Injili ya Dominika ya XXXII ya Mwaka 'C' inatoka Luka (Lk 20:27-38).Ujumbe umejikita katika kweli ya ufufuko wa wafu na maisha yajayo. Injili ya Dominika ya XXXII ya Mwaka 'C' inatoka Luka (Lk 20:27-38).Ujumbe umejikita katika kweli ya ufufuko wa wafu na maisha yajayo.  

Dominika ya 32 ya Mwaka C:Maisha ya baada ya kifo

Kila kiumbe hai kina sifa ya kufa.Sifa hii ni ya pekee kwani kila kiumbe hai huiogopa na kuimbia, hasa binadamu kwa kutaka kuishi milele duniani.Hii ni kwa sababu, roho ya mtu haifi,na mafundisho ya dini mbalimbali yanakiri ukweli huu.Hata dini asili za kiafrika zinakiri na kufundisha kuwa Mababu zetu waliokufa zamani,roho zao zinaishi na zina mahusiano na maisha ya watu.

Na Padre Paschal Ighondo –Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, Dominika ya 32 mwaka C wa kiliturujia katika Kanisa, kipindi cha kawaida. Tuko ukingoni na mwishoni mwa mwaka wa kanisa kilitrujia, ujumbe wa masomo unahusu maisha baada ya kifo, fumbo la maisha ya sasa na yajayo katika ulimwengu ujao. Kwa kuwa hakuna aliyeweza kuthibitisha kuwa hakuna maisha baada ya kifo, sisi tunaamini kuwa kuna maisha baada ya kifo na tunamuomba Mungu atustahilishe kuyashiriki. Ni katika tumaini hili zaburi ya wimbo wa mwanzo inasema hivi; “Maombi yangu yafike mbele zako, uutegee ukulele wangu sikio lako, ee Bwana” (Zab. 88:2). Na Mama Kanisa katika sala ya mwanzo anasali; “Ee Mungu Mwenyezi Rahimu, utuepushe kwa wema wako na yote yawezayo kutudhuru, tuwe tayari rohoni na mwilini kutimiza mapenzi yako pasipo kizuio”.

Somo la kwanza ni la kitabu cha kwanza cha Wamakabayo (2Mak 7: 1-2, 9-14). Ni simulizi la ndugu saba walivyokufa kifo dini kwa ujasiri, “kuliko kuzivunja amri za wazee wao”. Huu ni wakati wa mapinduzi ya Wamakabayo karne II KK, kipindi cha uongozi wa mfalme Antiokus, 175 KK. Hawa walikufa kifo dini wakitii sheria ya Musa iliyowakatakaza kula nyama tamu ikisema: “Na nguruwe, kwa sababu yeye anazo kwato, ni mwenye miguu iliyopasuka kati, lakini hacheui, yeye ni najisi kwenu. Msiile nyama yao, wala msiguse mzoga wao, huyo ni najisi kwenu” (Wal 11:7-8). Katazo hili bila shaka ni kwa sababu mnyama huyu alitumiwa kwa sadaka za kafara kwa wagiriki na wababilonia kwa miungu yao. Kwetu sisi wana wa Agano Jipya, hatukatazwi kula nyama yake, na Maandiko Matakatifu yanasema wazi kuwa kila alichokiumba Mungu ni kisafi, “hakuna kilicho najisi kwa asili yake, lakini kwake yeye akionaye kitu kuwa najisi, kwake yeye kile kitu ni najisi” (Rm 14:14). “Kwa maana kila kiumbe cha Mungu ni kizuri, wala hakuna cha kukataliwa, kama kikipokelewa kwa shukrani (1Tim 4:4). “Vitu vyote ni safi, lakini hakuna kilicho safi kwao walio wanajisi, wasioamini, bali akili zao zimekuwa najisi na nia zao pia” (Tit 1:15).

