Jimbo la mzimkulu:Watawa Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu. Jimbo la mzimkulu:Watawa Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu.  #SistersProject

Huduma na ushuhuda wa Masista Wamisionari wa Damu Azizi (CPS) kwa miaka 140 ya utume

Masista wamisionari wa damu azizi(CPS)wameadhimisha miaka 140 ya uwepo wa kimisionari,huduma na ushuhuda.Safari iliyoanzia kwenye vilima vya KwaZulu-Natal,Afrika Kusini na tangu wakati huo imetanda ulimwengu mzima.

Na Sr. Christine Masivo, CPS

Masista wamisionari wa damu azizi walikusanyika huko Mariannhill, Afrika Kusini, hivi karibuni tarehe 8 Septemba 2025 kuadhimisha Misa Takatifu wakiongozwa na Askofu Neil Augustine Frank wa  Jimbo la  Mariannhill na kumuenzi Mwanzilishi wao, Abate Francis Pfanner, aliyezikwa kwenye makaburi yao. Mahali alipozikwa bado ni ishara ya imani, ujasiri, na ukumbusho kwamba maono ya mtu mmoja yanaweza kubadilisha maisha ulimwenguni, na kazi yao inaendelea kuwa bora wanapotangaza upendo wa Kristo wa upatanisho. Askofu Mkuu Siegfried Mandla Jwara wa Jimbo Kuu la Durban, Askofu Thulani Victor Mbuyisa wa Jimbo la Kokstad, Shirika la  Wamisionari wa Mariannhill (CMM), na mjumbe wa Shirika la Mtakatifu Paulo, Mtawa wa Kwanza (OSPPE), Askofu Stanisław Jan Dziuba wa Jimbo la Umzimkulu pia walihudhurua sherehe hii.

Askofu Frank katika mahubiri alisema kwamba: "Ni mpango wa Mungu kwa shirika hili la masista kuwepo." Aliwakumbuka wanawake watano wa kwanza wenye ujasiri, ambao waliacha maisha ya zamani  ya faraja na kumtangaza Kristo kwa watu wa Afrika, kwa mwaliko wa Abate Francis kwenda Afrika Kusini. "Inahitaji ujasiri na ustahimilivu ili kuwa mmisionari, ni imani na malezi yao ambayo yamewafanya kutanguliza agizo la Injili lisemalo “Nendeni ulimwenguni kote mkafanye wanafunzi wa Mataifa yote,” alisema. Kwa kuongezea alikumbusha kuwa: “Hizi si sifa za kibinadamu bali ni karama za Roho Mtakatifu na nguvu za Mungu.”

Mahali alipozikwa Mwanzilishi wa Shirika Abate Francis Pfanner huko Mariannhill,Afrika Kusini.
Mahali alipozikwa Mwanzilishi wa Shirika Abate Francis Pfanner huko Mariannhill,Afrika Kusini.

Mwanzilishi mwenye maono

Historia ya masista hawa haiwezi kutenganishwa na maisha ya mwanzilishi wao, Abate Francis Pfanner, mtawa na Padre wa Kitrappisti anayejulikana kwa hali yake ya kiroho ya kina, ukimya, na maisha ya kutafakari. Matrappisti huishi maisha ya upweke, sala, na sheria nzito. Abate Pfanner alikuwa na maono tofauti, yaliyokaidi kanuni za wakati wake, aliona jambo jipya, alikuwa na nia ya kuwainua wanawake na wasichana kutoka hali ya chini nchini Afrika Kusini mwishoni mwa karne ya 19, Abate Pfanner alitambua kwamba uinjilishaji na mabadiliko ya kijamii yalihitaji uwepo wa kina wa wanawake watawa.  Akijitenga na masharti ya kitawa na kiutamaduni, alianzisha masista wamisionari wa damu ya azizi waliojitolea kwa maombi na vitendo ‘Ora et Labora’ wakifunga kwa sala, tafakari huku wakiwahudumia watu wote. Ndoto yake  ikiwa kuanzisha hili shirika la kimisionari la wanawake, kwa kuwainua maskini na waliotengwa hasa wanawake na mtoto wa kike katika KwaZulu-Natal, Afrika Kusini.

Mahali pa kuzaliwa - Mariannhill, Afrika Kusini

Masista Wamisionari wa Damu Azizi walianzishwa mwaka  1885, huko Mariannhill,  karibu na Durban, Afrika Kusini. Ndoto ya Abate Pfanner ilianza kutimizwa wakati wanawake vijana kutoka Ujerumani, walipofika Mariannhill wakiwa na bidii ya umisionari ambayo iliweka msingi wa shirika hili. Dhamira yao ilikuwa wazi kuelimisha, kuinua, na kuwawezesha wanawake na watoto wa kike, huku wakihudumia mahitaji ya kiroho, ya kimwili, ya kijumuiya mahalia, huduma za afya, na maendeleo ya kijamii. Hilo liliashiria kuzaliwa kwa Shirika  ambalo lingekua zaidi ya maono ya kwanza.

