapi tumekua tayari kusikilizana wakati changamoto zinapotokea? Mara ngapi tumekua tayari kuombana msamaha na kujishusha ili kutatua vyema changamoto zetu? Mara ngapi tunamshirikisha Mungu katika matatizo na changamoto zetu na kumwambia Mungu tusaidie tuvuke salama katika hili? Tuwaombe Yosefu na Maria watuombee kwa Yesu ili daima tujaliwe fadhila za kimungu ili zitusaidie kutatua kwa utulivu chagamoto tunazokutana nazo kila siku katika familia zetu.

Familia ni Kanisa Dogo la Nyumba, shule ya sala, haki na amani
Familia ni Kanisa Dogo la Nyumba, shule ya sala, haki na amani   (@Vatican Media)

Nne: Familia Takatifu inatukumbusha wajibu wa kulinda na kutetea uhai. Katika somo la Injili Takatifu tumesikia namna Yusufu na Maria walivyofanya jitihada ya kumlinda mtoto Yesu dhidi ya hatari ya kuuwawa na herode. Wanakimbilia Misri ambapo walikaa mpaka pale Herode alipofariki na kisha wakarejea tena Galilaya. Ndugu mpendwa, familia Takatifu inatukumbusha kuwa ni wajibu wa familia kulinda zawadi ya uhai ambayo ni zawadi kutoka kwa Mungu. Tunashuhudia katika jamii ongezeko kubwa la vitendo vya ukatili dhidi ya zawadi hii ya uhai. Utoaji wa mimba, matumizi ya vidhibiti mimba ni dhambi dhidi ya zawadi ya uhai. Tunakuwa sawa na Herode aliyewaua watoto wasiokuwa na hatia, wasioweza kujitetea. Pia tunashuhudia vitendo viovu vya ukatili ndani ya ndoa, unyanyasaji na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu. Tano: Kuisikiliza sauti ya Mungu na kumwalika akae daima katikati yetu. Yosefu na Maria daima walisikiliza na kutii Neno la Mungu. Yosefu hakuna sehemu yoyote alizungumza katika maandiko Matakatifu, lakini alisikiliza katika ukimya na utii mkuu na akatenda kila Neno aliloongozwa na Mungu kwa ajili ya Familia yake. Ndugu mpendwa, Sikukuu hii inatualika kutafakari upya uhusiano wetu na Mungu katika familia zetu. Je, familia zetu zinaongozwa na Mungu? Mipango yetu katika familia tunamshirikisha Mungu kwanza kabla ya kuanza? Tunasali pamoja sala za familia, kumwalika Mwenyezi Mungu akae daima katikati yetu? Ndoa nyingi zinavunjika, familia nyingi zinavunjika kwa sababu ya kukosa kuisikiliza na kuitii sauti ya Mungu, tunachukua muda mwingi kusikiliza na kufuata maongozi na hisia zetu, ushauri na maneno ya watu wengine kwanza kabla ya Mungu. Tumwombe Kristo aliyeazaliwa ndani ya familia azaliwe kwetu hata sasa. Atusaidie kufanya maamuzi sahihi, kutenda kwa haki na kuamua kwa busara. Tunapoisikiliza sauti ya Mungu ni dhahiri kabisa tutaweza kusikilizana sisi kwa sisi na kuchukuliana kwa upole, upendo na kujitoa sadaka kila mmoja kwa mwenzake.

Familia zilinde na kutetea Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo
Familia zilinde na kutetea Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo   (@VATICAN MEDIA)

Somo la Pili: Ni kutoka katika Waraka wa Mtume Paulo kwa Wakolosai 3:12-21. Katika somo la Pili Mtume Paulo anatuasa kuwa kwa njia ya Kristo sisi tumekua wateule wa Mungu, watakatifu, wapendwao na Mungu na hivyo tunapaswa tujivike moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole, uvumilivu, tukichukuliana na kusameheana. Zaidi ya hayo yote, tujivike upendo, ndicho kifungo cha ukamilifu. Hizi Ndugu zangu ndizo zilikua tunu za familia Takatifu. Zikishakuwepo fadhila za Kimungu ndani mwetu, mengine yote yatakwenda katika mstari. Tumwombe Yesu atusaidie ili nasi tuweze kuiga na kuziishi hizi tunu njema ambazo alipenda kuwashirikisha kwanza Maria na Yosefu ili nasi tuweze kuwa kilelezo cha familia bora za kikristo katika jamii yetu, jamii ambayo inakumbwa na changamoto mbalimbali zihusuzo familia siku hizi. Hitimisho: Katika Sikukuu hii ya Familia, tumshukuru Mungu kwa zawadi ya Familia hii Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu inayotupa mfano wa namna tunapaswa kuziishi fadhila za Kimungu katika familia zetu. 

Tafakari Familia Takatifu
27 Desemba 2025, 15:54