Siku ya Nyerere,Tanzania:Utekaji umepelekea ulinzi wa haki ya uhai iliyo msingi kupotea!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Katika mahubiri yake, Askofu Mkuu wa Jimbo kuu la Dar Es Salaam nchini Tanzania, alitoa wito kwa Serikali kupatia ufumbuzi wa matukio ya utekaji yanayoendelea kuibuka nchini na pia kutoa wito wa serikali kusikiliza wananchi wenye malalamiko juu ya haki za kisiasa.” Askofu Mkuu Jude Thadaeus Ruwa'ichi (OFMCap) wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar Es Salaam, Tanzania, na Mwenyekiti wa Tume ya Upendo, Haki na Amani ya Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Tanzania(TEC), aliongoza Misa Takatifu, ya kumbukizi ya Mwasisi wa Tanzania na Mtumishi wa Mungu, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, iadhimishwayo kila ifikapo tarehe 14 Oktoba ya kila Mwaka, katika kukumbuka siku ya kifo chake mnamo 1999, vilevile Umoja wa Wanaume Katoliki,(UWAKA), Jimbo Kuu la Dar Es Salaam kuwategemeza Masista Wafransiskani wa Shirika la Dada Wadogo, huko Visiga Pwani.
"Siione haya Injili"(Rm 1,16)
Mara baada ya masomo yote, Askofu Mkuu Ruwa’ich alianza na Neno la Mtakatifu Paulo lililosomwa lisemalo: “Siionei haya Injili”… (Rm 1,16). “Wapendwa Taifa la Mungu, leo tumekusanyika kwa wingi kuadhimisha mambo mazito yanayolihusu Kanisa na Taifa. Mwanzo wa adhimisho hili, nilidokeza kwamba leo tarehe 14 Oktoba, sisi kama Watanzania, na kama wakristo tunamtukuza Mungu kwa zawadi ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Baba wa Familia, mwana UWAKA wa mfano, lakini pia kama Kiongozi wa Taifa letu. Ameongoza kwa namna iliyotukuka akipitia katika vipindi vigumu, lakini alistahimili mpaka mwisho Na hata baada ya kustaafu kwake aliendelea kuishi imani yake na maadili yaliyompasa kama Mkristo.” alibainisha Askofu Mkuu Ruwa’ichi. “
UWAKA kutegemeza Masista wa Dada Wadogo
“Na pamoja na kuadhimisha hili, leo wana UWAKA kutoka Parokia zote 161 za Jimbo Kuu la Dar Es Salaamu, wana jambo lao leo hii: Wamekusanyika kutelekeza utume wao mahususi kwa kuwatunza na kuwawezesha Dada Wadogo katika utume, katika ufuasi, na katika maisha yao ya Wakfu.” “Asante kwa kujitokeza kwa wingi.” Askofu Mkuu aliwashukuru kwa majitoleo yao.
Wapo wasiofanana na Paulo wakidhani unaweza kuwa Mkristo ukabangaiza
Akirudi katika Neno la Mungu, Askofu Mkuu Ruwa’ichi alindelea kusema kuwa kwa kuadhimisha haya, ni neno la Mungu ambalo linapaswa kutusindikiza, kutujenga na kutuongoza, kwa sababu ni utashi wa Mungu mwenyewe kwamba, tutembee kama watu wake. Katika Somo la kwanza, Mtume Paulo ni Mwalimu, na kijadi alikuwa mtu wa kimo kidogo: lakini hakuwa mfupi kimawazo, wala kimsimamo bali alikuwa thabiti. Na hilo linajitokeza katika Somo la kwanza la Warumi, “Mimi siionea haya Injili”(Rm 1,16…. “Ni jambo zito.” Injili ni jambo jema, ya Yesu Kristo, Mwana wa Mungu aliyetesewa, akafa na kufufuka. Kwa hiyo tunapaswa kuiishi na kushuhudia. Hatupaswi kuipelekea kilelemama, bali kuiweka katika vipaumbele, na mitazamo yetu. Kwa bahati mbaya wapo wasio fanana na Paulo, wengine wanadhani unaweza kuwa Mkristo ukabangaiza, au kujiendea kivyako, Si hivyo. Ukristo wa namna hiyo ni upagani. Sisi hatujaitwa kuwa hivyo bali kuwa thabiti, kuwa na msimamo na mwelekeo,” alikazia Askofu Mkuu. Hata hivyo Askofu Mkuu aliwaonya na kusisitiza kuzinduka kwa wale ambapo wanaishi bila maisha yenye adhi, wala utukufu.