Lakini lengo la simulizi hili kwetu sio suala la kula au kutokula nyama hii tamu ya nguruwe, bali ni kutuimarisha kiimani kuhusu maisha baada ya kifo, na ufufuko wa wafu kama walivyokiri hawa ndugu wakisema: “Mungu wa ulimwengu, baada ya kifo atatufufua sisi tuliokufa kwa ajili ya amri zake, hata tupate uzima wa milele” (2Mak 7:9). “Kutoka mbinguni nalipewa hivi, na kwa ajili ya amri za Mungu…natumaini kuvipokea tena” (2Mak 7:11). “Ni afadhali kufa kwa mikono ya wanadamu na kuzitazamia ahadi zitokazo kwa Mungu, kuwa tutafufuliwa naye” (2Mak 7:14). Hivyo kwa walio waadilifu kwa amri za Mungu, maisha yajayo yatakuwa ya heri na furaha, lakini kwa wadhambi yatakuwa maisha ya mateso.

Yesu kuhusu fundisho hili alisema; “Mimi ndio huo uzima na ufufuo, Yeye aniaminiye, ajapokufa atakuwa anaishi, naye kila aishiye na kuniamini mimi hatakufa kabisa hata milele (Yn 11:24-26). Hili ndilo tumaini letu tunapozishika na kuziishi amri na maagizo ya Mungu, kuupata uzima wa milele mbinguni. Ni katika tumaini hili zaburi ya wimbo wa katikati inasema; “Ee Bwana, usikie ombi langu la haki, usikilize kilio changu, utege sikio lako kwa ombi langu, lisilotoka katika midomo ya hila. Nyayo zangu zimeshikamana na njia zako, hatua zangu hazikuondoshwa. Ee Mungu, nimekuita kwa maana utaitika, utege sikio lako ulisikie neno langu, unifiche chini ya uvuli wa mbawa zako. Bali mimi nikutazame uso wako katika haki, niamkapo nishibishwe kwa sura yako” (Zab. 17: 1, 5-6, 8, 15).

Somo la pili ni la waraka wa pili wa Mtume Paulo kwa Wathesalonike (2Thes 16-3:5). Ni mawaidha ya mtume Paulo, kuwaimarisha na kuwatia moyo wakristo wa jumuiya hii ambayo ilikuwa inateseka kwa hofu, wasi wasi na mashaka, kuhusu siku ya hukumu ya mwisho. Akiwatia moyo, anawaasa wasifikiri sana juu ya wakati ujao, waweke nguvu zao katika maisha ya sasa, waishi vyema kwa kutenda matendo mema bila wasi wasi, hofu wala mashaka. Kwani matendo mema ya sasa ndiyo yanayowahakikishia furaha ya maisha ya baada ya kifo. Hivyo wajikite katika kuishi kwa upendo wa kikristo, wavumilie yote kwa furaha, na wabaki imara katika kila neno na tendo jema. Lakini pia anawaasa wadumu katika sala wakiombeana na Bwana ni mwaminifu, atawafanya imara na kuwalinda na yule mwovu.

Injili ni ilivyoandikwa na Luka (Lk 20:27-38). Ujumbe umejikita katika kweli ya ufufuko wa wafu na maisha yajayo. Yesu anatoa fundisho hili akijibu swali la kizushi la Masadukayo kuwa mwanamke aliyeolewa na ndugu saba na wote wakafa bila kuacha uzao, atakuwa mke wa nani katika maisha yajayo? Ifahamike kuwa Masadukayo lilikuwa ni kundi la matajiri, wafanyabiashara na wenye ardhi, wasioamini juu ya ufufuko wa wafu na uwepo wa malaika, wala roho (rej. Lk Mdo 23:8). Tunaweza kushangazwa kwa nini hawa ndugu saba walimuoa mwanamke mmoja wakiachiana? Hii ilikuwa ni sheria iliyowekwa na Musa kwa lengo la kumpatia uzao ndugu wa kiume aliyekufa bila kuacha mtoto ili kwamba jina lake lisije likasahaulika katika Israeli (rej. Kumb 25:5-10).

Katika kujibu swali hili, Yesu anarejea Maandiko Mataktifu, kwamba wafu watafufuliwa na Mungu wetu ni Mungu wa wazima na sio Mungu wa wafu (Mk 12:24; Kut 3:6). Lakini pia maisha yajayo ni maisha ya utukufu, hivyo hakuna kuoa wala kuolewa, walioko huko hawafi tena; kwa sababu wako sawa na malaika, wana mwili wa utukufu. Kumbe basi maisha ya sasa sio aina pekee ya maisha, kuna maisha mengine tofauti na haya, maisha ya utukufu, na furaha isiyo na mwisho mbinguni. Zaidi sana jibu la Yesu linatufundisha kuwa maisha ya mwanadamu hayapo katika mamlaka na umiliki wa mwanadamu mwingine, uhai wa mtu haupo mikononi mwa mtu mwingine, bali kwa Mungu mwenye uwezo wote, aliyeumba vitu vyote.

