‘Mikono yangu ni sauti ya Mungu:’Utume wa mtawa Juliana kwa Wakatoliki Viziwi,Kenya
Na Sr. Christine Masivo, CPS- Vatican.
Juliana Muya, Mtawa kutoka Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi, CPS, alishuhudia tukio ambalo kiliadilisha maisha yake Dominika moja akiwa katika Parokia moja jijini Nairobi, Kenya. Kulikuwa na kijana mmoja kwa jina Paul, ambaye wenzake hawakumuelewa na walikuwa wanamdhihaki na wale aliokuwa nao, wakisema kuwa amewatukana akitumia ishara za ajabu. Lakini Mtawa Juliana aliyeshuhudia haya yote kwa umbali aligundua kitu tofauti.
“Niligundua kwamba Paul alikuwa kiziwi,” alikumbuka. “Hakuweza kujitetea, na aliondoka kwa uchungu. Nilitamani kwamba kama ningejua lugha ya ishara ningemsaidia.” Wazo hilo likawa mchipuko wa utume mpya rohoni mwake. Leo, Sr. Juliana ni mmoja wa wakalimani wa kiliturujia waliojitolea zaidi katika Jimbo Kuu la Nairobi, akihakikisha kwamba neno la Mungu linawafikia jamii ya viziwi. Ulimwengu utaaadhimisha Siku ya Kimataifa ya Watu Wenye Ulemavu mnamo tarehe 3 Desemba 2025. Siku hii ya Watu wenye Ulemavu,ilianzishwa kunako mwaka 1992 ili kukuza ushirikishwaji kamili na kulinda haki za watu wenye ulemavu. Lengo ni kuongeza uelewa wa changamoto wanazokabiliana nazo kila siku na kuongeza heshima yao katika kila nyanja ya jamii. Sr. Juliana ni mmoja wa watawa wengi wa mashirika Ulimwenguni na hata Mapadre wanaowahudumia watu wenye ulemavu kupitia ishara kwa lengo kutangaza Injili ya Kristo.
Kujifunza lugha ya mikono
Mnamo 2015, Parokia yake ilitangaza madarasa ya lugha ya ishara. "Nilifurahi sana," anasema, "lakini sikuweza kuanza mara moja kwa sababu ya huduma yangu na Watoto wa Kipapa wa Umisionari. Ilinibidi kuwafundisha wahuishaji mwaka mzima kabla sijawaacha wasimamizi kwa mwaka mzima." Hatimaye, alijiunga na darasa ya lugha ya ishara katika Parokia ya Mama Yetu wa Guadalupe, jijini Nairobi, akiwa amechelewa kwa majuma mawili, lakini alijipa moyo. "Kila Dominika nilihudhuria darasa na haikuwa rahisi, lakini nilivumilia na kila hatua ilikuwa na thamani," anasimulia. "Wakati mwingine nilikuwa nimechoka lakini niliendelea. Nilijua viziwi walihitaji mtu ambaye angeweza kutembea nao katika imani," anakumbuka.
Huduma
Baada ya masomo, mazoezi, na ushauri, alipewa jukumu la kuwa mkalimani wa liturujia siku ya Dominika ya Neno la Mungu. "Kanisa lilikuwa limefurika na wakristo, na jamii ya viziwi ilifurahi kuwa na mkalimani, na hii iliniongezea furaha," alisema. Sr Juliana, akipokea mshumaa wakati wa kuteuliwa kwake kama mkalimani wa lugha ya ishara katika Jimbo Kuu ya Nairobi kutoka kwa Padre Salvador Gomes MG, Padre wa zamani wa viziwi. Sr Juliana ametafsiri katika sherehe nyingi na Misa kwenye Televisheni ya kitaifa KBC, Dominika saa tatu asubuhi, kuashiria kuwa viziwi ni sehemu ya Kanisa la Ulimwengu wote.
Changamoto njiani
Huduma hii inachangamoto zake, alielezea, "Hakuna anayejua askofu au padre atahubiri nini. Wakati mwingine wao hutumia lugha ya juu sana ya kitheolojia, na lazima nipate haraka njia ya kuifanya ieleweke katika lugha ya ishara.” Mziki unaweza kuwa kikwazo kingine. "Wakati kwaya inapoimba kwa lugha nisiyoijua, lazima nijinyenyekeze na kuwaeleza kwamba sielewi na inanyenyekeza kuwa pamoja nao."
Kutia moyo na usaidizi
Anasisitiza msaada alioupokea. "Askofu Mkuu, Philip Anyolo, wa Jimbo Kuu la Nairobi anatutia moyo sana. Yeye hufuatilia yote ambayo jamii ya viziwi inafanya na hutoa msaada wa mawazo na hufuatia ratiba zetu za kila mwaka. "Mapadre ambao nimeshiriki katika tafsiri wakati wa Misa, pia hunitia moyo na kunihimiza kwamba utume huu unafaa," mtawa Juliana anasema kwa imani. Waamini pia wana jukumu lao, anasema. "Wanaheshimu sana. Daima huacha viti vya mbele kwa jamii ya viziwi. Ni jambo ambalo linaonekana dogo sana lakini kwa jamii ya viziwi, inamaanisha wanaonekana na kuthaminiwa."
Kiini cha utume wake
“Kila mara mimi husema kwamba, mikono yangu ni sauti ya Mungu. Hii hunipa nguvu, ili kuendelea kueneza kazi ya Mungu kwa viziwi ikiwa utume wangu kama mtawa," alisema. Anashuhudia kwamba imani ya jamii ya viziwi inamtia moyo kila siku, kwa kujitolea kwao kuhudhuria Misa na jumuiya ndogo za Kikristo na shughuli zingine. Wangependa sana kuwa kitu kimoja na yale yote yanayofanyika kanisani. Huu ni utume wa tatu kwa mtawa Juliana, kwani yeye katibu na mhasibu kwa taaluma.
Sauti kimya
Akitafakari Sr Juliana akishangaa jinsi kukutana kwake na yule kijana aliyekuwa kiziwi ilimpa motisha ya kuwasaidia viziwi kwa njia ya ishara. "Mungu alitumia wakati huo kufungua macho yangu. Leo, nawaona viziwi si kama kimya, bali kama wamejaa uhai na imani." Kupitia mikono yake, Neno la Mungu limepata sauti mpya. Kupitia huduma yake, viziwi hawako tena pembezoni, bali katika moyo wa Kanisa. Huduma yake ni daraja la ukimya. Paul kijana aliyemtia moyo kujifunza lugha ya ishara anashukuru kwamba yuko pale kutafsiri. Paul sasa ni katekista na husaidia kufundisha jamii ya viziwi katekisimu na mwaka huu parokia ilimkaribisha mshiriki mmoja kiziwi katika familia ya Kanisa. Anatamani kujiunga na upadre na anajifunza lugha ya ishara ya Kihispania anapojiandaa kwenda Hispania kujiunga na Jumuiya ya Mapadre viziwi, na Sr Juliana amekuwa msaada mkubwa anapomsaidia kujiandaa kwa safari yake ya Upadre na kuwasilisha lugha ya ishara popote anapohitaji.