Farisayo anamkaribisha Yesu
“Katika Injili Yesu anayefundisha, ni Mwokozi wa wote. Na leo amekaribishwa nyumbani kwa Farisayo. Ukisoma Injili karibu utaona Mafarisyo walikuwa waasimu wa Yesu. Japokuwa hawakuwa wahuni, walikuwa ni walimu wa imani. Lakini katika uwasimu wao, na katika uwalimu na viongozi wa dini, walidhani kwamba Yesu ni kikwazo na wakapanga kumpinga.” Askofu Mkuu aliendelea kusema kuwa “Mfarisayo mmojawapao amejifanya kumkaribisha, japokuwa bado anaendelea kumdadisi: Mwalimu anastahili kutambulika kama mwalimu au geresha. Aliona kwamba kuna jambo moja alilozembea, lile la kula bila kunawa.” Askofu Mkuu aliongeza Hata sisi tunapenda kunawa kabla ya kula. Je ni nani alimwambia kwamba kabla ya kwenda pale, lazima anawe pale. Yesu anatoa fundisho kuwa usimhukumu mtu kwa vigezo vya nje tu. Thamani ya Mtu inapatikana katika vipaumbele, fadhila na sifa za ndani. “Yesu anatufundisha kuwa tuweke vitu vizuri vya ndani na ili maisha yetu yamuenzi na kutumkuza Mungu, yamtumikie na kumtangaza Mungu. Huo ndiyo wito wa wanaume wakatoliki.”
"Tukio la uchaguzi Mkuu ni tukio la kikatiba!
Askofu Mkuu Rwa'ichi katika sehemu inayohusu kumbukizi ya Mwasisi wa Taifa Mwalimu, amejikita kufafanua kuhusu Uchaguzi unaotarajiwa hivi karibuni mwezi huu nchini Tanzania. Askofu Mkuu alianza kusema kuwa: Siku ya Mwalimu Nyerere, tunapomkumbuka Baba wa Taifa, tunatafakari pia juu ya Nchi yetu na ustawi wa Watanzania kwa ujumla wao. Tunatafakari katika Nchi yetu na katika historia yake na masuala ya uchaguzi mkuu. Ndugu zangu, tukio la uchaguzi mkuu, ni tukio la kikatiba, kwani hapo ndipo wananchi hutegemewa kuwapa waliyo wachagua dhamana ya kutawala na kuongoza Nchi. Ibara ya nane ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inaweka wazi kuwa, “mamlaka ya nchi yamo chini ya wananchi, na serikari huwajibika kwa wananchi, serikari ikiwa na wajibu wa kulea na kuleta usitawi wa watu wote bila ubaguzi wa aina yoyote.”
Tume ya haki na amani ya Baraza na Maaskofu Katoliki Tanzania, ambayo ninaiongoza kwa kulitazama tukio la uchaguzi Mkuu wa mwaka huu wa 2025, inasikitishwa na hali inayoendelea, bila kusitishwa, ya kupotea na kutekwa watu. Utekaji huu unaonekana unaendeshwa kwa mpango wa kikundi maalumu ambacho kinatekeleza uovu huu sehemu mbali mbali za Nchi yetu. Utekaji huu umepelekea ulinzi wa haki ya uhai ambayo ni haki ya msingi kupotea, kwani hatusikii walio hapa kulinda uhai wa Watanzania kulaani au kukomesha huu utekaji na kutoweka kwa watu. Ni takribani zaidi ya miaka miwili, matukio haya yamezidi kukithiri na kuwafanya Watanzania wajiulize: iweje watekaji hawa wawe na nguvu kuliko vyombo vya ulinzi wa watu na kuliko wale wenye mamlaka ya kuwaletea watu matumaini ya kuishi na usitawi wake?