Kila kiumbe hai kina sifa ya kufa. Sifa hii ni ya pekee kwani kila kiumbe hai huiogopa na kuimbia, hasa binadamu kwa kutaka kuishi milele duniani. Hii ni kwa sababu, roho ya mtu haifi, na mafundisho ya dini mbalimbali yanakiri ukweli huu. Hata dini asili za kiafrika zinakiri na kufundisha kuwa Mababu zetu waliokufa zamani, roho zao zinaishi na zina mahusiano na maisha ya watu. Ndio maana kukiwa na shida kama magonjwa ya ajabu, au vifo vya ghafla, wanasema mizimu ya mababu imekasirika kwa kukosewa. Na ili kujipatanisha nao linahitajika tambiko. Kwetu sisi wakristo tambiko letu ni sadaka ya Misa Takatifu, tambiko la milele. Lakini kifo sio ukweli wa baadaye, ni ukweli wa kutwa kuchwa, kwa maana tunakikabili kila siku (1Cor.15:31). Chanzo cha kifo ni adhabu kwa dhambi ya wazazi wetu wa kwanza, kukosa utii kwa Mungu. Lakini kwa kifo na ufufuko wa Yesu Kristo, kifo si adhabu tena bali ni njia ya kwenda mbinguni na hakuna njia ya mkato zaidi ya kifo, ukweli ndio huo na habari ndiyo hiyo.

Kumbe basi maisha ni suala la uhai na kifo. Kifo ni mabadiliko kutoka hali moja, kuingia hali nyingine. Mtu anayekufa, amekuwa anaishi, na anakufa ili aishi tena. Tena kila hatua ya maisha ni kifo na maisha, kuanzia mbegu za kiume na yai la kike vikifa mimba inatungwa, mimba inakufa kichanga kinazaliwa, uchanga unakufa, utoto unazaliwa; utoto unakufa, ujana unazaliwa; ujana unakufa, utu uzima unazaliwa, utu uzima unakufa, uzee unazaliwa na mwisho wa yote, maisha huingia kifo, na kifo huingia maisha. Kumbe ni katika kuishi tunakufa na katika kufa tunaishi; lakini mwisho wa yote, kifo kitaangamizwa na uzima utatawala (rej. Isa. 25:8), wakati “kifo na kuzimu vikatupwa ndani ya ziwa la moto” (Ufu. 20:14). Basi kama ni hivyo, kifo ni mapambazuko ya maisha mengine, maisha ya umilele. Kama giza linavyoupisha mwanga, vivyo hivyo kifo hupisha maisha, maana kifo ni nukta ya pekee kati ya maisha ya muda na maisha ya umilele.

Hivyo kama mlinzi angojeavyo kwa hamu kubwa mapambazuko ya siku nyingine (Zab. 130:6), ndivyo tunavyopaswa kukisubiria kifo ili kitukute katika hali ya neema tuweze kushirikishwa maisha ya milele kwa njia ya Kristo Bwana wetu (rej. KKK 1014). Ni katika tumaini hili mama kanisa katika sala ya kuombea dhabihu anasali hivi; “Ee Bwana tunaomba upende kuzitazama dhabihu hizi, ili tujipatie kwa hamu neema za fumbo hili la mateso ya Mwanao tunaloadhimisha”. Na katika sala baada ya komunyo anapohitimisha maadhimisho haya anasali; “Ee Bwana, sisi tulioburudishwa kwa neema takatifu tunakushukuru na kukuomba sana rehema yako. Nayo neema ya uchaji idumu ndani yetu sisi, tuliopata nguvu ya mbinguni kwa Roho wako”. Na hili ndilo tumaini letu.

Tumsifu Yesu Kristo.

Dominika ya 32 ya Mwaka C
07 Novemba 2025, 17:44