Wakati muhimu wa kusali na kuimba pamoja
Wakati muhimu wa kusali na kuimba pamoja

Kutoka Ulaya, kuzaliwa Afrika na kutanda dunia nzima

Mwanzo wa shirika ulikuwa na masista kutoka Ulaya, ikielekezwa katika njia za kiulya. Baadaye, misheni ilitanda zaidi ya mipaka, kwa kuitikia mahitaji ya Kanisa. Shirika hili lilitanda katika pembe kadhaa za Afrika, Ulaya, Amerika, Asia, na Oceania likikita mizizi katika tamaduni na jamii tofauti. Uwepo wao ulienea hadi kwenye misheni ya vijijini, miji, na maeneo yenye changamoto ambapo hitaji la upatanisho, huruma, na uponyaji ni kubwa zaidi. Misheni ilipopanuka, nyumba yao kuu, ambayo hapo awali ilikuwa Mariannhill, Afrika Kusini, baadaye ilihamishwa hadi Uholanzi, kuashiria Shirika lilikuwa la kimisionari na la kuhudumia wengi.

Watawa wakati wa miaka ya mwanzo ya kuanzishwa kwa Shirika
Watawa wakati wa miaka ya mwanzo ya kuanzishwa kwa Shirika

Uwepo wa kimataifa na huduma mbalimbali

Masista sasa wanahudumu katika nchi mbalimbali, wakiendeleza maono ya mwanzilishi wao. Wakihudumia nyanja mbali mbali na mahitaji tofauti ulimwenguni kote. Shirika hili lilianzishwa kwa malezi ya watoto wa kike na wanawake. Wanaendesha na kufanya kazi katika shule za ngazi zote, kuanzia shule za chekechea hadi vyuo vikuu, na kuwasaidia vijana kuwa raia bora. Wanazingatia sana maneno ya mwanzilishi wao ya kusoma majira za nyakati na kuboreshe huduma yao. Wanatumikia katika nyanja mbalimbali kama vile huduma za afya kwenye hospitali, zahanati, na huduma za afya zinazohamishika kuwafikia walio hatarini zaidi, katika vijiji na maeneo yaliyotengwa.

Kuitwa kutoka kila kabila,taifa na lugha kwenda kumtumikia Mungu kwa upendo
Kuitwa kutoka kila kabila,taifa na lugha kwenda kumtumikia Mungu kwa upendo

Masista hawa wanatoa huduma kubwa ya kichungaji ya kiroho kwa wagonjwa, wazee na walio katika hali ya kukata tamaa, katekesi katika parokia na shule, wanaendesha kituo cha katekesi, kutoa mafungo, na maombi ya maombezi na masista wakongwe ambao hawashiriki tena katika huduma. Kazi za kijamii na utetezi wa kuwezesha jamii zilizotengwa, kusaidia yatima, wanawake na wazee, na kuwahuduma waliotengwa. Masista hawa pia huwafunza wakulima kutumia mbinu za kilimo na utunzaji wa mazingira na  kukuza vyakula.  Mwanzilishi wao alikuwa wazi kwa watu wenye karama na vipaji mbalimbali, sanaa, muziki, na huduma za kiliturujia ambayo ni sehemu ya huduma yao katika kukuza ubunifu na kuimarisha ibada mahali  popote walipo, kwani wanatumia karama na talanta zilezile kuwawezesha wale wanaowatumikia.

Kuitwa na kwenda kuhudumia kwa upendo wa Kristo
Kuitwa na kwenda kuhudumia kwa upendo wa Kristo

Kuishi karama

Shirika hili limejikita kwa kuishi karama yake ya kuishi na kutangaza upendo wa ukombozi wa damu ya dhamani ya Kristo kwa njia ya upatanisho, uponyaji, na huduma, linaendelea kuitikia wito wa Mungu kwa ujasiri.

Wakati wa maadhimisho ya shirika
Wakati wa maadhimisho ya shirika

Mwangwi wa furaha

Mmoja wa mtawa mkongwe kwenye shirika hilo Sr. Mary Christine Pohland kutoka Ujerumani ambaye amehudumu kwa miaka 70 ya maisha ya kitawa nchini Afrika Kusini katika mahojiano alikuwa na haya ya kusema: "Sherehe inatuhimiza sisi watawa, washirika na wageni, kwamba tuwe na umoja wa kukumbukwa. Tunapaswa kuendelea bila kukata tamaa na kufanya upya roho zetu, kwa kuadhimisha miaka 140, hakika ni mafanikio ya ajabu kwetu. Miaka 140 tangu kuanzishwa kwa shirika letu  linaonesha urithi wa kudumu wa waanzilishi wetu wa kike na kiume. Kama haikuwa kwa kujitolea kwao, bidii, uvumilivu, hatungeweza kusherehekea hatua hii muhimu. Hatusherehekei yaliyopita, lakini pia tunatarajia siku zijazo yenye matumaini," alisema Sr. Oliver Nansitu.  "Lilikuwa tukio zuri sana, liliturudisha mwanzoni wa shirika hili katika wakati wetu, inaonesha kwamba baba mwanzilishi, alianzisha shirika zuri na tunamfuata," alitoa ushuhuda mwingine,  Sr  Dagmar Walz kutoka Ujerumani, huku akisherehekea miaka 64 ya maisha Kitawa. “Damu ya Thamani ni malipizi ya ukombozi wetu; kwa hivyo, lazima maisha yetu yawe wakfu kwa huduma na kujitolea," alisema Mtumishi wa Mungu, Abate Francis Pfanner

Watawa Afrika Kusini

Asante kwa kusoma makala hii. Ikiwa unataka kusasishwa,jiandikishe ili kupata habari za kila siku hapa: Just click here

 

08 Oktoba 2025, 14:10