Dalili za kukomesha utekaji hazionekani wala hatusikii kulaaniwa kwa matukio hayo. Ikumbukwe kuwa, “uhai wa kila mwanadamu unadhihirisha utukufu wa Mungu. Mwanadamu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Mwanadamu ni kiumbe wa pekee ambaye hakuna mwenye haki au mamlaka ya kumwondolea uhai wake. Kazi ya Serikali ni kulinda uhai wa kila mwanadamu. Kwa mujibu wa ibara ya 14 ya Katiba ya Tanzania, “kila mtu ana haki msingi ya uhai wake na kuhakikishiwa kuwa haki hii inalindwa kwa gharama zozote zile.” Maaskofu, tunataka serikali kuhakikishia raia na watu wote usalama wa haki ya uhai wa kila mtu bila ubaguzi wowote. Uchaguzi mkuu, una maana tu, endapo watu wanapata viongozi wenye kulinda na wenye kutetea uhai. Wagombea wa vyama na vyama vyao kwa mujibu wa ibara ya Tatu na Tano, walipaswa kuonesha uwezo na moyo wa kuwashinda watekaji na wauaji. Sheria zipo zinazoonesha jinsi ya kushughulikia wahalifu. Kwa nini basi waliopotea na kutekwa hawapatikani, katika mahabusu? Tunaitaka serikali izingatie kanuni ya utawala wa sheria na kuheshimu kimatendo haki ya Msingi ya kila mwanadamu.
Kuelekea Uchaguzi Mkuu: Tunawaomba raia wote, kwa kuongozwa na dhamiri safi, iliyo hai, na yenye kuongozwa na ukweli halisi, wenye kuzingatia hofu ya Mungu, utu wa Mtu, historia nzuri ya nchi Yetu, Dhamiri hai na safi yenye kufanya maamuzi sahihi, kuzingatia hofu ya Mungu na utu, wa mtu, Kama Mungu alivyo wakilisha kwenye dhamiri yake. Na hivyo dhamiri hii ni mahali pa kila mwanadamu kupima na kufanya maamuzi yanayobeba hadhi ya utu na kuwajibika kwake mbele ya Mungu. Mpiga kura na mpigiwa kura mnaalikwa kuheshimu dhamiri juu ya suala hili la Uchaguzi Mkuu. Usirubuniwe kwa vitisho, wala kwa rushwa, usirubuniwe kwa namna yoyote ile,. Naiomba Serikali na wale wenye mawazo tofauti, ya masuala ya uchaguzi , muongozwe na utamamaduni wa kuwa na mazungumzano katika kutelekeza haki msingi za kisiasa kadiri ya ibara ya 21, ambapo kila raia ana haki hizo.
Kwa wanasiasa kupitia vyama na serkali zungumzeni. Wahakikishieni watu haki zao. Nguvu ya wananchi iko kwenye hoja siyo kwenye mabavu na hila. Serikari kupuuza wanao lalamika, si afya, wala tija kwa taifa letu, wakati uliokubalika kuzungumza ni sasa na wala hamjachelewa, hatuchelewi kujisahihisha wala kutenda mema: Barua ya Pili ya Mtume Paulo kwa Wakortho 2(Kor 6:2.) Naiomba Serikari, iwasikilize raia wenye malalamiko yao ya haki zao za kisiasa. Unyenyekevu mbele ya raia ujengeka kwenye ukweli na uwazi. Kiongozi wa watu akiwa mnyenyekevu ni mkweli, na anaaminika na watu wote. Tukumbuke kuwa historia ya uchaguzi katika Nchi Yetu kuanzia mwaka 1992 mpaka 2005 zilidhibitika kuwa ziliaminika viongozi wanapatikana kutokna na chaguzi hizo, hata kama zilikuwa na mapungufu yake. Ninawatakieni Uchaguzi Mkuu wa haki, wa ukweli, wa uhuru, na wa kuaminika. Mwaka huu wa 2025.
Mahujaji wa matumaini, …
Jubilei 20225, …
Alihitimisha Askofu Mkuu.